Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kavuu
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote, kwanza ninamshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutujaalia afya njema na leo tuko kwenye Bunge lako Tukufu kuwasilisha Bajeti ya Wizara yetu ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninamshukuru sana Mheshimiwa Rais, kwa kweli, kwa kuniamini na kunipa nafasi ya Naibu Waziri, ambapo katika awamu zote hizi mbili nimefanya kazi katika Wizara mbili, chini ya Mawaziri saba. Ninawashukuru sana Mawaziri wote ambao nimefanya nao kazi, wamenijengea uwezo mkubwa sana wa kuelewa na kusimamia taratibu za Serikali.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninawashukuru sana Mheshimiwa Waziri wangu hapa, ana moto wa ujana na kwa kweli, ananisaidia sana, katika kusimamia shughuli hizi ambazo ananikasimu kila wakati, kwa ajili ya kutekeleza wajibu wa Wizara. Wanachamwino wasifanye makosa, turudishieni kamanda huyu, aweze kupiganisha jeshi la nchi kavu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kabisa, kama Waheshimiwa Wabunge walivyosema, Wizara hii changamoto zake ni nyingi sana, lakini ukweli toka Mheshimiwa Waziri amefika tunaona kuna mwelekeo na mabadiliko mapya ya Wizara hii.
Mheshimiwa Naibu Spika, tatu, niwashukuru sana wananchi wa Jimbo la Kavuu na leo kwa uwakilishi mdogo sana, wameweza kufika Viongozi wa Chama na Serikali, ambao tumemudu kuwaleta, waje wajionee tu mazingira ya kazi ambazo Wizara yetu imekuwa ikifanya kila panapokucha.
Mheshimiwa Naibu Spika, niishukuru familia yangu kwa jinsi ambavyo wamekuwa wavumilivu katika mapito yangu ya kazi za Serikali. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, maeneo yangu ni machache. Suala la kwanza, ni hizi Kliniki tunazoziendesha katika Wizara ya Ardhi. Ni kweli kabisa changamoto ni kubwa sana na katika uhalisia tumeona ni muhimu tuwe na vikao vya wazi katika kusikiliza matatizo ya Ardhi na ndiyo hizi Kliniki ambazo tumeendelea nazo. Tumeendelea kujifunza na kutekeleza kwa nguvu zote kuhusu suala la utatuzi wa migogoro ya ardhi na hasa hapa Dodoma.
Mheshimiwa Naibu Spika, Dodoma hii, chanzo kikubwa kabisa cha migogoro ya ardhi ambacho kimesababisha double allocation hapa Dodoma, moja, ilikuwa ni kuhama kutoka kwenye Mfumo wa CDA kuja Mfumo wa hizi Halmashauri. Mfumo wa CDA ulikuwa umeshajiwekea utaratibu wake, Mfumo wa Halmashauri ulipokuja kukawa hakuna ule uwiano wa makabidhiano ya kumbukumbu za CDA kwenda kwenye Miji na Halmashauri.
Mheshimiwa Naibu Spika, matokeo yake sasa vile viwanja ambavyo vilikuwa na namba tayari, vimeshakuwa plotted na vingine vilifikia mpaka hati, kwa wananchi wale waliokuwa wa asili, waliokuwa wameondolewa katika utaratibu wa awali wakarudi na Halmashauri zilishindwa kuzuia ule mwingiliano. Matokeo yake wananchi sasa kwenye kiwanja kimoja ambacho kilikuwa cha CDA, kilichokuwa na mtu mmoja, wale wa asili walivyorudi, walirudi watatu, wanne, watano. Hii ndiyo shughuli ambayo tunaendelea nayo. Kwa sasa tunaweza tukakiri kwamba, kazi kubwa imefanyika na tunaendelea.
Mheshimiwa Naibu Spika, tulikuwa na double allocation 3,000 sasa hivi tumebaki tunazungumza na double allocation karibu elfu moja, kama na mia mbili hivi, ambazo tunaendelea kuzitatua. Watuvumilie kwa sababu, kujenga ni kazi kubwa sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika hali ya kawaida migogoro yote ambayo imetajwa na Waheshimiwa Wabunge ni kweli, ipo kwa sababu, Wabunge wanatoka kwenye maeneo hayo na wanakiri kabisa kwamba, usumbufu huu wa migogoro bado umeendelea na hizi kliniki itakuwa ni zoezi na endelevu. Ingawa tunalitafutia dawa, kama tulivyoeleza mwanzo wakati wa hotuba ya Mheshimiwa Waziri kwamba, tukiunda hizi kamisheni zitakwenda kutusaidia kwa maana mfumo wa utendaji nao ilikuwa ni changamoto nyingine, kwamba, unakwenda inafika mahali Wizara inakatika, kule chini kuna watu wengine ambao wanakuwa na sauti na wale Watendaji. Kwa hiyo, kulikuwa kuna mwingiliano.
Mheshimiwa Naibu Spika, ile kamisheni inayokwenda kusimama sasa itatufikisha mahali ambapo tunatamani mpaka kwenye kijiji tuwe na Afisa Ardhi, kama taasisi nyingine zinavyofanya kazi, ili tuondokane na hii hadithi ya mwingiliano. Sasa hivi tunakwenda kwa kasi kubwa ya kupima, kupanga na kushirikisha katika kutatua hii migogoro.
Mheshimiwa Naibu Spika, tuna hii Tume ya Matumizi Bora ya Ardhi ya Vijiji, ambayo nayo huko ile ndiyo msingi wa kwanza ambao tunakwenda kuujenga kwenye vile vijiji, kwa ajili ya kwamba, hata ukuaji wake unapokuja unakuta mji upo tayari umeplaniwa (planned). Hata kama tutauhamisha kutoka kwenye level ya kijiji kwenda kwenye mji, bado yale maeneo yatakuwa yameshazingatiwa tayari kutoka kwenye mpango wa matumizi bora ya ardhi, kitakachokuwa kinafanywa pale ni kutanuliwa kuelekea kwenye uhitaji wa mji mdogo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, niwaombe tu Waheshimiwa Wabunge, kwa kweli, bajeti yetu ikipita, basi shughuli inaendelea. Kwa kweli, nimeona mawazo yote ambayo Waheshimiwa Wabunge wameyatoa, sisi tutayazingatia, tutakwenda kuyafanyia kazi kwa haraka sana na kama alichokisema dada yangu, Mheshimiwa mama Msambatavangu, jina gumu kabisa la balozi wetu huyu, katika uhalisia tumezingatia yote. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, suala la National Housing. Kama watakumbuka vizuri National Housing sasa hivi iko kwenye mageuzi makubwa ya kuelekea kwenye suala la kuleta miji mipya katika maeneo mengi sana. Kwa sasa hivi ni kweli, gharama za nyumba ni za juu sana, haziwezi kukidhiwa na watu wa kipato cha kati na kipato cha chini, hili ni jambo ambalo tunakwenda kuanzisha mazungumzo kati ya sisi, Wizara, pamoja na Wizara za wenzetu; Wizara ya Fedha, kwa ajili ya kuangalia hasa masuala ya kodi, ambayo kimsingi ndiyo yanayopandisha bei za ujenzi kwa sababu, vifaa vyetu hivi tunavyotumia, kwa ajili ya ujenzi vingi vimepanda bei.
Mheshimiwa Naibu Spika, ukija kwenye uhalisia, wakati wa kuuza ni lazima VAT ziingie na vitu vingine. Kwa hiyo, tunaendelea na mazungumzo ya awali na Wizara ya Fedha, ili kuona uwezekano wa kuhakikisha kwamba, lengo la National Housing liweze kurudi katika mfumo wake wa kawaida, kwamba, wananchi wajengewe nyumba zenye bei nafuu na wanazoweza kumudu kuzinunua.
Mheshimiwa Naibu Spika, mambo mengine yote ambayo yamechangiwa na Wabunge kwenye sekta hizi tunayachukua na mengine atakuja kuhitimisha Mheshimiwa Waziri. Nipende tu kukushukuru kwa kunipa nafasi.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninaunga mkono hoja. (Makofi)