Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

Hon. Prof. Patrick Alois Ndakidemi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Moshi Vijijini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

MHE. PROF. PATRICK A. NDAKIDEMI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nampongeza sana Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mheshimiwa Deogratius Ndejembi, Naibu Waziri, Mheshimiwa Geophrey Pinda, Katibu Mkuu Mhandisi Anthony Damian Sanga, Naibu Katibu Mkuu Ndugu Lucy Kabyemera, wataalam wa Wizara na wadau wengine kwa kazi nzuri wanazofanya.

Mheshimiwa Naibu Spika, mchango wangu utajikita kwenye umuhimu wa kutatua matatizo ya ardhi kwa kuwekeza nguvu ya ziada katika teknoloijia ya TEHAMA. Migogoro ya ardhi imekuwa ni changamoto ya muda mrefu sana nchini Tanzania, ikihusisha umiliki wa ardhi, mipaka na haki ya matumizi ya ardhi. Baadhi ya maeneo yanaathiriwa na migogoro ya kijamii kuhusu umiliki wa ardhi. Migogoro hii mara nyingi hutokea kutokana na ukosefu wa mifumo mizuri ya umiliki wa ardhi, michakato mibovu ya usajili wa ardhi pamoja na ukosefu wa taarifa sahihi za umiliki wa ardhi, ambapo husababisha mwingiliano wa madai ya ardhi kwa mmiliki zaidi ya mmoja.

Mheshimiwa Naibu Spika, migogoro hii imekuwa ikisababisha ugomvi wa kudumu na mauaji ya wananchi wanaogombea ardhi. Hapa nchini Tanzania, tumejionea migogoro mikubwa kati ya wakulima na wafugaji na kati ya wamiliki wa mbuga za wanyama, maeneo tengefu na wafugaji.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa ujumla idadi kubwa ya waathirika wa migogoro ya ardhi ni watu wa kipato cha chini na wenye uelewa mdogo wa kisheria, ambao wamekuwa wakiporwa ardhi zao na watu wenye kipato kikubwa na mabavu ya kifedha, kupitia kwenye sheria. Migogoro hii, hapa Tanzania, imekuwa ni kikwazo kikubwa cha maendeleo, hasa kwenye kutekeleza miradi inayotegemea ardhi.

Mheshimiwa Naibu Spika, Tanzania inayo mifumo miwili rasmi ya kumilikisha ardhi. Nchi yetu inatambua mifumo ya umiliki wa ardhi ifuatayo:-

(i) Umiliki kwa njia rasmi ya kupata hati toka Serikalini; na

(ii) Umiliki kwa kutumia hati za kimila; kwa kiasi kikubwa hati za kimila zimechangia migogoro kutokana na kutosomana na mifumo rasmi ya Serikali. Kutokana na tofauti za kiuendeshaji, mifumo hii miwili imetofautiana sana na kusababisha migogoro na kukwamisha juhudi za usimamizi na upangaji wa ardhi. Kwa mfano, mamlaka za vijiji kupitia mifumo ya umiliki wa kienyeji wanaweza kuamua juu ya matumizi au umiliki wa ardhi, lakini mifumo rasmi ya kisheria, mahakama au kamishina wa ardhi au Waziri au Rais, wakatengua maamuzi husika kutoka mamlaka za vijijini. Jambo hili linatakiwa lipatiwe suluhisho la kudumu.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ambalo huchochea migogoro ni changamoto katika utawala wa ardhi kutokana na kuwepo rekodi za ardhi zilizopitwa na wakati na kukosekana kwa taarifa sahihi katika usimamizi wa ardhi. Kwa mfano, ardhi zenye hati miliki zilizomaliza muda wake taarifa huwa hazitoki na wamiliki huendelea kutumia maeneo haya kinyume na sheria. Kadhalika, upatikanaji mdogo wa taarifa juu ya umiliki na utumiaji wa ardhi, ambao huambatana na vikwazo vya kupata taarifa za ardhi huchochea ukosefu wa uwazi na kuaminiana katika shughuli za usimamizi wa ardhi.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninaipongeza sana Serikali kwa hatua mbalimbali ilizochukua kwa kuweka mkazo kwenye kuongeza kasi ya upangaji, upimaji, umilikishaji na usajili wa ardhi mijini, vijijini na katika maeneo ya kimkakati. Pia, kuimarisha mifumo ya TEHAMA katika utunzaji wa kumbukumbu, utoaji wa huduma, ukusanyaji wa maduhuli na upatikanaji wa taarifa za ardhi na uthamini.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninaipongeza pia Serikali kwa kusudio la Wizara kuanzisha Kamisheni ya Ardhi, Land Commission, ambayo pamoja na mambo mengine itaweka mfumo mmoja wa usimamizi na utekelezaji wa shughuli za sekta ya ardhi katika ngazi zote, hivyo kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa majukumu ya sekta. Ili kufanikisha malengo haya makubwa ya Wizara, ninaishauri Serikali iimarishe mifumo yote ya kimtandao itakayobeba na kushughulikia utoaji wa hati za umiliki wa ardhi. Kupitia mifumo hii, wananchi watapata huduma kirahisi kwani mifumo hii itakuza uwazi na ushiriki wa wadau wenye mamlaka kwa ngazi zote.

Mheshimiwa Naibu Spika, ili kufanikisha hili, ni vyema yakatolewa mafunzo ya kujenga uelewa na uwezo kwa wadau wote, wa namna ya kufanya kazi kupitia kwenye hii teknolojia ya TEHAMA. Matumizi ya TEHAMA yataleta suluhu ya mageuzi katika kushughulikia michakato mbalimbali ya vibali na hati za ardhi hapa nchini Tanzania.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya maelezo yangu hapo juu, ninaunga mkono hoja.

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Naibu Waziri.