Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

Hon. Oran Manase Njeza

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mbeya Vijijini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

MHE. ORAN M. NJEZA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa namna ya pekee ninaomba kuungana na Watanzania wenzangu kumpongeza Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kutimiza vyema miaka minne ya kuongoza nchi yetu akiwa Rais wa Awamu ya Sita wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Tumeshuhudia mafanikio makubwa katika kuimarisha miundombinu, hususan barabara, reli, viwanja vya ndege, bandari, huduma za kiuchumi na kijamii, kama vile ujenzi wa madarasa, hospitali, zahanati na vituo vya afya, huduma za maji, utawala bora, pamoja na kuhamasisha uwekezaji na utalii.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba pia nimpongeze Mheshimiwa Dkt. Philip Isdor Mpango, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa kazi nzuri iliyotukuka ya kumsaidia Mheshimiwa Rais.

Mheshimiwa Naibu Spika, nitumie nafasi hii kumpongeza sana Mheshimiwa Balozi Dkt. Emmanuel John Nchimbi kwa kuteuliwa kuwa Mgombea Mwenza wa nafasi ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Kwa uzoefu na weledi wake, kama ilivyo kwa Watanzania walio wengi, nina imani kubwa kwa Mheshimiwa Nchimbi na kumtakia afya njema na kila la heri kwenye mchakato ujao.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninampongeza Mheshimiwa Dkt. Doto Mashaka Biteko, Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, kwa kutekeleza majukumu ya kumsaidia Waziri Mkuu, ikiwa ni pamoja na jukumu la kuendelea kuisimamia ipasavyo sekta ya nishati.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninapenda pia, kutumia fursa hii kumpongeza wewe binafsi, Spika na pia, uongozi wote wa Bunge kwa uongozi mahiri na wenye ubunifu wa hali ya juu katika kuongoza Mhimili wa Bunge.

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kumpongeza Mheshimiwa Deogratius Ndejembi, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, kwa hotuba nzuri iliyojaa ubunifu mkubwa na imedhihirisha utayari wa Taifa letu katika ya ushindani wa Kimataifa, National Competitiveness. Bajeti hii ambayo ni ya mwisho, inaenda sambamba na Dhima ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano 2021/2022 – 2025/2026, ambayo ni Kujenga Uchumi Shindani na Viwanda kwa Maendeleo ya Watu. Katika kipindi chake akiwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, tathmini zinathibitisha mafanikio makubwa ya utekelezaji na usimamizi wa Mpango wa Kwanza na wa Pili na kusababisha Taifa letu la Tanzania kufanya vizuri mno kuinua uchumi katika kipindi hiki kigumu.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninaishukuru Serikali kwa kwa kuanzisha mikopo inayotolewa, kwa ajili ya kupanga, kupima na kumilikisha (KKK) ardhi. Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya ni mnufaika wa programu hii na imekopeshwa shilingi 1,857,586,634. Mji Mdogo wa Mbalizi umepimwa viwanja 35,000 kwa gharama ya shilingi 1,273,038,500 na Kijiji cha Mwashoma, Kitongoji cha Inolo, vimepimwa viwanja 565 kwa gharama ya shilingi 584,548,134 na umefanyika kwa ufanisi mkubwa sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, kutokana na mahitaji makubwa na faida itayopatikana kwenye mauzo ya viwanja hivi ipangiwe matumizi yanayolenga kuendeleza ardhi, ikiwemo kuweka miundombinu kwenye maeneo yanayopimwa. Kutokana na mafanikio katika utekelezaji huu wa mwanzo, ninapendekeza Serikali iweke kipaumbele cha kuendeleza programu katika maeneo mengine, hususani yanayolizunguka Jiji la Mbeya, kutokana na mahitaji makubwa ya makazi yaliyopimwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninapendekeza Serikali iendeleze programu hii katika Vijiji vya Swaya, Lupeta, Nsenga, Ifiga, Nsongwi Mantanji, Nsongwi Juu, Izumbwe, Iwindi, Igoma, Ilembo, Idimi na Haporoto. Upimaji kwenye vijiji ambavyo vinakua haraka kuwa miji, growing towns, utawezesha kupunguza na hata kuondoa kabisa makazi holela na pia, kuongeza wigo wa walipa kodi.

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na programu ya makazi, Serikali iweke usimamizi wa matumizi bora ya ardhi ya kilimo, ambayo inaendelea kupotea kwa matumizi ya makazi. Katika kupanga matumizi mazuri ya ardhi, ihusishe Wizara za Kilimo, Wizara za Maji na Wizara inayosimamia mazingira. Kwa vile binadamu tunaongezeka ni muhimu kuhakikisha ulinzi kwa kuhifadhi ardhi inayofaa kwa kilimo na pia, kutenga ardhi, kwa ajili ya wafugaji.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninapongeza hatua zinazochukuliwa na Serikali kurejesha mahusiano mazuri kati ya TANAPA, Hifadhi ya Kitulo na Wananchi wa Kata za Ilungu, Igoma, Ulenje na Inyala; bado hakuna Suluhu, haijapatikana. Serikali ichukue hatua pia, za kumaliza mgogoro wa miaka mingi wa mpaka kati ya TFS na wananchi wa Kijiji cha Mwashoma. Wananchi wa Wilaya ya Mbeya wamekuwa walinzi wazuri wa hifadhi zetu na ni jukumu la Serikali kuhakikisha uendelevu huu na kuondoa migogoro ambayo haina maslahi kwa Taifa.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninaunga mkono hoja.