Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CHADEMA
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. HALIMA J. MDEE: Mheshimiwa Naibu Spika, ninakushukuru. Nitatambua umashuhuri wake wa kufanya kazi Mheshimiwa Waziri na Naibu Waziri pale ambapo watatatua mgogoro kati ya wananchi wa majimbo mawili; Jimbo la Kawe katika Mitaa ya Madale, Mbopo, Mabwepande na Jimbo la Kibamba pale kwa ndugu yangu Mtemvu, Mitaa ya Tegeta A, Msumi A, Msumi B na Kulangwa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa huu mgogoro, yeye ni Mheshimiwa Waziri wa tatu. Nilianza kueleza hapa Bungeni wakati Mheshimiwa Waziri akiwa Mheshimiwa Dkt. Mabula akashindwa kutatua. Nikaeleza Mheshimiwa Waziri alipokuwa Jerry Silaa, akakwama kutatua na sasa ni Mheshimiwa Waziri wa tatu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sifa anazopewa Mheshimiwa Ndejembi, ninaomba basi sifa hizo wananchi hawa zaidi ya 250,000 ambao wanaathirika kwa maeneo yao yaliyochukuliwa na DDC mwaka 1980 kwa kutokufuata utaratibu kwa sababu Serikali ya Kijiji haikushirikishwa, wala haikutoa baraka. Wakaenda kupata hati mezani, hati ilikuwa inawataka kwa maelezo yao wafanye kilimo na ufugaji. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, miaka 50 baadaye, hawajawahi kufuga kuku wala hawajawahi kulima bustani ya mchicha. Wameenda kutaka kuwaondoa wakazi wa asili na ambao wakazi wa asili kwa sheria za ardhi za kipindi kile, walikuwa wana umiliki halali na wao wameuzia wananchi wengine. Kwa hiyo, tunavyozungumza, watu 250,000 tunazungumza raia ambao walikuwepo kipindi kile kama wananchi ama wakazi wa asili na wananchi wengine waliokuja kununua maeneo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nimwombe sana, nimesoma hotuba yake anasema kwenye mwaka huu wa fedha 2025/2026 wanataka kutatua migogoro 3,000. Ninaomba kwa hisani kabisa, eneo hili ama mitaa hii saba niliyomtajia ambayo inaingia kwenye Jimbo la Kawe na Jimbo la Kibamba akatafute ufumbuzi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hali za wananchi ni ngumu tunavyozungumza. Ni bahati mbaya viongozi waliopewa dhamana kwenda kuhudumia wananchi, kwenda kuwasikiliza wananchi, kwenda kutatua migogoro kwa busara wamekuwa hawatumii hiyo busara. Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Mwenyekiti wa CCM wa Mkoa wa Dar es Salaam, Jeshi la Polisi na mitutu ya bunduki linawasumbua raia wa Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hapa nina matangazo mawili. Hili jambo lingeshughulikiwa na Mheshimiwa Dkt. Mabula, hili jambo lingeshughulikiwa na Mheshimiwa Jerry Silaa, haya matangazo mawili yasingetokea. Kuna tangazo la tarehe 10 Februari, 2024 limesainiwa na Mkurugenzi wa Manispaa ya Kinondoni anasema anaenda kuuza viwanja vya halmashauri Mabwepande. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tangazo la pili, tarehe 9 Mei, 2025, limesainiwa na Shedrack Maxmillian, anaenda kuuza maeneo na mbaya zaidi, watu wamejenga nyumba zao, watu wana viwanja vyao, viwanja vyenye nyumba na viwanja ambavyo havina nyumba vinauzwa wakati wananchi wapo ndani ya ardhi yao. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hii ni nchi huru. Ardhi ya Tanzania ni mali ya Watanzania. Mheshimiwa Rais amepewa dhamana, tunaomba asaidie kumaliza huu mgogoro. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ...
MHE. ISSA J. MTEMVU: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa.
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa taarifa.
TAARIFA
MHE. ISSA J. MTEMVU: Mheshimiwa Naibu Spika, anayezungumza anazungumza nusu vizuri, nusu haijakaa vizuri na kwa sababu kanishirikisha, ninayo nafasi ya kumpa taarifa.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imejitahidi kwenda na huu mgogoro kwa hatua na hatua ya kwanza waliyofanya chini ya Mkoa wa Dar es Salaam maeneo ambayo hayajavamiwa tayari... (Makofi)
MHE. HALIMA J. MDEE: Mheshimiwa Naibu Spika, si ungechangia, acha kunipotezea muda.
MHE. ISSA J. MTEMVU: Mheshimiwa Naibu Spika, maeneo ambayo hayajavamiwa katika eneo hilo...
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Halima.
MHE. ISSA J. MTEMVU: Mheshimiwa Naibu Spika, tayari Serikali imetangaza wananchi waombe, wapewe, lakini maeneo ambayo yamevamiwa Serikali imetoa maelekezo. Tayari wananchi walipie per square meter shilingi 3,000 badala ya yale ambayo hayajavamiwa square meter ni shilingi 15,000. Unaweza kuona tofauti hapa Serikali iliyofanya. (Makofi)
NAIBU SPIKA: Haya ahsante. Waheshimiwa tunaendesha Bunge kwa kanuni. Taarifa ni sehemu ya haki ya Mbunge ndani ya Bunge. Msemaji anayepewa taarifa jibu lake ni moja tu, kukubali taarifa au kuikataa anaendelea na shughuli zake. (Makofi)
Haina haja ya kutupiana maneno, haina haja ya kugombana, wala haina haja ya jambo lolote; ndiyo kanuni zinavyosema. Mheshimiwa Halima, wewe ni mwanasheria na hizi kanuni tumetunga pamoja; endelea. (Makofi)
MHE. HALIMA J. MDEE: Mheshimiwa Naibu Spika, sipokei taarifa na ninamshauri Mbunge...
NAIBU SPIKA: Ahhaa, acha acha. Hupokei taarifa, endelea na mchango wako.
MHE. HALIMA J. MDEE: Mheshimiwa Naibu Spika, sipokei taarifa, ushauri wangu ni kwamba akasome nyaraka zote za historia ya mgogoro huu, aende shule akajifunze. Mimi ni Mbunge wa mwaka wa 20 sasa, siwezi kusimama bila kuwa na nyaraka ya kuonesha historia ya huu mgogoro ulitoka wapi mpaka tumefika wapi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mgogoro huu unahusisha maeneo ambayo yana shule zaidi ya 15, yana vituo vya mafunzo vya Serikali, kuna zahanati zaidi ya tatu, kuna viwanda zaidi ya vitano, kuna taasisi za kidini zaidi ya sita, kuna makanisa, kuna ofisi za Serikali, kuna maeneo ya uwekezaji, kuna maeneo ya maziko na kuna vituo vya kulelea watoto yatima. Kwenye eneo ambalo linahusu ekari zaidi ya 5,000; kwa hiyo, nimalizie. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, juzi wananchi walikuja wakamwona Mheshimiwa Waziri pale Wizarani, amewaahidi wananchi ataenda kwenye maeneo husika kati ya tarehe 2 mpaka tarehe 7 mwezi Juni. Wananchi wameshajitangazia huko kwamba Mheshimiwa Waziri wa Ardhi anaenda kuwatembelea. Ninaomba ahadi yake itimie, akatatue mgogoro. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ushauri wangu mwingine, ushauri wa bure kabisa, Mheshimiwa Waziri aende kusikiliza pande zote. Watu ambao wanashiriki kukandamiza wananchi sasa hivi wakijua ana ziara watamuwahi wampotoshe. Mheshimiwa Waziri asikilize upande wa Serikali, asikilize upande wa wananchi upate ukweli, haki itendeke. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la mwisho; tunalalamika hapa na ninaomba Mheshimiwa Waziri atujibu. Tarehe 2 Februari, 2022 Benki ya Dunia iliingia mkataba na Serikali...
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)