Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kibamba
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. ISSA J. MTEMVU: Mheshimiwa Naibu Spika, ninakushukuru sana kwa nafasi ili niweze kuchangia kwenye Wizara hii muhimu sana kwenye nchi yetu. Kwanza, nitumie nafasi hii kumshukuru sana na kumpongeza Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan. Kwa kweli kwa jinsi ambavyo katika kila sekta muhimu kwenye nchi yetu ameweza kuigusa na kuitolea maelekezo muhimu ambapo Waheshimiwa Mawaziri hawa (Makamisaa) wetu wameweza kutafsiri maono hayo katika hali ambayo inafaa sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pili, nitoe pongezi sana kwa Wizara. Ndugu yangu Mheshimiwa Deo Ndejembi kwa kazi anayoifanya pamoja na Naibu Waziri, kaka yangu Mheshimiwa Pinda pamoja na wataalam wetu ambao wanawasaidia. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nitambue sana uwezo mkubwa wa Mhandisi Antony Sanga pamoja na Naibu Katibu Mkuu, dada yangu Lucy wakisaidiwa na mbobezi sana kwenye Wizara hii, Kamishna wetu Mathew na wataalam wengine. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hii Wizara kwa kiasi kikubwa ninaifahamu vizuri, lakini hakuna mwaka nimeacha kuichangia na leo nimepata bahati sana kuwaona wachangiaji; ni wale ambao mara nyingi wanachangia kwenye Wizara hii. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nimeangalia pia jinsi gani wanachangia na nimeona ni sehemu kubwa wanakubaliana na ushauri ambao tumewahi kuutoa zaidi ya miaka minne humu, mambo mengi yamekwenda vizuri. Kwa hiyo, ninawapongeza Waheshimiwa Mawaziri wote wa kisekta ambao wamewahi kupita hapo, lakini leo mwisho sana jinsi gani Ndugu yangu Ndejembi ameendelea kubeba maono yote na ushauri wote wa Waheshimiwa Wabunge kwenye Bunge hili katika nyakati zote zilizopita. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ninatamani kujielekeza katika maeneo machache ambayo na wengine wameyasema, lakini pia yamesemwa kwenye Taarifa ya Mheshimiwa Waziri kwenye Hotuba yake ya Bajeti, hasa katika eneo la urasimishaji na migogoro. Pia, jambo lingine dogo sana ni kumalizia hili ambalo limezungumzwa kwenye page ya 45 kuhusu upimaji wa viwanja na mashamba.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye urasimishaji miaka minne sasa ninasema humu, lakini leo nitoe pongezi sana kwa Serikali ya Awamu ya Sita. Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan amefanya maboresho makubwa ya kuona jinsi gani changamoto ya urasimishaji mijini ambayo inaenda sambamba na ile ya huko kwenye nje ya miji kwenye halmashauri zetu ya (KKK).
Mheshimiwa Naibu Spika, kwetu huku ni urasimishaji tu. Lugha yetu ni ndogo tu (urasimishaji) lakini ni ukweli katika miji mikubwa kama Dar es Salaam na majiji, hili eneo lilikuwa ni changamoto sana katika muda mrefu. Tunakubali tulianza zaidi ya miaka 10 nyuma kuwa na jambo hili la urasimishaji, lakini katika maeneo ndani ya Mkoa wa Dar es Salaam katika Wilaya kama ya Ubungo ilikuwa ina changamoto kubwa katika jambo hili.
Mheshimiwa Naibu Spika, niwashukuru sana Wizara kwa kuja na mipango kadhaa, lakini kubwa ambalo limetuvusha zaidi ya 50% kwa sasa ni hili la clinic ya ardhi. Ninawapongeza, ninawapongeza sana. Ni ukweli imeenda kutupa majibu kwamba changamoto hii siyo tu ya eneo moja kwamba ya Mamlaka ya Upimaji ambayo ni halmashauri zetu, lakini msimamizi wa sera ambayo ni Wizara yetu, mwenye jukumu la kutoa hati.
Mheshimiwa Naibu Spika, tumekuja kugundua hata wananchi tunaowaongoza pia ni changamoto kwenye sababu ya wao kutopata hati na kufikia yale malengo ya Mheshimiwa Rais kuona kila mwananchi anajiinua kiuchumi kwa kupata hati ambayo inaweza ikamsaidia. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa hili limeenda vizuri. Clinic za ardhi zimetusaidia. Wale ambao hawana migogoro kwa maana hawajavamia mashamba na hawajavamia maeneo ya watu, hao wanaweza kupata hati vizuri tu kwa sababu michoro itakamilika, lakini mwisho wa siku watalipia ankara zile ambazo wamehitajika kulipia.
Mheshimiwa Naibu Spika, tumebaki na wale ambao wamevamia maeneo ya watu. Wale watu bado wanamiliki hati zao. Watu hao inawezekana wapo ndani ya nchi au nje ya nchi, lakini unakuta wananchi wameingia, wamekuta mapori makubwa yamekaa muda mrefu, lakini wameyaingilia. Hao ni kweli wanaweza kuikosa hati lakini, mwisho wa siku wanaikosa hati kwa nini? Wanaikosa hati kwa sababu yule mwenye hati amekataa kuirudisha, ku-surrender hati husika. Kwa hiyo, hata mchoro pia hauwezi kukamilika.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, unaweza kumwona mwananchi huyu bado ana changamoto, lakini Wizara imeenda vizuri. Imetushauri tukatengeneze timu za kwenda kupiga magoti kwa wahusika waweze ku-surrender hati zile kwenye ardhi au na mashamba yao makubwa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Rais pia ameenda mbali amesamehe kodi zote ambazo hazijalipiwa katika mashamba ya muda mrefu ili watu hawa wamiliki wapate nafuu ya ku-surrender kwa sababu sina gharama nyingine ili wananchi wale waliovamia waweze kuingia na kuweza kukubaliana waweze kupata hati. Hii ninawapongeza sana Serikali, haya ni maono makubwa ya kuwasaidia Watanzania waweze kupata hati. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ni ukweli sasa tunavyokwenda hata kule kwangu Wilaya ya Ubungo, Jimbo la Kibamba tunakwenda sasa zaidi ya 50% tunakiri sasa tunaweza tukapata hati.
Mheshimiwa Naibu Spika, ushauri wangu kwa wananchi wenzangu na ninaowaongoza; waende wakatembelee Ofisi za Ardhi watakuta kuna majalada yao yamekamilika wanahitajika wakalipie ankara au bill ili waweze kupata hati.
Mheshimiwa Naibu Spika, ni ukweli, hakuna mtu wa kukudanganya eti anaweza kufuatilia hati yako. Hati ni kama cheque. Ni lazima ni wewe mwenyewe unahusika kuifuatilia na ulipie mwenyewe na mwisho wa siku uipate...
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Mtemvu, malizia.
MHE. ISSA J. MTEMVU: Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu eneo la migogoro. Hata hapa nitumie nafasi hii kuwapongeza sana Serikali. Mheshimiwa Ndejembi wewe ni mtu anayesikia sana. Leo mdogo wangu Kunambi amesema, (mimi sijawahi kumsikia Kunambi akisifia sana) lakini leo nimemsikia kwa mara ya kwanza akimtakia na uchaguzi ujao ashinde pale Chamwino na pia Mheshimiwa Rais amkumbuke kwenye nafasi hiyo ili aendelee kutuvusha. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ninaungana na Mheshimiwa Kunambi, mdogo wangu Mwanamorogoro katika hili, tunakuombea wewe kila la heri. Ukweli kwenye migogoro tumekuwa na migogoro mingi sana na mimi kwenye Wilaya ya Ubungo...
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Mtemvu, mengine andika. Ahsante. Mheshimiwa Jesca.
MHE. ISSA J. MTEMVU: Mheshimiwa Naibu Spika, ninaunga mkono hoja, lakini na kuwatakia kila la heri watumishi wote na Wizara hii. Ahsante sana kwa nafasi. (Makofi)