Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

Hon Abubakar Damian Asenga

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kilombero

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

MHE. ABUBAKARI D. ASENGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ninakushukuru sana kwa nafasi ya kuchangia Wizara yetu ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi. Nami naanza kwa kuunga mkono hoja mapema kabisa, hoja ya Wizara ya Wizara ya Ardhi, ambayo inaomba takribani shilingi bilioni 164.

Mheshimiwa Naibu Spika, kama walivyosema Wabunge wenzangu, ninaanza hapa kwa kuwapongeza sana Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri, Watumishi wote wa Wizara yako, Katibu Mkuu Eng. Sanga, Kamishna Methew, Makamishna wote na Watumishi wote wa Idara ya Ardhi na hasa katika Mkoa wetu wa Morogoro na Halmashauri yetu ya Mji wa Ifakara. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tunawaombea Mungu awasaidie, maana yake Wizara ya Ardhi na mambo ya ardhi kwa kweli ni changamoto kubwa sana sana. Tunawaombea sana Mungu na hata hapa Dodoma tunaona namna ambavyo mnavyoita majukwaa na mnaleta ma-tent yale ya kutatua kero kama hapa Bungeni, tunawapongeza sana, tunawashukuru sana, jambo hili liendelee na limesaidia wananchi wengi sana kwa utatuzi wa kero. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Morogoro pale tunamshukuru sana Kamishna Frank aliondoka pale na sasa hivi wametuletea Kamishna Kayela, ameanza kufanya kazi vizuri. Hata katika Halmashauri yangu ya Mji wa Ifakara wametuletea Mkuu wa Idara ya Ardhi mpya anaitwa Rajabu Bogwa. ninamwomba sana Mheshimiwa Waziri, nimesikia huyu amefika ana wiki tu anataka kuondoka. Ifakara ina changamoto kubwa za ardhi sana, tunaomba Rajabu abaki Ifakara Halmashauri ya Mji ili aendelee kutatua changamoto kubwa kubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, migogoro ya ardhi kama nilivyosema inahitaji kuwaombea Mungu viongozi wetu hawa kwa sababu hata hapa Dodoma ukiangalia sasa hivi wamemleta Kamishna mpya anaitwa Godfrey Mwamsojo, ninamwona anavyokaa pale, nami nilikuwa na migogoro yangu nimeenda pale unaona kabisa mpaka mvi zake zimeanza kuwa za brown. Anasikiliza mgogoro mpaka anasinzia, mgogoro unaenda mbele unarudi nyuma, unazunguka unaanzia mwanzo ulipoanzia, kwa hiyo, kwa kweli tunawaombea Mungu sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, unaona Kamishna Mwamsojo amekaa hivi, unaona mpaka anasinzia namna hii, maana yake mgogoro mwingine unasikilizwa unaenda huku unarudi huku, unarudi huku unaenda huku. Kwa hiyo, hii maana yake narudi pale kwenye hoja ya msingi, Mheshimiwa Waziri ambayo amesema hapa, hii Land Commission wakiianzisha itatusaidia kupunguza mambo haya. Wakienda kwenye mambo ya kidigitali watatusaidia kukamilisha mambo haya. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nitakwambia mimi kwenye Jimbo langu na Halmashauri yangu nilipata ule mpango wa Hati za Kimila, katika Halmashauri ya Mji wa Ifakara, Wilaya ya Kilombero. Katika vitu ambavyo vimepunguza migogoro kwa asilimia kubwa ni utoaji wa Hati zile za Kimila, ule mpango kwa sasa haupo kwa sababu sisi ni Halmashauri ya Mji, lakini wananchi kwenye mashamba yao wameenda wamepimiwa mashamba, wamepimiwa nyumba zao wamepimiwa makazi yao, wana hati. Changamoto ikawa kwenye uuzaji tu, lakini kwa kweli kila mtu ana kipande chake cha Hati ya Kimila, kimesaidia sana kupunguza kero kwa kikubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, Land Commission hii ikienda ki-digitalized ikiwa na vifaa vya kisasa, lazima mu-invest katika vifaa vya kisasa, mobile track na kadhalika ili muweze kutatua kero kwa wakati.

Mheshimiwa Naibu Spika, lingine hapa Mheshimiwa Waziri ni taasisi nyingine wanazoshirikiana nazo. Kwa mfano, nimejifunza Wizara ya Ardhi wanatakiwa washirikiane karibu sana na TAKUKURU, kwa sababu ninyi hawana wataalam wa kujua mikataba fake, kujua hati fake, kujua watu waliouziana, nani original nani siyo original. Sasa ni vizuri pia waka-push kule upande wa TAKUKURU, wakawawezeshwa vifaa, wakawezeshwa bajeti, wakawezeshwa pesa ili jambo la ardhi linapoenda TAKUKURU lirudi kwa wakati na wananchi waweze kupata haki yao.

Mheshimiwa Naibu Spika, ni imani yangu Mheshimiwa Waziri amesema atafanya ziara Mkoa wa Morogoro, utatusaidia kutatua migogoro ambayo ipo baina ya mipaka, kwa mfano kule Sanje, Ituli na Kidatu. Nami nimechangia hapa leo Mheshimiwa Waziri kukushukuru wewe, Mheshimiwa Rais alikuja tarehe 4 Agosti, 2024, tulizungumza kuhusu mgogoro wa Ifakara Mjini pale, Kata ya Mrabani, mbele ya Mheshimiwa Rais na Baba Askofu alikuwepo pale, kuna mgogoro mkubwa wa miaka mingi ya historia.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Rais alitoa maelekezo Mheshimiwa Waziri akabaki pale akakutana na Baba Askofu, leo ninataka nimwambie Mheshimiwa Waziri ameniambia hapa na Katibu Mkuu amenihakikishia, ziliombwa kama milioni 400 kasoro, wameshaweka shilingi milioni 150 za kukagua mgogoro huo. Hii inathibitisha Serikali ya Dkt. Samia Suluhu Hassan inasikiliza na inafanyia kazi yale ambayo Wabunge tunayasema na Wabunge tunayaombea. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba sana Mheshimiwa Waziri, kama hizo milioni 150 zimewekwa kwenye bajeti zipatikane kwa wakati kupitia Wizara ya Fedha, ziende kwa wataalam wetu wa ardhi wakapime Kata ya Mrabani. Wananchi wale wakishaona hati zao zipo wako tayari kuchangia ili kumaliza mgogoro huu mkubwa sana katika Halmashauri yetu ya Mji wa Ifakara, ni jambo kubwa kweli kweli.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna eneo kubwa pale la Kanisa limevamiwa na wananchi, wananchi wameshajenga makazi yao ya kudumu, kwa hiyo, wananchi wale wakipimiwa wakimilikishwa fedha zile zitapatikana kwa ajili ya kwenda kumtafutia Baba Askofu eneo lake lingine na hii amekuwa akiifuatilia kwa muda mrefu. Mheshimiwa Waziri ninaomba sana hizi fedha ziende kwa wakati ili tuweze kumaliza mgogoro huu, nilimpigia hata juzi nikiwa pale na Mtendaji wa Kata na akaniahidi kwamba analifanyia kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ninataka kuzungumzia kuhusu Shirika letu la Nyumba kidogo, ninaomba kutoa ushauri Mheshimiwa Waziri, Mheshimiwa Naibu Waziri hapa kwamba ni muhimu sana pia wakajielekeza katika Halmashauri za Mji zinazoendelea na zinazokua kwa kasi kama Halmashauri ya Mji wa Ifakara. Ina mipango pale ina ramani imepanga, Makao Makuu ya wilaya, kila kitu kimepangwa pale, lakini ni vizuri wakaanza kuweka bajeti sasa ya kujenga nyumba nafuu katika Halmashauri zetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, mathalani sisi kule tunachoma tofali kwa udongo, tofali jekundu, tunajenga kwa tope na wataalam wanakwambia kwa sababu kule kuna maji basi ukijenga kwa tope na zile tofali nyekundu nyumba inadumu zaidi kuliko kujenga kwa simenti. Wakituletea wataalam wa ardhi, wataalam wa nyumba wakaja wakafanya study ya kisayansi inawezekana wakapata nyumba rahisi zaidi za kujenga kwa wananchi wetu kuliko kutumia gharama nyingine. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tofali inachomwa, udongo unachomwa uleule, shimo la choo ndiyo linatoa udongo, tofali inachomwa inakuwa nyekundu inajengwa kwa tope. Mtu anapandisha mpaka juu, anakazia kasimenti kidogo anapaua. Kwa hiyo, ni mfumo wa nyumba ambao unaweza kusaidia sana Wizara hii. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ninataka kusimama hapa kwa unyenyekevu mkubwa. Niliomba dakika hizi chache za kushukuru Wizara hii kwa kumaliza mgogoro wa Mlabani na kuanza kutenga fedha kwenda kumaliza mgogoro wangu wa Ifakara Mjini wa kanisa na wananchi wangu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ninashukuru sana na ninaunga mkono hoja. (Makofi)