Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mtera
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. LIVINGSTONE J. LUSINDE: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nikushukuru sana kunipa nafasi hii ili nitoe mchango wangu kwa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninakushukuru wewe mwenyewe kwa uendeshaji bora kabisa wa Bunge letu, umekuwa mhimili mkubwa wa kumsaidia Mheshimiwa Spika na kwa kweli ukikaa hapo Wabunge wengi tunakuwa na morali ya kuchangia. Tunakushukuru sana Mheshimiwa Naibu Spika. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tunampongeza kocha, kocha wa timu hii, kocha wa Taifa letu, kocha aliyetengeneza Baraza bora kabisa la Mawaziri, Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan. Ukiitazama cabinet ilivyoundwa, kama ni mtaalam wa kutazama utagundua kwamba Mheshimiwa Rais kuna kitu anataka kutoka kwenye Baraza hili. Kuna Mawaziri wenye umri mkubwa kama Mzee wetu hapa, Mzee George. Katikati hapo amechanganya Mawaziri wa umri wa kati kina Mheshimiwa Dkt. Kiruswa, Mheshimiwa Pinda, Mheshimiwa George Simbachawene, lakini akaja akachanganya kundi kubwa la vijana.
Mheshimiwa Naibu Spika, ukimtazama Mheshimiwa Profesa Kitila Mkumbo, Mheshimiwa Ummy Nderiananga, wenzake hao wote hao kina Mheshimiwa Deo, Mheshimiwa Mavunde, Rais anataka speed ya ufanyaji kazi. Pamoja na akina Mheshimiwa Mchengerwa mtu kazi, Rais anataka speed ya namna ya kutatua kero za wananchi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, unaweza ukaona namna ambavyo Mheshimiwa Rais anataka. Katika Baraza la Mawaziri umri wa kati upo, umri mkubwa upo. Nimemwona Profesa alikuwa anatabasamu na yeye ninamweka kwenye kundi la umri wa kati, Profesa Waziri wa Elimu namweka kwenye kundi la umri wa kati. Mheshimiwa Waziri wa Ardhi yuko kwenye kundi la vijana pamoja na akina Mheshimiwa Ridhiwani. Mheshimiwa Rais anataka wafanye kazi na wanafanya, kinachotakiwa hapo ni speed. Waongeze speed ya kutatua kero za Watanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ninampongeza sana Mheshimiwa Waziri, Naibu wake, Katibu Mkuu Engineer Sanga, Kamishna wa Ardhi Methew, tunaona timu nzima ya Wizara yake namna ambavyo inachapa kazi usiku na mchana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kumekuwa na migogoro mikubwa ya ardhi, imeanza kutatuliwa wakati wa Mzee Lukuvi, lakini sasa hivi tunaona utatuzi wake namna ambavyo unakwenda kwa speed sana. Katika kutoa haki za watu Mheshimiwa Waziri aendelee na roho hiyo na sura ya ubandidu. Kuna baadhi ya watu ni dhulumati, wanadhulumu watu wa chini. Waendelee kusimamia haki za watu bila kujali.(Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, wengine wanamtumia message wanamtisha, wamepita Mawaziri wengi, sawa utapita, lakini achape kazi aache alama, aache alama! Suala la muda wa kukaa siyo la kwake ni suala la Mheshimiwa Rais, ataamua mwenyewe, lakini wakati huu anaaminiwa na Mheshimiwa Rais, wakati huu Watanzania tunamwombea, apige kazi, asaidie watu kwa haki zao. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kumekuwa na migogoro baadhi ya maeneo. Kwa mfano, hata kwenye Jimbo letu kwenye Wilaya yake ya Chamwino, kuna mgogoro kati ya mpaka wa Mpwapwa na Chamwino, aende akautatue ule. Pia kuna tatizo vilevile la upimaji na kutambua maeneo. Ninataka wajikite kwenye kupima maeneo ya vijijini na kuyatambua, kutenga maeneo ya wafugaji. Hapo kuna tatizo! (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, unajua utafiti lazima ufanyike wa kutosha. Kuna baadhi ya wafugaji kwenye maeneo yao hekari chache anaweza kulisha mifugo. Kuna baadhi ya wafugaji maeneo yao ni makame, lazima apate eneo kubwa zaidi ili aweze kulisha mifugo yake. Pia kuna baadhi ya wafugaji wanapewa ardhi ambayo haiwezi kuotesha majani ya kutosha, sasa unaenda kumweka kwenye eneo gumu, eneo la miamba, mfugaji atapataje kulisha mifugo yake? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, ni vema tukayatambua maeneo tukayapanga, halafu yakaheshimiwa. Maana kupanga jambo lingine, lakini kuyaheshimu ni jambo lingine. Kwa hiyo, ni muhimu sana hii Commission inayotaka kuundwa ikatazama maeneo hayo. Hawa wafugaji tunawahamisha kila siku hamia huku, hamia huku, hamia huku, wanakuwa kama siyo Watanzania, kitu ambacho siyo sawa. Kwa hiyo, namwomba sana Mheshimiwa Waziri hii Commission iwahishwe iwekewe sheria, isimamie na haki za walaji. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nikutolee mfano, nilikuwa napanga mimi mwenyewe, nilikuwa mpangaji na nilikuwa mlinzi usiku. Ikatokea siku moja mke wangu amejifungua watoto mapacha nimechelewesha kodi, unajua mwenye nyumba alichofanya? Alileta fundi akaja kung’oa bati. Eeh! akang’oa bati za nyumba yake. Kwa hiyo, Mama Neema ananiuliza vipi? Nikamwambia aah! wewe tulia, tulia tu hamna namna tutafanya, halafu usiku mvua ikanyesha. Kama alikuwa ametumwa yule bwana. (Kicheko)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, tunaposema Commission iundwe, iundwe kusimamia haki za walaji. Kwa sababu sisi wenyewe tumepitia mengi. Kuna baadhi ya wenye nyumba wanaonewa na wapangaji, kuna baadhi ya wapangaji wanaonewa na wenye nyumba. Kwa hiyo, ukiweka Commission na sheria nzuri maana yake italinda hata haki za walaji. Tunamshukuru sana Mheshimiwa Waziri kwa wazo hili, lakini tunaomba speed na ubora, ije hiyo sheria Waheshimiwa Wabunge waichambue ili iweze kufanya kazi yake kwa umakini. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu uundwaji wa hii Commission kusimamia Real Estate, hapa pamekuwa na matapeli wengi sana. Ni muhimu sana, kuna baadhi ya watu wanapelekana Mahakamani ardhi siyo yao, yaani wote anayemshtaki mwenzake anajua ardhi siyo yake, anayeshtakiwa anajua ardhi siyo yake. Hukumu ikipatikana wanaitumia ile hukumu kuuza ardhi ya mtu mwingine kabisa, halafu wanagawana kati ya aliyeshinda na aliyeshindwa! Sasa huu ni utapeli wa kiwango cha juu sana. Kwa hiyo, tunamwomba sana Waziri hili jambo lisimamiwe kikamilifu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hapa kwenye kutetea haki za watu ninarudia tena, hapa tusifanye mzaha. Kwenye sekta miliki hapa tuwamilikishe watu. Lakini hili jambo Mheshimiwa Rais aligusa hivi juzi akaanza kupima ardhi vijijini, ameona namna watu walivyochangamkia ile fursa. Tunaomba tupime mashamba ya watu, watu wapimiwe nyumba zao na tuanze kupanga miji yetu vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hii Dodoma kadri inavyokua Mji unatakiwa uhamie Mvumi. Mji uhamie kwenye centre kubwa kubwa kama Dabalo kule kwa Waziri. Kama maeneo makubwa ya Itiso, Mpwayungu, Manda na Mlowa barabarani. Maeneo yale yakipimwa yakapangwa vizuri, Haneti pale, ile ni Miji Midogo itakayosababisha Dodoma ipumue. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lazima tuwe tuna state za pembeni ambazo zimepangwa vizuri, mtu anafanya kazi mjini anaenda kuishi nje kidogo ya mji. Sasa hivi kuna usafiri wa treni ya umeme, watu wanaweza kuwahi kwenda makazini kwa wakati wowote. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hivyo ninamshukuru sana Mheshimiwa Waziri kwa hotuba yake nzuri, lakini tunaomba na Wizara ya Fedha itoe fedha za kutosha kwenye taasisi za Wizara ya Ardhi ili ziweze kufanya kazi kwa ufanisi, kwa sababu kama hawana pesa, nao vilevile uwezo wa kufanya kazi watakuwa hawana. Kupima nchi yote siyo jambo dogo, wanaweza wakatumia hata wapima binafsi ili waweze kusaidia baadhi ya maeneo kuweza kunyoosha mambo yaweze kwenda vizuri.(Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ninakushukuru sana na ninaunga mkono hoja, Mungu ambariki sana Mheshimiwa Waziri. (Makofi)