Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Rorya
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. JAFARI W. CHEGE: Mheshimiwa Naibu Spika, nikushukuru kwa kunipatia nafasi. Kwanza, nami nianze kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipatia nafasi ya kuchangia Wizara ya Ardhi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pili; kipekee kabisa nichukue nafasi kumshukuru sana Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa mambo kadhaa, lakini nitataja matatu.
Mheshimiwa Naibu Spika, wakati ninaingia kwenye Bunge hili mara ya kwanza nilikuwa ni Mjumbe wa Kamati ya Maliasili na Utalii. Nje ya hivyo nimekuwa niki-declare interest mara zote ambazo ninachangia kwenye wizara hii kwamba, mimi ni mdau wa sekta ya ardhi, pia ndiyo professional yangu ambayo imenikuza kwa miaka yote.
Mheshimiwa Naibu Spika, mambo makubwa matatu ambayo yamekuwa yakizungumzwa kwenye taarifa zote za kamati na michango ya Bunge hili. Moja; tumekuwa tukizungumzia sana umuhimu wa Sera ya Taifa ya Ardhi ya Mwaka 1995. La pili; tumekuwa tukizungumzia umuhimu wa RERA (Real Estate Regulatory Authority). Pia, tatu; tumekuwa tukizungumzia sana Kamisheni ya ardhi.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimesema nimeanza kutangulia kwa kipekee kabisa kuchukua nafasi kwa moyo wangu wa dhati kumpongeza sana Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Kwa sababu haya yote matatu ambayo tumekuwa tukisema kwenye Bunge hili kwa miaka minne, kwenye Taarifa zetu za Kamati, kwenye michango ya Wabunge na ndiyo yamekuwa mapendekezo ya Kamati kwa miaka yote.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunaona wakati huu wa Mheshimiwa Waziri Ndejembi, yametekelezwa na yamefanyika vizuri sana. Mheshimiwa Ndejembi hongera sana wewe pamoja na Naibu Waziri wako, watumishi wote wa Wizara kwa kweli wametufikisha vizuri sana. Hili si tu kwamba wamekosha Bunge lakini mmekidhi haja ya wadau wa sekta ya ardhi nchini. Sera ya Taifa ya Ardhi ya Mwaka 1995, tumekuwa tukiisemea sana ifanyiwe mabadiliko ili iendane na kasi ya ukuaji wa uchumi na sekta ya ardhi nchini. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Sera ya Taifa ya Ardhi ya Mwaka 1995 tumekuwa tukiisemea sana ifanyiwe mabadiliko ili iendane na kasi ya ukuaji wa uchumi, iendane na kasi ya ukuaji wa Sekta ya Ardhi nchini, lakini maeneo mengine ilikuwa inamwacha mwanamke katika sekta ya umiliki wa ardhi hasa sehemu ya mirathi.
Mheshimiwa Naibu Spika, leo kwenye Sera ya Taifa ya Ardhi tumeona inakwenda kumweka mwanamke kutambulika kumiliki ardhi, hata akinamama ambao wanakaa vijijini ambao kimsingi kwenye umiliki wa ardhi hasa maeneo ya mirathi walikuwa wameachwa, walikuwa hawana haki ya kumiliki ardhi, lakini sera hii inakwenda kutambua. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ninamwomba sana Mheshimiwa Waziri yale ambayo Mheshimiwa Rais ameyasema wakati anazindua sera hii, lakini pia malengo ambayo ameyaainisha kwenye taarifa yake na haya ambayo tumeyasema leo kupitia Bunge hili, nenda ukayafanye ili uweze kuboresha Sera hii ya Taifa ya Ardhi na iweze kufanya kazi vizuri sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la kwanza ambalo ningetamani kwenye maeneo hayo ni kutambua mabadiliko ya kanuni na sheria mbalimbali kwenye sekta ya ardhi ambazo zinashabihiana na sekta ya ardhi nchini. Waziri anapofanya mabadiliko ya sera lazima aende akatambue sheria mbalimbali ambazo zinashabihiana na sekta ya ardhi nchini ili na zenyewe ziweze kufanyiwa mabadiliko ziendane na kasi yake na ziendane na dhamira na mwelekeo wa Mheshimiwa Rais nchini.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimesema pia, lazima iendane na mabadiliko ya sheria na kanuni ya Wizara ya Ardhi peke yake. Kwa sababu zipo sheria, kama tunavyosema kwamba mwanamke sasa anakwenda kumiliki ardhi, tusipofanya mabadiliko ya Sheria ya Mirathi ya Ardhi maana yake itakuwa sera ipo, lakini mwanamke bado atakuwa hatambuliki katika umiliki wa sekta ya ardhi nchini.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninamwomba pia Mheshimiwa Waziri tena katika sekta hii kwamba Mamlaka za Upangaji na Upimaji, sheria inasema hivyo, tunatambua sheria inasema kwamba, mwenye mamlaka ya upangaji na upimaji ni Mamlaka ya Serikali za Mitaa na mimi ni Mjumbe wa Kamati ya TAMISEMI. Ninamwomba sana Mheshimiwa Waziri, atengeneze connection kati ya Wizara ya TAMISEMI na Wizara yake kwa kutambua sera mama ili angalau sera hii iende ikatengeneze usimamizi mahiri, kwenye usimamizi kwa upande wa TAMISEMI, Wakurugenzi waweze kusimamia hili zoezi ambalo linatamkwa kwenye sheria lakini halifanyiki vile ambavyo inapaswa kufanyika kwa sasa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri lazima atambue kwamba mfumo wa usimamizi wa ardhi nchini siyo rafiki sana. Mfumo wa usimamizi wa ardhi nchini hauko rasmi kwa sababu hatuna chombo kinachosimamia Real Estate Regulatory Authority. Hatuna chombo kinachosimamia watu wa Real Estate Agent, hatuna chombo kinachosimamia Real Estate Developers Consultant, hawa brokers ambao wanafanya kazi zao. Nimshukuru sana Mheshimiwa Waziri kuja na RERA. Nimeona sasa wanakwenda kuunda hii taasisi, kuunda mfumo ambao utawaratibu na kuwasimamia hawa watu, hawa watu hawakuwa wanatambulika.
Mheshimiwa Naibu Spika, National Housing anafanya kazi ya usimamizi wa miliki, lakini zipo private company nyingi zinafanya kazi ya usimamizi wa miliki lakini hazitambuliki. Hazina Regulatory ambayo inawaongoza namna nzuri ya kwenda na kwa kutokuwa na usimamizi mahiri maana yake Serikali inakosa kodi, wao wanakuwa hawatambuliki na hata wao wanakosa wakati mwingine mikopo kwenye taasisi za Serikali kwa sababu hawaeleweki wako wapi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ninamwomba Waziri hii RERA, Real Estate Regulatory Authority Mheshimiwa Waziri ipe kipaumbele sana kwa sababu watu wengi ambao ni brokers na Real Estate Agent wanakwama kwa sababu ya ukosefu wa kuwa na sheria ambayo inawasimamia.
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na hili lipo jambo lingine ninaomba nimshauri Waziri. Ni kwenye mkopo wa KKK - kwenye Kupanga, Kupima na Kumilikisha.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza ninamshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa kuendelea kutoa fedha kwa miaka mingi mfululizo. Tumeona alitoa mara ya mwisho bilioni 50 kwenda kwenye Mamlaka za Upangaji na imetumika kwenye kupanga maeneo mengi nchini na kwenye Halmashauri. Ninamwomba tuzingatie mambo mawili. Pamoja na kuwa tumegundua kwamba kuna changamoto kubwa sana fedha hizi namna ya kurudi, baadhi ya Halmashauri hazirudishi fedha ipasavyo. Ninaomba mambo mawili haya angeyafanyia kazi ili angalau hizi fedha ziendelee kuwa na tija. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la kwanza, wakati mikataba inasainiwa kati ya wakurugenzi na Wizara ya Ardhi, lazima TAMISEMI ihusike. Husisha TAMISEMI kama wasimamizi wa Wakurugenzi wale mnaosaini nao mikataba. Pili, anayetakiwa kuhusika, ni lazima umhusishe RAS wa Mkoa ili atambue na akusaidie namna ya kusimamia zile fedha zinazokwenda kwenye taasisi, kwenye maeneo ya Wakurugenzi. Haya mawili Mheshimiwa Waziri akiyafanya, itatusaidia sana kuhakikisha fedha hizi zinarudi kwa wakati. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ni lazima Wizara ya Fedha ihakikishe na yenyewe inahusika kwenye mkataba ule ili kurahisisha kusaidia zile fedha kurudi kwa wakati. Leo tunatoa bilioni 50, lakini Waziri mwenyewe anaona changamoto namna ya fedha hizi zinavyorudi, hii fedha ni revolving, inatakiwa irudi ili halmashauri zingine ziweze kupewa fedha, lakini hazirudi kwa wakati. Ninaomba sana Mheshimiwa Waziri hili alione na aone namna ambavyo wanaweza wakalifanyia kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine Mheshimiwa Waziri nimesema hapa ni Commission ya Ardhi Nchini. Kunakuwa hakuna connection kati ya Wizara ya Ardhi ambao ndiyo wanasimamia policy, TAMISEMI wanaosimamia sheria za utekelezaji wa ardhi, pamoja na watendaji wa maeneo yote mawili. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Commission hii inakwenda sasa kuwa sehemu ya kusimamia yote mawili, inakwenda kusimamia utendaji wa Wizara ninyi wenyewe kwa yale yote wanayozungumza katika kupanga, kumilikisha ardhi, lakini pia inakwenda kuwa sehemu ya katikati kama broker au kuwarahisishia mahusiano yao wao na Wizara ya TAMISEMI. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, maana yake ni nini? Kwanza itarahisisha upangaji na upimaji kwenda kwa kasi, itarahisisha master plan ambayo tumeizungumza ya sekta ya ardhi nchini itakwenda kwa kasi, pia itawasaidia kuondoa hilo gap ambalo mnalo kati ya sekta ya ardhi kwa maana ya Wizara ya Ardhi na TAMISEMI nchini. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, tunamshukuru sana Mheshimiwa Waziri kuliona hili, kuanzisha Commission ya Ardhi, nimeona hapa anasema anaianzisha, hii iende kwa kasi kwa sababu kuna wakati hawakutani sekta ya ardhi na mipango au usimamizi wa sera na kule wasimamizi wa utekelezaji wanaotekeleza sheria, hawana namna ambavyo wanakutana ili kuhakikisha haya wanayafanya. Akiwa na Commission ya Ardhi itamsaidia sana Waziri angalau kufanya regulation na kuhakikisha kwamba haya mambo yote yanakwenda sawasawa.
Mheshimiwa Naibu Spika, lingine amelisema Mwenyekiti wa Kamati hii, juu ya utengano wa watumishi wa ardhi, hasa Maafisa Ardhi, Surveyors, Town Planners, hawa ambao wanaitika wako chini ya Kurugenzi, lakini wanaitika ndani ya Wizara. Huu mkanganyiko kwamba wako chini ya Mkurugenzi kwenye Mamlaka za Serikali za Mitaa, lakini wanawajibika kwenye sekta kwenye Wizara ya Ardhi nchini, kuna mkanganyiko mkubwa sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, kama alivyosema Mwenyekiti ni kwamba, wakati mwingine Wakurugenzi wanashindwa kuwatambua kama wako chini yao, kuna wakati mwingine wanapata maelekezo kutoka Wizara ya Ardhi juu ya jambo lolote linalotakiwa kufanywa kwenye sekta ya ardhi, hapo hapo anapata maelekezo kwa Mkurugenzi ambaye ndiyo bosi wake kwenye eneo lile la Mamlaka ya Serikali za Mitaa, ile contradiction inawafanya wale watu wanashindwa kuelewa wasimamie lipi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tunamwomba sasa Mheshimiwa Waziri akae na Mheshimiwa Waziri wa TAMISEMI waamue hawa watumishi wakae upande upi. Ndiyo maana maeneo mengi hawa watu wanapata lawama kubwa sana, kwamba wanashindwa kutatua migogoro au wanashindwa ku-meet ile objective ambayo wamewapa ni kwa sababu ya hiyo contradiction, anapata maelekezo kwenye Wizara mbili tofauti, matokeo yake ni kwamba wanashindwa kusimamia na hawajui wasimamie lipi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba sana Mheshimiwa Waziri, kwa kuwa hili Wakurugenzi wako chini ya Mamlaka ya Serikali za Mitaa, wala hakuna sababu, wawarudishe kama walivyokuwa zamani, warudi kule chini ili wasimame kwenye command moja, ikitoka Wizara ya TAMISEMI inashuka mpaka kwa watumishi inakwenda, kuliko hivi ambavyo iko ilivyo hivi sasa. (Makofi)
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa mud awa Mzungumzaji)
NAIBU SPIKA: Ahsante Mheshimiwa ni kengele ya pili.
MHE. JAFARI W. CHEGE: Mheshimiwa Naibu Spika, nimalizie jambo la mwisho kabisa ambalo ni kubwa ninatakiwa kulizungumza ni juu ya kupunguza gharama ya kumiliki ardhi.
Mheshimiwa Naibu Spika, tumeona wamepunguza kiasi kikubwa sana cha fedha kwa wananchi wanaotaka kumiliki Hati ya Umiliki wa Ardhi nchini, ninamwomba sana hili Kamishna wa Ardhi atoke atoe semina kwa wananchi, ajue namna Mheshimiwa Rais alivyokubali na ameridhia kupunguza bei ya wananchi sasa kumiliki ardhi, zaidi ya asilimia kadhaa kwenye eneo hili ili angalau uweze kuongeza umiliki wa hati na ndiyo sehemu pekee inayoweza kutatua changamoto za ardhi nchini. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ninakushukuru sana na naunga mkono hoja. Hongera sana kwa Mheshimiwa Waziri kwa kazi kubwa nzuri, hongera sana Wizara ya Ardhi pamoja na watumishi wote. Ahsanteni sana. (Makofi)