Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

Hon. Godwin Emmanuel Kunambi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mlimba

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

MHE. GODWIN E. KUNAMBI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipatia fursa ya kuwa sehemu ya wachangiaji katika Hotuba ya Bajeti hii ya Wizara ya Ardhi. Nianze kwa kumshukuru Mheshimiwa Rais, ni Rais anayefanya mabadiliko katika sekta mbalimbali ndani ya Serikali.

Mheshimiwa Naibu Spika, pili, nimpongeze Mheshimiwa Waziri mwenye dhamana aya ardhi kaka yangu Deodatus Ndejembi. Nieleze haiba kidogo ya Mheshimiwa Waziri, ninadhani pia na Waheshimiwa Wabunge wataniunga mkono. Mheshimiwa Deo Ndejembi, ni Waziri kijana na siyo tu kijana ni Waziri ambaye ana fresh mind in a changing world. Ni kijana ambaye ana fikra mpya katika ulimwengu unaobadilika. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, akiwa Naibu Waziri, Wizara ya Utumishi na Utawala Bora alikuwa anamsaidia mama yangu Mheshimiwa Jenista Mhagama. Nilisimama hapa Bungeni na hoja ya kueleza mapungufu ya OPRAS. Bila shaka alimshauri Waziri wake wakafanya mabadiliko katika usimamizi wa Sekta ya Utumishi wa Umma, wakaja na Mifumo miwili ya PEPMIS na PIPMIS, OPRAS wakaachana nayo. Ndiyo maana nikasema leo sishangai haya yanayotokea kwenye Wizara ya Ardhi, kwa sababu ndiyo haiba yake. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tangu nimefika kwenye Bunge hili niimekuwa nikijenga hoja kwa habari ya ardhi na kwa nini leo hii ninampongeza Waziri? Ninampongeza kwa sababu amekwenda kumheshimisha Mheshimiwa Rais, kwenye hotuba yake. Ninamshukuru Mheshimiwa Rais kwa kuja na utashi wa kisiasa wa kuona sasa ana kusudi la kwenda kutatua migogoro ya ardhi kwa suluhisho la kudumu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niliwahi kusema hapa migogoro ya ardhi inatatuliwa kwa njia kuu mbili; ya kwanza, ni njia ya mahakama; na ya pili, ni njia ya utawala kwa mujibu wa sheria za nchi, lakini njia za utawala ni njia za temporary siyo za kudumu. Sasa, leo hii tunaona Mheshimiwa Rais ameelekeza na Waziri unatuletea hapa Bungeni, wanakwenda kuanzisha Kamisheni ya Ardhi na Matumizi Bora ya Ardhi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa hapa ninaomba nieleze kidogo. Kamisheni ya matumizi bora ya ardhi ndiyo inayokwenda kutatua migogoro ya ardhi nchini kwa suluhisho la kudumu. Sasa, nieleze kwa nini inakwenda kutatua? Kamisheni hii inakwenda kuwa kama chombo cha kusimamia sekta ya ardhi. Nami nishauri na katika hitimisho ninadhani utasema kidogo. Hii Kamisheni ni lazima iwe na instrument: instrument ya Kamisheni hii ni National Land Use Master Plan.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mpango Kabambe wa Kitaifa wa Matumizi Bora ya Ardhi, ndiyo utakaosaidia kusimamia mipango kabambe yote kwenye halmashauri. Kwenye halmashauri Mheshimiwa Waziri wa TAMISEMI ni lazima twende na kasi ya Wizara ya Ardhi kwenye kupanga na matumizi bora ya ardhi ya nchi yetu, kwa sababu wewe ni mdau muhimu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mujibu wa Sheria ya Matumizi Bora ya Mipango Miji Na.8 ya mwaka 2007, halmashauri ndiyo mamlaka za upangaji. Sasa, ni lazima halmashauri nazo ziwe na Land Use Master Plan na Infrastructures Master Plan (Mipamgo Kabambe ya Matumizi Bora ya Ardhi na Mipango Kabambe ya Miundombinu), maana yake nini? Hii National Land Use Master Plan itasimamia katika halmashauri mipango kabambe ya matumizi bora ya ardhi na infrastructures.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa, hayo ndiyo majukumu ya Kamisheni sasa iende ikafanye. Kwa mfano, yapo maeneo yameshapangwa, lakini tunaona bado kuna ujenzi holela. Sasa, Kamisheni hii itatusaidia kupitia, lakini sasa niseme ili kuondoa kuwa na taasisi nyingi kwenye Wizara moja, Kamisheni hii ninashauri iwe chini ya Kamishna Mkuu wa Wizara.

Mheshimiwa Naibu Spika, sijui watakavyopanga, lakini ninatamani kuona Kamishna Mkuu wa Wizara anakuwa ni sehemu ya Kamisheni. Isipokuwa Kamisheni hii isimamie Tume ya Mipango na Matumizi Bora ya Ardhi, pia isimamie RERA. Kwa kweli Waziri ninakushukuru Real Estate ni sekta muhimu katika uchumi wa nchi yetu, vijana wengi wanafanya huko shughuli zao na kwa kweli imekuwa ikikua kwa kasi sana miaka ya hivi karibuni. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spia, nimpongeze sana Mheshimiwa Rais, na nimpongeze Waziri kwa kuja na RERA (Real Estate Regulatory Authority). Mamlaka ya usimamizi wa sekta hii ya Real Estate itasaidia kusimamia hawa stakeholders (wadau) wa Real Estate ambao waliachwa kama watoto yatima leo hii wanakwenda kuwa na chombo cha kuwaratibu. Hongera sana kwa Mheshimiwa Waziri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, itoshe tu kusema migogoro ya ardhi mingi imekuwa ikitokea nchini siyo tu kwa sababu. Sababu tuliyokuwa nayo kubwa ni kwa sababu bado hatujakamilisha kupanga na kupima nchi yetu. Nchi hii ikipangwa, ikapimwa vizuri na wananchi wakamilikishwa ardhi yao, ninadhani hili tatizo la migogoro ya ardhi linakwenda kutatuliwa, kwa sababu tunafahamu katika Taifa letu tuna ardhi za aina tatu. Kuna ardhi ya jumla, ya hifadhi na ardhi za vijiji, sasa maana yake nini?

Mheshimiwa Naibu Spika, unavyofanya land administration Waziri wa Ardhi anaposimamia sekta, yeye siyo mtu wa mwisho kwenye kutatua migorogo ya ardhi, mtu wa mwisho ni mahakama na ndiyo maana nikasema migogoro ya ardhi nchini bado haiishi. Kwa hiyo, bado ninaendelea kusema, kupitia Kamisheni itakwenda kutusaidia nchi yetu ipangwe, ipimwe na wananchi wamilikishwe vipande vyao ya ardhi. Hii itaondoa kwa kiwango kikubwa migogoro ya ardhi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nimeeleza hapo kidogo, lakini matumizi ya TEHAMA ni muhimiu nayo nikayasema. Kwa hiyo, ninavyosema Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan ni transformative leader maana yangu ni nini? Ni Rais anayepokea na kutaka mabadiliko. Ndugu zangu haya mambo ninayosema leo siyo madogo kwenye sekta ya ardhi. Nchi yetu imekuwa ni nchi ambayo imepata changamoto nyingi sana kwenye sekta ya ardhi hasa hasa migogoro ya ardhi. Wenzetu majirani na nini huko. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, leo hii inayokwenda kufanywa na Mheshimiwa Waziri nimwombee, ikimpendeza Mheshimiwa Rais na Wananchi wa Chamwino, ashinde kuwa Mbunge, lakini Mheshimiwa Rais ampatie tena uwaziri wa Wizara hiyohiyo, ili kusudi haya unayosema yanayopangwa hapa akayasimamie. yeye ni kijana ninasema ni fresh mind in a changing world. Brother may God bless you. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho nieleze kidogo kuna kadhia kwenye halmashauri, kuna ombwe kwenye halmashauri. Sasa, halmashauri wanasema sisi mamlaka za upangaji Sheria Na.8 ya 2007 ya Mipango na Matumizi Bora ya Ardhi, inatambua halmashauri zote nchini kama ndiyo mamlaka za upangaji. Sasa, Waziri wa Ardhi anaunda Kamisheni anakwenda kupoka majukumu ya Madiwani?
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa, nimwombe atoe ufafanuzi kidogo, ili awaeleze wasio na mashaka Kamisheni hii inakwenda kusaidia halmashauri kuimarika katika sekta ya ardhi, wana sehemu yao kama mamlaka ya upangaji. Hiyo sehemu ni muhimu akaitolea ufafanuzi ili Watanzania wajue.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini mwisho nihitimishe, Mheshimiwa Waziri nikuombe…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungamzaji)

NAIBU SPIKA: Malizia

MHE. GODWIN E. KUNAMBI: Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba nihitimishe. Waziri ni mtu muungwana sana, nimwombe ikimpendeza Jimbo langu la Mlimba kuna migogoro mingi sana ardhi fanya siku moja ziara walau apite kule na yeye ni rafiki yangu katika hili Mungu atambariki sana na aseme neno moja tu na wananchi wa Mlimba watapona. Mungu ambariki sana. (Makofi)