Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

Hon. Timotheo Paul Mnzava

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Korogwe Vijijini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

MHE. TIMOTHEO P. MNZAVA: Mheshimiwa Naibu Spika, ninakushukuru kwa kunipatia nafasi ili niweze kutoa mchango kwenye Hotuba ya Bajeti ya Mheshimiwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi. Nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema ambaye ametujaalia uzima, lakini anaendelea kutuwezesha kuendelea kuwa kwenye nyumba hii, kuwahudumia Watanzania.

Mheshimiwa Naibu Spika, kipekee nitumie nafasi hii kwa dhati kabisa kumpongeza sana Mheshimiwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa kazi kubwa na nzuri anayoifanya yeye na timu yake pale Wizarani. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nimpongeze pia Mheshimiwa Waziri kwa hotuba yake nzuri ambayo imejaa ufafanuzi wa mambo yote makubwa na ya msingi ambayo Watanzania wa nchi hii wanatamani kuyasikia kwenye eneo la sekta ya ardhi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hotuba hii, ni matumaini yangu kama ambavyo taarifa ya Kamati yetu imeunga mkono Hoja ya Mheshimiwa Waziri, Waheshimiwa Wabunge tutaungana pamoja kuipitisha Hoja ya Mheshimiwa Waziri na kuiunga mkono, ili wakaendelee kufanya kazi ya kuwahudumia Watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na kazi hizi nzuri tunasema Mheshimiwa Waziri na timu yake wanafanya Wizarani. Nina mchango kwenye maeneo manne madogo sana ambayo ni ushauri.

Mheshimiwa Naibu Spika, eneo la kwanza; wakati wa kujadili Bajeti ya Hotuba ya Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa nilisema kidogo. Nchi yetu kwenye miaka ya 1990 tuliamua kuingia kwenye mfumo tukaleta sera mpya ya ugatuaji wa madaraka kwa maana ya D by D. (Decentralization by Devolution). Lengo letu kubwa lilikuwa ni kusukuma madaraka kwa wananchi kule chini kabisa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, wakati wa Hotuba ya Bajeti ya TAMISEMI tuliwashauri wenzetu TAMISEMI na tunashukuru walituikia na wakatuahidi kufanyia kazi. Kwamba, umefika wakati sasa wa kufanya mapitio ya sera ya ugatuaji wa madaraka ili kuona ufanisi wake na kuona changamoto zake na kuona namna gani ya kuhangaika nazo, ili kuboresha mfumo wa utawala kwenye nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tumeona TAMISEMI wenyewe walipoona barabara ujenzi unasuasua walianzisha TARURA, lakini upande wa maji tulipoona mambo yanasuasua tulikuja na RUWASA. Baadaye tuliona Serikali imechukua hatua ya kuwahamisha watumishi wa ardhi kutoka kuitika moja kwa moja halmashauri na kusimamiwa moja kwa moja na Katibu Mkuu wa Wizara ya Ardhi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo hili ni zuri, lakini bado tunayo changamoto. Kumekuwa na makanganyiko wa utendaji na kimajukumu kule kwenye halmashauri zetu. Zipo baadhi ya halmashauri ambazo zimedhani kwamba Maafisa Ardhi kwa sasa siyo sehemu ya utendaji kazi wa halmashauri kwa sababu tu wanasimamiwa kinidhamu na Katibu Mkuu wa Wizara ya Ardhi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na changamoto hiyo, kuna changamoto nyingine, ukisoma taarifa ya Kamati yetu kwa kipindi cha miaka mitatu mfululizo nyuma, Wizara ya Ardhi haijawahi kufikia 80% ya malengo ya makusanyo yake. Ukifanya uchunguzi wa kina sababu haiwezi kuwa ni uzembe, zipo sababu nyingi za kimfumo, kisheria ambazo zinafanya Wizara hii ishindwe kufikia malengo kwenye ukusanyaji. Moja ya sababu hiyo ni mkanganyiko wa kisheria, kiutendaji kati ya halmashauri na Wizara ya Ardhi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye eneo hili nimekusikia Mheshimiwa Waziri umesema na Mheshimiwa Rais wakati mnazindua Maboresho ya Sera ya Ardhi alitoa maelekezo. Tunaomba jambo hili wakaliwekee mkakati madhubuti, wakalifanye. Tuleteeni Kamisheni ya Ardhi, tuwe na chombo maalum na mahsusi cha kusimamia ardhi kwenye nchi yetu kuanzia juu mpaka chini. Kusiwe na mifumo mingi, sheria nyingi na mamlaka nyingi. Tuleteeni Kamisheni ya Ardhi kwenye nchi hii tuwe na mfumo mmoja ambao unaeleweka wa kusimamia sekta ya ardhi kwenye nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili; tafiti duniani zinaonesha kwamba moja ya njia bora za kuondoa changamoto ya migogoro ya ardhi hasa kwa maeneo ya vijijini ni kupanga mipango ya matumizi bora ya ardhi kwenye vijiji. Jambo hili ni kubwa sana, kupanga mipango lakini na kwenda kuisimamia. Katika vijiji zaidi ya 12,000 tulivyonavyo kwenye nchi hii mpaka mwaka wa fedha 2021/2022 tulikuwa tumetengeneza mipango ya matumizi bora ya ardhi ya vijiji kwenye vijiji 2,600 na kidogo tu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kipindi cha miaka hii miwili tuipongeze Serikali tumefika vijiji 4,822. Hatua hii ni kubwa kwa sababu tumeongeza vijiji zaidi ya nusu au mara mbili ya tulivyokuwa tumefanya mpango wa matumizi bora ya ardhi ya awali. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo hili halipaswi kuachwa, linapaswa kuwa endelevu. Ili jambo hili liweze kuwa endelevu ni lazima Tume ya Mipango ya Matumizi ya Ardhi itengewe fedha za kutosha kwa ajili ya kazi hii. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tumesema kwenye Taarifa yetu ya Kamati; pamoja na kazi nzuri ambayo Kamati na Bunge tunatambua kwamba Tume ya Mipango ya Matumizi ya Ardhi inafanya, bado kumekuwa na changamoto ya kupata fedha za kugharamia miradi ya upangaji wa matumizi bora ya ardhi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye bajeti anayoomba Mheshimiwa Waziri fedha za maendeleo kwa Tume zimepungua kwa zaidi ya 50% ukilinganisha na fedha zilizokuwa zimetengwa mwaka jana yaani mwaka wa fedha 2024/2025. Mwaka wa fedha unaokwisha Juni, 30 mwaka huu 2025. Tume walitengewa fedha za maendeleo bilioni tano. Mwaka huu wa fedha yaani 2025/2024 tunaoenda kuuanza au bajeti inayoombwa Tume imetengewa bilioni 2.5 ni zaidi ya 50% ya fedha zimepungua. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, katika mazingira kama hayo Tume hii haiwezi kufanya kazi vizuri. Haiwezi kuleta matokeo tunayoyatarajia kwa sababu Tume hii haina fedha. Tunajua bado bajeti hii haijakwisha, mchakato wa bajeti unaendelea mpaka siku utakapopitisha sheria ya matumizi ndani ya Bunge hili. Ni wakati wa Serikali kwenda kuangalia upya, tuone namna ya kuiongezea Tume ya Mipango fedha, ili ifanye jukumu lake la kutengeneza mipango ya matumizi bora ya ardhi kwenye vijiji. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la tatu ninalotaka kushauri ni kwa upande wa Shirika la Nyumba la Taifa. Shirika letu la Nyumba la Taifa linafanya kazi kubwa na nzuri sana na tunaridhika na kazi wanayofanya. Miradi yote ya kimkakati ambayo ilikuwa imesimama kwa muda mrefu, kwa busara na maelekezo ya Mheshimiwa Rais, miradi ile imeamika na sasa hivi kazi zinaendelea katika hatua mbalimbali.

Mheshimiwa Naibu Spika, kama ambavyo uligusia awali na Mheshimiwa Rais siku ya kuzindua maboresho ya sera alisema; kiu ya Watanzania wa nchi hii ni kupata nyumba au makazi kwa bei nafuu zaidi, kupata makazi kwa gharama ambayo ni nafuu. Pamoja na jtihada za Shirika la Nyumba la Taifa kujenga nyumba za gharama nafuu, lakini bado hazijawa nyumba za gharama nafuu kwa kiwango ambacho wanaweza kukimudu Watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Shirika letu linafanya shughuli za kibiashara, lakini ni ukweli kwamba siyo kwamba hawapendi tu kujenga nyumba za gharama nafuu, yapo mambo mengine humu ndani ikiwemo sera zetu za kikodi ambazo zinasababisha bei ya nyumba hizi iwe juu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ni wakati sahihi sasa Mheshimiwa Waziri, Shirika la Nyumba na Wizara wafanye tathmini ya kina ili tupate nyumba na makazi ya gharama nafuu kwa Watanzania. Kuna changamoto na vikwazo gani vya kikodi, kibiashara na kisheria, ili tuipelekee Serikali iamue kufunga mkanda, tukubali kupunguza baadhi ya maeneo, tukubali kusamehe baadhi ya kodi ili tuliwezeshe Shirika la Nyumba la Taifa kutengeneza makazi ya gharama nafuu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, bila kufanya hivyo ni jambo gumu. Shirika hili linajenga kama anavyojenga mtu mwingine binafsi, linanunua vifaa kama anavyonunua mtu mwingine binafsi, wanakatwa kodi kama wanavyokatwa mashirika mengine. Ni ngumu kupata nyumba za gharama nafuu bila kuangalia sana mfumo wa kikodi ili kuwezesha Shirika hili liweze kufanya kazi vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, eneo la mwisho nililokuwa ninataka nishauri; nimpongeze sana Mheshimiwa Rais amefanya kazi kubwa…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa malizia.

MHE. TIMOTHEO PAUL MNZAVA: Amefanya kazi kubwa kwenye kubatilisha miliki na mashamba makubwa ambayo yalikuwa hayajaendelezwa na ninaipongeza Wizara inafanya kazi kubwa sana. Kama Mheshimiwa Rais alivyotoa maelekezo, endeleeni kufanya tathmini juu ya maeneo haya, ili tuwasaidie Watanzania waweze kupata ardhi kwa ajili ya shughuli za uzalishaji ili maisha yao yaendelee kuwa mazuri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, ninakushukuru sana. Ninaunga mkono Hoja ya Mheshimiwa Waziri na ninaomba Waheshimiwa Wabunge tuiunge mkono. Ninakushukuru sana. (Makofi)