Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CHADEMA
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. KUNTI Y. MAJALA: Mheshimiwa Naibu Spika, ninakushukuru kwa kunipatia muda niweze kutoa mchango wangu kwenye bajeti hii ya ujenzi, bajeti yetu ya mwisho kwa kipindi cha miaka mitano.
Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote ninamshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutujalia afya na uhai na kuweza kulizungumza Taifa letu kwa ajili ya maslahi mapana ya nchi yetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba nianze alipoishia Mheshimiwa Kilumbe kuhusu suala la viwanja vya ndege na Mheshimiwa Waziri atakapokuja kuhitimisha kesho, nitaomba aje na ufafanuzi na majibu ya mambo yafuatayo:
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la kwanza, ninaomba uwaambie wananchi wa Jimbo la Dodoma Mjini, Kata ya Kiwanja cha Ndege waliopisha upanuzi wa uwanja wa ndege ule tangu mwaka 2016, walifanyiwa uthamini mpaka leo wamefanya upanuzi watu wengine wamewalipa fidia, wengine hawajawalipa, tunataka wananchi wa Dodoma kujua watu ambao hawajawalipa fidia na hawajawaambia chochote wanaendelea na lile eneo ama hawaendelei nalo? Nyumba zao zimeharibika, zimebomoka hawawezi kuendeleza, hawawezi kufanya chochote, ninataka aje na majibu. Je, yale maeneo bado wanayahitaji? Kama wanayahitaji mnalipa lini? Jambo la pili, kama hawayahitaji ni nini kauli yenu kuwasaidia kuwapa fedha ili waweze kurekebisha ama kukarabati nyumba zao ili waweze kuendelea na maisha yao? Hilo ni jambo la kwanza. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la tatu, atusaidie, Uwanja wa Dodoma wa Ndege wa Msalato unakamilika lini? Maana yake imekuwa ni kesho, keshokutwa, sasa hivi tunaona hata kazi zenyewe pale haziendelei ni majani tu ndiyo yanazidi kuota mle, kwa hiyo watusaidie pia uwanja wa ndege ni lini utaisha?
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo langu lingine, ni mwaka wangu wa 10 ninachangia bajeti humu ndani tangu mwaka 2016 mpaka leo mwaka 2025 ninachangia bajeti ya Wizara ya Ujenzi, nikizungumzia barabara ya Kibirashi – Kiteto – Chemba mpaka Kwamtoro – Singida, mwaka wa kumi! (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, barabara hii siyo ya leo siyo ya jana ni kwamba barabara hii imekuwa kwenye vitabu na ahadi za viongozi. Mheshimiwa Mkapa wa Awamu ya Tatu miaka yake kumi alimaliza, akaja Awamu ya Nne ya Mheshimiwa Kikwete miaka 10 akamaliza 20, amekuja Hayati John Pombe Magufuli miaka mitano kamaliza, leo yuko Mama.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninamshukuru Mheshimiwa Rais, ametoa kauli kwamba barabara hii iende ikajengwe kwa mfumo wa PPP. Mheshimiwa Waziri niliuliza swali hapa tarehe mbili na Mheshimiwa Naibu Waziri akanijibu kwamba mko kwenye mchakato. Mheshimiwa Waziri siamini kama Mheshimiwa Rais anatamani Watanzania wa nchi hii waendelee kusikia maneno yenu ya michakato na utaratibu. Mheshimiwa Rais anatamani kuona kazi inafanyika watu wako site, wananchi wanapata huduma na siyo maneno yao matamu wanayowapa Watanzania.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninataka Waziri akija kuhitimisha awaambie hususani wananchi wa Wilaya ya Chemba kwa sababu hawana barabara ya lami kabisa kwenye Wilaya ile, ni hii wanayotuambia ya Kondoa ni vijiji vitano tu ambavyo vinapitiwa. Barabara ile sisi ni wakulima tunawalisha mpaka ninyi, ile barabara mkitupatia mtatusaidia kukuza uchumi wa Wilaya ya Chemba na wananchi wake, lakini na Taifa kwa ujumla. Akija hapa atuambie michakato yao wanayoendelea nayo ni lini inakamilika ya barabara ya kutoka Kibirashi - Kwamtoro mpaka Singida inaanza kujengwa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na hilo miaka hii 30 leo ambayo wananchi hawa walisimamishwa pia na wao nyumba zao kujengwa walioko pembezoni, waliishawekewa ‘X’ wakafanyiwa uthamini, wana miaka 30 wanasubiri barabara ije haiji, wanasubiri fidia haiji. Atakapokuja kuhitimisha kesho, ninaomba aje aniambie na wananchi wa Chemba leo wanamsikiliza, kwamba ni lini mnakwenda kuwalipa fidia ambayo itakuwa ni stahiki ya leo siyo ya miaka 30 iliyopita, kwa wale ambao wanapisha hiyo barabara?
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la tatu ambalo natamani kulisema kwenye Wizara hii ni suala zima la uharibifu wa barabara zetu. Tunatumia gharama kubwa sana kujenga barabara, lakini matumizi yetu siyo rafiki pia. Leo ukipita barabara ya kutoka Dar es Salaam mpaka Mwanza, pembezoni unakuta ni parking ya malori, kila kona kingo za barabara zimekatika. Ninawaomba ninyi ni Serikali moja, wazungumze watu wa TAMISEMI, watu wa Uchukuzi, pia watu wa Wizara ya Mambo ya Ndani. Trafiki wetu wamekuwa wakianzisha vituo wanavyotaka wao kukamata magari barabarani, ambako wanasababisha pia uharibifu mkubwa sana wa barabara zetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunapolia barabara ni lazima tuweke na mifumo mizuri iliyo bora ya kuzitunza hizo barabara ili ziweze kutusaidia. Kwa hiyo ninaomba Wizara nilizozitaja, wakae chini, watengeneze mfumo rafiki wa kufanya majukumu yao bila kuziharibu hizo barabara, baada ya muda mchache tena tuwe tunarudi tunalia barabara. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ni suala la ukarabati wa hizi barabara. Ninaomba kuuliza wanisaidie, hivi hizi barabara wanapoweka viraka lazima kuwe na manundu makubwa yale? Yaani vile viraka wale watu wanaowapa kufanya ukarabati wa hizi barabara zetu, ukipita hii Barabara ya Dodoma – Morogoro, ukarabati wanaoufanya manundu vile viraka vimewekwa ni mafurushi, mafurushi ndiyo utaratibu, yaani ndiyo inavyotakiwa kufanywa hivyo ama ni nini? Kwa nini barabara zinazofanyiwa marekebisho zinakuwa zina manundu manundu? Hakuna namna bora inayoweza kuwekwa kukarabati zile barabara, hivyo viraka kuzibwa? Zikazibwa kiraka ambacho mtu akipita apite eneo ambalo liko limetulia badala ya kuweka yale manundu manundu?
Mheshimiwa Naibu Spika, tunaomba pia watusaidie zile ni fedha. Wanaweka yale manundu manundu baada ya dakika mbili yamebanduka wanarudi tena wanaenda kuweka yale manundu manundu. Kwa hiyo, ninawaomba pia waweze kuliangalia hilo kwenye suala zima la ukarabati wa barabara zetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la mwisho ni ujenzi wa Daraja la Kelemasimba, Wilayani Chemba, Kata ya Mondo. Mheshimiwa Naibu Waziri wewe umekuwa ni mzoefu, lakini na wataalam pia ni wazoefu Katibu Mkuu na viongozi wengine. Alienda Mheshimiwa Bashungwa kwenye daraja lile, alijionea hali halisi ya lile daraja. Ninamwomba Mheshimiwa Waziri kaka yangu Ulega hajawahi kushindwa na jambo, amefanya maajabu Wizara ya Mifugo na Uvuvi, ninamwomba hapa Dodoma Chemba siyo mbali, barabara tunayoipigia leo kelele hiyo ya Kibirashi, anaweza akatoka hapa akaangalia akaona namna gani hiyo barabara ina uhitaji, pili hilo daraja akajionee mwenyewe. Waziri alikuja akaahidi wananchi pale kwamba wataleta fedha ili tuweze kujenga lile daraja na ilikuwa likamilike tangu mwaka jana, lakini mpaka leo kimya. Wananchi wa Chemba wanatamani kujua daraja lile…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
NAIBU SPIKA: Malizia.
MHE. KUNTI Y. MAJALA: Mheshimiwa Naibu Spika, ninakushukuru. Wananchi wa Chemba wanataka pia wajue Daraja la Kelemasimba mtalijenga lini ili waweze kupita kwa amani na utulivu na kuendelea kuokoa vifo vinavyoendelea kutokea katika daraja lile.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninakushukuru kwa muda, ahsante. (Makofi)