Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ujenzi kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

Hon. Kilumbe Shabani Ng'enda

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kigoma Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ujenzi kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

MHE. KILUMBE S. NG’ENDA: Mheshimiwa Naibu Spika, ninakushukuru kwa kunipa nafasi ili niweke mchango wangu katika Wizara hii muhimu ya ujenzi. Kwanza ninaanza kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuendelea kutupa afya na uzima ili tuendelee kuwatumikia wananchi waliotuchagua.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kweli ningependa nichukue nafasi hii kwanza kupongeza sana hotuba nzuri ya bajeti iliyotolewa na Mheshimiwa Waziri. Kwa kweli wamejipanga na nimpongeze yeye Mheshimiwa Waziri maana hii Wizara ni mpya kwake. Ametoka kwenye ile Wizara ya kitoweo (Uvuvi na Mifugo) na akaja kwenye hii Wizara, ameanza vizuri na ameanza kwa kasi. Nimwombe Mheshimiwa Waziri asirudi nyuma, aendelee na hiyo kasi. Hawa wakandarasi hawataki kuchekacheka nao sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nimpongeze vilevile, Mheshimiwa Naibu Waziri, askari huyu wa infantry. Anafanya kazi vizuri na tumekuwa tukishirikiana naye hapa Bungeni, anajibu maswali yetu mara kwa mara. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kweli kwa ujumla, nipongeze Mamlaka ya TANROADS kuanzia Mtendaji Mkuu, na pongezi za pekee nimpe Meneja wangu wa mkoa Engineer Choma ambaye ameibadilisha sura ya Mji wa Kigoma, Manispaa ya Kigoma Ujiji kuwa ya kisasa na kwa kweli ukifika utajua kwamba TANROADS ipo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ninataka nianze kwa kuzungumzia suala la upanuzi wa Uwanja wa Ndege wa Kigoma na hatua ya maboresho makubwa ambayo yanafanyika. Hapa nilitaka niseme, niipongeze sana Kamati kwani imefanya uchambuzi wa kutosha na kueleza kazi ya maboresho yanayofanyika katika uwanja wa ndege iko kwenye 16%, lakini hawakusema ni kwa muda gani. Mimi ninataka nieleze, ni 16% katika kipindi cha miaka sita.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa hili jambo siyo jema kwa sababu zabuni ya upanuzi wa Uwanja wa Ndege wa Kigoma na hasa maboresho ya jengo la abiria control tower na hayo mengine ilitangazwa mwaka 2019. Mwaka 2020 waka mu-award mkandarasi waliyempa hiyo nafasi ambaye ni Kampuni ya Kichina inaitwa CRCEG, lakini mwaka 2021 hadi 2022 pamoja na kumu-award mwaka 2020 hakuna kilichofanyika na ikapita miaka miwili kimya kabisa.

Mheshimiwa Naibu Spika, mwaka 2023 Januari, wakasaini mkataba na mkandarasi huyu, mwaka 2023 Septemba ndiyo kazi ikaanza, leo tuko mwezi Mei, 2025 miaka sita ndiyo tunazungumza 16% ya kazi hiyo iliyotangazwa mwaka 2019. Kwa hiyo, jambo hili lazima niseme ninyi mngekuwa ni wananchi wa Mkoa wa Kigoma kwa kweli wangeona kero ya kazi hii ambayo imesuasua kwa kiasi kikubwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, moja ya jambo ambalo linafanya kazi hii isuesue ni suala zima la kuchelewa kuanza kwa kazi hii na hawakufanya ile kitu inatiwa price adjustment, mkandarasi anapiga kelele kwamba amepewa kazi wakati gharama zimeshapanda kwa kiwango kikubwa, anaanza kazi katika kipindi cha miaka mitatu tangu wam-award na Serikali imepewa mapendekezo na mkandarasi na mpaka sasa hawajajibu.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninamwomba Mheshimiwa Waziri, namwona kwa kasi yake asaidie mjibu hizi hoja za mkandarasi zinazohusu price adjustment, wafanye adjustment ili waweze kumpa fedha aweze kuendelea. 16% katika miaka sita ni aibu! Kwa hiyo, jambo hili nilitaka nilisemee. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, suala la uwanja wa ndege wa Kigoma lina project mbili, moja ni hiyo ya maboresho na pili ni ya kupanua na kuongeza running way kutoka kilomita 1.8 hadi kufikia kilomita tatu. Sasa kuna wananchi pale ambao mli-earmark maeno yao kwamba hawa watapaswa watoke kwa ajili ya kupisha upanuzi wa hiyo running way. Kilichotokea tangu mwaka 2023 mwishoni walipowafanyia makadirio ya gharama za kufanya compensation mpaka leo wananchi wale hawajalipwa, wanashindwa kuendeleza maeneo yao, kwa maana hiyo project haiwezi kuanza.

Mheshimiwa Naibu Spika, hapa Kamati imesema Wizara ya Ujenzi maeneo ambayo inatakiwa kuwa-compensate wananchi ni thamani ya shilingi bilioni 123.63. Hivi kweli hiki ni kiwango kikubwa cha kutufanya sisi tugombane na wananchi wetu? Kila ukifika huko au wanataka huyu Mama Rais wetu mpendwa aliyefanya kazi nzuri sana akienda huko kwenye kampeni watu waanze kubeba mabango ya compensation? Ninawaomba kama wanafikiri hawana mpango wa kuendelea na project ile kwa sasa walipeni wale wananchi halafu wao wataendelea taratibu, lakini kwanza wale wananchi wawe wamewatoa. Kwa hiyo, jambo hili kwa kweli limekuwa ni kero. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ambalo ninataka nilizungumze ni mradi wa barabara itokayo Tabora kuja Kigoma. Ninataka niipongeze sana Serikali, nimpongeze Mheshimiwa Rais pamoja na Wizara nzima wamefanya kazi nzuri, mpaka sasa eneo lililobaki ni kama kilometa 17 tu ndiyo linalotakiwa kukamilishwa kuwekwa lami, pamoja na eneo la daraja kuelekea pale Kibaoni. Hata hivyo, taarifa zinasema kwamba mpaka sasa ni nguvu ya wafadhili ndiyo inakwenda. Ile 10% maana pale tuna wafadhili wale wa OPEC na Abu Dhabi, ile 10% ya Serikali mpaka sasa hamjaweka, sasa tusije tukaenda huko mbele mkandarasi akakwama.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo ninachokiomba ni kwamba Wizara wasimamie ile 10% ya Serikali iweze kulipwa na wakamilishe kazi hii kwa wakati unaopaswa.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la mwisho ambalo ninataka kulizungumza hapa ni suala la kibajeti ambalo…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Kilumbe malizia.

MHE. KILUMBE S. NG'ENDA: Mheshimiwa Naibu Spika, hivi ni kengele ya pili? Kwa kuwa haya bado tuna muda wa kuyazungumza, kwa kweli ninaunga mkono hoja, ahsanteni sana. (Makofi)