Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kyela
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. ALLY A. J. M. JUMBE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Tumshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa kutupa Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan. Huyu ni Rais ambaye amekuja kutimiza ahadi ya Mwenyezi Mungu kuiweka Tanzania kuwa nchi ya asali na maziwa. Ni Rais ambaye pamoja na misukosuko mikubwa ambayo nchi yetu ilikuwa inaipitia, ikiwemo korona na vita vilivyotokea lakini yeye amesimama imara ameijenga nchi hii.
Mheshimiwa Naibu Spika, hata leo hii ukiangalia kuna watu wanazungumza kufunguka kwa madaraja makubwa kama Kigongo - Busisi huko Sengerema. Pia, leo tunazungumza ma-flyover yanayojengwa pale Jijini Dar es Salaam. Ninaomba niseme tumebarikiwa sana na ninaomba tuendelee kumuombea sana Mheshimiwa Rais pamoja na wasaidizi wake. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, katika hii Wizara tumepata Waziri bora kabisa ndugu yetu Komredi Ulega, akisaidiwa na ndugu yangu Mhandisi Godfrey Kasekenya. Hawa watu wanafanya kazi kubwa sana, lakini nitakuwa mnyimi wa fadhila nisipowashukuru watendaji, hasa Mtendaji wa TANROADS kwa kazi kubwa anayoifanya. Anazunguka Tanzania nzima, anahangaika lakini anahakikisha kazi zinafanyika. Pia, wapo wanaomsaidia nao ni ndugu zetu dada yetu Balozi Aisha Amour na Naibu Katibu Mkuu, mtu wa chapuchapu wa kufanya mambo yaende ndiyo maana sasa hivi mambo yanabadilika harakaharaka.
Mheshimiwa Naibu Spika, nitakuwa mnyimi wa fadhila nisipomshukuru Meneja wa TANROADS Mkoa wa Mbeya, kaka yangu Engineer Masige. Anafanya kazi nzuri, halali usingizi, chochote kinachotokea hata kwenye Wilaya yangu ya Kyela, kilometa 130 hata iwe usiku asubuhi utamkuta amefika, ninamshukuru sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika hili nimshukuru na niishukuru Serikali kwa ujenzi wa madaraja mazuri mawili ambayo yalikuwa yameharibika kabisa; nalo ni Daraja la pale Nsesi ambalo sasa limewekwa vyuma, lilikuwa ni mbao. Pia, Daraja la Ipyana lilikuwa ni mbao lakini pamoja na bajeti ndogo aliyonayo, amejitahidi ameweka chuma na daraja linapitika vizuri. Ninakushukuru sana kaka yangu Engineer Masige na ninamwomba Mungu aendelee kumpa uhai ili aendelee kuwatumikia wana Mbeya.
Mheshimiwa Naibu Spika, nina baadhi ya maombi; tunapozungumza utajiri na uchumi wa Tanzania, huwezi ukazungumza haya yote bila kuzungumza Barabara ya TANZAM. Unapozungumza mambo yote ya uchumi, unapozungumza Bandari ya Dar es Salaam, huwezi kuzungumza bila kuitaja Barabara ya TANZAM. Mheshimiwa Waziri, ninaomba Barabara ya TANZAM kutoka Igawa kwenda mpaka Tunduma imekwisha kabisa, pamoja na kile kipande cha Nsalaga. Nimpongeze, jembe amekuja, sasa hivi wakandarasi wanapiga hatua, tunaomba ashikilie hiyo speed wale watu wamalize ile barabara. Barabara ya njia nne pale Jijini Mbeya inakwenda kwa kasi, ameifanya hiyo kazi na tunawashukuru sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna Barabara inayotoka Uyole kuelekea Kasumulu. Ninaomba, ile barabara sasa hivi inatimiza miaka 35, ilijengwa na kampuni ya Sogea. Sasa ile barabara mpaka sasa hivi bado iko hai. Ninaomba badala ya kusubiri ife kabisa hebu tufanye utaratibu tuweke layer ya overlay, itasaidia sana kusogeza muda mpaka tutakapopata pesa.
Mheshimiwa Naibu Spika, ombi la kwanza; ninaomba twende tukasaini mkataba wa Barabara ya Ibanda - Itungi Port - Kanjunjumele, (barabara yako ya Kanjunjumele). Ombi la pili; twende tukawalipe Wanakanjunjumele fidia zao; Wanakyela wanasubiri haya.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba sana tuendelee kusisitiza ujenzi wa barabara ambazo zitaleta manufaa na zile za ulinzi. Leo hii ninaomba nikushukuru Mheshimiwa Waziri kwa kuendelea kusaidia uwezekano wa ujenzi wa barabara inayotoka Matema kuelekea Ikombe na kuunga kwenye Wilaya ya Ludewa. Ninafikiri hii ni barabara muhimu sana kwa wananchi na pia kwa ulinzi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tunazo barabara nyingi ambazo zinahitaji ujenzi, lakini bado tunapambana na bajeti ambayo ni ndogo. Ninaomba sana kwa Mkoa wa Mbeya tuongezewe bajeti ya barabara. Ninasema haya kwa sababu kuu mbili; sababu ya kwanza ni tofauti ya mazingira yaliyopo kwenye huo Mkoa, kila eneo lina mazingira tofauti. Kule Kyela unapojenga barabara tupo chini kabisa, usawa wa bahari ni mita 400 tu. Kule barabara zote zinatakiwa ziinuliwe zaidi ya mita mbili kwenda juu ndipo utakapoweza kupita, lakini unapofika Rungwe unatakiwa uchunge mlima mita tano ndipo uikute barabara. Sasa kwa bajeti hii ndogo hatuwezi kufanikiwa. Ninaomba sana bajeti kwenye Mkoa wa Mbeya iongezeke. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba sana, hebu sasa hivi twende tutengeneze teknolojia mpya ambazo zilikuwa zikitumika huko nyuma kupunguza gharama. Ninaomba tuanze kujenga madaraja ya mawe (arch bridges). Hayo madaraja mengine yapo lakini sehemu ambazo tunaona hatuwezi kutumia gharama kubwa hebu twende tujenge arch bridges kwani zinasaidia sana kupunguza gharama kubwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba Wizara ijifunze sana kwenye makosa ambayo yamekuwa yakifanyika nyuma hasa tunapojenga hizi barabara. Kwa mfano, pale Jijini Dar es Salaam tunaendelea kujenga barabara kwa mtindo ambao tulitumia kwenye BRT ya hapa Ubungo na Kimara, lakini kwa sasa hivi tunaenda Mwenge. Sasa zile barabara kwa nini bado tunaruhusu watu wapite juu ya barabara? Kitu gani kinasumbua watu wawe na underpass? Mimi ninaomba haya mambo tuyarekebishe.
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ni mtaala wa elimu ya usalama na udereva kwenye barabara zetu. Sidhani kama mitaala yetu ilikuwa na barabara…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Ally, malizia.
MHE. ALLY A. J. M. JUMBE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Bado hatujajifunza kuendesha kwenye barabara mbili, ninaomba elimu hii itolewe ili tuweze kuzitumia vizuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninaunga mkono hoja, ahsante sana. (Makofi)