Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Sengerema
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. TABASAM H. MWAGAO: Mheshimiwa Naibu Spika, ninakushukuru sana. Kwa niaba ya wananchi wa Jimbo la Sengerema ninawiwa kuchangia bajeti hii ya Wizara ya Ujenzi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa moyo wa dhati kabisa kutoka moyoni ninaomba kumpongeza sana Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa aliyoifanya katika masuala ya miundombinu hasa ya madaraja, barabara na miundombinu ya treni ya mwendokasi. Mheshimiwa Rais hakuwa peke yake, ni kwamba amefanya kazi hii akiwa pamoja na Makamu wa Rais, Waziri Mkuu na Mawaziri wa Ujenzi waliopita kwenye Wizara hii. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sisi kule Sengerema, wananchi wa Jimbo la Sengerema wamenituma nishukuru; asiyeshukuru binadamu hata Mwenyezi Mungu hawezi kumshukuru. Kazi kubwa iliyofanywa kwanza kupata shilingi bilioni 730 kwa ajili ya kulipa mkandarasi ili amalize daraja, juzi nimepita daraja lipo 99% na Sengerema tumepitia wakati mgumu sana. Sasa wamenituma kwanza nije nimshukuru Mheshimiwa Rais na kumwambia Mheshimiwa Waziri Ulega, amekuja Sengerema darajani pale ameona, tulikuwa naye tunakwenda kuangalia miundombinu ya ferry, hizi ferry zilizotengenezwa ambazo ziko katika package ya kuja kufunguliwa na Mheshimiwa Rais.
Mheshimiwa Naibu Spika, tumezunguka kote tumekwenda naye mpaka Buyagu kwenda kuangalia ferry ya Buyagu – Mbarika na ameona kabisa hali ilivyo. Wananchi wa Sengerema tulichosikitika ni kwamba, kila daraja likitajwa linatajwa kwa jina la Kigongo – Busisi, lakini wakati Marehemu Mfugale anali-design lilikuwa linaitwa Kigongo - Misungwi na Busisi - Sengerema.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa kama hamtaki kuita Kigongo - Misungwi, huku kwangu iteni Kigongo – Busisi - Sengerema ili na sisi tuingie kwenye orodha ya madaraja makubwa duniani, kwamba Sengerema lipo daraja. Ninamwomba sana mtani wangu katika hilo. Baba Tulia, akija Sengerema aandike ule ubao, tunakwenda kufungua Daraja la Busisi - Sengerema.
Mheshimiwa Naibu Spika, wanufaika wa hili daraja tuliopata machungu ya kutoka Sengerema kwenda Mwanza ni sisi watu wa Sengerema. Wale watu wa Misungwi wanasafiri kwa barabara ya lami kwenda mjini, lakini sisi Sengerema mpaka tuvuke, watu wa Geita mpaka wavuke, watu wa Kagera mpaka wavuke na watu wa Kigoma mpaka wavuke. Kwa hiyo, watu wote unaowaona wanaotokea njia hiyo kabisa wako pamoja na Mheshimiwa Rais kumuunga mkono wanasubiri tarehe tu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, leo watu wa Sengerema wamenituma nikuulize lini Mheshimiwa Rais anatia timu pale Sengerema na ufunguzi wa daraja usifanyike upande mwingine ambao hawalihitaji. Ufunguzi wa daraja unakuja kufanyika Sengerema, sawa Bwana mkubwa? Ninamwomba sana katika hilo jambo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ufunguzi uwe Sengerema kwa sababu sisi ndiyo tutakaokuja pale. Zaidi ya wananchi wa Sengerema tupo 450,000, lakini ninamhakikishia 100,000 tutatia timu Busisi. Yeye aandae tu nyati wa kutosha, kama anatuletea ngamia tule ngamia na kama ni ng’ombe wawe ng’ombe wa kutosha. Kwa hiyo, tunakuja kufanya na sisi Sengerema tuna jambo letu katika hilo daraja. Mtani, ninafikiri Waziri amenielewa? Ninaomba nirudie tena, ananielewa Baba Tulia katika hili jambo? Ninamsihi sana yaani kwamba sherehe inafanyika Sengerema. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, watu waliofanya kazi katika daraja lile tunaomba waandikwe kwa wino wa dhahabu. Alikuwepo pale Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wa Awamu ya Tano, Marehemu Magufuli. Pamoja na kufikiria, lile jambo lilionekana ni kubwa sana, lakini aliungwa mkono na wataalam wakiwemo Mawaziri waliokuwemo kwa wakati huo. Sasa hao nao waingie katika orodha, Makatibu Wakuu waliokuwepo waingie katika orodha. Pia, ma-engineer waingie katika orodha hii. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kinachonisikitisha, pale tunaye engineer anaitwa Ambrose. Huyu Bwana anakaimu hii nafasi yaani toka ujenzi wa daraja mpaka anamaliza daraja bado wanamkaimisha tu, huwajamwamini tu kweli kama Wizara na kama anafaa kuwa engineer? Kasimamia madaraja yote, kasimamia maeneo ya kuweka vivuko na magati. Kwa hiyo, huyo hafai kweli kuwa engineer mtu wa namna hiyo, wanataka waadilifu gani? Inaumiza maana tukiwa tunakwenda naye pale ninamwona namna anavyokuwa mnyonge, kwa sababu kwanza hajiamini.
Mheshimiwa Naibu Spika, leo ninataka kushukuru tu katika hili jambo, lakini tuna barabara zetu; tumemaliza kazi kubwa tunaishukuru Serikali. Hizi barabara zetu zina changamoto. Kwa mfano barabara ya kutokea Kamanga - Sengerema ilikuwa imewekwa katika mfumo wa lami kilometa 32. Nimeshajengewa kilometa mbili na nilikuwa nimeweka kwenye bajeti zote mbili ya 2023/2024 na 2024/2025 kilometa 10, lakini yule mkandarasi hajalipwa pesa. Kwa kuwa tumemaliza kazi kubwa ya daraja kubwa, basi wafikiriwe na hawa wakandarasi. Pia, tunazo barabara zingine tena ambazo ni za moramu zinazohudumiwa na wakala wetu wa barabara (TANROADS).
Mheshimiwa Naibu Spika, ushauri wangu kwa Wizara, hebu wajazeni fomu wawape Waheshimiwa Wabunge wa nchi nzima tulioko hapa, barabara ambazo ni za muhimu kabisa zinazopita kwenye majimbo yetu sisi tuwajazie fomu kwamba ikitengenezwa barabara hii, ina changamoto hii na mahali hapa kunahitajika daraja; sisi tujaze hizi fomu. Kwani akitugawia fomu kesho, tukamjazia sisi akajua ukubwa wa kazi, wanaokuja kule kufanya upembuzi wa hizi Barabara, hao watu wa Mheshimiwa Waziri, ma-engineer wake wa mikoa si wanaangalia zile fomu ambazo Wabunge tumeelekeza? Sisi ndiyo tunaozijua barabara na ndiyo tunaoishi na watu.
Mheshimiwa Naibu Spika, maeneo mengi ambayo ninataka nimshauri pia ni sehemu za mitaro. Hebu angalieni sana hii mitaro, hizi catchwater na mitre ndiyo ulinzi wa hizi barabara. Pia, tunataka tumshauri akipata mzabuni akaagiza package kubwa China, anunue Armco culvert. Hizi barabara zinakuja kujifunga kwa sababu tu ya kukosa Armco culvert ambapo wakinunua wakawa nazo za emergency, barabara nyingi zingekuwa zinafunguka. Kwa mfano, kama barabara ya Lindi…
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Tabasam, malizia.
MHE. TABASAM H. MWAGAO: Mheshimiwa Naibu Spika, ninakushukuru. Ninampongeza sana Mheshimiwa Ulega kwa ujenzi wa ferry na sisi Wilaya ya Sengerema, tumepata ferry mbili; ferry moja ipo kwa pacha wangu kule Mheshimiwa Eric Shigongo najua tarehe 30 tunakwenda kuzindua na ferry nyingine iko Buyagu – Mbarika. Hii tunaiombea pesa, kule imebakia pesa kidogo ile ferry na yenyewe tuichukue ili wakati tunafungua daraja na ile ferry iwe inapelekwa Buyagu – Mbarika kwani magati yameshamalizwa kujengwa na sisi tuwemo kuonekana Watanzania tulionufaika na Tanzania.
NAIBU SPIKA: Ahsante, malizia.
MHE. TABASAM H. MWAGAO: Mheshimiwa Naibu Spika, ninaunga mkono hoja. (Makofi)