Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Bagamoyo
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. MUHARAMI S. MKENGE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa nafasi. Kwanza kabisa ninapenda nimpongeze Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mama yetu Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa anayoifanya ya kuweka miundombinu ya barabara katika nchi yetu vizuri kabisa.
Mheshimiwa Naibu Spika, pili, ninapenda nimpongeze Mheshimiwa Waziri wa Wizara ya Ujenzi Mheshimiwa Alhaj Abdallah Ulega kwa kazi kubwa anayoifanya na pia nimpongeze Mheshimiwa Naibu Waziri Mheshimiwa Engineer Godfrey Kasekenya, Katibu Mkuu Balozi Aisha, Naibu Katibu Mkuu ndugu yangu Charles Msonde na wafanyakazi wote wa Wizara.
Mheshimiwa Naibu Spika, moja kwa moja niende katika baadhi ya barabara kwenye Jimbo langu la Bagamoyo. Miaka mitatu iliyopita pale katika Daraja la Mpiji linalounganisha Bagamoyo pamoja na Dar es Salaam, Serikali iliingia mkataba wa ujenzi wa daraja lile na wananchi wote katika vyombo vya habari wameona.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini mpaka leo ni mwaka wa tatu sasa tumeambiwa kwamba daraja lile makandarasi alinyang’anywa tenda kwa sababu utendaji wake siyo mzuri. Lakini baadaye tukaja kuambiwa kwamba mto umepanuka feasibility study inafanyika upya, kwa hiyo mpaka sasa hivi wananchi wa Kiembeni hawaelewi lile daraja litakwisha lini na lile daraja ni kiungo kizuri sana kati ya Dar es Salaam na Bagamoyo. Vilevile ni sehemu ambayo inaweza ikapunguza foleni kubwa sana katika Mji wa Bagamoyo pamoja na Dar es Salaam.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninamwomba sana Mheshimiwa Waziri, alitupie macho daraja hili kwa sababu wananchi wana matumaini makubwa kwamba mkataba umeshaingiwa na litajengwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile napenda nizungumzie Barabara ya Mingoi – Kiembeni, barabara hii ni barabara ambayo ilikuwa katika ahadi ya Mheshimiwa Rais mwaka 2020 barabara hii ina urefu wa kilomita nane, imeahidiwa kwamba itajengwa kwa kiwango cha lami, lakini sasa hivi barabara hii imerudishwa mikononi mwa TANROADS baada ya kuwepo kwa TARURA kwa muda mrefu.
Mheshimiwa Naibu Spika, barabara hii mpaka sasa hivi bado haijajengwa na hali sasa hivi na mvua zinazoendelea ni mbaya sana wananchi wa Kiaraka, Kiembeni, Minazi Minane, Tungutungu wanapata shida mno. Maji yanapita katika barabara kuu kama ni mto unatembea vile. kwa hiyo, tunaomba Serikali ichukulie umuhimu sana barabara hii ili wananchi hawa nao waweze kupita vizuri kabisa katika maeneo yao.
Mheshimiwa Naibu Spika, barabara ya tatu ambayo nataka kuizungumzia ni barabara ya Makofia – Mlandizi, barabara hii ya muda mrefu sana na ipo ndani ya Ilani ya Chama Cha Mapinduzi karibu kipindi cha nne au cha tano sasa hivi bado inazungumziwa na ujenzi bado haujafanyika.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimwombe Mheshimiwa Waziri, namfahamu wewe ni jembe la kazi, watu wanasema kwamba mzigo mzito mpeni Mnyamwezi, lakini bahati nzuri Mzaramo amepewa mzigo huu mzito. Ninaomba barabara hii ya Makofia – Mlandizi kitu cha kwanza fidia kwa wananchi kabla ujenzi haujaanza. Wananchi hawa wakipata fidia itakuwa kidogo imeleta nafuu fulani, halafu ndiyo ujenzi uendelee pale pesa zitakapopatikana.
Mheshimiwa Naibu Spika, nina matumaini makubwa katika hotuba ya Waziri, amezungumzia barabara hii, niombe Mheshimiwa Waziri ajitahidi kupambana na barabara hii, kwa sababu ni ya muda mrefu sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, barabara nyingine ambayo ninataka kuizungumzia ni Barabara ya Boko – Bagamoyo kama mnavyojua Bagamoyo kuna kongani kubwa ya viwanda ambayo itakuja kutokana na hotuba za Waheshimiwa Mawaziri waliopita pamoja na Bandari ya Bagamoyo. Kwa hiyo, niombe Mheshimiwa Waziri, barabara hii ya kutoka Boko kuja Bagamoyo ijengwe sambamba na hiyo. Kuna fidia ambayo watu wamefanyiwa tathmini mwaka wa nane kwa ajili ya upanuzi wa barabara hii bado haijafanyika, basi ninaomba wawasaidie fidia zao wale watu na hii barabara ikianza ujenzi wake kupanuliwa ili mambo ya maendeleo yaendelee vizuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, barabara nyingine ninayotaka kuizungumzia ni Barabara ya Tamko – Baobao – Mapinga. Barabara hii ni ya siku nyingi, nimeshuhudia mweyewe utiaji saini wake pamoja na Mradi wa DART awamu ya tatu walitia saini siku moja katika ujenzi, lakini bahati mbaya mpaka leo hii tunavyozungumza barabara hii inasuasua sana haiendi vile inavyotakiwa, miaka inaondoka vipande vinavyojengwa vidogo vidogo.
Mheshimiwa Naibu Spika, tulikuwa tunaomba kabisa barabara hii nayo itiliwe mkazo imalizike ilimradi wananchi wanaotoka Kibaha kuja Bagamoyo na maeneo mengineyo waweze kufaidika na barabara hii.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninataka nizungumzie barabara ya mwisho, Barabara ya Tanga – Pangani – Makurunge. Niishukuru Serikali barabara hii ujenzi unaendelea kama ilivyozungumza, lakini nina ombi moja Mheshimiwa Waziri, hii barabara ina umuhimu sana kwa Bagamoyo na sehemu zinginezo.
Mheshimiwa Naibu Spika, leo hii barabara imeanzia Tanga, lakini niombe kama kungekuwa na uwezekano kukawa na mkandarasi ambaye anaweza kuijenga kuanzia Makurunge angefanya hivyo kwa sababu barabara hii inachechemua uchumi wa Bagamoyo na nchi kwa ujumla. Kwa sababu barabara hii itakapoanza kujengwa pale Makurungwe itakuwa na mambo ambayo yatasaidia kwanza mbuga ya Wanyama Saadan itafikika kirahisi watalii wengi watakwenda kutembelea Mbuga ya Wanyama Saadan itakapojengwa barabara kwa kupitia huku. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, la pili, kuna miradi ya uzalishaji chumvi katika maeneo ya Kitame pamoja na Saadan chumvi kule inazalishwa karibuni kila mwaka tani 100,000 zinashindwa kutoka kipindi hiki cha mvua kwa sababu barabara haipitiki. Kwa hiyo, ninaomba waitilie mkazo barabara hii.
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la tatu, kuna kiwanda kikubwa sana cha Bagamoyo Sugar ambacho kipo kule huduma zao za uzalishaji wa miwa na sukari zinakwama kipindi hiki cha mvua, hakuna kinachoendelea kutokana na barabara inakuwa mbovu haipitiki maroli makubwa hayawezi kwenda. Kwa hiyo, shughuli nyingi za maendeleo zinalala. Vilevile barabara hii itakapotengenezwa basi wazalishaji miwa wa pembeni out growers watapata fursa sasa ya kupeleka miwa yao katika Kiwanda cha Bagamoyo Sugar kwenda kuuza na kujiongezea kipato.
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine na la mwisho ni taa za barabarani TANROADS wamejitahidi sana kutuwekea taa za barabarani Bagamoyo, lakini bado hazitoshi barabara inayoanzia round about katika mzunguko wake kutokea Kichemuchemu...
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Mkenge malizia.
MHE. MUHARAMI S. MKENGE: Mheshimiwa Naibu Spika, zinahitajika taa za kutosha. Kwa haya, machache ninaiomba Wizara iyatilie mkazo mambo hayo ninaomba kuunga mkono hoja. Ahsante sana. (Makofi)