Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. JACQUELINE N. MSONGOZI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ili niwe miongoni mwa wachangiaji katika bajeti hii ya Wizara ya Ujenzi ya mwaka wa fedha 2025/2026 leo hii tarehe 5 Mei, 2025.
Mheshimiwa Naibu Spika, kama ilivyo ada ya system ya uchangiaji wangu lazima nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kazi nzuri ya kuhakikisha kwamba miundombinu ya nchi hii inakaa sawasawa. Pia, nimpongeze sana Waziri mwenye dhamana kaka yangu Mheshimiwa Ulega, baba Tulia pamoja na Naibu Waziri wake pamoja na delegation yake kwa kazi nzuri ambayo anaifanya. Ni Waziri bingwa ambaye yuko makini na ameonesha wazi kwamba ana uwezo mkubwa wa kufanya kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nichukue nafasi hii vilevile kumpongeza sana Meneja wa TANROADS Mkoa wa Ruvuma, ama kwa hakika wametupatia chombo na chombo hiki kwa kweli kinaenda vizuri sana. Anafanya kazi nzuri sana, sana, sana, ni msikivu, mwenye uelewa mkubwa. Tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa kumteua huyu bwana ili aweze kuisimamia miundombinu yetu ya Mkoa wa Ruvuma.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba sasa niende Songea Mjini nitachangia kiwilaya wilaya. Ninaomba nizungumzie Barabara ya Bypass ya Songea Mjini yenye urefu wa kilometa 16 ambayo kimsingi nimekuwa nikisema hapa Bungeni na hata mwezi Februari niliuliza swali ndani ya Bunge lako hili Tukufu kuhusiana na hii barabara. Majibu ya Naibu Waziri alisema kwamba Mkandarasi yuko kazini. Sasa nikajipanga na wanawake wenzangu ambao wamekuwa wakipata changamoto mbalimbali katika Manispaa ya Songea, twende tukaone vifaa vilivyoko site, lakini hatujaona hivyo vifaa. Ninaomba leo Waziri atakapokuwa ana windup anieleze ni lini barabara hii ya bypass itaanza kujengwa katika Manispaa ya Songea? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ni barabara ya kutoka Songea kwenda Makambako yenye urefu wa kilometa 395 ambayo kimsingi inahitaji ukarabati. Barabara ile ina vingundura, yaani ina viraka; mabonde yanafika mpaka kwenye viuno kwa kweli inaleta shida. Kimsingi kutoka Songea mpaka kufika Makambako kwa kawaida unatakiwa utumie masaa manne, lakini tunatumia mpaka masaa sita mpaka saba.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba sana hii barabara ianze kujengwa, tumeambiwa kwamba wanalipa fidia, lakini wananchi wamesubiri kwa muda mrefu mno, maswali yamekuwa ni mengi kila tunavyorudi tunatoa mrejesho wa Vikao vyetu vya Bunge, tumekuwa tukiulizwa maswali mengi sana hii barabara ni kero ina malori mengi sana yanayobeba makaa ya mawe. Kwa hiyo, ninaomba sana hii barabara ni muhimu, kwa hiyo ikiweza kurekebishwa, aidha kuongezwa kama ambavyo inasemekana basi tutashukuru sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba Songea Vijijini nizungumzie Barabara ya Likuyufusi – Mkenda yenye urefu wa kilometa 124 inayounganisha Nchi ya Mozambique na Tanzania, ni barabara muhimu sana ya kimkakati. Barabara hii tuliambiwa mwaka jana hapa imetengewa fedha ya kujenga kilometa 60, barabara hii haijaanza kujengwa hata kilometa moja. Sasa ninaomba, kwa kuwa Mheshimiwa Ulega ni Waziri kijana ambaye tunamwamini na tunajua kabisa yaani angepewa pesa yote rangi zake zote tungeziona; lakini pamoja na hayo hiyo pesa ndogo ambayo anapewa ahakikishe kwamba anaenda kuanza kujenga ile Barabara ya Likuyufusi – Mkenda walau kuanza kwa kilometa 10.
Mheshimiwa Naibu Spika, tutakuwa na amani na wananchi wa kule wanaendelea kuiamini Serikali yetu ya Chama Cha Mapinduzi, lakini hebu watendeeni haki kwa kuanza angalau hata kwa kilometa 10. Hali kadhalika, Barabara ya Maposeni – Mgazini yenye urefu wa kilometa 70 tunahitaji ijengwe kwa kiwango cha lami kwa sababu ni barabara ya kimkakati na ni barabara ambayo tunaamini kabisa itaendelea kuchagiza uchumi katika Wilaya ya Songea na kwa wananchi wa Songea pamoja na nchi nzima kwa ujumla. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa ninaenda Namtumbo. Pale Namtumbo pana Barabara ya Lumecha – Londo – kwa Mpepo yenye zaidi ya kilometa 300. Ninawaomba sana hapa imekuja lugha ya EPC+F, sijui plus Five ambayo tumekuja huko tena imeanza sijui nini, bado hii barabara haijaeleweka. Ninaomba Mheshimiwa Ulega atakapokuja hapa atueleze Barabara ya Lumecha – Msindo – Hanga – Kitanda, tujue hii barabara inaanza lini mpaka Londo kule kwa Mpepo. Ni barabara ya kimkakati ninaona Mbunge wa pale Mikumi anachekelea sana, ahsante sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna barabara hapohapo Namtumbo, Barabara ya Mtwara Pachani – Tunduru yenye urefu wa kilometa 305 inatoka Mtwara Pachani – Lumecha – Ligela – Lingusenguse mpaka kule Mchomolo na kufika kule Mbesa mpaka Tunduru Mjini kilometa 305. Barabara hii kila bajeti inapokuja, ninalia na hii barabara ni kwa nini Serikali haipeleki pesa kuanza kuijenga kwa kiwango cha lami? Sasa, ninaomba Waziri aje na majibu mazuri ili ioneshe kwamba baba Tulia yuko makini, ahsante sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa ninaenda Barabara za Nyasa. Nichukue nafasi hii kuishukuru sana Serikali ambayo kimsingi miaka miwili iliyopita mimi nilipiga magoti hapa kikwetu tunasema “niligalauka” ndani ya Bunge, kulia kwamba Daraja la Mitomoni ambalo lilikuwa na changamoto watu wengi wamepoteza maisha pale. Alhamdullilah, sasa hivi Serikali tayari imeshaanza kujenga daraja lile, ambapo imeleta matumaini makubwa sana kwa Watanzania wanaoishi katika maeneo yale. Tunaishukuru sana Serikali, tunamshukuru sana Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, mitano tena kwa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pia, ninaomba nichukue nafasi hii kuizungumzia Barabara ya Mbamba Bay – Litui, hapohapo Nyasa. Mbamba Bay – Litui, ina zaidi ya kilometa 100 tunaomba hii barabara ni barabara ambayo inahusisha masuala ya utalii inapita pembezoni mwa Ziwa Nyasa, hebu tujengeeni kwa kiwango cha lami ili na sisi tuendelee kuchanua kiuchumi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile naomba nizungumzie Barabara ya kilomita 56 Kigonsela – Mbaha. Barabara hii sasa hivi imeenda kuwa tunu zaidi. Ninaomba sasa wapende wasipende watuwekee, hii barabara ndiyo atakayokuwa anapita Mheshimiwa Makamu wa Rais, sasa sijui itakuwaje Mheshimiwa Ulega, Mheshimiwa Makamu wa Rais, anatoka pale Kigonsela anakwenda mpaka kule Mbaha kilomita 56. Tunaomba sasa ijengwe kwa kiwango cha lami Mheshimiwa Makamu wa Rais ajae ndiyo atapita hiyo barabara. Ahsante sana
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba sasa nizungumzie Barabara ya Kitahi – Ruanda, yenye urefu wa kilomita 40, lakini barabara hiyo inakwenda mpaka Lituhi – Ndumbi kilomita karibu 50 au 60, pale Ndumbi pana bandari kwa hiyo, tukitoka pale Kitahi kwanza yule mkandarasi hajalipwa, hajalipwa kwa muda mrefu.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba sasa bajeti hii itoe mwelekeo wa kwenda kuwalipa wakandarasi wote ambao wamekuwa wakidai pesa zao, wanafanya kazi wanakuwa na madeni wengine wanapoteza maisha, wamekuwa na mapresha hawawezi hata kutoka ndani wanadaiwa na mabenki, wanadaiwa na watu binafsi tunaomba...
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa haya malizia.
MHE. JACQUELINE N. MSONGOZI: Mheshimiwa Naibu Spika, achia kidogo niunge mkono hoja. Baada ya maneno hayo ninaomba nikushukuru sana kwa kunipa fursa hii na wewe ni mtu makini, mtu mahiri. Ninaunga mkono hoja. (Makofi)