Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mbulu Mjini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. ZACHARIA P. ISSAAY: Mheshimiwa Naibu Spika, ninakushukuru sana kwa kunipatia nafasi hii. Nichukue nafasi hii kumshukuru sana Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema kwa baraka zake kwetu sote wakati huu na nyakati zote. Pia, nichukue nafasi hii pia kumpongeza sana Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa namna ya pekee katika utekelezaji wa Ilani ya CCM kwa miaka yake minne katika kuingoza Serikali yetu. Kazi kubwa sana imefanyika katika Jimbo la Mbulu Mjini na maeneo mengine kwa kadiri tulivyofanya ziara na kwa kweli tunamwombea tutamlipa kwa fadhila. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nichukue nafasi hii pia kumpongeza Waziri mwenye dhamana ya Wizara hii na Naibu Waziri kwa kadri ambavyo wanaiongoza Wizara hii;na wale wote waliotangulia wakati ule wakiongoza Wizara hii, lakini kwa ajili ya maslahi mapana ya Taifa letu walipata kubadilishiwa majukumu yao. Nichukue nafasi hii vile vile kumpongeza Katibu Mkuu Balozi Aisha, na Dkt. Charles, Naibu Katibu Mkuu pamoja na Watendaji wote wa Wizara kwa kazi kubwa wanayoifanya kwa ajili ya Wizara yetu hii.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Wananchi wa Jimbo la Mbulu Mjini pia, nichukue nafasi hii kwa namna ya pekee, leo nina mchango mdogo sana. Mchango wangu kwanza utajikita sana kwenye utekelezaji wa hii miradi ya barabara. Barabara inayoitwa Karatu – Mbulu- Haydom – Sibiti ni barabara inayounganisha mikoa mitano nchini. Tulifurahi sana tulipopata ule mpango wa awali wa kujengwa kwa EPC+F, lakini hadi sasa barabara hii kwa miaka mitatu hatujafanikiwa kupata hata kipande cha lami, baada ya kusaini mkataba mwaka 2022. Eneo hili la Mbulu – Garbabi limekuwa kero kubwa sana na kwamba hii kazi Mkandarasi ameitelekeza, ameshaondoka lakini pia hayuko site.
Mheshimiwa Naibu Spika, kipande hicho kimekuwa kero kwa sababu mvua ikinyesha barabara zingine zote ni nzuri hata kutoka Karatu – Mbulu na kuendelea, lakini hicho kipande cha kilometa 25 hali ni mbaya sana. Kwa kuwa Mkandarasi hayuko site, wananchi wanapata shida kwa ajili ya kutengenezewa ile sehemu ya kilometa 25 kwa maana ya barabara ya mchepuo ama barabara ya kupita pembeni kwa ajili ya huduma. Jambo la kushangaza ni kwamba, kama upande wa lami umekwama sana tumepiga kelele muda mrefu kwa kutaka walau hata hiyo sehemu ya wananchi kupita kwa maana ya barabara ya kawaida, njia ya mchepuo haipo, hali ni mbaya sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo ninategemea Waziri kwa namna anavyoona nimezungumza, nimeuliza maswali kadhaa hapa Bungeni, nimemsihi mara nyingi, lakini aache hiyo ya lami ambayo kwa sasa inasubiri malipo, atakapokwenda pale atuambie huyu Mkandarasi analipwa lini na atatengeneza hii barabara ya udongo kwa muda gani? Kwa sababu miaka mitatu hatuna kipande cha lami.
Mheshimiwa Naibu Spika, mbaya zaidi tunasaini mikataba ambayo mbele ya safari au huko tuendako ni athari kwa Taifa na hata kwa huduma ya wananchi. Mkandarasi huyo amepewa kazi kule Dareda kwa Mheshimiwa Sillo, Jimbo la Babati Vijijini kilometa 25 bado hajaanza na Labay - Haydom kilometa 25 hajaanza na hii ya miaka mitatu aliyoisaini ameitelekeza hayuko site na wala vifaa haviko. Sasa wananchi wa Mbulu Mjini na maeneo mengine wangependa kufahamu, kwa sababu kadri ambavyo kazi imesimama athari ni kubwa sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimemtumia Mheshimiwa Waziri picha nyingi za magari yanavyokwama kwenye hicho kipande na jinsi ambavyo athari ni kubwa. Pia kama itawezekana ni nafuu akatengeneza barabara ya kawaida halafu hiyo ya lami akasubiri hayo malipo yake ya lami, kwa sababu kila mwaka tunapitisha bajeti hapa ni kwa ajili ya huduma na kwa ajili ya hiyo huduma hicho kipande angeendelea kuhudumia huduma za kawaida za wananchi.
Mheshimiwa Naibu Spika, sikuwa nimefurahi sana kushika shilingi ya Waziri, lakini nitampelekea ki-memo, majibu yake yasiponiridhisha, ni nafuu kwa niaba ya wananchi nichukue hatua hiyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, la pili, ni kule Mlima Magara. Tunashukuru kazi kubwa imefanyika kwenye ile Barabara ya Magara, lakini daraja limejengwa. Pia, kwa namna ya pekee, Mlima Magara umepata zege kwa kilometa sita kati ya 15, lakini eneo hilo ni tete, mvua moja tu ikinyesha Mlima Magara magari hayapiti, barabara inakatikakatika. Sina chuki sana na hii Wizara lakini wao wanavyosaini mkataba wana matumaini, lakini Wizara ya Fedha haiwawezeshi hawa na wanakwama sana kwa sababu wao kama hawawezi kumlipa Mkandarasi, Mkandarasi ni lazima aondoke site na hili tutalizungumza kwenye bajeti kubwa ya Serikali. Pia, eneo zima na barabara nzima ya Magara tayari usanifu ulishafanyika na kwa mujibu wa Serikali, Serikali inatafuta fedha kwa ajili ya kujenga lami Barabara ya Mbuyu wa Mjerumani - Magara - Mbulu. Eneo hilo ni muhimu linatuunganisha sisi na Mbuga za Wanyama, lakini pia na Mkoa wetu wa Manyara.
Mheshimiwa Naibu Spika, bila kupoteza muda nichukue tena nafasi hii kwa namna ya pekee kuona kwamba pengine hata katika ile hali ya utiaji saini wa hii mikataba au tunavyosaini, gharama ni kubwa sana ya ucheleweshaji baadaye tutadaiwa kama Serikali na kama nchi. Ili tusidaiwe tuangalie bajeti tunayopitisha kama inakidhi haja kwa ajili ya kulipa yale madeni, kwa sababu tumeambiwa 45% ya fedha za TANROADS ama za Wizara hii zimetolewa kwa maana ya utekelezaji wa majukumu mbalimbali. Hata hivyo, nina hofu pengine katika hizo 45% nusu yake ni kulipa madeni ya miaka iliyopita ambayo inakuja kuvuruga bajeti ya mwaka huu ambayo tupo nao. Hili ninalizungumza kwa sababu, kama miaka mitatu iliyopita katika kilometa 25 za Mbulu – Garbabi hakuna hata kipande kimoja cha lami. Hatuoni kuwa madeni haya baadaye na bajeti tunazopitisha zinakosa tija kwa wananchi na kwa namna ambavyo wananchi walitarajia huduma hiyo?
Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho lakini siyo kwa umuhimu, ninamwomba Waziri atakapoenda hapo pamoja na kwamba atamlipa lini na huduma hiyo ya barabara ya udongo itajengwa lini na yeye anatarajia kwenda Mbulu lini, mimi nitatangulia atanikuta kule Mbulu. Kwa sababu ninatarajia hata kuita Vyombo vya Habari vizungumzie hali halisi ya barabara hiyo kwa jinsi ambavyo hali ni tete. Mheshimiwa Waziri tunampenda, hana muda mrefu kwenye hii Wizara, lakini ameyakuta ayafanyie kazi ili walau Watanzania wapate amani, kwa sababu barabara ni kiungo muhimu sana kwa kadri ambavyo tunapata athari, hasa pale ambapo inajifunga na pale ambapo wananchi walitegemea lami, sasa ya udongo imekuwa kero. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ufafanuzi wa EPC+F. Je, hizo barabara...
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
NAIBU SPIKA: Ahsante Mheshimiwa Issaay, ya pili hiyo, malizia.
MHE. ZACHARIA P. ISSAAY: Mheshimiwa Naibu Spika, ninashukuru na ninaunga mkono hoja. (Makofi)
NAIBU SPIKA: Malizia sekunde mbili, tatu.
MHE. ZACHARIA P. ISSAAY: Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hii ya EPC plus Finance Waziri akija hapa atuambie zile barabara saba ikiwemo: Mbulu – Karatu – Haydom – Sibiti. Zile barabara nyingine kwa ujumla ziko saba, zina kilometa 2,035, tunazijenga vipi ili Watanzania wasikie hali hii kwamba walau mpango wa sasa wa Serikali baada ya ule wa awali kukwama sasa tutakwendaje hata basi kwa namna ambavyo wananchi wawe na taarifa kwa ujumla kupitia Bunge hili.