Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ujenzi kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

Hon. Dr. John Danielson Pallangyo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Arumeru-Mashariki

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ujenzi kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

MHE. DKT. JOHN D. PALLANGYO: Mheshimiwa Naibu Spika, ninakushukuru kwa nafasi hii ili nichangie kwenye hoja iliyoko mezani kuhusu bajeti ya Wizara ya Ujenzi, Wizara ambayo ni muhimu sana na ambayo inasimamia wahandisi ambao kimsingi ndiyo ambao wanabadilisha dunia yetu tuweze kukaa hapa.

Mheshimiwa Naibu Spika, nianze kwa kumpongeza sana Mheshimiwa Rais wetu, Dkt. Samia Suluhu Hassan ambaye ndani ya miaka minne akiwa ofisini ameandika historia. Ametufanyia kazi kubwa ambazo zote zimelenga kuboresha maisha ya Watanzania. Ninampongeza Mheshimiwa Waziri, Abdallah Ulega na Naibu wake, kwanza kwa hotuba nzuri lakini pamoja nao, Katibu Mkuu, Naibu Makatibu Wakuu na watendaji wote wa Wizara kwa kazi nzuri sana ambayo wanaifanya pale Wizarani.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninahudumu katika Kamati inayosimamia uwekezaji wa mitaji ya umma, kwa hiyo nimepata neema ya kutembea na kukagua miradi ambayo Serikali imewekeza. Nimeona miradi mikubwa kama vile Daraja la Kigongo – Busisi, ni mradi mkubwa wa kielelezo. Sasa hivi umemalizika na kazi hiyo imefanywa na Wizara hii ikisimamiwa na TANROADS. Vilevile Daraja la Tanzanite pia limemalizika, nalo limesimamiwa na TANROADS; nalo ni daraja kubwa; pamoja na barabara za lami nyingi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Mkoa wa Kigoma sasa hivi ni mkoa wa kimkakati. Mara ya mwisho tumekwenda kutembelea kule, kuna Barabara ya kutoka Kasulu kwenda Nyakanazi, ni mkeka. Kuna barabara inajengwa kutoka Kasulu kwenda Manyovu, nayo kazi inaendelea vizuri. Kwa kifupi sasa hivi Mkoa wa Kigoma ni accessible by air, kwa barabara na kwa treni pia. Nimpongeza Mheshimiwa Waziri kwa kazi nzuri ambayo inafanyika. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na hayo mazuri ambayo wanayafanya nchini nina machache ya kusema kuhusu hali ya barabara jimboni kwangu. Ninaomba niseme moja baada ya nyingine. Barabara ya Mbuguni, barabara hii inaunganisha mikoa miwili ya Arusha na Manyara; ni barabara ya siku nyingi sana. Ninashukuru Serikali imekwishafanya usanifu japo kwenye taarifa yake inasemekana kwamba usanifu umekwishamalizika.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nilikuwa ninategemea utoe mafungu mwaka huu huu ili ianze kujengwa. Hata Mbunge wa Kiteto hapa jirani, amesema anaiomba hiyo barabara ijengwe ili Manyara na Arusha ziweze kuwasiliana kiurahisi. Siyo hivyo tu, ni kiungo muhimu sana kwa biashara ya Tanzanite ambayo inachimbwa pale Mererani kwa ajili ya kupelekwa kwenye masoko Jijini Arusha. Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri, nilikuja kwenye desk lako mwaka huu usiiache, ianze hata angalau kidogo kidogo hii itatujengea heshima sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna Barabara ya King’ori kuanzia Malula – Kibaoni – Ngarenanyuki, barabara hii inahudumiwa na TARURA, lakini tuliomba ipandishwe hadhi iweze kuhudumiwa na TANROADS. Barabara hii ni ya kimkakati kwa sababu inaunganisha barabara mbili kuu, barabara inayotoka Nairobi - Namanga – Arusha na Arusha – Moshi – Dar es Salaam, inazunguka Mlima Meru ikaifungia Arusha National Park katikati pale. Kwa hiyo, ikitengenezwa na kujengwa kwa kiwango cha lami itakuja kuungana na barabara inayohudumiwa na TANROADS kutoka pale Usa River – Oldonyosambu na kuhakikisha kwamba wananchi hawa ambao wanaishi upande ule maisha yao yatakuwa bora. Barabara hii inahudumia wananchi wa kata nane. Kwa hiyo, nimwombe Mheshimiwa Waziri, sasa achukue initiative, hiyo barabara ipandishwe hadhi, kwa sababu TANROADS wana access na fedha kuliko TARURA. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niliwahi kuomba hapa kwamba sasa hivi Barabara ya kutoka Tengeru pale Sangisi kuelekea Holili, ambayo inajengwa ni njia nne, sasa hivi itajengwa mpaka Usa River kilometa tisa. Niliomba kwamba usanifu utakapokuwa unafanyika itengenezwe route barabara ya kuingia Tengeru Sokoni kwa ajili ya kuliboresha lile soko. Hii inawezekana, kwa sababu tunajua hii miradi mikubwa inakuwaga na CSR. Sasa ile CSR ambayo itakwenda halmashauri, badala ya kwenda halmashauri moja kwa moja wajenge ile barabara ya kuingia sokoni, lakini pia na kuboresha miundombinu fulani pale sokoni kwa ajili ya kuwasaidia wananchi wetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna barabara nyingine tena inakwenda Tengeru pale Chuoni. Hii barabara zamani ilikuwa ni ya lami, barabara nzuri sana, lakini iliachwa ikaharibika kabisa, kabisa. Mheshimiwa Waziri atakumbuka mwaka juzi tulikwenda kule chuoni, aliona Barabara hiyo ilivyokuwa imeharibika, lakini ile barabara ilikuwa ni ya lami, nzuri na imepandwa miti pembeni na ile barabara ni ya TANROADS, maana yake ndiyo inakwenda kuungana na barabara ya kwenda Mbuguni. Ninaomba iingizwe kwenye mpango ili iwekwe lami ili wanafunzi na watu wengine wanufaike. Kuna vyuo vingi sana pale eneo lile kuna Chuo cha Kilimo; kuna Chuo cha Mifugo; lakini kuna Nelson Mandela, ni taasisi ambazo ni muhimu zinahitaji kuwa accessed kiurahisi. Kwa hiyo, tunaomba sana barabara hii nayo ijengwe kwa kiwango cha lami ili iunganike na Barabara ya Mbuguni ambayo imeshafanyiwa usanifu.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimalizie na kusema kwamba nilikwenda Arusha National Park wanalalamika kwamba, sasa hivi wana shida kubwa, magari ni mengi yanaingia hifadhini, kwa hiyo wanashindwa ku-maintain zile barabara. Ndiyo maana nimesema Barabara ya King’ori ni ya kimkakati, kwa hiyo niombe, ninarudia tena Mheshimiwa Waziri, Barabara ya King’ori iondoe TARURA ili ipande hadhi kama tulivyoomba, japo walisema kwamba haikidhi vigezo, lakini inakidhi vigezo kwa sabbau inahudumia na inapita kwa wananchi wengi sana kata nane. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya haya machache, niseme ninaunga mkono hoja na ninashukuru sana kwa muda. (Makofi)