Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ujenzi kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

Hon. George Natany Malima

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mpwapwa

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ujenzi kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

MHE. GEORGE N. MALIMA: Mheshimiwa Naibu Spika, ninakushukuru kwa kunipa nafasi ili nichangie bajeti ya Wizara hii ya Ujenzi. Ninaomba nianze na kumshukuru Mwenyezi Mungu ambaye ametupa afya na tumeweza kuhudhuria katika Bunge lako Tukufu. Pia, ninamshukuru Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa sana anayoifanya katika nchi yetu. Tumeshuhudia kiwango kibwa sana cha miradi mikubwa ya maendeleo ikiendelea kutekelezwa na mingine ikikamilika. Mfano ni Daraja la Busisi. Binafsi nimefika, nimeona ni daraja la kisasa kabisa ambalo wengi wamesema; ni daraja refu kuliko madaraja yote katika Ukanda wa Afrika Mashariki. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ujenzi wa viwanja vya ndege pia unaendelea takriban nchi nzima. Nimepata nafasi ya kuona baadhi ya viwanja; Kiwanja cha Msalato, Nduli kule Iringa, Shinyanga na maeneo mengine. Kwa hiyo, tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa kazi hii anayoendelea kufanya. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ninawapongeza Mheshimiwa Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega, Naibu wake na timu nzima kwa jinsi ambavyo wanaendelea kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi mkubwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, nianze na kuchangia kuhusu Bodi ya Mfuko wa Barabara (Road Fund). Kuna shida kwenye mtiririko wa fedha kutoka kwenye makusanyo. Mwaka wa fedha 2024/2025 Mfuko wa Barabara ulikuwa umepanga kukusanya shilingi bilioni 856.78, lakini inapofika mwisho wa kutoa hii taarifa walikuwa wamefanikiwa kukusanya shilingi bilioni 819.66. Kiasi ambacho makusanyo siyo mabaya, ni mazuri, lakini kilichotokea ni kwamba fedha zilizokuwa zimehamishiwa kwenye Mfuko wa Barabara mpaka kipindi hicho wakati taarifa inatoka ilikuwa ni shilingi bilioni 289 tu, ambayo ni sawa na 35.37%. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, utaona fedha nyingi hazipelekwi. Shilingi bilioni 529.72 hazikuhamishwa kwenda kwenye Mfuko wa Barabara, ambayo ni sawa na 64.63%. Hii imeathiri sana ujenzi wa barabara na ukarabati wa barabara na madaraja. Kwa sababu fedha nyingi zinakusanywa kweli lakini hazipelekwi kwenye Bodi ya Barabara kwa wakati.

Mheshimiwa Naibu Spika, kati ya miradi ambayo imeathirika sana na utaratibu huu ambao ninaona haufai ni pamoja na Barabara yetu ya kule Mpwapwa yenye urefu wa kilometa 98 inayoanzia Kongwa Junction – Mpwapwa – Kibakwe. Mkataba wa barabara hii ulisainiwa mwaka jana mwezi Februari, lakini baadaye mwaka jana karibu na mwezi Agosti mwishoni mkandarasi alihamia site. Mpaka leo tunavyozungumza hapa ujenzi haujaanza; ni kwa sababu ya uhaba wa fedha; lakini fedha zimekusanywa kwenye Mfuko huu ambazo zilitakiwa ziende kule ili hawa wakandarasi walipwe na ujenzi ungeendelea. Wananchi wa Mpwapwa wanatamani kuona ujenzi umeanza na baadaye waone barabara yao inapitika. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ninashauri, fedha zikikusanywa kwa ajili ya Mfuko huu wa Barabara basi ziende kwa wakati na pia ziende ku-support miradi yote inayosubiri fedha hizi. Kwa hiyo, sisi wa Mpwapwa katika Mkoa wa Dodoma ndiyo wilaya pekee ambayo haijaunganishwa na barabara ya lami. Sasa tuna kiu ya kupata barabara. Kila siku tunamwona mkandarasi site lakini kazi haijaanza; na ujenzi huu umesemwa utajengwa kwa awamu. Kutoka Kongwa Junction mpaka Mpwapwa Mjini ni kilometa 32 tu, awamu ya kwanza itakuwa ni hiyo, lakini awamu ya pili itaanza Mpwapwa kuelekea Kibakwe. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, wananchi wa Wilaya ya Mpwapwa, majimbo yote mawili, tunatamani na sisi tuunganishwe na mkoa kwa kutumia barabara ya lami.

Mheshimiwa Naibu Spika, lingine ambalo ningependa kuchangia, linahusu madeni ya wakandarasi. Haya pia yanatuletea shida kwenye Wizara hii. Kwenye taarifa tumeambiwa kwamba Februari, 2025 Serikali ilikuwa inadaiwa shilingi trilioni 1.29 na shilingi bilioni 136.98 ilikuwa ni madeni kwa ajili ya riba inayotokana na kuchelewesha kulipa wakandarasi. Fedha hii ingeweza kutosha kujenga ile Barabara ya kutoka Kongwa mpaka Kibakwe, lakini tunawalipa wakandarasi kama riba kwa sababu ya kuchelewa kuwalipa. Kwa hiyo, wakati mwingine maendeleo yetu tunayachelewesha sisi wenyewe. Kwa nini hatuwalipi kwa wakati ili fedha hizi za riba zitumike kufanya kazi nyingine? Zitumike kujenga miradi mingine ya maendeleo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ninashauri sana mtiririko au madeni haya yalipwe kwa wakati ili tuepuke riba kwa sababu riba inaleta hasara kwa Serikali. Shilingi bilioni 136 si fedha ndogo, inalipwa na bado itaendelea kulipwa kama hatuwezi kubadilika tukawalipa wakandarasi kwa wakati. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ni ushirikishwaji wa wakandarasi wadogo. Nimeona kwenye…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Malizia Mheshimiwa.

MHE. GEORGE N. MALIMA: ... ripoti tumeelezwa kwamba Serikali inajitahidi kuwashirikisha wakandarasi wadogo, lakini ninaona bado haitoshi. Wakandarasi hawa ndio hawa hawa ambao hawalipwi na ni hawa hawa ambao wanashirikishwa kwa kiwango kidogo. Kwa hiyo, wale walioshirikishwa wamefirisika...

NAIBU SPIKA: Ahsante Mheshimiwa.

MHE. GEORGE N. MALIMA: ... ninaomba sana wakandarasi walipwe kwa wakati...

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa, unga mkono hoja.

MHE. GEORGE N. MALIMA: ... washirikishwe kwenye miradi hii mikubwa ya maendeleo ili waweze kukua na wakikua baadaye miradi hiyo mikubwa mikubwa wanaweza kufanya wakandarasi wadogo ambao ni wazawa wa nchi yetu ya Tanzania. Ahsante sana.