Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ujenzi kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

Hon. Antipas Zeno Mngungusi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Malinyi

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ujenzi kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

MHE. ANTIPAS Z. MGUNGUSI: Mheshimiwa Naibu Spika, nitajitahidi mchango wangu uwe mfupi kwa sababu, kuna mambo ninayotaka kuyasema kuhusu Malinyi. Mheshimiwa Waziri tulikuwa naye kule siku chache zilizopita, alitua na helkopta Malinyi, alijionea hali yetu. Kimsingi nina mawili; jambo la kwanza ni hali ya Barabara yote kutokea Ifakara mpaka Malinyi, lakini la pili, ni kuunganisha Wilaya ya Malinyi na Mlimba kupitia pantoni kwenye Kivuko cha Kikove.

Mheshimiwa Naibu Spika, kabla ya kuendelea niishukuru Serikali, Mheshimiwa Rais na timu yake yote. Kwanza mwaka huu tumetengewa, kwenye bajeti hii ya leo, kilometa 112 kutoka Ifakara mpaka Mtimbila, Malinyi. Kwa hiyo, ninaomba kwa niaba ya Wanamalinyi wenzangu basi, hilo jambo lianze mapema zaidi hata kama ni kidogokidogo, tunasubiria kwa hamu tuweze kupona. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ninawashukuru pia, watendaji wote wa Wizara; Katibu Mkuu wa Wizara, Mkurugenzi wa TANROADS na wengine wote. Wamekuwa wakinipa ushirikiano mkubwa sana katika kipindi hiki cha mafuriko na masika, kukatika kwa barabara na hata katika hali ya kawaida tumekuwa tukifanya nao kazi kwa ushirikiano mkubwa sana kwa hiyo, ninawashukuru. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mambo yangu makubwa ni mawili. Jambo la kwanza ni, Malinyi mpaka hivi ninavyozungumza hapaingiliki; hakuna gari linaingia wala kutoka kwa maana pamekatika sehemu mbili, barabara yetu kutoka Ifakari. Barabara ya kwanza imekatika jana, kwa maana na leo mawasiliano hakuna. Ukitoka Ifakara huwezi kusogea sehemu ya Namhanga, kipande cha Ulanga kimekatika, maana yake ni magari hayaingii wala kutoka. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sehemu ya pili ambayo Mheshimiwa Waziri amefika wiki iliyopita, pamekatika pale Malinyi Mjini, kilomita chache tu kufika kwenye mji hapaingiliki, barabara imefumuliwa na maji ambayo yametokana na Mto Furua. Kwa hiyo, sasa ni adha kubwa sana, maana yake ni wananchi kwenye baadhi ya vijiji, nyumba zimeingiliwa na maji, nyumba nyingine zimeanguka na changamoto zinazofanana namna hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa katika haya nina ushauri wa machache tu. La kwanza, ninajua TANROADS wanaendelea na tunashukuru tena, tumepata fedha bilioni 18 za Benki ya Dunia kwa ajili ya kujenga daraja hapa ambapo ninasema pamefumuka wiki iliyopita na hata hapa ambapo pamefumuka jana palishapangiwa tayari kujengwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa ninaomba tu, ninafikiri kuna haja ya kufanya design mpya kwa uharaka kulingana na hali maana kama pamefumuka, maana yake pameongezeka urefu tofauti na vile vipimo vya awali.

Mheshimiwa Naibu Spika, kubwa pale Madumba kwa maana ya Fuluwa, kuna ule mto ambao unatusumbua Malinyi siku zote na huwa ninauelezea hapa. Mto Fuluwa hauna kina, hauna kingo na ndiyo unaofurumusha maji kuweza kuharibu barabara za TANROADS na TARURA.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa kila mwaka tumekuwa tukipata fedha kwa ajili ya marekebisho hayo ili kutibu barabara kutokana na adha ya Maji ya Mto Fuluwa, lakini mwisho wa siku pamoja na daraja ambalo tutakwenda kujenga, tunashukuru lakini maana yake daraja litapitisha maji mengi zaidi. Pia, vijiji vya mbele navyo kule kwenye barabara za TARURA kuna uhitaji wa kutoa karavati. Pengine wenzangu wa TAMISEMI kama wapo hapa waweze kusikiliza na kuona kuna haja nao ya kufanya kama wanavyofanya ujenzi, kuyapokea maji yanayotoka Fuluwa kwa maana kujenga daraja ili tutoe zile karavati.

Mheshimiwa Naibu Spika, hata Kiwale pia kuna haja ya kufumua zile box karavati, kuweka daraja kwa maana maji yatapita mengi sana kwenye daraja jipya ambalo TANROADS wanatarajia kujenga.

Mheshimiwa Naibu Spika, suluhiso kubwa la kudumu ni ku-deal na Mto Fuluwa wenyewe. Watu wa Ofisi ya Rais, Mazingira, wenzangu wa TAMISEMI wenye TARURA na TANROADS wenyewe, watu wa bonde na watu wa TANESCO, wamefanya Ifakara pale Mto Lumeno kwa ndugu yangu Asenga wametusaidia; wamechimba tuta kubwa na wametengeneza kina, sasa hivi angalau kuna unafuu. Kwa hiyo, ninaomba jambo la namna hii lifanyeke na Mto Fuluwa, itakuwa tumesaidia kwa kudumu kabisa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la mwisho ni jambo la kuunganisha Mlimba na Malinyi. Kwa mara ya kwanza tangu dunia imeumbwa tunatarajia kwa mwaka huu hilo jambo likatokee. Ni ahadi ya muda mrefu. Wakandarasi wamekuwa site na tumehangaika nao kwa muda mrefu na wengine tumewafukuza, tuna mkandarasi mpya sasa. Sijajua changamoto ni nini lakini kazi inakwenda taratibu sana. Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri wa Ujenzi ahangaike na watu wake pia; kwa maana ya TEMESA, ndiyo wana-deal na kile kivuko cha kutuvusha pale pakipona. TANROADS ndio wanaojenga lile gutter pale Kikoyo ili kutuunganisha na Ngalimila kule Mlimba.

Mheshimiwa Naibu Spika, kabla ya kufikia kwenye maji kuna section ya TARURA, kuna sehemu kuna tobo linahitaji box karavati, kama milioni 315. Ninafikiri Serikali yote iko hapa, basi watu wa TAMISEMI na TARURA waone hili jambo. Nimeahidiwa na Mkurugenzi kwa maana ya Chief wa TARURA. Tunaomba msaada zaidi, tunakumbushia, tuhakikishe kwamba kwenye ile sehemu panajengwa box karavati kwa wakati na TANROADS wanamaliza ile gutter kwa wakati. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kivuko kile cha TEMESA kidogo kuna changamoto. Kiko Mwanza, Songoro Marine anatengeneza, lakini nimeambiwa bado kidogo sana asilimia kama saba kumaliza ila ninadhani yule bwana anadai dai kidogo fedha. Hebu Serikali muangalie namna ya kufanya ili tusaidike kwa uharaka.

Mheshimiwa Naibu Spika, matamanio yangu ni kuona pengine tukichelewa sana by Christmas mwaka huu, Malinyi tuweze kwenda kule Mlimba kupitia shortcut ya pantone. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ninakushukuru; ni hayo tu kwa leo. Hata hivyo, kwa kuwa Mheshimiwa Waziri alifika basi ninaomba mambo haya yatekelezeke kwa uharaka sana. Manager wangu wa TANROADS wa Mkoa, Mkuu wa Mkoa na Mkuu wa Wilaya wananipa ushirikiano mkubwa sana na wananchi wote wa Malinyi tunawapa pole sana. Ofisi ya Mheshimiwa Waziri Mkuu Maafa, tunaomba tusaidike maana kuna nyumba kadhaa zimeanguka na kuna nyumba zimeingiliwa na maji, tunahitaji msaada kidogo wa madororo, wengine vyakula na vitu vya namna hiyo. Kwa hiyo, ninaomba sana tusaidike. Ahsante sana. (Makofi)