Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ujenzi kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

Hon. Njalu Daudi Silanga

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Itilima

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ujenzi kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

MHE. NJALU D. SILANGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ili niweze kuchangia Wizara hii muhimu, ambayo imebeba uchumi wa Taifa letu, imefanya kazi kubwa na nzuri. Tunawapongeza sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, nianze kumpongeza sana Mheshimiwa Rais kwa kazi kubwa na nzuri anayoifanya, hasa sisi watu wa Kanda ya Ziwa kwa kukamilisha Daraja la Busisi. Ni kiungo kikubwa sana kwa Wananchi wa Kanda ya Ziwa, kwa maana ya kwamba, litawafaidisha sana kiuchumi katika maeneo ya kanda yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niwapongeze Mheshimiwa Waziri na Naibu wake. Niwapongeze watendaji, wakiongozwa na Katibu Mkuu, bila kuwasahau watendaji wangu wa Mkoa wa Simiyu, Engineer Mkumbo na timu yake, kwa kupanga mikakati mizuri katika mkoa wetu na kuhakikisha kwamba, mambo yanakwenda vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niombe tu Mheshimiwa Waziri na timu yako, yapo maombi na mipango mizuri, ambayo tumeifanya katika Mkoa wetu wa Simiyu kupitia Kamati ya Ushauri ya Kimkoa. Zipo barabara ambazo zinatakiwa kupandishwa hadhi, nimwombe sana Mheshimiwa Waziri, ukifika muda katika mpango huu ambao tumependekeza na kuupeleka kwake, barabara hizi zitaunganisha kiuchumi mikoa tunayokutana nayo. Ninaomba nimwambie Mheshimiwa Waziri Barabara hizo ni Luguru – Lagangabilili – Migato – Ndololezi Bumera – Nyangokolwa – Somanda ni barabara ambayo inaunganisha wilaya tatu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukija barabara nyingine ambayo tumeleta maombi katika maeneo yako inapita kwenda Ndololezi – Nkuyu inakwenda mpaka Igegwa, ambapo kuna machimbo, kuna madini na vilevile kuna airport, ambayo inajengwa kwenye maeneo hayo. Nimwombe sana Mheshimiwa Waziri, basi maombi hayo ayafanyie kazi kwa kupanua mtandao wa barabara. Barabara nyingi anazozijenga katika maeneo yetu, kwa mfano ya Simiyu, ni barabara moja ambayo inapitika kwa muda wote. Kwa hiyo, kila baada ya muda mfupi wa miezi miwili, barabara lazima iharibike, lakini kwa barabara ambazo tumemtajia hizi, akizifungua, atatengeneza mwanya kwenye maeneo mengine ili iende vizuri zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ipo pia Barabara nyingine ya kutoka Gambasingu – Nkoma kwenda Mwamigagani, ambayo hii ikitengenezwa inakwenda kukutana na Wilaya ya Magu, kwa maana ya unaingia Mkoa wa Mwanza, katika hali ambayo wataalam wako Mheshimiwa Waziri walikuja kutuelekeza jinsi gani ya kufungua barabara. Kwa hiyo, niombe, barabara hizi ni muhimu sana, ukiichukua itatusaidia. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ni Makao Makuu ya Wilaya yetu ya Itilima. Kwenye utaratibu wa TANROADS kuna Barabara ambayo inatoka Bariadi – Kisesa, tunaomba uithibitishe. Ninaamini wataalam wetu walishakuletea taarifa, basi kipatikane kipande cha lami katika maeneo ya Makao Makuu, ili wananchi wa Itilima waweze kupata lami katika maeneo hayo, hasa kwenye upande wako wa TANROADS. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini tumetumia fedha nyingi kujenga Daraja la Shibiti ambalo linaunganisha Mkoa wa Singida na Mkoa wa Manyara. Niombe, mwaka jana hapa kwenye Wizara ya Ujenzi, Wabunge wenzetu waliomba na waliongelea sana suala hili; nikuombe sana Mheshimiwa Waziri, utaratibu wa fedha nyingi ambao tumewekeza kwenye Daraja la Sibiti, kama hatutatengeneza zile barabara za kutoka Sibiti – Kisesa kwenda Lalagu, ukitoka Lalagu unakuja Bariadi, unaenda Magu, itakuwa haina maana yoyote kwa sababu, tumewekeza fedha nyingi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nikuombe Mheshimiwa Waziri na timu yako, hili Daraja la Sibiti na barabara zake zote basi zifunguliwe, ili kusudi muda wote kazi zifanyike. Mheshimiwa Waziri akifungua Barabara ya Shibiti – Itilima – Kisesa mpaka Bariadi atakuwa ametusaidia sana katika kutekeleza majukumu yako. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Barabara hii ninayoizungumzia ya Kisesa, sasa hivi tunaenda kufungua Daraja la Busisi. Maana yake ni malori yanayotoka Dar es Salaam, yanayokwenda Uganda, yatatoka Dar es Salaam yakifika Singida yatapita Shibiti, yatapita Kisesa – Bariadi – Magu – Busagala yananyooka moja kwa moja kwenda Bukoba na maeneo mengine. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, tunapofungua hizi barabara zina umuhimu mkubwa sana kwenye nchi yetu, lakini vilevile tunapanua miji kwa maana ya kwamba, miji ambayo itakuwa haipitiwi itakuwa imepata uchumi wa kutosha maana tutakuwa na pato kubwa la Taifa. Kwa hiyo niendelee kuishauri Serikali kwamba, upo umuhimu sana wataalam wetu kupitia TANROADS, kwenye maeneo ambayo tunayazungumzia kila tukija katika Bunge lako Tukufu hili, basi uyafanyie kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ni, barabara zetu hizi tunazozitengeneza. Barabara ya kutoka Shinyanga – Migumbi – Musoma, barabara hii katika ujenzi wake imekuwa na viraka vingi sana, ni hatari kubwa sana kwa Taifa. Nimwombe sana Mheshimiwa Waziri na wataalam wake, hasa Barabara ya kutoka Mwigumbi – Maswa – Bariadi, barabara hiyo kwa muda mchache haitamaniki, imekuwa na mabonde mengi sana kwa muda mchache. Kwa hiyo, nimwombe sana Mheshimiwa Waziri na timu yake, wapite tena kuangalia jinsi gani ya kumaliza tatizo hilo katika maeneo hayo; yapo mabonde makubwa sana utadhani lami imejengwa zaidi ya miaka saba, wakati ni lami ya miaka miwili, mitatu. Jambo hili tunapolizungumza basi wataalam walifanyie kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kubwa zaidi kwa Mkoa wetu wa Simiyu, tuna Barabara moja tu ya TANROADS ndiyo maana tunaizungumzia sana, Barabara ya Kisesa – Bariadi – Itilima – Magu. Ikimpendeza Mheshimiwa Waziri nimwombe sana Mheshimiwa Waziri, aweze kutembelea maeneo hayo ajifunze mwenyewe haya maneno tunayoyazungumza, ili kusudi akifika, basi akikaa na timu yako atakuwa anajua tunakushauri nini na kwa wakati gani. Tunayo barabara moja tu, ambayo ni inaungana na mikoa mingine nje kwa nje. Kwa hiyo, nimwombe sana Mheshimiwa Waziri, achukuwe hili wazo ili alifanyie kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, la mwisho, zaidi niwapongeze sana Watumishi wa TANROADS kwa ushirikiano mkubwa wanaotupa sisi Waheshimiwa Wabunge, lakini ni maana ya kwamba, nidhamu hii imejengwa kutoka Wizarani, wanateremka mpaka chini. Basi tuwapongeze, lakini tunachohitaji sisi ni kupata utendaji ulio bora, ili wananchi wetu waweze kupata huduma safi katika maeneo ambayo tunayazungumzia. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema haya, ninaunga hoja mkono na ahsante sana. (Makofi)