Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ujenzi kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

Hon Abubakar Damian Asenga

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kilombero

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ujenzi kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

MHE. ABUBAKARI D. ASENGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ninakushukuru sana kwa nafasi ya kuchangia Wizara yetu ya Ujenzi. Sisi, kama Wajumbe wa Kamati ya Bunge ya Miundombinu, chini ya Mwenyekiti wetu komredi, Mheshimiwa Selemani Kakoso kwa kweli, tumeisimamia sekta hii kwa karibu sana. Komredi Kakoso ni miongoni mwa watu wazoefu sana katika Sekta ya Miundombinu, amekuwa akituongoza katika Kamati kutokana na uzoefu wake kufuatilia miundombinu ya nchi hii, hususan katika Sekta ya Ujenzi. kwa kweli angekuwa Engineer sijui ingekuaje, kama hapa tu sio Engineer, lakini ana uzoefu mkubwa kiasi hiki. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ukweli ni kwamba, leo tuna-discuss bajeti ya Wizara ya Ujenzi hapa na Wizara ya Ujenzi inashika miundombinu yote ya nchi hii. Waziri au Mheshimiwa Rais hata angekuwa na uwezo akatenga Bajeti yote ya Serikali, sidhani kama ingetosha asubuhi ya leo kumaliza barabara na changamoto zote ambazo zinatukabili sisi katika nchi yetu. Hayo nimejifunza kutoka katika Kamati yetu ya Miundombinu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, changamoto ambazo zipo katika nchi yetu ni kubwa sana na kadri zinavyopatikana fursa za kupunguza changamoto hizo, tunaishukuru Serikali na tunampongeza Mheshimiwa Rais na Wizara kwa ujumla; Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri, Katibu Mkuu, Chief of TANROADS, Mohamed Besta na wengine. Tunaona Mheshimiwa Waziri unahangaika, umekuja kule kwetu na helikopta, Mheshimiwa Waziri haujapanga mafuriko yale, yametokea tu, unaambiwa barabara imekatika inatakiwa pesa; umeenda Mtwara inatakiwa pesa. Kwa hiyo, yote haya yanataka pesa za nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hawa watu wengine wanaolalamika, Mheshimiwa Waziri, ninawaambia walishawahi kukaa siku moja wakasikia bajeti ya Serikali? Tunaposema trilioni 44 mathalani na wanaposema nchi yetu hii ni tajiri inaweza ikatoa kila kitu, walishawahi ku-calculate wakaona kwamba, kwa rasilimali tulizonazo tunaweza tukafanya yote kwa siku moja? Kwa wakati mmoja? Kwa miaka hata mitano au mitatu? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hatuwezi kumaliza yote. Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri tunachokizungumza hapa ni umuhimu na sisi, kama Wabunge, tunatoa maeneo yenye changamoto nyie myapange kutokana na vipaumbele vyenu ili muweze kutatua sekta ya miundombinu katika nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, suala la pili, sisi Kilombero, Mkoa wa Morogoro, ni miongoni mwa mikoa ambayo tunalalamika kila siku iunganishwe na mikoa mingine. Tuna Barabara yetu ile ya kutoka Kilombero kuunganisha Ulanga – Lindi, unaifahamu, ilikuwa EPC+F. Tuna Barabara yetu ya Ifakara – Malinyi – Njombe, kuna Barabara yetu ya Ifakara – Mlimba – Njombe na ile nyingine inaenda mpaka Songea.

Mheshimiwa Naibu Spika, barabara hizi zinataka fedha nyingi sana na sisi tumeelewa Mheshimiwa Waziri, kama point niliyosema mipango ya Serikali, tunaiomba siku ikipatikana fedha, ikapatikana fursa, watusaidie sana kufungua barabara hizi. Tunaishukuru Serikali kwa sababu tumeambiwa tayari Barabara ya Ifakara – Lupilo kwenda Malinyi iko katika mpango. Hii inadhihirisha yale niliyoyasema kwamba, wakati wote tunalalamika, mwaka 2021 tumelalamika, mwaka 2022 tumelalamika, mwaka 2023 tumelalamika, leo tupo mwaka 2025 barabara ile imewekwa kwenye mpango. Kwa hiyo, hilo ndilo tunalosisitiza sana Mheshimiwa Waziri, tunavyozungumza hapa tunaomba sana watusaidie, inapopatikana fursa basi waweze kufanya hizo barabara ambazo tunazilalamikia wakati wote. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa ujumla kutoka katika Kamati yetu, ninalotaka la kwanza ni kusaidia uchumi wa nchi yetu kutokana na tathmini ambazo zimefanywa na wataalam, hasa kuhusu bandari yetu kuunganisha na barabara na malori ambayo Wabunge wengi wameyasemea. Sisi tumeenda Dar es Salaam zaidi ya mara mbili, mara tatu na Kamati ya Bunge ya Miundombinu; Mheshimiwa Waziri katika vitu vinavyotuchelewesha ni kutokuunganisha reli yetu ikaenda kwenye Wizara ya Uchukuzi ama na barabara maalum, hata kama za chini, kuchukua yale makontena bandarini na kuyatoa nje ya Dar es salaam kwa utaratibu maalum. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hatuwezi kuendelea kuwa nchi ya namna hiyo Mheshimiwa Waziri. Pita pale Buguruni, huwezi tena kuwahi na wewe ni Mbunge wa Dar es Salaam, shahidi wa jambo hili. Njia gani wataalam wetu wa barabara wanaweza kufanya kuhakikisha kuna njia hata ya underground ama njia yoyote, kama ya juu ama ya wapi na hiyo SGR itaingia baadaye bandarini. Tutoe ma-container hata kama ni saa sita usiku, saa saba usiku, ili tusi-disturb watu wa Dar es Salaam kwa sababu, ni uchumi wetu mkubwa sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mtu kama analalamika anaweza kukaa Dar es Salaam peke yake saa 24 hajatoka bandarini, hajatoka kilomita 50. Hiyo ni changamoto kubwa sana katika uchumi wa nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, suala la pili, kama alivyosema Mbunge mwenzangu, ambaye ni Mjumbe wa Kamati ya Miundombinu, suala la malipo kwa wakandarasi. Mheshimiwa Waziri sisi tulitoa maoni na tulishauri, kama kuna uwezekano, wakandarasi wengi wanadai na ninajua wengine watalipwa, wangekuwa wanakaa nao hawa mara kwa mara waweze kujithibitishia kwamba, anasubiri atalipwa mwezi wa ngapi. Hii itatupa picha nzuri sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ninajua changamoto niliyonayo pale Kilombero. Kwa mfano, Barabara ya ifakara – Kidatu, mkandarasi yupo pale, ukienda kukutana naye, Raynods analalamika. Sisi tuna Barabara hii ya Ifakara kwenda Mlimba, mkandarasi ndiyo jana nimeenda nimemkuta na Chief of TANROADS, jana, anamshinikiza aanze angalau kufanya ukarabati wa ile Barabara ya Ifakara – Mlimba. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, wanaweza wakagawanya wakaanza na wakatuambia, Waheshimiwa Wabunge kwamba, hawa kumi ndiyo watakaolipwa wataanza site. Hii itatusaidia sana, huwezi kufanya yote, Mheshimiwa Waziri, utapasuka na sisi tumeshakuelewa kuwa, wewe unasema hili sio shamba la bibi, tumeelewa ile lugha, lakini huwezi kufanya yote. Kwa kweli, kama utatuambia wakandarasi safari hii, miezi sita ama miezi hii mitatu, wanalipwa hawa 10 wa barabara moja, mbili, tatu; wewe Mheshimiwa Asenga subiri, wewe Mbunge fulani subiri, watu watasubiri Mheshimiwa Waziri. Tunaomba sana hii iwekwe wazi kwa sababu, kwenye Kamati imekuwa kila siku ni kero za malipo ya wakandarasi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kingine ninachotaka kuzungumzia ni TEMESA. Mheshimiwa Waziri katika Kamati yetu kwa kweli, katika taasisi ambayo tunaona kidogo nayo inaminywaminywa, basi ni hii ya TEMESA. Unakutana na Mkurugenzi Mkuu wa TEMESA anakuangalia usoni, hazungumzi, lakini unajua kuwa kuna changamoto za upatikanaji fedha za kutosha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeenda kule kwa Mheshimiwa Waziri Aweso, Jimboni kwake, kuna kivuko pale kimekaa muda mrefu hakuna pesa. Tumeenda Kigamboni pale, tumeona kuna geti la Kigamboni, hakuna pesa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tunaomba sana. Mbunge wa Mwibara ananiambia hapa, TEMESA hawana hela. Sasa TEMESA ikikosa pesa hata magari yenu, V8 hizi, yote yanakuwa kwenye changamoto kubwa sana ya kupata service na ni hatari kubwa kwa sababu, hata mimi kule Kilombero nina TEMESA. Kwa hiyo, haya nilikuwa ninazungumza kwa ujumla Mheshimiwa Waziri, kutoa maoni yangu, lakini kwenye jimbo langu, specific, unajua na kwenye kamati nimesema kuhusu Mangula Kona, Mheshimiwa Waziri, na umetuahidi utaisaidia kufanya kazi.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninapata mashaka sana ninavyosikia baadhi ya wakandarasi wanahofia kuukata mlima kwamba, utamumunyuka na wakati tuna wakandarasi wasomi wazuri. Katibu Mkuu wa Wizara ni Engineer mzuri, Engineer Besta yupo pale, Engineer wetu Mkumbo ni Engineer mzuri kabisa, ambaye anasimamia Mkoa wa Morogoro vizuri sana na ameniambia ameshaandika kitaalam kuhusu hiyo Barabara ya Mangula Kona. Ikikupendeza, wakati unajibu, Mheshimiwa Waziri, ukiizungumzia hiyo Mangula Kona utakuwa umenipa faraja kubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine, ni taa za barabarani. Mheshimiwa Waziri, kwa kumalizia, kuna hoja ya taa za barabarani; tuliahidiwa katika Mji wa Ifakara, Jimbo la Kilombero. Ninaomba sana taa hizo zifanyiwe kazi.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba kuunga mkono hoja na ahsante sana. (Makofi)