Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ujenzi kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

Hon. Ritta Enespher Kabati

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ujenzi kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

MHE. DKT. RITTA E. KABATI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ili niweze kuchangia jioni hii ya leo. Nami ninaomba nimtangulize Mwenyezi Mungu katika mchango wangu na nianze kabisa kumpongeza Mheshimiwa Rais wetu Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kazi kubwa ambayo ameendelea kuifanya, kuhakikisha miundombinu Tanzania inakuwa ya uhakika na kuwatendea haki wananchi wote wa Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ninawaomba Watanzania wote sasa kwa kila mtu kwa dini yake aweze kumwombea Mheshimiwa Rais wetu ili tuweze kumpa kura za kishindo, kura za uhakika kwa kazi nzuri ambayo amekuwa akiifanya katika nchi yetu. Niendelee kumpongeza Waziri wetu Mheshimiwa Abdallah Ulega, kwa kweli kwa kazi nzuri ambayo amekuwa akiifanya na tuliona moto wake alipoteuliwa tu akaenda Dar es Salaam pale akatoa moto kwa wakandarasi ambao wamekuwa wazembe. Ninaomba moto huo uendelee afike nchi nzima akague miundombinu yote, lakini asiache kuja Iringa na aje katika Wilaya ya Kilolo ili aone miundombinu yote na akague barabara zetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ninampongeza sana pia Naibu Waziri Mheshimiwa Engineer Kasekenya, ambaye amekuwa akifanya kazi nzuri ya kumsaidia Waziri, lakini na kujibu maswali yetu vizuri sana hapa Bungeni. Nisimsahau pia ninampongeza Katibu Mkuu Balozi Engineer Aisha, kwa kweli nikupongeze kwa sababu ni mama ambaye ameonesha anaweza, hii Wizara siyo mchezo mchezo ni Wizara dume, lakini wewe mwanamke umeitendea haki. Nimpongeze pia Naibu Katibu Mkuu Engineer Masonde ambaye kwa kweli na yeye kwa kipindi kifupi ameunganisha nguvu sana katika Wizara hii. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nitakuwa sijamtendea haki Meneja wangu wa Mkoa wa TANROADS, Engineer Msangi kama sitakuwa nimempongeza amekuwa ni kaka ambaye amekuwa akitujali hata Wabunge wa Viti Maalum akitusikiliza na kuendelea kufanya kazi pamoja. Kwa hiyo, ninampongeza ninamshukuru sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba mchango wangu sasa niuelekeze katika Kiwanja cha Nduli cha Iringa. Ninawapongeza sana Serikali ninaishukuru sana, sasa hivi tayari hata ndege zimeanza kutua katika Uwanja wetu wa Iringa pongezi nyingi sana kwa Serikali. Mheshimiwa Rais alikuja kuzindua na sasa hivi ndege zimeanza kutua. Nimpongeze pia Waziri wa Uchukuzi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niombe kitu kimoja kwamba pale bado jengo la abiria halijajengwa, tunaomba waje wajenge na tower lakini pia kuna Shule ile ya Nduli ambayo kwa kweli watoto wamekuwa wakipata shida sana, hata Mbunge alichangia asubuhi, ninaomba wale watoto waletewe pesa kwenye Halmashauri iondolewe kwa sababu wamekuwa wakipata shida hata ufaulu wao sasa unapungua. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nipongeze pia ujenzi wa Barabara ya Msembe, ambayo inakwenda Ruaha National Park. Kwa kweli, tunawashukuru sana kwa sababu, sasa hivi itajenga uchumi mkubwa wa Iringa na nchi nzima, lakini utalii na kazi zitaongezeka; wananchi wengi watajiajiri kupitia utalii katika Mkoa wetu wa Iringa. Niombe sasa fidia zilipwe kwa wakati, ili hii barabara iweze kujengwa wakati fidia za wananchi hawa wa Msembe zikiwa zimeshalipwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, niielezee Barabara ya Kitonga. Hii barabara nimekuwa nikiiulizia mara nyingi sana, ni barabara muhimu sana kwa uchumi wa nchi yetu ya Tanzania, lakini barabara hii inaunganisha uchumi na Lango la nchi za SADC, lakini ujenzi wake umekuwa ukisuasua sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hii barabara magari yanakwama kuanzia saa tatu, nne, saa sita, hata siku nzima. Tunaomba sasa utakapokuwa unajibu, Mheshimiwa Waziri, utuambie suluhisho ni nini?

Mheshimiwa Mwenyekiti, tulikuwa tumeshaomba, ikiwezeka, kuna barabara ile inayotoka Mahenge – Udekwa – Wotalisoli – Mlafu mpaka Ilula, utuambie suluhisho la hii Barabara, wananchi wanateseka sana. Nitashika shilingi kesho kama sitapata jibu la uhakika. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nipongeze barabara inayojengwa kutoka Iringa kwenda Kilolo kwa sababu, inaunganisha Majimbo matatu, Iringa, Kilolo na Kalenga. Kwa hiyo, ninawashukuru sana, lakini ninaomba sasa, ikiwezekana ijengwe pia, kutoka Kilolo – Kibaoni – Dabaga kwa njia ya lami ili kuweza kusaidia uchumi wetu wa Kilolo. Pia ombi langu lingine ni Barabara ile ya Dabaga – Nang’ange mpaka Boma la Ng’ombe; hii barabara imekuwa ikipitisha magari makubwa sana. Niombe, sasa hivi hii barabara ipelekwe kwenye hadhi ya mkoa iweze kukarabatiwa kila wakati ili uchumi wa Kilolo usiweze kukwama. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tunayo Barabara nyingine ambayo inatoka Dabaga – Itonya – Muhanga inakwenda mpaka Morogoro. Tunaomba hii barabara sasa ifunguliwe ili iweze kufungua uchumi wa hii mikoa miwili, itakuwa inawasaidia wananchi wengi sana kiuchumi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna Barabara hii ya Ilula – Mlafu – Wotalisoli – Mkalanga, inapita Kising’a inakwenda mpaka Kilolo, Makao Makuu, hii barabara ni ya kisiasa, lakini pia ni ya kiuchumi. Tunaomba sasa hii barabara, hata kutokana na ufinyu wa bajeti, ikarabatiwe iweze kupitika kila wakati kwa sababu, sasa hivi kufika Makao Makuu ya Wilaya ya Kilolo wananchi wanazunguka, wanakwenda mjini ndiyo waende Kilolo. Ninaomba hii barabara iangaliwe kwa uzito wake na ikiwezekana ijengwe kwa kiwango cha lami. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niipongeze pia, Serikali kwa utaratibu wa ujenzi wa PPP. Tunayo ile Barabara ya Mafinga – Mtiri – Mgololo, hii barabara ilikuwa ijengwe kwa Utaratibu wa EPC+F, lakini hatutajua itajengwa kwa utaratibu gani. Hii barabara pia, ni ya kiuchumi, kuna viwanda vya chai. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho kabisa, ninaomba sasa wakandarasi walipwe madeni yao kwa sababu, wanapolipwa pia na miradi mingi inakuwa inajengwa kwa haraka. Tunaomba, wamefanya kazi nzuri sana katika nchi hii, lakini wakandarasi wa ndani wajengewe uwezo kwa kulipwa mapema na barabara zetu ziweze kupitika muda wote. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho kabisa niombe, hii Barabara ya Dodoma – Iringa ijengwe upya kwa sababu, viraka ni vingi mno. Kila sehemu viraka, kila sehemu viraka, sasa hii barabara ijengwe yote. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana na ninaunga mkono hoja. (Makofi)