Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. SYLVIA F. SIGULA: Mheshimiwa Naibu Spika, ninakushukuru sana kwa kunipa nafasi. Nianze kwa kumshukuru Mungu mwingi wa rehema kwa kuniwezesha leo kusimama katika Bunge lako hili Tukufu.
Mheshimiwa Naibu Spika, nianze kwanza kwa kumpongeza Mheshimiwa Rais, kwa kazi kubwa sana anayoifanya hasa katika Sekta hii ya Miundombinu. Ni hapa katikati tu nchi yetu imepita katika changamoto nyingi za kuwa na mvua nyingi, lakini Mheshimiwa Rais alipambana na kuhakikisha Wizara hii inapata fedha na kwenda kutatua changamoto za wananchi, ninampongeza sana Mheshimiwa Rais. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa namna ya pekee sana ninapenda nimpongeze Mheshimiwa Waziri, Mheshimiwa Naibu Waziri, Katibu Mkuu pamoja na timu nzima. Sisi wote ni mashahidi tunaona namna ambavyo wanapambana huko barabarani kuhakikisha kwamba Sekta hii ya Ujenzi inakuwa imara. Tunawapongeza sana Mheshimiwa Waziri pamoja na timu yake nzima. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na pongezi zote hizo ambazo nimezitoa, tunatambua kuwa maendeleo ni hatua na nchi yetu katika Sekta ya Ujenzi tumeona watu wengi wanapenda sana kubeza, lakini sisi Wajumbe wa Kamati tumezunguka nchi nzima, tumeona miradi mingi na mikubwa ambayo inafanywa na Serikali hii kwa kweli tunawapongeza sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hapa ningependa sana niongee na Watanzania niwaambie tunapenda sana kuwa watu wa kulaumu ka kudharau vya kwetu, lakini leo sisi Kamati ya Miundombinu tumepokea Wabunge kutoka nchi za wenzetu wanakuja kujifunza Tanzania ni namna gani tunatekeleza miundombinu yetu. Kwa hiyo, niwaombe sana Watanzania tuwe na tabia na tamaduni ya kujali vya kwetu na kuvipenda. Tanzania kwenye Sekta ya Ujenzi tunafanya vizuri sana na ninawapongeza sana Mheshimiwa Waziri. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, niungane na maoni na mapendekezo ya Kamati na hapa katika changamoto ambazo Kamati ilizibaini, ningependa sana kuzungumzia suala la ulipaji wa fidia kwa wananchi wanaopisha maeneo hasa kwenye miradi hii ya barabara. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, wananchi wa Tanzania ni waelewa na maeneo mengi Serikali imekuwa ikiyataka kwa ajili ya kufanya uendelezaji ili kuleta maendeleo na wananchi bila wasiwasi wametoa maeneo yao ili kuhakikisha miradi hii hasa ya barabara inatekelezeka katika nchi yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa kumekuwa na changamoto ambayo sisi kama Kamati tumezungumza kuanzia Bunge hili limeanza mpaka hili Bunge la mwisho na majibu ya Serikali yamekuwa ni kwamba wanafanyia kazi. Ukiangalia maeneo ambayo wananchi wametoa kwa ajili ya ujenzi wa barabara na hapa ningependa nitumie Rukwa kama case study lakini ni maeneo nchi nzima. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna barabara nyingi ambazo wananchi wamepisha ili zitengenezwe, lakini wananchi wale mpaka leo bado hawajapewa fidia zao na kwingine wanakwenda zaidi ya miaka 10, miaka 15 na miaka 20. Tunaona kabisa hili si sawa kabisa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, suala la fidia kwa wananchi waliotoa maeneo yao siyo hisani, hii ni haki yao wanapaswa kupewa kwa wakati na wanapaswa kupewa fidia iliyo kamili. Sasa leo ukienda Mkoa wa Rukwa ukianzia Wilaya ya Nkasi, Wilaya Kalambo na Wilaya ya Sumbawanga kote utakutana na malalamiko ya wananchi wanaodai fidia kwa Serikali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa ningependa nizitaje barabara hasa ukienda Chala pale zaidi ya nyumba 40 zimevunjwa na wananchi zaidi ya miaka 10 hawajapewa fidia zao. Wananchi hao wanaumia wana mapenzi na Serikali yao, lakini wanaumia kwa sababu hawatendewi haki. Kwa hiyo, ningependa sana Mheshimiwa Waziri…
MHE. VINCENT P. MBOGO: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa.
NAIBU SPIKA: Taarifa.
TAARIFA
MHE. VINCENT P. MBOGO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi. Nipende kumpa Mheshimiwa Sylvia taarifa Mji Mdogo wa Chala ambao sema kuna wananchi zaidi 40 ambao wanadai fidia zaidi ya miaka 11. Wananchi hao wamekuja, kila siku wana kikao, taarifa ambayo amejibiwa na TANROADS ni upotoshaji. Silaumu TANROADS, lakini ni taarifa ambayo hapa katikati haina uhakika wa kuwapa haki yao, haki yao inataka kunyang’anywa nao hao viongozi ambao wanaongoza kunyimwa haki yao ni Mzee Kilokoto na Mzee Kailinyi katika Mji Mdogo wa Chala.
NAIBU SPIKA: Sasa Mheshimiwa Mbogo, hiyo ni taarifa au unachangia? Wewe mpe taarifa Mheshimiwa Waziri alifanyie kazi, Sawa?
MHE. VINCENT P. MBOGO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. (Makofi)
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Sigula.
MHE. SYLVIA F. SIGULA: Mheshimiwa Naibu Spika, kama ambavyo nimesema Mkoa wote wa Rukwa tuna changamoto hiyo na hata ukienda Wilaya ya Sumbawanga DC, kuna barabara ambazo zimepita ukianzia Barabara ya Muze -Ntendo pale kuna wananchi wametoa maeneo yao zaidi ya miaka 10 hawajapewa fidia. Pia kuna Barabara ya Kalambanzite kwenda Ilemba pale kuna wananchi wanadai fidia, lakini kuna barabara ya Ntendo - Luwa pale kuna wananchi pia wanataka fidia. Kwa hiyo, niombe sana Mheshimiwa Waziri na hii tunaiongea tukiwa serious, tukiwa tunamaanisha. Kwa kuwa, hili ni Bunge la Mwisho ninapenda Waziri atakapokuja kutoa majumuisho aje na majibu ya msingi kutaka kujua hatma ya hawa wananchi na kama Serikali bado hatujajipanga kuwalipa fidia basi tuwarejeshee maeneo yao tutakapokuwa tayari tutayachukua tena ili wananchi hawa waweze kuendeleza maeneo yao kwa sababu wamekaa kwa muda mrefu hawajui wafanye nini hawaruhusiwi kuendeleza maeneo yao.
Mheshimiwa Naibu Spika, sheria inataka wasipolipwa kwa wakati kila mwaka iongezeke riba ya asilimia sita, kama Serikali hii pia itakuwa ni hasara kwetu. Kwa hiyo, ninaomba sana Mheshimiwa Waziri utakapokuja kutoa majumuisho uje na majibu kuhusu hawa watu wa fidia za maeneo yao. Ninakushukuru kwa nafasi na ninaunga mkono hoja. (Makofi)