Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ujenzi kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

Hon. Miraji Jumanne Mtaturu

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Singida Mashariki

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ujenzi kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

MHE. MIRAJI J. MTATURU: Mheshimiwa Naibu Spika, ninakushukuru kwa kunipa nafasi nianze kuchangia hoja iliyopo mezani kwetu, hoja ya Bajeti ya Wizara ya Ujenzi kwa mwaka wa fedha 2025/2026 kama ilivyowasilishwa na Mheshimiwa Waziri mahiri kabisa Ndugu yetu Abdallah Ulega.

Mheshimiwa Naibu Spika, nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema kunijalia uzima na kuweza kusimama mbele ya Bunge lako Tukufu kuweza kuchangia hoja iliyopo mezani. Pili, nichukue nafasi hii kumpongeza na kumshukuru sana Mheshimiwa Rais, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kazi kubwa anayofanya katika kuongoza Taifa letu na zaidi katika sekta hii ameitendea haki kwani fedha nyingi zimetoka ambazo zimetekeleza miradi kama ambavyo Mheshimiwa Waziri ameeleza. Ni dhamira ya dhati ya Mheshimiwa Rais katika kuhakikisha kwamba miundombinu ya nchi hii inatekelezwa kwa vitendo kama ambavyo iliahidiwa kwenye Ilani ya Chama Cha Mapinduzi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nichukue nafasi hii kumpongeza Waziri ndugu yetu Mheshimiwa Abdallah Ulega pamoja na Naibu Waziri ndugu yetu Mheshimiwa Engineer Kasekenya, Katibu Mkuu pamoja na Watendaji wote kwa kazi kubwa ya kusimamia Sekta ya Ujenzi ambayo kimsingi ni sekta inayochochea maendeleo ya sekta zingine. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kazi kubwa wanayoifanya na hata Mheshimiwa Ulega, tulimwona kule Kusini akisimamia kwa dhati kazi ambayo ilikuwa imefanyika pale tatizo kubwa lililotokea la kuchukuliwa madaraja pamoja na barabara kufungwa alikaa takribani siku nne kuhakikisha kwamba wananchi wa Kusini wanaenda kupata mawasiliano. Hongera sana Mheshimiwa Waziri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya shukrani na pongezi hizo na mimi ninapongeza sana nimeona barabara zimejengwa katika taarifa madaraja lakini kama ambavyo haitoshi tumeona zaidi ya 66% imetoka kwa ajili ya kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo, nami nikiwa Mjumbe wa Kamati hii tumeendelea kuona taarifa mbalimbali na tumetembelea miradi, tumeona mpaka Daraja la Pangani, tumeona Daraja lile la Kigongo Busisi ambalo leo sasa hivi limefikia 99% wananchi wale wa Kanda ya Ziwa wanaenda kufaidika na daraja lile ambalo ni refu kuliko lolote katika Ukanda huu wa Afrika Mashariki na Kati. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwetu kama Tanzania tunajivunia sana kuwa na mradi mkubwa kama ule na fedha Serikali imetoa hivi tunavyoongea hali inaenda vizuri, hivi karibuni wataenda kuzindua, tunaipongeza sana Serikali kwa dhamira ya dhati katika eneo hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, zaidi nipongeze kwenye eneo hili la Chuo ambacho kipo pale Morogoro Taasisi ya Teknolojia ya Ujenzi (ICoT). Chuo hii ni muhimu sana, tumekitembelea mwaka juzi na mwaka huu tulivyoenda kutembelea tumekuta wameshatenga fedha na jengo limeanza kujengwa wametenga zaidi ya shilingi 2,000,000,000 ambazo kimsingi majengo haya yakiboreshwa kile chuo kitarudi kuwa na hadhi yake ambayo inastahili kwa sababu itaenda kuandaa mafundi ambao ni mafundi wa kati, wale artisan ambao ni watenda kazi katika Sekta ya Ujenzi ambao kwenye maeneo mengi wanapotea. Kwa maana ya Serikali kuendelea kukiboresha chuo kile inaonekana dhamira yake ya kuendelea kuwaandaa mafundi wa kati ambao watakuwa ni kichocheo cha shughuli za ujenzi katika nchi yetu. Tunampongeza sana Mheshimiwa Waziri kwa kazi kubwa mnayoifanya pale Morogoro ya kuboresha chuo kile ambacho kimsingi kinarudi kwenye heshima yake. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ninaendelea kuomba na kushauri tusije tukawaza kuanza kufikiria kianze kuchukua watu wa digrii kibaki vilevile ili tuweze kupata mafundi wa kati ambao wataenda kusaidia kwenye sekta ya ujenzi. Kwa sababu hawa wanaomaliza digrii wengi ni mameneja lakini hawa ambao tunawapata kwenye chuo kile wanakuwa ni watenda kazi ambao wataenda kufanya kazi kwenye maeneo mbalimbali ikiwemo kwenye reli na maeneo mbalimbali. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la tatu, ninaipongeza Serikali kwenye jukumu la kuweza kupunguza foleni Dar es Salaam, tumeenda kutembelea BRT pale tumeona miradi mbalimbali inafanyika tumeona commitment ya Serikali katika kuhakikisha kwamba Mji wa Dar es Salaam unafunguka ni mji wa kibiashara ule. Kupunguza mwendo wa watu kwenda kwenye maofisi na kwenda kwenye huduma mbalimbali kumaliza zile barabara kwa maana ya mwendokasi pale Dar es Salaam. Ni mradi ambao ni muhimu sana tumeona hata wa Gongo la Mboto sasa pana funguka ili watu waweze kwenda haraka kwenye shughuli zao za kiuchumi.

Mheshimiwa Naibu Spika, niendelee kuomba jambo moja tu Mheshimiwa Waziri, tuhakikishe kwamba miradi ile inakwenda kwa kasi ili kazi iishe. Hivi tunavyoongea kuna baadhi ya maeneo imefunga inasubiri tufungue ili watu waendelee na shughuli zao. Kwa hiyo, kwa sababu ujenzi unaendelea maeneo mengi yamefungwa, kwa hiyo imekuwa tena ni tatizo katika Mji wa Dar es Salaam. Tuwaombe wakandarasi waongeze kasi kama tulivyoshauri kwenye Kamati ili tuhakikishe kwamba lengo letu linatimia la kupunguza ile foleni pale Dar es Salaam. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kama haitoshi Mheshimiwa Waziri nilikuwa nimeulizia suala la EPC+F nimeona kwenye hotuba yako umeeleza kwamba mme-review upya mpango huo sina haja ya kurudia lakini wananchi walikuwa wanataka kujua mwisho wa miradi hii kwa sababu ni kilomita zaidi 1,035.

Mheshimiwa Naibu Spika, hili specific niongelee hii barabara ya Handeni - Kibirashi kuja Kwa Mtoro mpaka Singida. Nimefurahi ameeleza na nimpongeze Mheshimiwa Rais kwa kuona namna ambavyo ameamua kwamba sasa ujengwe kwa upande wa PPP ili isaidie kwenda haraka kuweza kuunganisha na Bandari ya Dar es Salaam ambayo tumewekeza zaidi ya shilingi bilioni 421 ili thamani ya fedha tuipate. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tunaomba twende haraka hiyo barabara tunahitaji sana tunaisubiri mikoa zaidi ya minne, lakini itawasaidia wateja wanaotoka Bandari ya Dar es Salaam kwenda haraka kupeleka mizigo yao kwenye Mikoa ya Magharibi. Kwa hiyo, niombe sana Mheshimiwa tunaomba hii barabara kilometa 460 iweze kujengwa haraka na wenzetu wa TANROAD pamoja na TPA wamalize mchakato wa mazungumzo ili tuweze kuona matokeo na hamu ile ya Mheshimiwa Rais iweze kutimia. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, zaidi niongelee barabara yangu Mheshimiwa Waziri, Ikungi - Mang’onyi – Londoni kwenda Solya. Barabara hii wameanza kutujengea pale Ikungi wametujengea kama kilometa tatu hivi mpaka hospitali ya Wilaya na pale Halmashauri. Tunaomba wakitujengea kama kilometa 50 kwenda mpaka kwenye Mgodi wa Shanta ambao unazalisha fedha nyingi na kodi inatoka pale ili tuweze kuweka lami kuondoa vumbi ambalo linatimka kwa sababu magari mengi yanatumia ile barabara ili kusaidia afya ambazo zinaharibika za wananchi wetu, kuweka lami itasaidia kuongeza kasi ya uchumi. Wananchi watafaidika na mradi ambao umeweka pale kwa ajili ya kuleta uchumi mkubwa kwa wananchi wetu. Kwa hiyo, barabara hii pia tunaisubiri tunaomba Waziri atusaidie sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho, ni suala la Mfuko wa Barabara, ninaomba sana fedha ambazo zinatengwa ziende kwenye maeneo yale kwa ajili ya kuboresha barabara ambazo zimeharibika nchini kwetu, kama Barabara ya Dodoma kwenda mpaka Singida imekufa kabisa. Tunaomba Waziri aiangalie kwa jicho la pekee. Baada ya maneno haya, ninaunga mkono hoja asilimia mia moja ili tuweze kuendeleza kazi nzuri waliyofanya. Ahsante sana. (Makofi)