Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ujenzi kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

Hon. Jesca Jonathani Msambatavangu

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Iringa Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ujenzi kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

MHE. JESCA J. MSAMBATAVANGU: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi. Nami nichukue fursa hii kwanza kabisa kumpongeza Mheshimiwa Waziri kwa hotuba nzuri na nia njema ya Wizara ya Ujenzi pamoja na Serikali kuhakikisha kwamba miundombinu katika nchi yetu inaboreshwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaungana na Wizara kwa kauli yao kwamba bajeti yao itaendana pamoja na kazi na utu. Nami ninawapongeza kwa sababu utu wameshaanza kuonesha kwa kiasi kikubwa. Mambo mengi yaliyofanyika kwenye sehemu mbalimbali katika nchi yetu katika Wizara hii yanaonesha utu. Yanaonesha kwamba mna ana nia ya dhati ya kuhakikisha Watanzania wanakuwa vizuri kiuchumi na shughuli zao za maendeleo na za kijamii zinaendelea kila siku. Kwa hiyo, ninawapongeza sana na kwa niaba ya wananchi wa Iringa, kwanza kabisa niwapongeze. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niliposimama hapa kwa mara ya kwanza mwaka 2020 niliongelea Barabara ya Ruaha National Park na nikaitengenezea art ambapo niliongeza masuala ya utelezi na ikanipa pia nickname kuitwa utelezi. lakini sasa wameonesha utu wa dhati kwa kutupatia barabara ile ambayo inakwenda kuchachamua uchumi wa wananchi wa Mikoa ya Kusini kwa kuendelea kuchachamua utalii wa Nyanda za Juu Kusini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunawashukuru sana kwa barabara ile tulii-sign na tunaona kwa kweli kuna maandalizi yanaendelea. Tunaisubiri kwa hamu kubwa sana ile Barabara ya Ruaha National Park kilomita 104 na zaidi ya hapo kwa kuendelea kutu-connect kwenye utalii. Tunawashukuru sana pia, kwa ujenzi wa barabara ya lami ambao umeanza kuanzia Iringa mjini kuelekea Kilolo kilometa 33.7.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue nafasi hii pia kuwashukuru kwa kutaka kuufanya mji wa Iringa, kuwaongezea utu wananchi wangu wa Iringa Manispaa kwa kuwatengenezea Iringa bypass kilometa 7.3. Tunajua wamejenga mita 450, tunashukuru lakini tunafahamu vile ni vigongo ni milima mikali sana inayopasuliwa. Madaraja saba wameyakamilisha, ninashukuru kwamba walipoona mkandarasi anasuasua wamefanya tena revisit ya kutupatia Mkandarasi mzuri na Februari walitupatia tena shilingi bilioni nne kwa ajili ya barabara ile.

Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara ile kwetu sisi ni ya muhimu sana, hasa kwa kufanya Mji wa Iringa uendelee kuwa lango la Utalii Kusini, hasa kwa kuangalia vivutio au kuangalia miundombinu ya utalii inayowekwa katika Mji wetu wa Iringa ikiwepo kivutio cha Kihesa Kilolo. Kwa kweli tunahitaji malori makubwa yanayokatisha katika Mji wa Iringa yakiwa yamebeba mbao na makaa ya mawe yakielekea mikoa sita ya Kaskazini, mikoa sita ya Kanda ya Ziwa na kwenda kwenye nchi nyingine za jirani za Tanzania ambazo zipo Kaskazini, tunaomba sana malori yale yasiendelee kukatisha katikati ya Mji wa Iringa, yapite Iringa bypass. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba sana Iringa bypass ikamilike wakati wanaendelea kupigapiga ili pale tusiendelee kuleta maneno mengi sana na watumiaji wengine wa kimataifa wa barabara ile, basi tunaomba waangalie namna ambavyo barabara nyingine za mchepuo zinaweza zikawekwa katika mji wa Iringa, kwa kuwa ni malengo yao kuangalia miji inayokua kwa haraka ingawa Iringa hawajaitaja, lakini Iringa ni moja ya mji unaokua kwa haraka sana ingawa ni Manispaa. Tuendelee kuwa na barabara za mchepuo ambapo wakitupatia ile Wilolesi ambayo tumeomba pia kama kilomita ngapi hivi ili ipite mchepuko basi watu wasiendelee kutumia ile barabara kubwa tuachie magari makubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninawashukuru pia kwa ajili ya Barabara ambayo inaanzia Iringa kwenda Itunundu - Pawaga ambayo ni kilometa zaidi ya 71.9. Wametupatia pale Iringa kwamba tutakuwa na Ikonongo - Pawaga kama kilomita tano wanatupatia. Tunaomba sana hizo kilomita tano mapema, kwa sababu wananchi wenzetu wa Jimbo lingine lile la Kalenga wanatumia sana huduma za kijamii zilizopo Iringa Manispaa, zikiwepo shule pamoja afya kama vituo vya afya pamoja na hospitali za wilaya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakitupatia zile kilomita tano watatusaidia sana wale akinamama wengi wanaowahishwa kuja kwenye hospitali yetu ya rufaa ya Mkoa Iringa na ile ya wilaya watakuwa wakija vizuri sana na ndiyo utu wenyewe kuhakikisha kwamba akinamama wanapokuwa wanaongeza wapigakura wa Taifa hili wanasafiri kwenye sehemu salama ikiwepo barabara ya lami.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru sana pia kwa kuendelea kutambua kampuni zile za Mtwivila, GSM zilizopo Iringa lakini utu sasa ni kuhakikisha wale pia wanalipwa jamani, wanalipwa fedha zao wanazotudai, kwa sababu wale wana network kubwa. Huku wana watu wanaowauzia nondo, wale wenye nondo wameajiri watu, wale nao wanasomesha watoto. Kwa hiyo usipomlipa mkandarasi, kuna mnyororo mkubwa wa watu wengi huku ambao wanaendelea kupata shida.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo utu ni kuhakikisha ule mnyororo mzima unao mtegemea mkandarasi wa Tanzania unakuwa na wenyewe una utu, unapata hadhi unajisikia raha kuendelea kuishi katika Taifa hili kwa kuwalipa wakandarasi ili yeye mkandarasi akalipe dukani, ili yule mtumishi wa dukani naye aweze kumhudumia mke wake, ili mke wake naye aweze kupika vizuri watoto wapate afya nzuri tusiwe tena na watoto waliodumaa, huo nao ni utu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninamshukuru sana Mheshimiwa Waziri. Katika viwanja vya ndege ambavyo wamejenga katika nchii hii ni Uwanja wa Ndege wa Iringa ambao umekamilika kwa 93%. Tunaomba kile kipande kilichobaki kwa ajili ya jengo la abiria na tower ya kuongozea, waanze kuijenga haraka kwa sababu ndege kubwa zimeshaanza kushuka katika Mji wa Iringa. Sasa bado tunakosa jengo la abiria na ile tower kubwa ya kuongozea ndege.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunawashukuru, lakini ndani ya Uwanja wa Ndege wa Iringa tuna Shule ya Msingi moja pale, Imeche ipo ndani ya uwanja wa ndege. Nimeongea sana na Waziri wa Elimu, nimeongea na TAMISEMI, nimechangia kwa maandishi TAMISEMI, ninaomba tena nimwambie Mheshimiwa Waziri wa Ujenzi, kwa sababu ndiye aliyekuwa na dhamana ya kutulipa fidia katika ile shule, tunaomba shule ile ihame ndani ya uwanja wa ndege iende nje ya uwanja wa ndege. Huo nao ni utu, kuwafanya watoto wale wasipate mapresha ya ndege kubwa zinaposhuka, lakini wasome katika mazingira ambayo ni mazuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru sana na ninaunga mkono hoja. (Makofi)