Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ujenzi kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

Hon. Omari Mohamed Kigua

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kilindi

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ujenzi kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

MHE. OMARI M. KIGUA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza ninachukua nafasi hii kumshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema ambaye amenipa nafasi na uhai kwa siku ya leo kuweza kusimama katika Bunge lako Tukufu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, halikadhalika ninakushukuru wewe kwa kunipa nafasi. Nichukue nafasi hii kumpongeza sana Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, naye si mwingine ni Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, ambaye kwa hakika ameweza kuisimamia nchi hii na kutuongoza vizuri na hakika tuseme kwamba tumepiga hatua kwa sababu ya uongozi wake bora sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, halikadhalika nichukue nafasi hii kumpongeza Waziri wa Ujenzi ndugu yangu Mheshimiwa Ulega, Naibu Waziri Mheshimiwa Engineer Godfrey Kasekenya, Katibu Mkuu Mheshimiwa Balozi Aisha na Naibu Katibu Mkuu ndugu yangu Msonde. Wote kwa pamoja wamekuwa wakifanya kazi nzuri. Tumekuwa tukiwaona wakitokea katika maeneo mbalimbali ku-rescue situation pale pahali ambapo barabara zimekuwa zikiharibika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimesimama leo mbele ya Bunge lako Tukufu niweze kumpongeza kwa dhati kabisa Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kauli yake aliyoisema pale Tanga siku anamalizia ziara yake Bandari ya Tanga. Alisema maneno yafuatayo:-

“Ninakuelekeza Waziri wa Ujenzi na Waziri wa Uchukuzi, muone kwa namna gani mnaweza mkaisimamia Barabara ya Handeni – Kibirashi – Singida ijengwe kwa utaratibu wa PPP”. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, yale yalikuwa ni mawazo makubwa yenye busara ya hali ya juu sana. Sote tunatambua kwamba Serikali hii ya Mheshimiwa Dkt. Samia imewekeza shilingi billioni 421 kwenye Bandari ya Tanga. Huu ni uwekezaji mkubwa sana. Utazirejesha fedha hizi kubwa kama barabara hiyo ambayo inaunganisha mikoa minne, kwa maana Mkoa wa Tanga, Mkoa wa Manyara, Mkoa wa Dodoma na Mkoa wa Singida haijaunganishwa kwa kiwango cha lami? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, halikadhalika, barabara hii ndiyo ambapo Bomba la Mafuta la ule Mradi unaotoka Hoima hadi Chongoleani – Tanga linapita. Sasa, ni barabara ambayo kwa hakika ina uhitaji mkubwa sana wa kujengwa kwa kiwango cha lami. Hatuwezi tukaacha kuijenga kwa kiwango cha lami kwa sababu kwa sasa hivi haipitiki. Mikoa yote ya Kaskazini yote inategemea barabara hii, lakini kipindi cha mvua inakuwa haipitiki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninamwomba sana Mheshimiwa Waziri, hebu walisimamie elekezo hili la Mheshimiwa Rais. Uzuri ninampongeza kwamba ameisemea, sasa isibaki tu maneno Mheshimiwa Waziri, hebu nendeni mkakae kwa pamoja na Waziri wa Uchukuzi, waweze kuijenga barabara hii iweze kupitika kwa sababu economic viability yake ni kubwa sana. Tunatarajia shilingi bilioni 421 ziweze kurejeshwa ziweze kutengeneza barabara nyingine katika nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine ambalo ninataka kuchangia kwa siku ya leo ni barabara ambayo Mheshimiwa Shangazi ameizungumzia, Barabara ya Chalinze – Segera. Ni barabara ambayo ilijengwa miaka ya 1980. Lifespan yake imekwishapita, na barabara hii siku za karibuni hasa maeneo ya Segera pale na maeneo ya Mkata kumekuwa kunatokea ajali mara kwa mara barabara hii imekuwa finyu. Watanzania wa miaka ile, idadi ya magari ya miaka ile sasa hivi magari ni mengi sana; shughuli za kiuchumi ni nyingi sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kweli kuna umuhimu sasa kwa wenzetu wa Wizara ya Ujenzi, mwangalie ni namna gani ambavyo wanaweza wakatafuta fedha waweze kuijenga au kuikarabati upya. Nimeona amezungumzia Barabara ya Kusini kuanzia kwake Mkuranga kwenda Mtwara. Upo umuhimu kwa sasa hivi kuiangalia barabara hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaishukuru Serikali hii ya Awamu ya Sita na Serikali Awamu ya Tano walijenga Daraja la Wami ambayo ilikuwa changamoto kubwa sana, tunashukuru. Sasa daraja lile lazima liende sambamba na kupanua Barabara hii ya Chalinze hadi Segera kwa sababu shughuli za kiuchumi ni nyingi, magari ni mengi. (Makofi)

Mheshimiwa Mweyekiti, nimwombe sana na wataalam wanasema, mimi si injinia. Wataalam wanasema barabara ikichukua muda mrefu sana, ile lifespan yake ikiisha maana yake atakapokuwa amechelewa zaidi, gharama ya kuja kuijenga upya itakuwa ni gharama kubwa sana. Twende tuepuke hilo Mheshimiwa Waziri, twende tuweke fedha tuweze kuijenga barabara hii iweze kuwa vizuri zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikienda kwenye eneo langu la Wilaya ya Kilindi, ninakuomba Mheshimiwa Waziri; wakati tulikuwa na mpango wa kujenga Barabara hii ya Handeni – Kibirashi – Singida tuone umuhimu sasa wa kujenga Barabara ya kuunganisha sasa kutoka Kibirashi kwenda Makao Makuu ya Wilaya Songe, ije iunganishe na Barabara ya Ngiloli hapa Gairo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni barabara ambayo ni shortcut na ambayo wananchi wengi wa maeneo hayo wataitumia. Hata wale wanaotoka Dodoma kwenda Tanga mara nyingi wanaitumia barabara hiyo. Mheshimiwa Waziri ninaomba alichukue eneo hilo na alifanyie kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri, ameamua kujenga Madaraja ya Chakwale na Nguyami. Wametenga fedha nyingi sana. Madaraja yale yamekuwa na usumbufu kwa muda mrefu na madaraja yale ninataka niseme kwa ujumla kwamba, baada ya kukamilika yatasaidia wafanyabiashara, yatasaidia wakulima kuweza kupitisha mazao yao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeona mkandarasi yuko site; ninaomba wawasimamie vizuri madaraja hayo yakamilike ili yaweze kupanua shughuli za kiuchumi na halikadhalika za kibiashara kwa wananchi wetu ambao wanaitumia barabara hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho, niseme jambo moja kuhusu madeni kwa wakandarasi wetu. Upo umuhimu wa kuweka utaratibu. Nimeona wanafanya jitihada za kulipa madeni, lakini spidi iongezeke. Watu hawa baadhi ya wakandarasi wazawa wamekopa katika benki na wanadaiwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ili tusifanye mali zao kuchukuliwa, basi ninyi watu wa Wizara ya Ujenzi shirikianeni na Wizara ya Fedha waweke utaratibu yale madeni ya muda mrefu waanze kuyalipa ili tuwape nguvu Watanzania hawa ambao wana nia nzuri ya kuhakikisha kwamba na wao wanaijenga nchi yao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine nimwombe Waziri wa Ujenzi, mkandarasi yule ambaye wamempa kile kipande cha kilometa 20 kuanzia Handeni kuja Mafureta kilomita 20, kwa kweli anasuasua. Mheshimiwa Waziri amekuja amesema hata Waziri yule ambaye ni mtangulizi wake au wa nyuma alikuja akazungumza jambo hili. Nimwombe sasa, hebu atume timu yake wawasimamie mkandarasi huyu wa Kichina, ambaye hivi ninavyozungumza hayupo site na alikwishalipwa fedha zake zote, haidai Serikali sisi ndiyo tunamdai fedha na kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninamwomba Mheshimiwa Ulega, nina uhakika yeye na timu yake wanaweza kumsimamia mtu huyu aweze kujenga barabara hii. Kwa sababu wananchi wa Wilaya ya Kilindi, wananchi wa Handeni wanahitaji barabara hii na wameisubiri kwa muda mrefu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema haya, nikushukuru sana sana kwa kunipa nafasi. Ninaunga mkono hoja na ahsante sana. (Makofi)