Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ujenzi kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

Hon. Mariamu Nassoro Kisangi

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ujenzi kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

MHE. MARIAM N. KISANGI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi nami niweze kuchangia Wizara hii muhimu, Wizara ya Ujenzi. Kwanza ninamshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuniwezesha siku ya leo kusimama hapa mbele kuweza kuchangia mchango wangu katika Wizara hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, ninapenda kumpongeza Mheshimiwa Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuweza kuitekeleza Ilani yetu ya Chama Cha Mapinduzi kwa asilimia inayozidi 90. Ilani ya CCM Kifungu cha 29A kinasema, “Chama Cha Mapinduzi katika uongozi wake wa mwaka huu (Mwaka 2025) kitaimarisha miundombinu mbalimbali...”, Ninanukuu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, “...kitaimarisha miundombinu mbalimbali pamoja na huduma za bandari, viwanja vya ndege reli, meli, vivuko, gati, na njia za usafirishaji wa umeme. Aidha, mitandao ya barabara za lami pamoja na madaraja mbalimbali yatakayounganisha nchi yetu na nchi nyingine”. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaona jinsi gani Daraja la Kigongo na Busisi linakwenda kukamilika. Daraja hilo muhimu limefanywa na Serikali ya Chama Cha Mapinduzi, kinachoendeshwa na Mwenyekiti wake Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan. Si jambo dogo, ni jambo kubwa sana. Pamoja na hayo, nimeshuhudia madaraja mbalimbali yakijengwa katika Mkoa wetu wa Dar es Salaam. Daraja la Kigamboni, Daraja la Kijazi, Daraja la Mfugale, Daraja la Chang’ombe VETA, Daraja la Kurasini Uhasibu, lakini kivuko cha juu cha Kawe pamoja na miundombinu mingi tu ya Mwendokasi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni mambo makubwa sana yaliyofanywa na Serikali yetu hii ya Chama Cha Mapinduzi. Ninatambua katika Jiji la Dar es Salaam kumekuwa na ongezeko kubwa la watu. Idadi ya watu kulingana na Sensa ya mwaka 2022 ni watu 5,383,728. Kwa nini nimesema hivyo? Idadi ya watu inaenda sambamba na uboreshaji wa miundombinu. Sambamba na idadi ya watu pia kuna ongezeko la vyombo vya barabarani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla sijaanza mchango wangu ninaomba niipongeze Wizara hii. Mheshimiwa Waziri wa Ujenzi, Naibu Waziri, Makatibu Wakuu wote pamoja na watendaji wote wa Wizara hii. Ninawapongeza kwanza kwa kuchukua hatua za dharura katika kurekebisha mawasiliano katika uharibifu wa kwenda pale Rufiji. Walifanya kazi kubwa sana usiku na mchana. Hongera sana kwa mwanangu Mheshimiwa Waziri. Hongera sana sana sana pamoja na watendaji wake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikija kwenye upande wa barabara nitaanza kuchangia nyumbani, Barabara ya Kilwa Road. Barabara ya Kilwa Road, kwanza niipongeze Serikali kwa kutoa fedha kwa ajili ya kuboresha kutoka kipande cha Mbagala Rangi Tatu mpaka Kongowe, ujenzi wa barabara nne. Ni jambo la muda mrefu lakini ninaishukuru Serikali imelipa fidia na kufanya hivyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na kujenga barabara zile nne kutoka pale Rangi Tatu kwenda huko, bado turudi nyuma, msongamano umekuja sasa Rangi Tatu mpaka Zakiem msongamano wa watu. Je, kule tumekupangia mipango gani katika kuzitatua zile barabara, angalau tupate barabara nane sasa? Idadi ya watu imeongezeka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mbagala ina watu takribani zaidi ya milioni moja kwa sasa hivi. Pia, kuna mwingiliano wa stendi za Kusini. Wananchi wanaotoka Kusini wote wanakuja pale Mbagala Rangi Tatu na maeneo mengine. Hivyo, Serikali iangalie njia madhubuti ya kuhakikisha tunaondoa msongamano kwa kuongeza zile barabara, tuweze kupata barabara nane kama kutoka Kimara mpaka Kibaha. Tuangalie huko twendako, tufanye hivyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niipongeze Serikali kwa kuamua sasa kuweka kivuko Kigamboni cha watu wengine wa kampuni nyingine. Ni vizuri Serikali ikaungana na wadau katika kuboresha huduma ile. Sasa, changamoto ya kivuko cha Kigamboni, mwananchi wa Kigamboni ana uhuru wa kuchagua; nipande Bakhresa au nipande kivuko cha Serikali. Hayo ni mambo mema sana na niiombe mambo hayo mema yaendelezwe katika sekta nyingine. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, rai yangu niiombe, naona Barabara ya Mwendokasi ya kutoka Mbagala Rangi Tatu – Temeke – Bendera Tatu imekamilika mpaka Gerezani, lakini hatujaona mabasi ya mwendokasi. Tunaanza lini mabasi hayo? Mheshimiwa Waziri atakaposimama hapo ninataka leo aniambie, mabasi hayo yana changamoto gani mpaka leo hayajaanza? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama tunaona vinginevyo, basi tuhakikishe tunaingia ubia kama tulivyoingia ubia wa Kigamboni kwa Sekta Binafsi, nayo ichangie katika mabasi, tuweze kupata mabasi. Barabara zile miundombinu ile ya Serikali imetengenezwa kwa gharama kubwa kwa lengo la kuwasaidia wananchi wake. Sasa tunaomba kabla ya uchaguzi huu, tunaomba mabasi ya mwendokasi yaanze kuja Temeke. Kutoka Gerezani – Temeke – Mbagala Rangi Tatu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikitoka kwenye Barabara ya Kiwalani, nayo pia maeneo ya Mtoni Mtongani kwa Aziz Ali nako kumeanza kuwa na foleni. Ninaomba waangalie ni nini hasa kinachojaza foleni? Tumeona changamoto nyingi za barabara. Wanaongeza Barabara, lakini barabara ziendane; ushauri wangu barabara. Sasa TANROADS waangalie jinsi barabara zitaendana na vituo vya mabasi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mabasi hayana maeneo ya kusimama. Vituo maalum havipo, matokeo yake mabasi yanasimama katikati ya barabara, jambo ambalo linasababisha msongamano mkubwa. Hivyo basi, twendako niiombe Serikali yangu sikivu, wanapopanga bajeti ya ujenzi wa barabara wahakikishe wanaweka na bajeti za vituo vikubwa vya daladala, vikae mahali pa wazi na penye nafasi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine nitaongelea Barabara ya Devis Corner mpaka Jet Corner. Barabara hii ni mkombozi kwa Wanatemeke lakini tunakoelekea nayo itakuwa na changamoto kubwa maeneo ya Buza. Buza sasa imekuwa ni sehemu ambayo ina mkusanyiko wa watu wengi. Watu wanaotoka Kilungule, wanaotoka Mwanagati, wanaotoka Temeke, wanaotoka huku, magari yanajaa Buza, matokeo yake sasa Buza nayo itakuwa kama Mbagala Rangi Tatu, hakuna pa kupenyea. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara ile ilikuwa muhimu sana kwa sababu ukitoka Temeke ukienda Buza, ukipita Makangarawe Buza, unaingia unaenda sana Kilungule unatokea Mbagala ilikuwa ni msaada mkubwa na kimbilio la wananchi wa Mbagala. Tuendako msongamano unazidi kuwa mkubwa. Niiombe Serikali waangalie na wafanye tafiti. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikija hapo hapo kwenye barabara eneo la Temeke, Barabara ya Mandela: Barabara ya Mandela kutoka Kurasini Bandarini. Niipongeze Mamlaka ya Bandari; kwa kushirikiana na Serikali waliboresha kipande kile cha kutoka Bendera Tatu mpaka Kurasini, lakini kule kwingine bado. Barabara ile ni ya muda mefu sana, hata mwenyewe sijazaliwa ninaona (ile Mandela). Bado na yenyewe ninaomba itengewe fedha kuhakikisha barabara ile inakwenda. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kumekuwa na changamoto kubwa ya malori, kutoka Sokota mpaka ukifika TAZARA yaani hapo barabara inakuwa mtihani. Hata akitokea mgongwa kumpitisha inakuwa mtihani. Kila kitu pale kinakuwa mtihani. Kwa hiyo, niiombe pale TAZARA paangaliwe. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tulikuwa na Barabara nzuri sana ya Mchicha…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Mheshimiwa Mariam Kisangi, muda wako umekwisha.

MHE. MARIAM N. KISANGI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninamalizia mchango wangu. Tulikuwa na Barabara ya Mchicha, lakini sasa barabara ile nayo imevamiwa. Niiombe Serikali ipange utaratibu wa haya malori, mbona yanakwenda kila kona ya Mkoa wa Dar es Salaam? Barabara zetu zinaharibika. Je, wakati wa kujenga walilenga kwamba hizo barabara zitapitisha malori au yatapita magari ya kawaida ya wananchi?

MWENYEKITI: Ahsante sana.

MHE. MARIAM N. KISANGI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaunga mkono hoja na ninakushukuru sana sana. (Makofi)