Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ujenzi kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

Hon. Halima James Mdee

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ujenzi kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

MHE. HALIMA J. MDEE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninashukuru kwa nafasi. La kwanza, kwa mujibu wa randama mafanikio ya utekelezaji wa bajeti; barabara mwaka huu mlipania kujenga kilomita 100 lakini utekelezaji wenu ni 26%. Wamejenga kilomita 100 (26% performance). Barabara za Mikoa wamejenga kilomita 20 sawa na 20.9% performance. Ukarabati wa kiwango changarawe, wamekarabati kilomita 213 sawa na 23% performance. Madaraja performance yao ni 13%.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ndugu zetu hapa wanaongea kwa mbwembwe, lakini ukija kwenye ufanisi ni chini ya 25%. Kwa hiyo, haya mambo siyo ya kujivunia sana. Siku zote nimekuwa nikisema ni muhimu sana wataalam wetu wa kuandika hizi hotuba wajaribu kufupisha maandiko ya hotuba. Wanajaza barabara nyingi, nyingine zinahusisha barabara ambazo zilishamalizwa. Kuna barabara zangu za Jimbo la Kawe toka mwaka 2020 zimekwisha lakini wanaziandika. Sasa, kwa nini tunakuwa tunajaza maneno mengi bila ufanisi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu hizi fedha za Mfuko wa Barabara, hili ni takwa la Kikatiba. Amezungumza hapa kwa niaba ya Mwenyekiti wa Kamati Ibara ya 135(2) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano inaeleza kabisa fedha zilizotengwa kwa madhumuni maalum, hazipaswi kuingizwa katika Mfuko Mkuu wa Serikali na tulitungia sheria. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Sheria ya Barabara, Sura 220, vilevile imeitaka TRA ambayo ni Mamlaka ya Mapato kukusanya kwa niaba na kuziwasilisha kwenye mamlaka husika. Taarifa ya Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali ya Mwaka huu inasema kwenye yale maeneo yote manne yenye Mifuko, inasema Ukaguzi wa TRA ulionesha kwamba jumla ya shilingi trilioni 2.59 zilikusanywa na wao kwa niaba ya REA, Mfuko wa Maji, Mfuko wa Reli na kuhamishiwa Hazina which ni makosa, lakini bahati mbaya zilipohamishiwa Wizara ya Fedha, kilichotolewa kwenye Mifuko husika ni shilingi trilioni 1.4 tu. Shilingi trilioni 1.14 hazikupelekwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hiyo ni ya miaka iliyopita ambayo ni mwaka mmoja uliopita Mkaguzi ametoa taarifa mwezi Machi mwaka huu. Anatuambia hapa Mwenyekiti wa Kamati ya Ujenzi kwamba, kwenye eneo la TANROADS ama Mfuko wa Barabara kwa mwaka huu walitakiwa wapewe shilingi bilioni 800, wamepewa shilingi bilioni 200 halafu mnategemea miujiza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Taarifa ya Mkaguzi Mkuu katika zile shilingi trilioni mbili na kadhaa nilizozisema, Mfuko wa Barabara ulitakiwa upewe shilingi trilioni 1.4. Walichopewa ni shilingi bilioni 800 na shilingi bilioni 648 zimebaki Wizara ya Fedha. Kwa mwaka jana, shilingi bilioni 648, kwa Mfuko wa Barabara. Mwaka huu kwa mujibu wa Kamati ya Bunge 600 imebaki. Waziri wa Fedha na Wizara ya Fedha wanavunja Katiba halafu tunawaangalia tunajifanya kama hatujui na Bunge tunalalamika. Hatuwezi kuendesha nchi namna hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nirudie kusema kwamba ni muhimu sana kama Bunge tukasimama tunapotakiwa tusimame. Kama tuna Waziri anayeweza kukiuka maelekezo ya Katiba ya Nchi si mara moja fedha zinatozwa kutokana na tozo tulizozitoa kwa wananchi wa Tanzania kuchangia kwenye mafuta. Kila lita moja ya mafuta kwa mdundulizo wa mabadiliko ya sheria ya miaka zaidi ya sita, mwananchi anachangia si zaidi ya shilingi 500 au shilingi 600 tokea sheria hii ya tozo ianze. Sheria zinavunjwa, tunaangalia, fedha haipelekwi, kila mtu analalamika barabara hapa, unakuta barabara zimeandikwa nyingi. Wabunge waende wakasome randama. Una kilometa moja, una kilometa mbili, una kilometa tatu, sasa barabara ya kilometa 200 wewe unapewa kilometa moja na unapiga makofi eh! Tumepata barabara. (Makofi)

MHE. ABUBAKARI D. ASENGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, Taarifa.

MWENYEKITI: Taarifa.

TAARIFA

MHE. ABUBAKARI D. ASENGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na mchango mzuri wa Mheshimiwa Mdee dada yangu ninataka nimpatie taarifa tu kwamba Serikali imenikamilishia barabara ya kilometa 67 kwa lami nzuri na sasa hivi wanaanza kunifungia taa.

MHE. HALIMA J. MDEE: Usinipotezee muda bwana sisi tunazungumza…

MWENYEKITI: Mheshimiwa Halima unaipokea taarifa?

MHE. HALIMA J. MDEE: Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi vitu cheap hivi ndiyo vinaangamiza Taifa. Ninazungumza katika broader aspect. Ndiyo maana sijakaa hapa nikazungumza Barabara za Kawe kwa sababu ninazungumza masuala ya Kitaifa, nchi hii inahitaji barabara. Tumetunga sheria ili fedha za wananchi kupitia kununua mafuta ziweze kusaidia kurudisha maendeleo kwao. Fedha zinakatwa, zinakusanywa na TRA anabaki nazo Dkt. Mwigulu Nchemba pale Wizara ya Fedha zinafanya nini? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, labda watuambie kuna matumizi mengine ya ziada ambayo Bunge halijui. Kwa sababu kama Bunge tunasema tunakusanya shilingi trilioni 44, au 46 kwenda kutekeleza mipango ya maendeleo, wanatuambia zimekusanywa. Ikija kwenye utekelezaji 20% wanapeleka wapi fedha? Watujibu. Isije ikawa tunapoteza muda hapa, fedha zinakusanywa zinaishia mifukoni kwa watu. Lazima watupatie majibu ya mantiki, hilo la kwanza. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, wakandarasi wazawa. Ukiangalia mwaka 2018/2019 wazawa walipata kazi ya thamani ya shilingi bilioni 187, wa kigeni wakapata kazi ya thamani ya shilingi bilioni 591. Mwaka wa Fedha 2022/2023 wazawa wakapata kazi ya shilingi bilioni 42, wageni wakapata kazi ya thamani ya shilingi trilioni 5.532. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia barabara zetu hatuzungumzi kilomita moja au barabara za vumbi, hizi kazi za njaa njaa, tunazungumza za bilioni, Chinese companies more than 80%. Nendeni kwenye randama mwangalie hizi shilingi trilioni 5.5 zingebaki kwa wakandarasi wetu wazawa kama hatuwazeshi tungefika wapi. Hivi kuna Kampuni ya Kitanzania ya Wakandarasi ina ubavu wa kwenda China na kupewa kazi? Nimeangalia Airports zetu tunazojenga, tunajenga viwanja vya ndege 15. Miradi mitatu bado kandarasi hazijapatikana, mradi mmoja ndio yule jamaa anaitwa Mayongo Construction ambaye amejenga Geita. Miradi 11 yote ni ya kigeni. Wakati yule aliyejenga Geita ameambulia shilingi bilioni zake 59 za kandarasi, Chinese companies shilingi bilioni 880, viwanja 15 vya ndege.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii nchi yetu, nilikuwa ninaangalia wakandarasi waliosajiliwa wako 13,000. Kuna Mfuko ule wa kusaidia wakandarasi ambao wana uwezo duni, ukisema wana uwezo duni. Eti Wizara imetenga shilingi bilioni nne! Yaani Mfuko Maalum wa kusaidia Wakandarasi wa Tanzania ambao labda wana uwezo wote mwingine isipokuwa pesa, shilingi bilioni nne? What a shame? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme; hakuna wa kuibadilisha hii nchi zaidi ya sisi wenyewe. Tunasomesha watoto wetu, tunasomesha vijana wetu wakawe na hizi taaluma za ujenzi na majenzi, tutumie akili zaidi tusaidie Taifa hili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru sana. (Makofi)