Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kilwa Kaskazini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. FRANCIS K. NDULANE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipatia nafasi ya kujadili hii Bajeti ya Wizara yetu muhimu ya Ujenzi. Kwanza nitangulie kwa kumshukuru Mheshimiwa Rais wetu wa Serikali ya Awamu ya Sita, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa uwekezaji mkubwa katika Sekta ya Ujenzi na hivyo kufanya fedha nyingi kupelekwa katika sekta hii. Tumeona miradi mingi imetekelezwa ikiwemo lile Daraja kubwa kabisa Afrika Mashariki lenye urefu wa kilometa tatu la Kigongo – Busisi. Pia tumeona namna Mheshimiwa Rais wetu alivyotupambania wananchi wa mikoa ya kusini na kuweza kuleta fedha nyingi ambazo miradi inaendelea ya ujenzi wa madaraja mapya. Tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninamshukuru pia Mheshimiwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye siku ya tarehe 16 Aprili, mwaka huu tuliambatana naye pamoja na Waziri wa Ujenzi, na Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa kwenda kuangalia namna ambavyo Serikali inaendelea na ujenzi wa yale madaraja yaliyoathiriwa na Kimbunga Hidaya na Mvua za El-Nino pamoja na hatua nyingine muhimu zilizochukuliwa katika kufanya mawasiliano ya Barabara ya Kibiti – Lindi – Mingoyo yaweze kufanyika kwa ufanisi mkubwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpongeze Mheshimiwa Abdallah Ulega, rafiki yangu na ndugu yangu kwa kweli anafanya kazi kubwa sana. Alikesha na wananchi wetu pale ilivyokuwa inatokea Barabara yetu ya Kibiti – Lindi – Mingoyo ilikatika katika maeneo ya Somanga – Mikereng’ende na kule Mto Matani. Kwa kweli amefanya kazi kubwa sana, ninampongeza sana. Pia, ninampongeza Naibu Waziri ambaye mara kwa mara alikuja kuangalia kazi na ubora unaoendelea kutekelezwa katika maeneo ambayo yanatengenezwa barabara hizi, madaraja na makalavati. Ninakumbuka kuna wakati tulikwenda naye mpaka kule Kipatimu kwa ajili ya kuangalia yale makalavati yanayojengwa na Kampuni ya ME, pale njia nne Kipatimu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpongeze pia Katibu Mkuu dada yangu Balozi Engineer Aisha Amour, kwa kweli anafanya kazi kubwa na anaonesha namna alivyo mbobevu katika fani hii ya ujenzi wa barabara. Nimpongeze pia Dkt. Charles Msonde kwa kazi nzuri. Vilevile, nimpongeze pia Mheshimiwa RAS wangu wa Mkoa wa Lindi dada yangu, Mheshimiwa Zainab Telack, kwa kweli na yeye amekuwa akikesha kwenye yale maeneo ambayo yalikuwa yanaleta matatizo kati ya mwaka jana mpaka mwanzoni mwa mwaka huu, wakati tayari Serikali imeshachukua hatua mbalimbali za ujenzi wa yale madaraja. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpongeze vilevile, pia Mheshimiwa DC wetu wa Wilaya ya Kilwa, Mheshimiwa Comrade Abdallah Nyundo anafanya kazi nzuri sana katika kusimamia ile miradi iliyopo pale Kilwa. Nimpongeze Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya TANROADS Engineer Besta pamoja na Engineer wetu ambaye anasimamia Barabara za Mkoa wa Lindi, Engineer Zengo kwa kazi nzuri. Kwa kweli wametuonesha mfano mzuri na kwa kweli wanawajibika ipasavyo katika kuhakikisha mambo yanakwenda sawasawa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile, nipongeze hatua ambazo Serikali imechukua siyo tu kujenga madaraja bali pia kuangalia uwezekano wa kujenga sasa barabara zote ambazo zinaelekea Mikoa ya Kusini. Hizi barabara nyingi zimejengwa muda kidogo; ukiondoa ile barabara inayotoka Mtwara kwenda Masasi kupitia Mnazi Mmoja – Lindi na ile ambayo ilijengwa hadi kwenye tuta la Daraja la Mkapa. Barabara ya kutoka Somanga kwenda Masaninga ndiyo barabara ambayo ilifuata na imeonekana mara nyingi kunatokea changamoto nyingi. Ndiyo hiyo inaonesha maeneo ya Somanga, Mikereng’ende na kwingineko ambako Mheshimiwa Waziri umekuwa ukifanya kazi na juhudi kubwa kuhakikisha mambo yanakwenda sawasawa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niliomba katika vile vipande ambavyo vitaanza kushughulikiwa hiki kiwe namba moja cha Somanga – Masaninga kwa sababu ndicho cha zamani zaidi na kimeharibika zaidi halafu kifuate kile cha kutoka Nyamwage kwenda Somanga kwa sababu hayo ndio maeneo barabara zake zina hali mbaya zaidi. Kwa hiyo, ningeomba hilo lizingatiwe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitakuwa mchache wa fadhila kama sitozishukuru kampuni ambazo zinajenga yale madaraja yaliyoathiriwa na Mvua za El-Nino na Kimbunga Hidaya. Mheshimiwa Waziri hapa umetuongoza kuzitathmini zile kampuni za kizalendo, ninaomba niseme hujakosea na ndiyo maana Mheshimiwa Rais amekuweka kwenye hiyo nafasi kwa sababu ameona upo makini na una uwezo wa kulitumikia Taifa hili kwa kiwango toshelevu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Kampuni ya MAKAPO aliyoitaja ambayo inaongozwa na Ndugu Joseph Mkuyu kwa kweli inafanya kazi ya kipekee, hajakosea kabisa. Kuna kampuni moja hujaitaj inaitwa ME Constructors Limited inaongozwa na ndugu yetu Bwana Makundi ambayo inajenga tundu 10 za makalavati kutoka Njia Nne kwenda Kipatimu. Ninajua ramani ya Kilwa unaijua umeshawahi kuwa DC kule Kilwa. Kwa kweli Kampuni ya ME Constructors inafanya kazi nzuri sana, nayo ninaomba aiongeze katika orodha yake ya kampuni za kizalendo zinazofanya vizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hii inaonesha kwamba, kampuni zetu sasa zimeiva. Ninaomba Serikali iendelee kuziamini siyo tu kwenye ujenzi wa madaraja na barabara bali pia hata kwenye maeneo mengine ya miradi ya maji na mingineyo, kwa kweli waweze kuaminiwa na kupewa nguvu, ili mzunguko wa uchumi wetu uweze kubaki hapa nchini na uongeze tija kwa Wananchi wetu wa Tanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hizo kampuni za kigeni zimeajiri pia ma-engineer wazalendo. Pale tuna Kampuni ya Hainan ina wazalendo kina Engineer Kazungu wapo wanafanya kazi usiku na mchana. Kwa kweli tunashukuru kazi inakwenda vizuri ya ujenzi wa madaraja na makalavati. Pia, niishauri Serikali ninaomba Wizara na TANROADS ziendelee kuimarisha usimamizi, ili kuhakikisha hii miradi inayoendelea iweze kutekelezwa kwa wakati na iweze kujengwa kwa ubora unaotakiwa, ili kwa miaka mingi kama siyo kwa miaka yote basi tuweze kushuhudia hizi barabara zikipitika kwa ubora na hivyo tuweke historia sasa. Haya mambo yaliyotokea yawe kama historia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu wa pili, ninaomba Serikali itenge fedha ya kutosha kwa TANROADS, ili kile kitengo kinachohusika na uchunguzi wa barabara kabla hawajatangaza zabuni, kiweze kufanya kazi yake vizuri ya kupembua hizo barabara na kuona ubora na udhaifu wake ikiwemo hiyo ya Somanga – Masaninga na Ndundu – Somanga, ili kuhakikisha kwamba itakavyokuja kujengwa basi iwe na ubora ambao utadumu kwa miaka mingi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba na kuishauri Serikali kwamba kuna vipande viwili vya lami pale Eneo la Nasaya katika Kata ya Kipatimu mita 300 tayari Mkandarasi ameshapatikana anaitwa Vesma na kuna Mkandarasi anaitwa Hardcom International mita 700 pale Kipatimu na taa zake. Ninaomba wale wakandarasi wasimamiwe haraka na kwa sababu kiangazi kinaanza kuanzia mwezi huu, basi waweze kufanya kazi kwa haraka na tija iweze kupatikana ya barabara ile.
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa Francis Ndulane.
MHE. FRANCIS K. NDULANE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana na ninaunga mkono hoja. (Makofi)