Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mlalo
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. RASHID A. SHANGAZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, ninashukuru kwa kunipa nafasi hii ya kuchangia katika Wizara hii muhimu kabisa kwa ujenzi wa miundombinu ya barabara zetu hapa nchini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze na pongezi; nimpongeze sana Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa namna ambavyo ameendelea kuwa kinara wa uboreshaji wa miundombinu ya barabara zetu vijijini kupitia TARURA pamoja na barabara zetu kuu kupitia Wakala wa Barabara (TANROADS) kwa kazi nzuri ambazo zinaendelea kufanyika. Pamoja na changamoto mbalimbali za mvua, lakini tumeona commitment ya hali ya juu sana ya Wizara chini ya Waziri Abdallah Hamis Ulega, Engineer Amour, Naibu Waziri Godfrey Kasekenya, Mtendaji Mkuu wa TANROAD, Mohamed Besta na Watumishi wote wa Wizara hii; kwa kweli wanastahili maua yao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeona namna ambavyo hawalali ili kuhakikisha kwamba miundombinu kila mahali inarudi katika ubora wake, haswa yale maeneo ambayo yaliyokumbana na changamoto ikiwemo kule Kusini na kule Morogoro, lakini hata kule Tanga ipo barabara yetu moja ilipata kadhia, Meneja wa TANROADS Mkoa alifika kwa wakati na kurejesha mawasiliano kwa haraka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya pongezi hizo nianze na ziara ya Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan aliyoifanya hivi karibuni katika Mkoa wa Tanga. Mheshimiwa Rais alizungumza maono yake anayotoka kuiona Tanga. Akasema na kubainisha kwamba anataka kuiona Tanga ambayo imefunguka kwa upande wa miundombinu, iweze kuwasiliana na Mikoa mingine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunazo barabara zetu ambazo zinatutambulisha hivyo. Barabara ya kwanza ambayo kwa bahati nzuri ameitaja ni hii ya kutoka Handeni – Kiberashi hadi Singida. Tunampongeza kwa hatua hiyo ya kusema sasa itajengwa kwa utaratibu wa PPP. Sambamba na hilo tunayo barabara yetu hii ya Tanga – Pangani – Bagamoyo ujenzi unaendelea na sasa tuko katika ujenzi wa daraja pale Mto Pangani. Ni imani yetu kwamba watazidi kusukuma Mafungu ili barabara ile iende kwa kasi zaidi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hiyo tunayo Barabara ya kutoka Mabokweni kwenda Maramba – Umba hadi Mkomazi. Barabra hii ipo kwenye Ilani ya Chama Cha Mapinduzi na ni barabara ya kimkakati ya kuondoa msongamano katika Barabara ya Chalinze – Segera kwenda Mikoa ya Kilimanjaro na Arusha na hata mpaka Musoma. Tunaomba sana na barabara hii sasa waitengee fedha ili sasa shughuli ziweze kuanza. Tukifanya hivyo tutakuwa tumesaidia sana kufungua Mkoa wa Tanga.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba nimkumbushe Mheshimiwa Waziri jambo moja. Barabara hii ya Chalinze – Segera ni barabara ya siku nyingi; na barabara hii kwa mujibu wa taratibu zao, kwamba uhai wa barabara ni miaka 15, hii ni zaidi ya miaka 30; na barabara hii sasa tunaweza tukasema imesha-expire haifai tena kwa matumizi. Kwa hiyo ninachoomba ni kwamba ni lazima kuwe na mpango wa kuiboresha barabara na hii. Kwanza ni nyembamba sana na mwaka huu imesababisha ajali nyingi sana. Inamgharimu sana Mkuu wetu wa Mkoa anashindwa kufanya kazi nyingine za maendeleo wakati wote yupo barabarani ili kuhudumia wananchi mbalimbali wanaopata shida kutokana na ufinyu wa wembamba wa barabara hii. Kwa hiyo niwaombe sana waangalie uwezekano wa kuipanua barabara hii ambayo sasa imekuwa finyu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hii pia inatokana na ufanisi ambao umeongezeka katika Bandari ya Tanga. Shehena kubwa inashuka katika Bandari ya Tanga kwa hivyo inahitaji barabara pana ili magari haya yaweze kupishana kwenda kuchukua mizigo mbalimbali katika Bandari ya Tanga. Sambamba na kutoka Segera kwenda Same hadi Kilimanjaro ni barabara ambayo pia ni nyembamba na inapaswa kuongezwa haswa katika zile kona kuwe na upana wa kutosha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ni Barabara ya kutoka Mombo - Lushoto kwenda mpaka Mlalo. Barabara hii na yenyewe imejengwa miaka 30 iliyopita. Ninakumbuka wakati huo mkandarasi alikuwa anatoka Kampuni ya GBG, ninadhani hata sasa hivi hapa nchini haipo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara hiyo tumeshaweka viraka vya kutosha lakini sasa imechakaa na haifai. Tunaomba na yenyewe sasa ije ifanyiwe upanuzi kwa sababu magari yanayoingia katika Wilaya ya Lushoto ni mengi sana, yameongezeka zaidi ya mara tatu wakati wana-design hii barabara iliyopo sasa. Kwa hiyo, niombe kilometa 36 kutoka Mombo mpaka Lushoto na kutoka Lushoto kwenda Mlalo mpaka Mtae na yenyewe imeahidiwa kujengwa kwa kiwango cha lami, tunaomba waongeze kasi ya ujenzi katika barabara hiyo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine ambalo ningetaka kuchangia ni kuhusu viwanja vya ndege. Mheshimiwa Waziri, Tanga ni Jiji, lakini katika Majiji Sita ya Nchi hii ni Tanga pekee ambayo ina kiwanja cha ndege ambacho ndege kubwa haziwezi kutua. Nimwombe sana, hakikisha katika viwanja vile ambavyo vinajengwa katika Mikoa ya Tabora, Shinyanga, Kigoma na Mara (Musoma) basi mweke mkazo pia katika Jiji la Tanga. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hivi tunao Mradi mkubwa wa Bomba la Mafuta, lakini kama ambavyo Mheshimiwa Rais ameahidi kuufungua Mkoa wa Tanga kiuchumi na kwa kilimo pia. Ni muhimu pia kuwa na uwanja mkubwa wa ndege ambao utawawezesha wawekezaji kuweza kufika Tanga kwa urahisi. Kwa hiyo, ni aibu sana katika Majiji yote sita ni Jiji la Tanga pekee ambalo kiwanja cha ndege kinaruhusu ndege ndogo tu ambazo si za zaidi ya abiria 12 kutua. Niombe sana kwamba, hili liwepo katika vipaumbele vya Wizara kuhakikisha kwamba tunaboresha ule uwanja wa ndege uweze kuwa na uwezo wa kutua ndege hata aina ya bombardier hizi ambazo zinakuja Dodoma na maeneo mengine basi ziweze kutua katika Mkoa wetu wa Tanga, ili tuweze kurahisisha shughuli za kiuchumi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho lakini siyo kwa umuhimu, ni ile changamoto ya kukarabati barabara ambazo zimekatika kutokana na hii kadhia ya mvua. Tunaomba sana na tunatambua kuwa mwaka huu ni mwaka wa uchaguzi, lakini pamoja na uchaguzi ni muhimu sana tukawekeza fedha kwenye yale maeneo muhimu ambayo barabara hizi angalau ziweze kupitika katika kipindi hiki ambacho tunatafuta mafungu makubwa kwenda kukamilisha miradi hii. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema maneno hayo ninashukuru sana na ninaunga mkono hoja. (Makofi)