Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

Hon. Fatma Hassan Toufiq

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

MHE. FATMA H. TOUFIQ: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana nami kwa kunipa fursa ya kuchangia hoja iliyopo mbele yetu. Niendelee kumshukuru sana Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Rehema, Mwingi wa Ukarimu kwa kunipa fursa na afya njema kuweza kuongea katika hili Bunge Tukufu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nami naomba niungane na Waheshimiwa Wabunge wenzangu katika kuendelea kumpongeza sana Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kazi nzuri anayoifanya kwa ajili ya maendeleo endelevu ya Watanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa namna ya kipekee, naomba pia nimpongeze Mheshimiwa Waziri Mkuu, Mheshimiwa Niabu Waziri Mkuu, pamoja na Waheshimiwa Mawaziri wote kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu; Mheshimiwa Lukuvi, Mheshimiwa Ridhiwani, Waheshimiwa Manaibu Mawaziri, Makatibu Wakuu pamoja na Watendaji wote wa Ofisi ya Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa hotuba nzuri ambayo wameiandaa ambayo imesheheni taarifa nzuri, dhima kuu ikiwa ni kuleta maendeleo endelevu kwa ajili ya Watanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, halikadhalika, naomba niwapongeze pia Watendaji Wakuu wa taasisi ambazo zipo chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu ambao nao wamekuwa wakifanya kazi nzuri sana kwa ajili ya kuleta maendeleo ya Watanzania. Naomba niwataje kwa majina; Ndugu Masha Mshomba, Mtendaji Mkuu wa NSSSF; Ndugu Bandru, Mtendaji Mkuu wa PSSSF; Bi. Khadija Mwenda Mtendaji Mkuu wa OSHA; na Dkt. John Mduma, Mtendaji Mkuu WCF.

Mheshimiwa Mwenyekiti, watendaji hawa kwa kweli ni wazalendo na tumeona kabisa kazi ambazo wanazisimamia, wamezifanya kwa weledi mkubwa sana. Kwa hiyo naomba pia niwapongeze sana kwa sababu taasisi ambazo wamekuwa wakiziongoza zimekuwa zina matokeo chanya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika ukurasa wa 14 wa hotuba hii Serikali imezungumzia kuhusu mazingira wezeshi ya kupanua wigo wa ajira kwa kipindi cha mwaka 2020 hadi Februari, 2025, kwamba, jumla ya ajira milioni 8,640,204 zilikuwa zimezalishwa. Naipongeza sana Serikali kwa kazi hii kubwa ambayo imefanya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na pongezi hizo, nina ushauri kwamba, kwa kuwa vyuo vikuu, vyuo vya kati, na taasisi mbalimbali zimekuwa zikizalisha wahitimu wengi, bado uhitaji wa ajira ni mkubwa sana. Tunatambua kabisa kwamba pamoja na juhudi kubwa ya Serikali ambayo imeandaa mazingira wezeshi kwa ajili ya vijana kujiajiri au kuajiriwa, bado kuna ombwe kubwa sana la vijana hawa katika kuajiriwa. Kwa hiyo, niendeee kuipongeza kwamba kumekuwa kuna programu mbalimbali za kuhakikisha kwamba vijana wanaajiriwa, ikiwemo miradi ya BBT na mingineyo na mazingira wezeshi na mikopo na kadhalika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo kubwa ambalo nilikuwa nataka, na ninatamani kuishauri Serikali ni kwamba katika Ofisi ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, Kazi, Ajira, Vijana na Wenye Ulemavu kuna ule Mfuko wa Maendeleo ya Vijana. Mfuko huu umekuwa ukitengewa bajeti, lakini bajeti yake ilikuwa haitoshi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba niishauri Serikali, ili kusudi vijana wengi waweze kujiajiri, waweze kukopesheka na pia kuajiri wenzao, ni budi Serikali ikaangalia upya kuuongezea mfuko huu fedha ya kutosha ili kusudi kundi kubwa la vijana waweze kupata mikopo hii na hatimaye waweze kujiajiri na kuajiri vijana wenzao wengine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo, nilikuwa natamani kuendelea kuishauri Serikali. Natambua kabisa kwamba ajira zilizopo ni haba, lakini pia kuna nchi za wenzetu huko ughaibuni ambazo wamekuwa wakihitaji vijana wa fani mbalimbali kwenda kufanya kazi huko, yaani diaspora. Kwa hiyo, bado naona kwamba kasi ya kuwaunganisha vijana na zile nchi ambazo zinahitaji wataalamu au vijana mbalimbali kwenda kufanya kazi kule, bado ni ndogo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nilikuwa naomba niishauri Serikali kuweka mkakati maalum wa namna ya kuandaa dirisha maalumu la kuhakikisha kwamba vijana wengi zaidi wanaunganishwa na hizi ajira za nje ili kusudi waweze kwenda kufanya kazi kule ughaibuni. Wakifanya kazi kule ughaibuni maana yake ni kwamba yale mapato ambayo yatatokana na zile kazi wanazozifanya kule ughaibuni yatasaidia nchi yetu kupata kipato.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa uchache tu ni kwamba, wenzetu Nigeria wamefanikiwa, kwamba walau wanapata dola bilioni 25. Pia wenzetu Kenya mwaka 2023 ilipokea dola bilioni 4.2 kutoka diaspora; na sisi Tanzania tunaweza na tunaweza tukapata zaidi tukitafuta zile fursa kwa ajili ya vijana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo nilitamani kulizungumzia, lipo kwenye ukurasa wa 23 wa taarifa hii ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, ambayo imezungumzia kuhusiana na suala zima la upatikanaji wa maji. Naipongeza sana Serikali, nampongeza sana Rais wangu, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuhakikisha kwamba anamtua ndoo mwanamke kichwani kwa kuhakikisha kuwa anapata maji kutoka katika maeneo ya karibu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikija katika Mkoa wetu wa Dodoma, bado suala la upatikanaji wa maji limekuwa ni tatizo kidogo katika baadhi ya maeneo na hasa katika Jiji la Dodoma. Natambua kwamba uhamiaji wa Makao Makuu umesababisha pia uhaba huo. Hata hivyo, kwa kuwa Serikali ilikuwa imebaini kwamba watajenga lile Bwawa la Farqwa, basi nilikuwa naomba niishauri Serikali ifanye haraka kujenga lile bwawa ili kupunguza hili ombwe la upungufu wa maji katika maeneo mbalimbali ya Mkoa wa Dodoma, Jiji la Dodoma viunga vyake na hasa eneo la Nkuhungu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo, wananchi wamekuwa hawana taarifa yoyote kuhusiana na maendeleo ya Bwawa hili la Farqwa. Ni vizuri Serikali iwe inatoa taarifa za mara kwa mara ili wananchi nao wajue ni nini kinaendelea ili waache kulalamika. Nadhani wakipata taarifa na maarifa, itawasadia kujua kwamba Serikali yao Tukufu ipo mbioni katika kutafuta pesa na miundombinu mbalimbali ili kuhakikisha kwamba bwawa hili linafanya nini? Linajengwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa uchache niliona niseme hayo. Baada ya kusema hayo, nakushukuru sana kwa kunipa fursa, naunga mkono hoja. (Makofi)