Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Bahi
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. KENNETH E. NOLLO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nakushukuru kwa kunipa nafasi ili niweze kuwa mchangiaji. Kwa dhati kabisa nachukua nafasi hii kuipongeza Serikali kwa kazi kubwa ambayo imefanya katika sekta mbalimbali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunampongeza sana Mheshimiwa Rais kwa umadhubuti wa kuliongoza hili Taifa na namna ambavyo shughuli za Serikali, kama nilivyosema, hasa katika miradi ya maendeleo, imeweza kufanyika katika maeneo mengi na kwa upana zaidi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nilitaka nijikite zaidi katika ufanisi wa Serikali. Pamoja na mambo yote ya mafanikio makubwa ya miradi, bado tunahitaji ufanisi zaidi wa Serikali katika kuwapa wananchi huduma.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa nina mambo mawili ambayo, kama nchi, ni lazima tuangalie ni namna gani tunaweza tukaliweka suala hili. Tumekuwa na sikukuu mbalimbali, zile public holidays, lakini kutokana na hilo jambo ukienda kwenye hospitali nako kunakuwa na sikukuu. Kwa hiyo, tunapoteza maisha ya wananchi wengi wa Taifa letu kwa sababu tu kunakuwa na sikukuu, basi na huduma nazo zinaenda sikukuu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali iangalie ufanisi wa jambo hili. Wapo watumishi ambao mtawapanga kipindi cha sikukuu wafanye kazi kama kawaida, lakini sikukuu imeingia Alhamisi, hospitali hakuna huduma mpaka Jumatatu. Tunapoteza maisha ya wananchi wetu. Jambo hili ninaishauri sana Serikali, tutoke kwenye huu utamaduni kwamba, ikiwa sikukuu wote tunaenda sikukuu. Zipo sekta ambazo hazitakiwi kwenda sikukuu. Naomba hili suala tuliangalie sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine, sisi Wabunge ni mashahidi, kumekuwa na malalamiko kuwa mgonjwa akifariki inatakiwa gharama zile alizokuwa anatibiwa zilipwe. Serikali imetoa tamko kwamba, hakuna jambo kama hilo, lakini hili jambo linaendelea. Mtu ameshafariki, unataka faida gani tena na huyo alikuwa ni mlipakodi wako, kama Serikali?
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ni kuachilia kwamba, ameshafariki. Jambo hili limejirudia mara nyingi sana na Serikali imekuwa inatoa majibu kwamba, hakuna maiti inayozuiwa, lakini ukweli ni kwamba, maiti zinazuiliwa baada ya mgonjwa kufariki. Sasa ifike mahali Serikali iseme kabisa jambo hili na zile hospitali waambiwe kwa maana wanasema hayo ni matamko ya wanasiasa tu, lakini ni wanasiasa gani? Ni suala la Serikali. Kwa hiyo, naomba jambo hili nalo liweze kuangaliwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine, mwaka huu sisi Mkoa wa Dodoma tumepata mvua kidogo na ukweli ni kwamba, hatujapata kabisa mazao. Sasa njaa imeanza. Kwa mfano kilo 20, sisi tunaita debe, kwa sasa linauzwa mpaka 22,000. Ina maana kufika mpaka Novemba, bei inaweza ikaongezeka zaidi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hoja yangu ni kwamba, nilitaka niseme, kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu, tathmini ifanyike katika maeneo yetu, kwanza tujue upungufu wa chakula mapema ili kama ambavyo NFRA huwa inaleta chakula cha bei nafuu, jambo hili lifanyike mapema zaidi, ikiwezekana ndani ya Mwezi wa Sita wananchi wetu wauziwe chakula cha bei nafuu. Kwa kufanya hivyo, wataweza kuwahi kuliko bei kupanda, ili kila watakachonunua waweze kukihifadhi walau kiwafikishe katika miezi mingine ambayo inafuata.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa ujumla katika Jimbo langu la Bahi, naishukuru sana Serikali na kama kupendelewa na Mheshimiwa Rais, mimi Bahi nimependelewa sana. Nimefanyiwa mambo makubwa. Suala zima la afya, hospitali yetu ile ya wilaya imeboreshwa kwa kiasi kikubwa. Ongezeko la majengo ikiwepo emergency na wodi mbalimbali za wanaume nazo zimeongezeka. Pia tumepata kituo cha afya, na juzi tumeahidiwa hapa na fedha ninasikia zimeanza kuingia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tutapata kituo kingine cha afya na kile kituo mimi niliwahi kuki-propose, kitaenda katika Kata ya Mtitaa ambacho kitahudumia Tarafa nzima ya Mwitikila.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumejenga zahanati 17. Vijiji 19 havikuwa na zahanati, kwa hiyo, tumejenga zahanati 17 tumebakisha vijiji viwili tu ambavyo havina zahanati; Kijiji cha Mchito na Kijiji cha Ngome. Ni matumaini yangu kwamba, hivi navyo tutavimalizia ili kwamba, huduma ianze kupatikana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa umeme, tumepewa vitongoji 15 na kazi kubwa inafanyika. Naipongeza Idara ya TANESCO, Wilaya ya Bahi wanafanya kazi kubwa na tunaiomba Serikali iongeze zaidi kama ambavyo tuliahidiwa vitongoji 90 mpaka 70, basi hili jambo liweze kuja haraka, wananchi wetu wana shauku ya kupata umeme katika maeneo yao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu suala la maji, kwanza naishukuru sana Serikali kwa namna ambavyo mmeweza kusambaza na kuleta miradi mingi. Kipekee nawashukuru Shirika la Water Mission kwa Bahi, wamefanya kazi kubwa. Tumepata miradi nane ambayo imeleta manufaa makubwa kwa wananchi wetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu suala la Barabara, madaraja mengi yamejengwa. Kwa Bahi tulikuwa na shida kubwa ya makorongo, lakini kwa sasa tumebakiza madaraja machache. Daraja la Mayamaya – Mkondai ninaambiwa fedha ziko tayari na mkandarasi amepatikana. Tuna daraja la Chifutuka lililojengwa na mkoloni, hilo nalo linatakiwa liwekwe jipya. Kwa hiyo, naishukuru Serikali kwenye suala la Barabara, tumeweza kufungua barabara kubwa za kimkakati.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la elimu. Nimepata shule nne mpya za sekondari na shule za msingi 14. Naomba Serikali iendelee kuboresha suala zima la elimu kwa maana, sisi Wilaya ya Bahi tunafanya vizuri Kitaifa, tumekuwa wa pili mwaka huu katika shule za msingi. Kwa hiyo, Serikali ina sababu maalumu, kwa sababu tunafanya vizuri, iendelee kutupatia shule za kutosha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu suala la ufugaji. Naishukuru Serikali, nilipata madume 20 ya mbegu bora. Madume yale yanafanya kazi kubwa na tunafanya utaratibu, linatoka hapa wiki moja, linakaa wiki nyingi linaenda kwenye maboma mengine. Kwa hiyo, tuongezewe ili tuweze kupata madume ya kutosha na wakulima wetu waweze kupata ufugaji mzuri wa kisasa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema haya, nampongeza Mheshimiwa Waziri Mkuu na Ofisi yake kwa namna uratibu wa Serikali unavyoenda.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kikubwa zaidi, naunga mkono hoja, nakushukuru sana. (Makofi)