Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. SUMA I. FYANDOMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nami nafasi ya kuweza kuchangia kwenye bajeti ya Mheshimiwa Waziri Mkuu. Awali ya yote, napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu ambaye amenipa uzima na afya njema nami nimeweza kusimama mbele ya hili Bunge Tukufu kutoa mchango wangu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa, nampongeza Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan na Amiri Jeshi Mkuu kwa kazi kubwa ambazo amezifanya kwenye Taifa hili la Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kulikuwa na miradi mkubwa sana ambayo Mheshimiwa Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan amekwenda kuikamilisha, sasa hivi kwenye Mradi wa SGR ni mteremko, ni mtelezo na Watanzania tunafaidika. Tunaenda Dar es Salaam kwa haraka na tunakuja Dodoma kwa haraka. Pongezi kubwa sana kwa Mheshimiwa Rais. Pia, mradi wa Bwawa la Mwalimu Nyerere ni mradi mkubwa sana ambao Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ameukamilisha. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na miradi hiyo mikubwa, kuna miradi ya maji, miradi ya barabara, miradi ya shule na miradi ya vituo vya afya na zahanati, Mheshimiwa Rais amegusa kila mahali na kila mahali ujenzi umeendelea na umekamilika, kwa hiyo, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan anastahili sifa na pongezi kubwa sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye hizo pongezi za Mheshimiwa Rais, nampongeza kwa sababu, pamoja na kazi kubwa anazozifanya, bado ndani ya Taifa letu la Tanzania amekwenda kuibua Rais wa Mabunge Duniani, Mheshimiwa Dkt. Tulia Ackson. Haijawahi kutokea. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hii imekuwa ni heshima kubwa sana kwetu Wananchi wa Tanzania. Tunasikia sifa na fahari kubwa sana. Hivyo, Mheshimiwa Rais siyo tu ameibua hawa watu ambao wameibuka kwenye Mataifa mbalimbali, ni wengi; siyo tu Mheshimiwa Dkt. Tulia Ackson. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kipekee nampongeza sana Mheshimiwa Waziri Mkuu, yeye pamoja na Mawaziri; Mheshimiwa Lukuvi, Mheshimiwa Ridhiwani pamoja na Manaibu Waziri kwa kazi kubwa anayoifanya ambayo inafanya kwa weledi mkubwa sana kwenye kazi inayoendelea kwenye hili Taifa la Tanzania. Mheshimiwa Waziri Mkuu aliwasilisha hapa vizuri sana bajeti yake ambayo imesheheni kila sehemu, ambayo inatakiwa kukamilishwa kwa majukumu yaliyobaki.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza sana Naibu Waziri Mkuu, Mheshimiwa Dkt. Doto Biteko. Mheshimiwa Naibu Waziri Mkuu huyu amekuwa ni kiongozi ambaye ana hofu kubwa ya Mungu. Mara nyingi kila akisimama kuongea Watanzania wanamwelewa, kwa sababu hapendi mambo ya kujikweza. Amekuwa akiongea kwamba, ukiwa na cheo hupaswi kupandisha mabega, unatakiwa uwe mnyenyekevu, unatakiwa uwe msikivu, kwa maana cheo ni dhamana, leo kipo, kesho hakipo. Mheshimiwa Dotto Biteko, Mwenyezi Mungu akubariki sana kwa namna ambavyo unaeleweka vizuri sana kila unavyosimama kuongea. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naipongeza sana Wizara ya Maji. Mheshimiwa Waziri Jumaa Aweso ni msikivu sana, amekuwa akisikiliza ukienda kumwambia juu ya shida ya maji. Naishukuru Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya Dkt. Samia Suluhu Hassan. Pale Tukuyu Mjini kulikuwa na tenki ambalo lilitakiwa lijengwe, mara nyingi nilikuwa nikiuliza hapa, lakini bado nilikuwa nikimfuatilia Mheshimiwa Waziri, ili kuuliza hilo tenki linakamilika lini?
Mheshimiwa Mwenyekiti, tenki hilo sasa hivi limekamilika. Natoa shukurani sana kwa niaba ya wananchi wa Tukuyu ambapo maji sasa hivi yatakuwapo. Ni maji ambayo lengo kubwa la Rais, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa wanawake wengi ni kumtua ndoo mama kichwani. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, bado Serikali ilitoa fedha kiasi cha shilingi 4,700,000,000 ambapo chanzo kilikwenda kutolewa Busokelo, kwa ajili ya maji ya wananchi wa Wilaya ya Kyela. Wilaya ya Kyela wanakwenda kunufaika na mradi mkubwa wa maji haya. Mheshimiwa Rais wetu Dkt. Samia Suluhu namna ambavyo tunamwombea kwa Mwenyezi Mungu, tunaamini anampa macho ya rohoni, Mawaziri wake hawa wanafanya kazi kubwa nzuri na njema sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna Waziri wa Kilimo, Mheshimiwa Hussein Bashe, anafanya kazi nzuri sana. Kazi ya Mheshimiwa Hussein Bashe inaeleweka mpaka kwa macho. Yaani kwenye jambo la kilimo, Mheshimiwa Hussein Bashe anatosha na chenji inabaki.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sijawahi kuona hata mara moja namna ambavyo hiki kipindi cha Nane Nane ya mwaka 2024, Mheshimiwa Bashe alileta mambo makubwa sana, ukizingatia ma-power tiller, kwa ajili ya wakulima, alitoa kwa wananchi power tiller 800 kwenye hiyo Wizara, trekta 500 na pikipiki 6,444 kwa wafanyakazi wa huko vijijini na mambo mengine mengi. Hivyo, Mheshimiwa Bashe anatosha na chenji inabaki, anafanya kazi njema sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho naishukuru sana Serikali kwa kuleta fedha kwenye Barabara ya Mbeya Mjini ambayo inaanzia Uyole mpaka Ifisi. Barabara ile inaeendelea kujengwa, lakini pia, ninaomba niishauri Serikali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Barabara ya kuanzia Igawa – Tunduma, kwanza ni nyembamba, lakini imechakaa kiasi kwamba inasababisha ajali nyingi sana, na kwenye ajali vifo vingi sana vinatokea kwa sababu ya barabara ambayo imechakaa. Naiomba Serikali iitizame barabara hiyo kwa jicho kubwa, kwa jicho pana, kwa jicho la uhuruma na upendo, ili wananchi ambao wanatumia barabara hiyo waweze kupona, ukizingatia hiyo barabara kwa sehemu ni ya Kimataifa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye barabara hiyo, hata magari ya nje ya nchi mengi sana, yanapita kwenda Congo, Zambia, Burundi, Zimbabwe na Malawi. Kwa hiyo, naiomba sana Serikali muichukulie kwa uzito sana ile barabara, imekuwa nyembamba zaidi, lakini pia imechakaa vibaya sana, inagharimu maisha ya watu, wengi wamebaki vilema na wengine wamepoteza maisha. (Makofi)
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MHE. SUMA I. FYANDOMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naona kengele inanikatisha hapa. Naishukuru Serikali ya Awamu ya Sita ya Dkt. Samia Suluhu Hassan namna ambavyo inafanya vizuri sana. Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan mwezi wa Kumi utusubiri, wewe kaa tu, sisi kwako ni kukupitisha moja kwa moja, kwa sababu, umepita, na kazi yako ambayo unaifanya vizuri sana ni njema, tunajisikia kunenepa tu kila mahali kwa jinsi unavyofanya vizuri, tunajidai popote tunapopita. Hongera sana Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja. (Makofi)