Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mbinga Vijijini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. BENAYA L. KAPINGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi nami niweze kuchangia. Ninaanza kwa kuunga mkono hoja hii kwa asilimia mia moja. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa, nampongeza Mheshimiwa Waziri Mkuu na Waheshimiwa Mawaziri waliopo katika ofisi hii; Mheshimiwa Lukuvi na Mheshimiwa Ridhiwani Kikwete kwa kufanya kazi nzuri sana pamoja na Waheshimiwa Naibu Mawaziri pamoja na wataalam wote katika Wizara hii ya Ofisi ya Waziri Mkuu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kipekee nampongeza Mheshimiwa Waziri Mkuu mwenyewe kwa namna anavyofanya kazi vizuri. Hongera sana Mheshimiwa Waziri Mkuu. Wamesema wenzangu hapa, umelitendea haki sana Taifa hili, na ni kweli kabisa. Sisi wananchi wa Mbinga tunakupongeza mno. Mara kadhaa wewe mwenyewe umekuwa shahidi, unafanya ziara pale Jimboni, Wanambinga wamekupokea kwa bashasha, na ile bashasha siyo ya bure, ila ni kwa sababu ya mambo mazuri unayolifanyia Taifa hili ikiwemo Mbinga Vijijini. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi wa Mbinga tunayo kawaida, tunapofarijika na kazi nzuri, huwa tunagalauka ama kukwara. Sasa wananchi wa Mbinga mara kadhaa wamekuwa wakifanya hivyo, wakigalauka na kukwara kumpongeza Mheshimiwa Waziri Mkuu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa kipekee nawaomba Wataalamu wa BAKITA wayaweke maneno haya mawili kwenye msamiati sahihi wa Kiswahili. Kwa nini ninasema hivi? Mwaka 2024 Mheshimiwa Rais alifanya ziara Mkoani kwetu. Dada yangu Mheshimiwa Jenista aliongoza wananchi kugaragara. Nikisema kugaragara, ninapunguza ubora wa tendo lenyewe hili, ni kugalauka na ndiyo maana nawaomba sasa wataalam wa Kiswahili waliweke hili neno kama lilivyo, kugalauka. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukisema kugaragara inakuwa ni kitu fulani kinachoshusha hadhi yake, lakini kugalauka ni kuonesha kuridhika na mambo mazuri ya yule mtu unayemgalaukia pale mbele. Kwa hiyo, nawaomba wataalam wa Kiswahili waliweke neno hili au maneno haya kwenye Kiswahili ili yasilete usumbufu kama yalivyoleta mwaka 2024. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, maana yake alipokuja Mheshimiwa Rais, Mheshimiwa Jenista kuonesha kuridhika na utendaji mzuri wa Mheshimiwa Rais, akawaongoza akina mama wale wa Mkoa wa Ruvuma kugalauka na kukwagha. Khaa! Ilileta shida kweli kweli! Watu wakasema hee, heee! Kumbe ni jambo la kawaida kabisa.
MWENYEKITI: Mheshimiwa Benaya, hilo jina kugalauka ni la Kiswahili?
MHE. BENAYA L. KAPINGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kugalauka siyo neno la Kiswahili, ni maneno yanayoingiliana na ya Kiswahili. Kingoni na Kimatengo humo humo ndani yake, ndiyo maana sasa nikawaomba hawa wataalam wetu wa Kiswahili waliingize kwenye kamusi. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, unajua mambo mazuri kama haya ni lazima tuyaweke ili watu waendelee kujifunza, tusiyaache tu hivi hivi halafu yanaenda kuleta shida, watu wanaona kwamba siyo kawaida, kumbe sisi kule kwetu mtu akifanya hivyo maana yake anaonesha kuridhika na heshima kubwa juu ya mtu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hili linafanyika hata kwenye level ya familia. Mtu anafanya siyo ili uonekane au kujipendekeza. Ah ah, Hili ni jambo la kawaida ku-appreciate kile kitu kizuri alichofanya huyu. Kwa hiyo, natumia nafasi hii kuwaomba wataalam wetu wa Kiswahili wayaweke maneno haya ya kukwagha na kugalauka kwenye kamusi ili Watanzania wote wajifunze utaratibu huu mzuri unaofanyika Mkoani Ruvuma. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, naishukuru sana Serikali hii ya Awamu ya Sita, imefanya mambo mengi mazuri. Hata tukianza kuyataja hapa hatutamaliza leo. Nasema tu, naishukuru sana Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wetu mpenzi na Mama yetu, amefanya mambo mengi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa niseme tu kuhusiana na suala la migogoro. Mheshimiwa Rais mara kadhaa amekuwa anatoa maelekezo ya namna gani Serikali hii anayoisimamia iweze kuwahurumia Watanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pale kwangu nilikuwa na mgogoro mmoja wa muda mrefu, wa Ndika. Naishukuru sana Serikali hii ya Awamu ya Sita, kwanza kwa kutuletea viongozi wazuri. Mkuu wa Mkoa, Kanali Abbas, Mkuu wa Wilaya, Mheshimiwa Makori, Mkuu wa Wilaya ya Nyasa na Mkurugenzi wa Halmashauri yetu, wamefanya hii kazi ikawa nyepesi mno. Mgogoro wa miaka saba hadi nane ulitatuliwa kwa muda mfupi sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii wananchi wa Maeneo yale ya Ndika wana amani, hawana tena vita na hamna tena kupigana risasi. Naipongeza na kuishukuru sana Serikali hii ya Awamu ya Sita. Baada ya kumaliza huu mgogoro, kulikuwa na maelekezo ya kuyafanyia kazi. Wenzetu wa TFS walipewa wajibu na Wakurugenzi kwa nafasi yao, Mkurugenzi wa Nyasa na Mkurugenzi wa Mbinga DC naye alikuwa na maeneo yake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kwa sababu miezi sita ndiyo imekamilika hivi karibuni, imekamilika tarehe 12 juzi, wale wananchi ilikuwa walipwe fidia. Wananchi wale wamekuwa watulivu, wameendelea kusubiri na bado wanaendelea kusubiri. Naomba sana wahusika sasa walimalize hili jambo moja kwa moja ili wananchi wale waendelee kunufaika na utendaji mzuri wa Serikali hii ya Awamu ya Sita. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa tulipofikia, naishukuru sana sana Serikali hii kwa utendaji huu mzuri na leo hii ile vita na mgogoro vimetulia kabisa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine naipongeza sana Serikali hii ya Awamu ya Sita. Mwaka jana 2024 Mheshimiwa Rais alipofika tulimwomba kuhusiana na suala la barabara. Tulikuwa na ujenzi wa Barabara ya Amani Makolo – Ruanda hadi Lituhi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Rais alivyo msikivu, pale pale aliachia fedha ambazo zimeanza kufanya kazi. Tayari kilometa tano zimeshakamilika, lakini ile barabara ina kilometa 35, pia awamu ya pili ina kilometa karibu 50. Naiomba sana Serikali sikivu ya Awamu ya Sita, kwa vile mkandarasi yupo site, basi iharakishe kutoa zile fedha ili kile kipande kilichoanza cha kilometa 35 kiweze kukamilika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi wamenituma, nishukuru kwa hizo kilometa za awali ambazo tayari lami inaonekana, lakini naendelea kuiomba Serikali, zile kilometa zilizobaki sasa watoe fedha kwa sababu mkandarasi bado yuko site ili ikamilike. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia, tunaishukuru Serikali kwa upande wa pili kutoka Ruanda hadi Lituhi na Lituhi hadi Ndumbi, tayari mkandarasi amepatikana, kilichobaki ni mkandarasi kupewa advance ili aanze kazi. Tunaishukuru sana Serikali hii ya Awamu ya Sita kwa sababu inaona, inasikiliza na inatekeleza. Tunaishukuru sana Serikali hii. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile, nashukuru mwaka ule wa 2020, Mheshimiwa Rais, huyu huyu Mama Samia alikuja pale akaiona barabara nzuri ya kutoka Kigonsera – Matiri hadi Mbaha yenye kuleta maendeleo, akatamka, “nitaijenga barabara hii kwa lami.” Nafurahi kusikia kwamba tayari mkandarasi wa upembuzi yakinifu wa barabara hii, tayari yuko site anafanya kazi. Kilichobaki sasa, ni muda mfupi tu, natambua Serikali hii itaweka fedha na hii barabara nayo itapata lami. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, vivyo hivyo kwa barabara inayotoka Mbinga kwenda hadi Litembo, na barabara hii nayo inaenda mpaka Nkiri – Nyasa kwa dada yangu Mheshimiwa Eng. Stella Manyanya, zote hizi tayari wakandarasi wako site na wanaendelea kufanya kazi ya upembuzi yakinifu, ninawashukuru sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile, niongelee suala la barabara ya Nyoni kwenda hadi Maguu. Barabara hii nayo inakwenda Kipapa inamalizikia hadi Ziwani Nyasa. Barabara hii ni ya kimkakati, Mheshimiwa Rais alipofika nilimwomba apeleke fedha kwa sababu tayari upembuzi yakinifu umefanyika na ipo kwenye Ilani, tayari kazi imeanza kufanyika. Tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais ili sasa ikikamilika ombi letu la yeye kuja kuifungua barabara hii, liweze kukamilika miaka mitano inayofuata. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, na ninaunga mkono hoja. (Makofi)