Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

Hon. Rehema Juma Migilla

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Ulyankulu

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

MHE. REHEMA J. MIGILLA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipatia nafasi nami jioni hii niweze kuchangia Hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu. Awali ya yote, napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa uhai na afya ambayo inanifanya niweze kusimama katika Bunge lako Tukufu kwa jioni hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa moyo wa dhati na kipekee kabisa, napenda kumshukuru Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa maono yake na mapenzi yake mema kwa Watanzania hususan wananchi wangu wa Ulyankulu. Ameweza kutufanyia mambo makubwa sana tangu alipoingia madarakani, nami kama Mbunge wa Jimbo la Ulyankulu, tangu niingie madarakani kuna mabadiliko makubwa sana na maendeleo makubwa sana ambayo yamepatikana katika Jimbo langu la Ulyankulu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Ulyankulu ya mwaka 2020 siyo Ulyankulu ya mwaka 2025. Kiufupi niseme, naishukuru sana Serikali ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan na wasaidizi wake wote ambao wanamsaidia katika kuhakikisha wananchi wa Tanzania na wa Jimbo la Ulyankulu tunapata maendeleo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia, napenda kumshukuru Mheshimiwa Waziri Mkuu na timu yako, kwa kweli wanafanya kazi nzuri ya kuhakikisha huduma zinawafikia wananchi kwa ukaribu na kwa raha zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kuchangia mchango wangu wa leo kwa kuanza na sekta ya kilimo. Jimbo la Ulyankulu kwa kiasi kikubwa asilimia kubwa ya wananchi wake kama siyo yote, wanashiriki kwenye shughuli ya kilimo kama ndiyo shughuli yao mama ya kuwaingizia kipato.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunapenda kuishukuru Serikali yetu kwa mambo makubwa sana ambayo imeweza kuyafanya kwenye sekta ya kilimo, kwani tunaona sasa hivi tayari kuna mbolea ya ruzuku ambayo imetolewa kutoka shilingi 150,000 mpaka 60,000. Hayo ni mabadiliko makubwa na ni faida kubwa sana kwa wananchi wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia, tunaona pembejeo zinatolewa na zinakuja kwa wakati katika Jimbo langu, na bado wananchi wanapata katika maeneo yao yaliyo karibu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia, kwenye zao hili la tumbaku tunaona bei elekezi imetolewa na wananchi wetu wanauza tumbaku yao kwa bei ambayo ina manufaa kwa maendeleo yao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikisalia hapo hapo kwenye tumbaku, pamoja na haya mazuri yote ambayo yamefanyika kwenye hili zao letu la tumbaku, bado zao hili linaonekana kama halina tija kwa mkulima wetu. Kwa mfano, mwaka jana 2024 ilinyesha mvua kubwa sana. Mwenyezi Mungu alitupatia baraka ya mvua, lakini baraka hii ilikuwa ni kilio kwa wananchi wangu wa Ulyankulu ambao wamelima tumbaku.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mashamba mengi yalilowa na bani zao nyingi zilianguka, hivyo wakawa kwenye madeni na kwenye sonona kubwa sana, lakini kupitia Mama Samia, akatuletea ruzuku ya tumbaku kufidia yale madhila ambayo wananchi wameweza kuyapata. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi tunavyoongea, tulimsikia Mheshimiwa Bashe hapa amesema zimetengwa shilingi bilioni 13 kwa ajili ya kuwalipa fidia ya ruzuku wakulima wote wa tumbaku hapa Tanzania, lakini cha ajabu mpaka hivi leo tunavyoongea wakulima wangu wa tumbaku hawajalipwa hii ruzuku na hatufahamu ni kwa nini? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mbaya zaidi wananchi na wakulima hawa wamesainishwa saini hewa bila kujua amesaini shilingi ngapi ambazo atakwenda kulipwa. Sasa Mheshimiwa Waziri Mkuu na Mheshimiwa Waziri wa Kilimo tunataka tufahamu, hivi kuna usiri gani kwenye hii fedha? Kama mlisema hawa wakulima watalipwa kulingana na idadi ya mifuko ya mbolea waliyotumia, leo mnakwenda kuwasainisha wakulima wetu saini hewa, kuna usiri gani hapo? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo mtu anasaini hajui anaenda kusaini shilingi ngapi na kwa nini mfanye hivyo? Mnafanya makusudi au vipi? Leo mtu anasaini lakini hajui analipwa shilingi ngapi? Je, ukienda mkulipa fedha ambazo ni tofauti na idadi ya mifuko ambayo ametumia, ataenda kudai wapi wakati tayari ameshaweka saini yake?

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba Mheshimiwa Waziri Mkuu na Mheshimiwa Waziri wa Kilimo mtueleze hili suala na wananchi wetu wajue, kuna watu wamesaini miezi miwili iliyopita na mwezi mmoja uliopita lakini mpaka leo wanaendelea kuhangaika hawajui fedha zao watalipwa lini? Naomba hili suala lichukuliwe kwa umuhimu mkubwa na wananchi wetu wajulishwe kwa nini mpaka leo hawajalipwa hizi fedha? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hapo hapo kuna kampuni ya wazawa ya Voedsel inayonunua tumbaku. Mpaka hivi tunavyoongea, wakulima waliolima tumbaku msimu wa mwaka jana 2024, hawajalipwa fedha zao na Kampuni ya Voedsel mpaka leo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nina wakulima wangu 86 kutoka Kijiji cha Usonga hawajalipwa hata shilingi moja na tayari tuna msimu mwingine na hivi tunavyoongea, soko linaenda kuanza tarehe 28, lakini hawajalipwa. Naomba hawa wananchi wangu waweze kulipwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna suala lingine la barabara. Naendelea kuipongeza Serikali kwa kuweza kutuongezea bajeti kwenye Halmashauri yetu ya Wilaya ya Kaliua. Mwaka 2020 bajeti yetu ya barabara ilikuwa ni shilingi milioni 985, lakini leo tunavyoongea, tayari bajeti ya barabara imefika shilingi 4,300,000,000. Kwa kweli haya ni mafanikio makubwa. Tunachoiomba sasa Serikali yetu, iweze kuzitumia hizi fedha vizuri na hizi fedha ziweze kufika huko chini kwa sababu barabara nyingi zimeharibika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mvua ya mwaka 2024 imetuharibia barabara karibia zote, lakini mpaka hivi leo tunavyoongea, kuna baadhi ya wakandarasi hawajalipwa na wamekimbia kwenye maeneo. Vifusi vingi viko kule na havijasambazwa, barabara hazijatengenezwa na wakandarasi wamekimbia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii inasababisha kuwaongezea wananchi wetu mzigo wa maisha, wanasafiri kwa tabu sana kwa sababu inawalazimu waweze kutembea kwenye njia ambazo ni ndefu sana kwa sababu zile njia ambazo zina vifusi hazipitiki. Hivyo, naiomba Serikali kusimamia na kuiongezea TARURA bajeti ili iweze kuzihudumia barabara zetu kwa umakini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia, naipongeza Serikali, imeweza kuanzisha hii Samia Bond ambayo inawawezesha wakandarasi wa ndani kupata fedha kuanzia 30% mpaka 70%. Hali hii itawezesha barabara zetu kutengenezwa kwa umakini, lakini pia na hawa wakandarasi wawepo site na wawe na uhakika wa kuweza kutengeneza hizi barabara zetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivyo, naishukuru Serikali, lakini pia naomba Serikali isilegelege, ihakikishe inaweza kufunga mkanda kuhakikisha hizi fedha zinatoka na wakandarasi wanapata ili waweze kwenda site.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ni suala la maji. Ni nia ya dhati kabisa ya Mheshimiwa Rais kuhakikisha anatutua kina mama ndoo kichwani, lakini suala hili kwa watu wa vijijini bado kabisa. Mimi nikirejea kwenye Jimbo langu la Ulyankulu, lina Kata 15 lakini katika hizi Kata 15 tumepata mradi wa maji wa bwawa la Ichemba ambao unagharimu shilingi bilioni 3.98, lakini mpaka hivi tunavyoongea mradi huu umeingiziwa fedha shilingi 598,000,000, fedha ambayo ni ndogo kabisa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tujue kwamba Jimbo la Ulyankulu, maji kutoka chini ya ardhi yako chini sana, mbadala wake ni maji kutoka Ziwa Victoria. Mheshimiwa Waziri Mkuu, maji kutoka Ziwa Victoria yameshafika kwenye Jimbo la Kaliua lakini sasa ninachoshangaa, umbali wa kutoka Kaliua mpaka Ulyankulu ni kilometa kama 98, imewezekana kuyafikisha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kwa nini haya maji yasifike kwenye Jimbo langu ilhali kuna mradi mfano kwenye Jimbo la Nanyumbu pale wametengewa shilingi bilioni 38 ili kupata maji kutoka kwenye Mto Ruvuma ambao ni kilometa 100? Wakati huo huo, inawezekana kabisa kuyatoa maji katika Mji wa Kahama ambapo kutoka kwangu kwenye Jimbo la Ulyankulu mpaka Kahama ni kilometa 42, kwa nini inashindikana? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naiomba kabisa Wizara ya Maji na Mheshimiwa Waziri Aweso ananisikia, haya maji yaweze kufika na Ulyankulu ili na wananchi wetu wafungue maji kutoka bombani. (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante.

MHE. REHEMA J. MIGILLA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja. (Makofi)