Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. MARY F. MASANJA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi hii ili nami niweze kuchangia katika bajeti ya Waziri Mkuu. Awali ya yote, namshukuru sana Mwenyezi Mungu ambaye ametupatia afya njema na leo tumeweza kukutana hapa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kipekee kabisa, nichukue nafasi hii kumpongeza na kumshukuru sana Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa aliyoifanya ya utekelezaji wa Ilani ya uchaguzi ya mwaka 2020/2025. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukitazama miradi mikubwa ya kimkakati iliyofanyika katika Mkoa wa Mwanza na Kanda ya Ziwa kwa ujumla, siwezi kuielezea hapa kwa siku moja. Miradi ni mikubwa na imetekelezwa kwa zaidi ya 98%. Nikienda kwa upande wa Kigongo - Busisi katika Sekta ya Ujenzi tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais. Daraja hili liliachwa likiwa 25% na mtangulizi wake, lakini hivi ninavyoongea, daraja hili sasa limefikia 98%. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wanamwanza tunajiandaa kwenda kusheherekea ufunguzi wa daraja hili. Daraja hili lina ukubwa wa kilometa 3.2, Tanzania hapa halipo, Afrika Mashariki nadhani ndiyo tunaongoza, lakini ukiliangalia linatupa sifa nzuri ya nchi yetu na linatangaza utalii wa Kanda ya Ziwa hususan Mkoa wa Mwanza. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, faida ya daraja hili itakuwa ni faida nyingi, lakini kikubwa daraja hili linakwenda kuokoa vifo vya mama na mtoto. Wakati ule tunatumia kivuko, akinamama walikuwa wanakaa zaidi ya masaa sita pale kwenye kivuko wanasubiri kivuko na wakati huo wanakimbizwa kwenda kujifungua. Leo hii pale tutatumia dakika chache tu na akinamama watawahishwa na usalama wa mama na mtoto utapatikana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiacha hilo, kuna faida nyingine ya uchumi. Uchumi utakuwa mkubwa na utafungua mikoa ya jirani ikiwemo Mkoa wa Geita, Mkoa wa Kagera, Simiyu, na mikoa ya jirani inayozunguka daraja hilo kwa maana ya Mkoa wa Mwanza. Pia nchi jirani zitaweza kufaidika kwa sababu kutakuwa na urahisi sasa wa kuzunguka kwa maana ya kupitisha biashara mbalimbali kwenda ndani ya nchi na nje ya nchi. Ukiacha faida hizo, daraja hili linaenda kuokoa muda ambao ulikuwa unapotea kwa kusubiri kivuko kwa muda mrefu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie sasa kuhusu Sekta ya Nishati. Sisi akinamama tunamshukuru sana Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kututua kuni kichwani. Tangu mababu na mababu zetu wamekuwa wakitumia nishati chafu ya kupikia. Mama zetu hasa upande wa Kanda ya Ziwa wamekuwa wakisingiziwa wengine wana mambo ya kishirikina kwa ajili ya macho mekundu, lakini moshi huu huu unaenda kuathiri mapafu. Mapafu haya yanapata athari kubwa na madhara mengine makubwa ya kiafya na matokeo yake wananchi wetu wanatumia gharama kubwa kwenda kujitibia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii tunamshukuru Mheshimiwa Rais kwa sababu ameibeba kama ajenda ya kitaifa, na hii ajenda ni ya kidunia, lakini mama ameibeba kama ajenda ya kitaifa. Leo hii hakuna mama asiyejua matumizi bora ya nishati safi ya kupikia. Tunamshukuru sana, lakini naiomba Wizara ya Nishati itusaidie akinamama kwa sababu sasa kuna mwamko mkubwa wa kutumia nishati safi ya kupikia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, changamoto iliyopo ni kwamba bei ya ku-refill au kuongeza ile gesi ni kubwa sana, ukizingatia uchumi wa akinamama upo chini sana. Tunaiomba Serikali iendelee kuongeza ruzuku ili hawa akinamama wasiishie kukaa na mitungi ikiwa mitupu. Waendelee kurudi kwenye hali ile ya zamani ambayo kwa sasa hivi ninavyoongea tayari tunaenda kuokoa ukataji wa miti ovyo, na mazingira ambayo yalikuwa tayari yanaendelea kuharibika, sasa hivi yanaenda kuimarika vizuri. Naiomba Serikali yangu Tukufu ilione hili ili iendelee kutoa ruzuku katika eneo hili. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba pia nizungumzie suala zima la Sekta ya Uchukuzi. Sekta ya Uchukuzi kwa mujibu wa sensa ya mwaka 2022, Mkoa wa Mwanza ni mkoa wa pili Kitaifa kwa kuwa na idadi ya watu wengi. Ukiacha hilo, Mkoa wa Mwanza ni wa pili kwa kuchangia pato la Taifa. Pia, Mwanza imepakana na mikoa zaidi ya mitano ambayo huwa inatumia suala zima la matumizi ya uwanja wa ndege wa Mwanza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kinachosikitisha ni kwamba, hakuna route ya kutoka Mwanza kuja Dodoma na kurudi Mwanza. Wasafiri wanaotoka Mara, Simiyu, Shinyanga, Kagera, na Geita inatulazimu kufunga safari zaidi ya masaa 10 kutoka Mwanza kuja Dodoma kufuata huduma za Kiserikali kwa maana ya wananchi, lakini hata sisi wenyewe Waheshimiwa Wabunge tunapokuja Bungeni. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia kama Mkoa huu tu pekee ni wa pili kwa kuchangia, inachangia 7.2%, kwa nini kusiwepo na route inayotoka Mwanza kuja hapa Dodoma na kurudi? Ni nini kinachokwamisha? Pia, naiomba Wizara ya Uchukuzi, pale Mwanza kuna upanuzi wa jengo la abiria. Upanuzi wa jengo hili utasaidia Uwanja huu upate sifa ya kuitwa Uwanja wa Kimataifa wa Mwanza. Tunakwama na tunakwamisha uchumi mkubwa katika Mkoa wa Mwanza kwa sababu Mwanza ni lango zuri kwa suala la utalii. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, watalii wanazunguka, wanapita Arusha, wakitoka Arusha wanaenda kilometa zaidi ya 500 kwenda kuiona Serengeti, lakini ukiwa Mwanza kwenda Serengeti ni kama kilometa 134, umefika lango la Serengeti. Hata hivyo, kwa sababu uwanja huu siyo wa Kimataifa, ndege kubwa haziwezi kushuka pale kwa sababu tu ya jengo la abiria ambalo mpaka sasa limekwama.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naiomba Serikali yangu, kupitia Wizara ya Uchukuzi iweze kulitilia maanani suala hili ili tufungue uchumi wa Mwanza na usafiri wa anga uweze kuimarika katika Mkoa wa Mwanza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niendelee kumshukuru Mheshimiwa Rais kwa namna ambavyo aliweza kuzindua huduma ya usafiri wa reli. Usafiri huu ni wa raha, ni usafiri ambao hakuna Mtanzania ambaye hajaufurahia. Sote tumeufurahia na wote tumeonja raha ya usafiri wa reli.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa sababu ametupa heshima kubwa Kitaifa na Kimataifa. Sasa hivi usafiri wa reli hakuna mtu asiyeupenda, na nimeiona bajeti ya Mheshimiwa Waziri Mkuu ya kwamba vipande vilivyobaki ni vipande vya Mwanza – Isaka, kuna Makutupora – Tabora, Tabora – Isaka na Tabora – Kigoma. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunatamani sana reli hii tuonje utamu wanaoupata wengine kwenye upande wa pili. Nasema hivyo kwa sababu tukiweza kuunganisha reli hii ikakamilika, kwanza tutaokoa muda, na uchumi utakuwa pamoja na kurahisisha muda wa wananchi kusafiri kutoka sehemu moja kwenda nyingine kwa wakati. Pia tutapunguza ajali…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MWENYEKITI: Ahsante.
MHE. MARY F. MASANJA: Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, naunga mkono hoja. (Makofi)