Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mtera
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. LIVINGSTONE J. LUSINDE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kunipa nafasi hii. Namshukuru Mungu sana kwa kunipa mimi, na Waheshimiwa Wabunge wewe afya njema pamoja kwa ajili ya kujadili bajeti ya Mheshimiwa Waziri Mkuu na bajeti nzima ya nchi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pongezi nyingi sana zimetolewa kwa Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, nasi pia kwa niaba ya wananchi wa Jimbo la Mvumi tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa sababu, kama kulikuwa kuna kimeo cha muda mrefu na kichomi ilikuwa ni barabara yetu ya Ntyuka Junction - Mvumi Mission - Kikombo kwenda kutokea Handali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninayo furaha kwamba Mheshimiwa Rais ametupatia pesa na sasa hivi mkandarasi yupo site anafanya mobilization vifaa vyake ili aweze kuanza ujenzi mara moja. Tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa kuliona hilo. Kwa hiyo, Waheshimiwa Wabunge mkija kutibiwa tena pale hamtakutana na vumbi, mtakutana na mkeka tu kutoka hapa mpaka Mvumi unaunganisha Kikombo Makao Makuu ya Jeshi unakuja kutokea Chamwino Ikulu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumpongeze sana Mheshimiwa Waziri Mkuu na Baraza zima la Mawaziri, wamefanya kazi kubwa kumsaidia Mheshimiwa Rais kutafsiri maono yake pamoja na ndoto zake, lakini nataka niseme mambo machache hapa. Jambo la kwanza, nchi ikitaka kubadili hali ya uchumi wa nchi kwa haraka na uchumi wenyewe siyo ule unaoonekana kwenye karatasi, bali ule unaohusianisha watu na unaozingatia kilimo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kilimo pekee yake ndiyo kinaweza kikabadilisha maisha ya watu wengi kwa haraka, na ni maono ya Mheshimiwa Rais akaona kwamba ni vyema kuwekeza nguvu kubwa kwenye kilimo, Mheshimiwa Rais akanunua magari kwa Maafisa Ugani wa mikoa yote, akanunua pikipiki kwa Maafisa Ugani wa kata zote, akanunua mashine za kupimia udongo kujua afya ya udongo, karibu kata zote zimegawiwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Rais hakuishia hapo, akanunua photocopy machine, kwamba ukipima udongo unaweka kwenye photocopy machine inatoa majibu kwamba shamba hili linahitaji uweke mbolea gani? Linahitaji ulime zao gani ili mkulima aweze kupata tija? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, bado hatuoni hizo mashine na hizo pikipiki zikifanya kazi ambayo Mheshimiwa Rais ameikusudia. Leo hii tukitaka tutembee kwenye kata za Waheshimiwa Wabunge, ni kata ngapi ambazo tutakuta Afisa Ugani amebandika pale wakulima aliowatembelea, vipimo vilivyopimwa na tija waliyopata? Ni tofauti kabisa na mawazo ya Mheshimiwa Rais. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tunaitaka Serikali kusimamia haya maono yatokee kwa vitendo ili yaweze kusaidia wananchi kusonga mbele. Kama huwezi kuuza nje mazao makubwa kama mkonge, kahawa, korosho, na zabibu kwa maana ya mvinyo, unainuaje uchumi wa hilo Taifa?
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni maono ya Mheshimiwa Rais kwamba Maafisa Ugani watembee kwa wakulima. Leo tukifanya sensa, hatuwezi kukuta Afisa Ugani, siyo tu kwa wakulima, hajatembea shamba la Diwani; hajatembea shamba la Mbunge; hajatembea shamba lake yeye mwenyewe. Sasa hii siyo sawa. Hatumtendei haki Mheshimiwa Rais, na hatutendei haki maono ya Mheshimiwa Rais. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, juzi Mheshimiwa Rais amekaa hapa na Maafisa Ugani akaagiza, anzisheni Wakala wa Ugani kwa maana ya namna ya kufanya kazi, itakuwa rahisi. Tuwe na wakala kama ilivyo TANROADS na TARURA. Tuwe na wakala wa namna hiyo kwa Maafisa Ugani ili kuweza kuwa na speed ya kuwakagua. Mpaka leo nataka kujua, imefikia wapi? Maana tunaona mpaka tunamaliza mpo kimya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kuzungumza hapa hapa kwenye kilimo. Mheshimiwa Rais ametupatia shamba kubwa sana lipo Mlazo pale. Ukienda utaona matokeo, vijana wa BBT wameripoti, wamelima alizeti, zimekubali, lakini tuna tatizo. Tatizo letu kubwa ni kwamba wataalamu wetu hawapiti kushauri. Kazi yao kubwa ni kupanga tu mwaka huu ushuru gunia moja shilingi 5,000/=. Shilingi elfu tano, umelima wewe! Elfu tano, umemsaidia nini huyu mkulima?
Mheshimiwa Mwenyekiti, huyu mkulima hujamsaidia kumshauri, hujamsaidia mbegu, hujamsaidia mbolea, hujampimia ardhi yake, wewe unapanga tu kwamba mwaka huu tunataka ushuru wa gunia uwe shilingi 5,000. Hivi hii ndiyo elimu mliyopewa jamani! Elimu gani hii ambayo mmepewa ya kupanga tu bei bila kusaidia watu? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, angalia kero anazopata mkulima. Mkulima analima kwa tabu, hakuna mtu anamshauri, akishapata mazao yake akiyaleta sokoni, anakutana na barrier pale Mkonze, anakamatwa, anaambiwa gunia limezidi kilo 20, unalipa shilingi 500,000.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tukubaliane leo kwenye Bunge na Mheshimiwa Waziri akisimama atusaidie hapa, kwani gunia Serikali inavyolitambua ni kipimo au ni kifungashio? Kama gunia ni kipimo, kwa nini watu wa TBS wanaruhusu gunia linalozidi kilo mia kuwa sokoni? Kwani anayelileta gunia ni mkulima? Wanaolileta gunia ni watu wengine, limegongwa muhuri wa TBS, mkulima ananunua, akilijaza linaingia kilo zaidi ya mia moja, anakuja anakamatwa anaambiwa faini shilingi 500,000, vinginevyo mazao tunayataifisha. Sasa mnataka kutuambia kila mkulima pamoja na shida na tabu za kulima, kila mkulima awe na mizani? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, kila mkulima anunue mizani aweke shamba? Huu utaratibu wa wapi? Hii siyo sawa. Haya mambo ndiyo Mheshimiwa Rais anayakataa kila siku. Katika Serikali kuna baadhi ya watumishi wetu huku chini wanaonea watu. Haiwezekani, kwa sababu gunia hakutengeneza mkulima. Kwa nini tusimshtaki yule anayetengeneza gunia kwamba umetengeneza gunia ambalo linachukua zaidi ya kilo 100?
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama kweli tunataka kutenda haki, kwa nini Maafisa wetu wa Vipimo hawakai kwenye mizani anapokuja kuuzia? Akifika pale anaambiwa bwana utalipa ushuru kulingana na kilo utakazopima, limeisha. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nini twende tuwadhulumu watu mazao yao? Inakuwa tabu kwenye kulima, na tabu kwenye kuuza na tukumbuke kwamba mkulima wa kawaida siyo mfanyabiashara wa mazao. Yeye anakuja kulima na kuuza mwaka mmoja mara moja, anataka zile pesa zisaidie familia yake. Kwa hiyo, hili jambo mimi nimeona limekuwa likileta uchungu sana na malalamiko makubwa sana kwa wananchi. Ni lazima tusimamie haki za wakulima. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ninalotaka kulizungumza hapa, ni kuhusu mfumo wa kupambana na majanga kwenye kilimo. Hii ni tofauti na mifumo mingine yote ya taasisi. Leo hii ukitokea moto, utaona zimamoto wanaenda kwa haraka sana. Ikitokea nguzo zimeanguka, TANESCO wataenda kwa haraka sana, lakini ikitokea janga kwenye kilimo, ndugu zangu ni matatizo makubwa sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo kikianguka viwavijeshi, anatakiwa Afisa Ugani wa Kijiji amwandikie Afisa Ugani wa Kata, Afisa Ugani wa Kata amwandikie Afisa Ugani wa Wilaya, Afisa Ugani wa Wilaya amwandikie DAS, DAS amwandikie RAS, RAS aandike Wizarani, hilo shamba utalikuta? Huwezi kulikuta. Yaani huo mlolongo wa kuandikiana na kupeana taarifa utakuta shamba limeshakuwa jeupe. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, halafu bahati mbaya sana, fidia za Serikali ni za ajabu sana. Leo hii mtu akiua tembo analipa karibu shilingi milioni 15 au 30, lakini huyo huyo ndovu akiua mtu, kifuta machozi ni shilingi milioni moja. Leo hii mtu akifanya abortion anashtakiwa kwa mauaji kwamba ameua mtoto ambaye alikusudiwa kuzaliwa, lakini shamba la mtu likiliwa kabla halijaiva wakati wa kufanya uthamini yale mazao, wanasema asingepata gunia 40. Kwa nini asingepata gunia 40 wakati yeye ndio uwezo wake wa shamba lake?
Mheshimiwa Mwenyekiti, tuthaminishe sawa sawa. Leo binadamu anauliwa, mnasema shilingi milioni moja kifuta machozi. Shamba zima ekari 20 zimeliwa, mnalipa gunia moja. Hivi gunia moja mtu anaweza akala mwaka mzima? Huu utaratibu wa wapi? Hiyo siyo sawa! (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nashauri kwamba Serikali tusimamie haki za wakulima. Ikitokea matatizo, tuwe serious kama tunavyochukulia matatizo ya sehemu nyingine. Unavyopeleka mgonjwa kwa speed kuwahi matibabu, ndivyo upeleke ndege ya kuua ndege kwenye mashamba ya wakulima kwa sababu ukichelewa wakishamaliza mazao, huyu mkulima hana kitu. Halmashauri haina kodi na wala mwenyewe hawezi kutunza familia yake pale. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine, tumezungumza sana kuhusu ajira na hili mimi nalirudia tena hapa. Nilishauri kama tunaona hatuwezi kuwaajiri Watanzania wote kupitia Ajira Portal, ajira hizi tuzigawe kwenye halmashauri. Kila halmashauri, wewe ajira zako 20, wewe ajira zako 10, wewe ajira zako 30. Wakikosa kupata mtu mwenye elimu hiyo ambayo inatakiwa kwenye hiyo ajira, watairudisha ile ajira kuipeleka mkoa mwingine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, huu utaratibu wa kuwaleta wote Pamoja, hivi, hivyo vyeti mlivyowapa mnavikagua unasema hiki cheti chako original kabisa, halafu baadaye unamwingiza kwenye mtihani wa dakika moja ndiyo umkoseshe mtoto ajira! Haiwezekani. Tunawa-stress watoto wetu. Hii siyo sawa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wewe umekagua cheti chake; cheti cha Ualimu mtu amesoma zaidi ya miaka mitatu, yaani wewe unakuja kumpa mtihani wa dakika mbili, unafuta yote haya! Masomo yote aliyosoma miaka mitatu yanaonekana hayana maana kwa sababu ya mtihani wa dakika mbili! Hapana, hii siyo sawa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama uwezo wetu tunaajiri watu 15, tuseme ajira 15,000 tunazigawa katika halmashauri, nendeni muajiri bila kusumbua watu, mnawajaza hapa. Wanakuja wanalala nje, watoto wa watu wanakuja na nauli za kukopa, wakija hapa wanaishi maisha magumu sana. Hii siyo sawa. Sasa badala ya kuondoa kero, tunazalisha kero. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hii inakuwa siyo sawa, kwani ukisema kwamba tuna uwezo wa kuajiri watu 15,000, leteni vyeti, ukavikagua, ukawaajiri, si jambo limeisha? Sasa leo hii unakuja unanipa mtihani, mtihani wenyewe wa dakika moja, halafu huu huu mtihani wa dakika moja unaniondolea sifa yote niliyosoma, halafu huyo huyo aliyefeli mwaka huu, amekosa; mwakani anafaulu. Hiyo inakuwa siyo sawa. Kwa hiyo, ni lazima tuwatendee haki kabisa wananchi wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia, nimezungumza sana kuhusu lango la utalii. Kutoka hapa kwenda Iringa ukitumia barabara ya lami uje kuingia mpaka kwenye mbuga za Wanyama, mzunguko wake ni mkubwa.
Mheshimiwa Mwenyekit, tuna barabara ya mkato, tunaishauri Serikali kwamba ukitoka hapa mpaka Mpunguzi kwa Mheshimiwa Anthony Mavunde, ukitoka pale Mpunguzi nenda moja kwa moja, nyoosha moja kwa moja mpaka Huzi, ukitoka Huzi nenda moja kwa moja Manda, ukitoka Manda jenga pale daraja la kuingia kwenye mbuga. Hii inakuwa rahisi sana kwa watalii, na sisi huku tutaguswa na maendeleo kwa haraka kwa sababu na sisi mbunga yetu huku tunakutana na Mzee Lukuvi kule pamoja na kwamba ananong’ona pale. Tunaomba watusaidie kurahisisha lango la utalii lipitie Ilangali badala ya kupitia sehemu nyingine. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja, ahsanteni sana kwa kunisikiliza. (Makofi)