Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

Hon Abubakar Damian Asenga

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kilombero

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

MHE. ABUBAKARI D. ASENGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa nafasi. Maana ni bahati iliyo njema kupata nafasi jioni hii kuchangia katika hotuba ya bajeti ya Ofisi ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, na wenzangu wengi hapa wameshachangia mambo mengi makubwa kudhihirisha kwamba Serikali ya Chama cha Mapunduzi ipo kazini na inaendelea kufanya kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, huko nje naona kuna baadhi ya watu wachache wanafikiri Wabunge wa CCM kazi yao ni kusifia, lakini tunasifia kutokana na yaliyotokea na kutendeka. Wabunge tuna akili timamu, na kama sisi ni waongo, ina maana wananchi wetu watatukuhumu. Mimi nasifia hapa kwamba Serikali imefanya mambo makubwa na Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan amefanya mambo makubwa, na nitayataja. Kama nasema uongo, wananchi kule watanijua kwamba huyu Mbunge amesema jambo hili lipo hapa, wakati halipo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tunataka kuwapa moyo wananchi waendelee kutuelewa ambavyo tunavyopongeza Serikali yetu kwa sababu ni Serikali ya Chama cha Mapinduzi, ipo madarakani chini ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan na Mawaziri wote, Waziri Mkuu na Mawaziri wote wanaomsaidia, Waheshimiwa Wakuu wa Mikoa na Waheshimiwa Wakuu wa Wilaya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi tulivyoomba 2020 kuchaguliwa kuwa Wabunge, zipo ajenda zilikuwa zinagusa Jimbo letu la Kilombero na yalikuwa mambo makubwa yanayotugusa wananchi wote. Tunavyosema leo, yamekamilika na kwamba changamoto lazima ziendelee tu mpaka mwisho wa dunia siyo lakini yale makubwa yamekamilika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikisema barabara ya lami Kidatu mpaka Ifakara imekamilika, wananchi Jimboni wanajua Mbunge anasema kweli au anasema uongo. Nikisema tumeshasaini mkataba wa kujenga barabara ya Ifakara kwenda Ulanga, wameona kwenye vyombo vya habari tumesaini mkataba. Tukisema mkandarasi wa barabara ya Ifakara ya lami kutoka Ifakara kwenda Mlimba, wanajua mkandarasi yupo site. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikisema leo tangu Wilaya ya Kilombero iumbwe safari hii ya Mama Mheshimiwa Dkt. Samia awamu hii ndiyo tumejenga Hospitali ya Wilaya, wanaiona Hospitali ya Wilaya. Nikisema vituo vya afya viwili; tulikuwa na kituo cha afya kimoja, miaka yote tumejenga viwili wakati wa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, wanajua Kituo cha Afya cha Msola Station na Kituo cha Afya cha Mbasa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tukisema umeme ulikuwa na changamoto za kukatika, Waziri wa Nishati amekuja, tumepewa karibu shilingi bilioni 25, tumejenga substation, umeme zaidi ya mwaka haukatiki, wanayo substation ipo Ifakara na umeme haukatiki. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi Mbunge siwezi kusema kwamba umeme haukatiki, halafu umeme unakatika na mwaka huu ni mwaka wa hukumu. Kwa hiyo, Mbunge unavyozungumza hapa, unazungumza jambo la ukweli. Tangu dunia iumbwe katika kipindi hiki cha miaka mitano tumejenga sekondari za O’ Level 12. Yaani nimemzidi mpaka Mheshimiwa Waziri Aweso kwa Shule za Sekondari.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeona Mheshimiwa Waziri Aweso anamwomba Mheshimiwa Rais, Kata zake nyingine hazina sekondari. Mimi nilishamaliza Kata 19 sekondari za O’ Level na ninajenga nyingine za kurudia. Tunajenga Sekondari za advance tano, tumejenga shule ya ufundi hizi za amali imekamilika na wanafunzi wameanza kusoma. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna mradi wa maji wa Kiburubutu shilingi bilioni 41 unajengwa Ifakara Mjini, Kata tisa kuongoza kutatua changamoto ya maji. Wilaya tangu imeumbwa ilikuwa haina Kituo cha Polisi cha Wilaya, tumeshakijenga mpaka viyoyozi (AC) Mheshimiwa Rais kanunua.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna Mahakama ya Wilaya ya ghorofa. Kwa mara ya kwanza gari la zimamoto wananchi wameliona, kwa mara ya kwanza magari ya Polisi Ambulance na kadhalika. Kwa hiyo, nataka kutia msisitizo, hapa tunasema changamoto haziwezi kwisha, maendeleo ni hatua. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kule Ifakara kwangu kuna maeneo wanapima viwanja, wananchi wanaanza kujenga. Wakijenga, wanataka Barabara, wanataka umeme, wanataka maji. Hiyo ni kazi yetu viongozi kufanya. Tunajua changamoto yao kubwa ni kazi yetu kama Bunge kusimamia na kuishauri Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baadhi ya wananchi wachache wanafikiri kwamba ukiwa Serikalini, basi ni kuiba, ni wizi. Wanatushauri sana Wabunge tuwaambie Serikali, anapotokea mwizi, mbadhirifu, akamatwe, achukuliwe hatua. Hii ni kazi ambayo sisi sote tunaweza kuifanya. Kwa hiyo, hilo la kwanza nataka kusisitiza kwamba mambo makubwa yamefanyika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili ni changamoto na matarajio. Katika bajeti ya Serikali ya Waziri Mkuu, nimesoma karibu kurasa zote. Nimeona kuna changamoto na tunasema hapa ili Serikali izichukue, iziandike ikazifanyie kazi, na kuna fedha nyingi ya mwakani itakuja itayabeba mengine katika Uchaguzi Mkuu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, la kwanza, nataka kuzungumza hapa kuhusu sekta ya kilimo. Nimeona Mheshimiwa Waziri Mkuu amezungumzia hapa. Sisi tuliomba kiwanda kipya cha sukari karibu shilingi bilioni 700 tumejengewa kiwanda kipya cha sukari, lakini tunaiomba Serikali, na Mheshimiwa Naibu Waziri wa Kilimo namwona hapa. Nimekutana na wakulima, na juzi wakulima walikuja Dodoma hapa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna changamoto ya ulipaji bei, kuna siasa inataka kuchezwa katika kilimo cha muwa. Tunaomba Serikali imulike, nimemwambia Waziri wa Kilimo, nimemwambia Naibu Waziri na ninawaambia viongozi wote wa Serikali watazame.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna watu tulivyobadilisha sheria ya kuruhusu kuingiza sukari kwa ajili ya kuwa-favor wananchi wasinunue sukari kwa bei mbaya, wanatumia gap hiyo kufanya siasa na siasa hizo zinahusisha wakulima wengi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nina asilimia karibu 60 ya wananchi wangu ambao ni wakulima wa miwa. Sasa wamejenga kiwanda kipya cha sukari shilingi bilioni 700. Mkulima alikuwa anauza muwa tani shilingi 110,000 kwa shilingi 103,000, leo wanaambiwa shilingi 87,000. Mkulima akishauza muwa, anasubiri sukari iuzwe, sukari ikishauzwa analetewa fedha zaidi iliyobaki. Sasa hivi anaambiwa hakuna makato.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mkulima huyo huyo alikuwa anauza kwa sucrose ya kumi ya muwa anapata shilingi milioni karibu tatu kwa gari, sasa hivi anaambiwa karibu shilingi 600,000. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wazee wa Kilombero pale wameniita wakaniambia, Mbunge hiki kiwanda kipya kinaweza kisifanye kazi, watu watakosa moyo wa kulima muwa endapo Serikali haijachukua hatua za kutosha. Nimeshukuru sana Bodi ya Sukari, niliambiwa ilienda kufanya mkutano kule.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nami ninasisitiza hapa tumejenga kiwanda kipya cha shilingi bilioni 700. Jambo kubwa ilikuwa ahadi yetu, sasa lazima tukawasikilize wakulima hawa na Mheshimiwa Waziri ameniambia au Naibu Waziri, tutaenda kukaa nao, tutawasikiliza ili kiwanda kile kiweze kulipa kama ilivyokuwa inalipa mwanzo shilingi 110,000 kwa tani na wananchi wapate fedha zao kwa wakati. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine tuna changamoto na TARURA. TARURA hawajapata fedha wakandarasi wengi kila Mbunge hapa anazungumza. Mimi nina imani sana na Waziri wa TAMISEMI, najua akija hapa atakuja na solution ya vituo vya afya vya kimkakati ambako sisi tunajenga kule Michenga na Lumemo kituo kimoja cha afya, lakini Mheshimiwa Waziri wa TAMISEMI atakuja na majibu kuhusu TARURA.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa Jimboni jana, nimepita Ifakara Mjini sehemu inaitwa Mbasa Mjini, Ifakara ambako Mbasa Kwa Mfuga Punda Soko la Kariakoo, wanapita wananchi pale kama maji kwenye bomba, mkandarasi amejenga karavati ameondoka ameacha bila kufunika. Nimeongea na viongozi wa TARURA, mkandarasi yule hajalipwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimepita Katindiuka Ofisi ya Kata pale kuna Barabara, kuna makaravati. Mji wangu ule wa Ifakara upo mbondeni kidogo, barabara ili ipitike miaka yote lazima uichonge uweke changarawe uweka na makaravati. Sasa hali ile kwa Kata zote 19 kwa kweli ni mbaya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba viongozi wangu wa TARURA tuweke angalua bajeti ya kueleweka na mpango maalumu wa kilometa kumi kumi katika Kata tupate kilometa 190. Itasaidia Jimbo letu na kuliondoa na barabara za TARURA. Hii ni changamoto kubwa sana. Pale pale Ifakara Mjini ukitoka Lumemo ukivuka tu daraja la Lumemo pale barabara ya TANROAD unaenda Mlimba ina mashimo manne makubwa na jana nimemtumia Chief of TANROADS barabara hiyo na ameiona. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa nishati, ninafurahi ninamshukuru sana Mheshimiwa Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, kwani mara zote amekuja Jimboni kutufanyia siasa nzuri. Katuondolea tatizo la kukatika kwa umeme, vijiji vyote tumeshafikisha umeme. Namwomba katika vile vitongoji 15 najua wakandarasi wapo kule, wanaendelea, a-push kidogo nipate vitongoji vyangu 15, mkandarasi a-supply umeme katika vitongoji na juzi nilikuwa katika Kitongoji cha Upendo na Tupendane Michenga, hali bado ni ngumu sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi ni miongoni mwa watu waliopata Mradi wa TACTIC. Mji wa Ifakara unakua, Mji wa Ifakara benki hazifungwi Jumamosi na Jumapili kwa sababu tu ni wakulima wazuri na ni wafugaji wazuri. Tumepata soko jipya, Waziri wa Viwanda na Biashara amekuja pale, Mheshimiwa Jafo amezungumza pale na amevaa suti imempendekeza kabisa, na akatuambia Asenga linakuja hili soko Ifakara Mjini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba Serikali ituletee lile soko haraka kabisa, kwa sababu pale wafanyabiashara wa Soko la Ifakara Mjini wameshapisha ujenzi, wameenda kusogeza fremu zao mbali, wameacha lile eneo. Tumeambiwa soko zuri la ghorofa katika Mradi wa TACTIC linakuja. Tunaomba kazi hiyo ianze haraka iwezekanavyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mji wetu wa Ifakara umesongamana, na barabara ya Mjini pale haina uwezo tena. Tunaomba sana Serikali itusaidie Mradi wa TACTIC wa stendi mpya kama ambavyo ilivyopanga. Mheshimiwa DC pale naona anasimamia vizuri, anafuatilia sana jambo hilo. Mradi huu wa TACTIC utaambatana na barabara za lami. Tunaomba nao uanze kwa wakati, kwa sababu kwa kweli ni changamoto kubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, huku nikimalizia, nataka kuzungumzia suala la maafa. Tunamshukuru Mwenyezi Mungu, mpaka sasa Halmashauri ya Ifakara na Jimbo la Kilombero hatujapata maafa kwa kiasi kikubwa, lakini mvua zimeanza. Naendelea kuwaomba na nilimwomba Mheshimiwa Naibu Waziri Mkuu anisaidie, TANESCO walijenga tuta upande mmoja wa mto, wajenge na upande wa pili. Nimepeleka barua Ofisini kwake, wanisaidie ili tuweze kupunguza hilo suala la tuta. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kuzungumza kwenye suala la ardhi. Naishukuru sana Wizara ya Ardhi, kwa kweli kwa kiasi kikubwa imepunguza sana changamoto za migorogoro ya ardhi, na tangu wakati ule, tangu Mheshimiwa Lukuvi akiwa Waziri, tulianza kupata hati za kimila. Wananchi wakaona ardhi yao imepanda thamani, na kasi kubwa, wanauza. Tunawasihi kila siku wasiuze ardhi yao, lakini sasa kuna changamoto moja ya Baba Askofu pale Kanisani, nilizungumza Mheshimiwa Rais alivyokuja tarehe 4 Agosti, mwaka 2024.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Serikali isikilize jambo hili ili iweze kutusaidia. Kwa heshima kubwa, naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja, ahsante sana. (Makofi)