Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mbulu Mjini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. ZACHARIA P. ISSAAY: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi. Kwanza nichukue nafasi hii kuungana na Wabunge wenzangu wote kumshukuru sana Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Rehema aliyetujalia wakati huu muhimu na nafasi hii muhimu ya kipekee.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa namna ya kipekee, pia naipongeza na kuishukuru sana Serikali yangu kwa kazi kubwa iliyofanyika kote nchi nzima na hasa Jimbo la Mbulu Mjini. Sisi Kamati ya TAMISEMI tumetembea karibu mikoa yote, na kazi kubwa imefanyika. Naipongeza pia Ofisi ya Waziri Mkuu na Wizara, Idara mbalimbali zilizopo chini yake pamoja na Baraza zima la Mawaziri kwa kazi kubwa iliyofanyika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nami nichukue nafasi hii kutoa mchango kwa baadhi ya maeneo. Kazi kubwa imefanyika. Eneo la kwanza ni eneo la pembejeo kwenye kilimo. Kuhusu pembejeo ya ruzuku, tunaiomba sana Serikali ije kwa wakati na kwa aina mbalimbali kwa kadiri ya mahitaji ya wananchi na wakulima kote nchini. Eneo hili tukiboresha, tutakuza uchumi wa wananchi, lakini pia kilimo chenye tija kwa kila mwananchi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kadiri tunavyofahamu, Watanzania walio wengi ni wakulima na eneo hili mara nyingi tumeboresha, na kazi kubwa imefanyika. Ushauri wangu ni kwamba, pembejeo ziletwe kwa wakati, na pia vile vifungashio vya kilo 25 kwenye mbolea ni vya muhimu sana kwa ajili ya uwezo wa wananchi na wakulima wetu, lakini pia ngazi za kata kuwa na mawakala kwa ajili ya kurahisisha upatikanaji na ufikaji kwa wananchi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine kwenye kilimo ni Jenga Kesho iliyo Bora, (BBT). Ni kwamba tumewekeza, na tunataka kuona matokeo na tulitarajia kwa sasa tunafika kwenye ngazi nyingine za halmashauri baada ya center kuboreka na vituo tulivyoanzisha. Eneo hili ni eneo lenye tija sana kwa sababu linagusa sekta hiyo ya kilimo. Kwa sasa tufanye tathmini ya Jenga Kesho iliyo Bora kwenye kilimo na namna gani tunaondoa vikwazo vilivyopo na namna ya maboresho zaidi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na muda, eneo hili tukifanyia kazi, tukaleta matawi kwenye halmashauri zetu, na kwenye wilaya, itasaidia sana kwa sababu ya kupanua wigo, lakini kwa manufaa zaidi kwa Watanzania hasa kundi hili la vijana na wakulima wenye nia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine ni ujenzi wa Vyuo vya VETA. Tulijenga VETA kwenye halmashauri nyingi, tunaipongeza sana Serikali. Sisi ambao hatukupata fursa hii, tulipoambiwa FDS zetu kwa maana ya vyuo vya maendeleo ya wananchi, vitakuwa VETA B, bado tunahitaji maboresho kwa ajili ya kukamilisha kwanza ujenzi ule wa miundombinu, lakini kuboresha mitaala na mwisho wa yote kuleta tija ili mwanafunzi wa vyuo vya maendeleo ya wananchi awe ni sawa na yule wa VETA katika taaluma wanayoipokea. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ni miradi ya Barabara. Eneo hili tumeumia sana. Naishukuru Serikali, japo tulipata wakati mgumu sana kule Mbulu Mjini na Mbulu Vijiji. Barabara ya Mbulu - Garbabi ambayo imekwama muda mrefu, walau Serikali imeanza kuchukua hatua za kutafuta fedha na kuweza kunusuru hiyo hali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nadhani hao wakandarasi tunaowapa kazi, pia kama tatizo ni malipo ya awali, basi tutazame eneo la kuboresha sheria zetu na malipo yale ya awali ili tukishawalipa wale kwa namna ya pekee, basi kazi ifanyike kwa wakati kuliko mradi mdogo wa kilometa 25 unakwama kwa miaka mitatu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo hili nilifikiri ni Mbulu tu, kumbe nilipoenda Singida pia wamekwama kilometa 25. Kule Lindi wamekwama kilometa 25, maeneo kadhaa wamekwama kilometa 25, miradi imesimama muda mrefu. Ombi langu kwa Serikali ni kwamba itazame utaratibu wa namna ya kuingia mikataba na namna ya kulipa fedha za awali ili walau miradi inayoanza ipatikane kwa wakati na gharama za ucheleweshaji na gharama mbalimbali tuweze kuepuka. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaipongeza Ofisi ya Waziri Mkuu pia kwa mikopo ya vijana. Huu mradi wa mikopo ya vijana kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu bado haujaeleweka vijijini. Vijana wengi hawapo kwenye mtandao, vijana wengi hawaelewi hii ni fursa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kama inawezekana, kuwe na forum kwa maafisa vijana katika halmashauri yetu, lakini na vipindi maalumu vya vyombo vya uhabarishaji kwa maana ya media mbalimbali ili vijana wetu wengi wafahamu suala hili la mikopo Ofisi ya Waziri Mkuu, na kwa sababu fedha zile ni nyingi na zinasaidia vijana ili waweze kunufaika kwa namna inayowezekana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, fedha za TARURA, kuna mradi upo Jimboni Mbulu na maeneo mengine tumekuta tulipokwenda Shinyanga. Tunaiomba Serikali itazame utaratibu wa kuboresha fedha za TARURA namna ya kuongeza fungu kwa fedha za TARURA. Fedha za Mfuko wa Jimbo ni karibu miaka miwili zimeyumba. Tunaomba fedha za Mfuko wa Jimbo zitolewe, kuna mradi umekwama sana kule Mbulu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza Mheshimiwa Waziri Mchengerwa, walau yule mkandarasi wa Mbulu Mjini amepewa fedha juzi, lakini hatua hii imechelewa sana kwa zaidi ya mwaka, na ni mita 600 tu pamoja na daraja hapo Katikati, lakini wananchi wamepata adha kubwa sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, japokuwa Serikali tayari imechukua hatua, tunaipongeza Serikali, lakini tutazame maboresho zaidi ili kuokoa hali hii inapotokea wakati fulani fulani. Fedha hizi za tozo na Mfuko wa Jimbo ndiyo fedha zinazotusaidia sana sisi Wabunge wa Majimbo kwa sababu tunapotembea walau wananchi wanatuomba ahadi mbalimbali, lakini kwa namna ya pekee zinatutatulia kero kwa wananchi wetu. Tumeongeza barabara nyingi sana kupitia TARURA fedha za TARURA kwa sasa hazitoshi. Tunaiomba sana Serikali itazame upya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ni mafao ya wastaafu. Tunaipongeza Serikali, kwa mafao ya wastaafu wale waliokuwa wanalalamikia kikokotoo, Serikali imesikia, tunampongeza sana Mheshimiwa Rais kwa kilio kile kusikika, lakini pia kuboresha. Eneo hili la wastaafu wale wa zamani wanalipwa shilingi laki moja na kitu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hali ya kawaida, shilingi laki moja na kitu au shilingi laki moja, haimsaidii yule mstaafu. Kwa hiyo basi, tulikuwa tunaomba kama inawezekana, Serikali itusaidie. Hawa ni wastaafu wazee waliotumikia Taifa hili, na bado wanaiomba Serikali yao iwaone kwa jicho la pekee ili mafao yao ya yaweze kuangaliwa na yaboreshwe kulingana na hali ya sasa, kwani nao wanakabiliwa na changamoto lukuki. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine ni malipo ya viongozi wa Serikali za Mitaa. Wenyeviti wa Mitaa na Wenyeviti wa Vijiji tumewatumia muda mrefu. Hawa viongozi wameomba sana, wameikumbusha sana Serikali, tumezungumza kwenye vikao, Waheshimiwa Madiwani wote hao ni nguzo muhimu katika Serikali yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mwaka huu wa fedha kupitia bajeti zetu hizi, tuendelee kuona eneo hili ni la umuhimu mkubwa wa kuweza kuongeza fedha na walau wapewe hata kama ni kidogo ili wajisikie nao ni sehemu ya viongozi wa kuchaguliwa. Vilevile, kila kinachofanyika, humkosi Mwenyekiti wa Mtaa, humkosi Diwani, na wote hawa wanaunga mkono juhudi za Serikali. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la ajira na usaili kwa vijana, sisi tunaokaa na wananchi wachaguliwa, tunasikia mambo mengi sana. Eneo hili la usaili limelalamikiwa sana na vijana nchini. Eneo hili litazamwe upya, kwani eneo hili linaliliwa, eneo hili limeumiza, familia wamekata tamaa kusomesha vijana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa namna ya pekee, tunaomba Serikali itazame utaratibu mzuri ambao hauleti manung’uniko lakini pia kwa kuwa wao walishasoma wakapewa vyeti, eneo hili lisiwe kigezo kikubwa sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, inasikitisha mwalimu mwanafunzi anafundisha shule jirani, anakaa miaka mitatu kwenye kufundisha anafaulisha vizuri, lakini kwenye usaili hajafanikiwa. Yule aliyepo kijiweni yawezekana Mungu amemsaidia, amefaulu, lakini kwa namna ya pekee unakuta yule kijana aliyeajiriwa hakuwa ametoa hata uzalendo wa kusaidia kizazi cha hao vijana waliopo shuleni, na kwa namna ya pekee tunakatisha tamaa hao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hebu tutazame vijana hawa wengi waliopo kwenye kujitolea. Je, leo wakiondoka kwenye nafasi za kujitolea, kwa nafasi hizo tutakuwa tumepata pengo kiasi gani? Kwa namna ya pekee, ili walau tuongeze jitihada za uzalendo wa watu kutumikia bila kujali anapewa nini?
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hayo, nashukuru. Kutokana na mambo mengi niliyonayo, nitachangia kwa maandishi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja. Ahsante sana kwa nafasi hii. (Makofi)