Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

Hon. Zuena Athumani Bushiri

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

MHE. ZUENA A. BUSHIRI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi nami nichangie bajeti hii ya Mheshimiwa Waziri Mkuu. Nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mama yetu Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa anayoifanya kwa kuifungua nchi yetu kwa miradi mingi sana nchini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi ni Mjumbe wa Kamati ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma. Tumezunguka kukagua miradi mingi sana, miradi ya kimkakati kama Mradi wa CAG, Daraja la Busisi, Bwawa la Mwalimu Nyerere pamoja na miradi mingine mingi sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nitakuwa mchoyo wa fadhila kama sitampongeza Mheshimiwa Waziri Mkuu pamoja na Mawaziri wenzake wote kwa kazi nzuri wanazozifanya katika kuhakikisha kwamba wanamsaidia Mheshimiwa Rais katika utekelezaji wake wa kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia, nampongeza Mheshimiwa Spika wetu wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na Naibu Spika na wenyeviti wote kwa jinsi mnavyoliongoza Bunge vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitaongelea Mkoa wangu wa Kilimanjaro. Mkoa wetu wa Kilimanjaro sisi tumepata fedha shilingi trilioni 1.2. Fedha hizi zinatekeleza miradi 2,345 ikiwemo miradi ya maji, miradi ya miundombinu na miradi mingine mingi. Haijawahi kutokea katika Mkoa wa Kilimanjaro kupata fedha nyingi sana za miradi ya maendeleo kama kipindi hiki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, miradi hii imegusa katika maeneo mengi kuanzia ngazi ya matawi, kata, wilaya, na mkoa. Kwa kweli tunamwambia Mama, tunashukuru sana, Kilimanjaro tupo pamoja naye na atatuona kwa kuwa sisi tumemshukuru kiasi kikubwa, tutamlipa deni lake ifikapo Oktoba. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitaanza na mradi wa maji wa Same - Mwanga na Korogwe. Ni hivi juzi tu ambapo Mheshimiwa Rais alikuja kuzindua mradi ule. Huu ni mradi ambao umewakwamua wananchi wa Same na Mwanga kwa tatizo la maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni ukweli usiopingika kwamba mradi huu ulikuwa unasuasua siku nyingi sana, lakini mama kwa jinsi anavyomjali mwanamke, ameupigania mpaka leo mradi huu umefunguka na tumeanza kupata maji. Pongezi sana kwa Mheshimiwa Rais. Niseme neno moja tu, chanzo cha maji haya ya mradi huu kinatoka kwenye Ziwa Jipe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Ziwa Jipe lina changamoto ya magugu, nilishaliongelea tena katika Bunge lako hili. Kutokana na changamoto hiyo ya magugu yanavyoendelea kuwa mengi, inaonekana, baada ya muda, maji yatakuwa kidogo. Naiomba Serikali ya Chama cha Mapinduzi kupitia Mheshimiwa Rais ihakikishe inatoa magugu yale ili zoezi la mradi huu liwe endelevu bila kukwama mahali popote. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niongelee kuhusu mikopo ya wanawake. Kwanza nampongeza Mheshimiwa Rais kwa kuendelea kuruhusu mikopo ya 10% (4:4:2). Mikopo hii inakwamua wananchi kiuchumi hasa akina mama wahangaikaji. Katika Manispaa yetu ya Moshi tumepata vikundi 32 ambavyo tayari vimeshakopeshwa, imetoka shilingi bilioni 1.171. Tunampongeza sana Mheshimiwa Rais kwa kuwa sasa hivi wananwake wa Kilimanjaro, wafanyabiashara wakubwa, nadhani mnatuona pale tumebeba ndoo za maparachichi, vitunguu maji, tumebeba kila kitu sisi tunauza, tunachotaka ni pesa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, wanawake kwa kupata mitaji hii, wanajikwamua kiuchumi. Naomba sasa Maafisa Maendeleo ya Jamii wawasaidie wale akina mama wa chini ambao hawawezi kujaza vizuri ule mfumo, inawachukua muda mrefu sana ili kukamilisha utaratibu mzima. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ni kuhusu afya, na niongelee Hospitali ya Rufaa ya KCMC. Nampongeza sana Mheshimiwa Rais kwa kujenga jengo la mionzi. Wagonjwa wetu wote wa Kanda ya Kaskazini na jirani wakipata matatizo ya mionzi ni lazima waende Ocean Road, lakini sasa hivi jengo hili limejengwa kwa shilingi bilioni 5.3 na limefikia 94.5%, kilichobakia pale ni vifaa ambavyo vinatakiwa viingie ili kazi ianze. Wananchi wa Kilimanjaro na wananchi wa mikoa jirani kwa maana ya Kanda ya Kaskazini pamoja na nchi jirani ya Kenya, nadhani watakuwa wametoka katika matatizo hayo ya kwenda Ocean Road.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya afya, nitarudi tena katika Hospitali yetu ya Rufaa ya Mawenzi. Tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais, tena sana, kwani ametusaidia sisi akina mama kwa kuhakikisha amekamilisha kwa 88% jengo la mama na mtoto. Hapo zamani ulikuwa ukienda Mawenzi unakuta kitanda kimoja, wamelala wanawake watatu na watoto wao. Sasa hivi japo halijakamilika lote, lakini hali inaridhisha kwa akina mama kulazwa katika wodi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jengo hili likikamilika kwa sababu sasa hivi sakafu ya chini inafanya kazi, ghorofa ya kwanza inafanya kazi, bado ghorofa ya pili na ghorofa ya tatu, ikikamilika wananchi watafurahia huduma hiyo ambayo itawasaidia sana na ninadhani kila mwanamke atataka kujifungua sasa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme tu, Kilimanjaro sisi Mama hatudai. Tuna deni la Mheshimiwa Rais, na deni letu tutalilipa ifikapo Oktoba katika sanduku la kura. Tunamwombea kwa Mungu, Mwenyezi Mungu ampe afya njema, ampe maisha marefu tukutane siku hiyo ndiyo atajua kwamba Kilimanjaro ametugusa. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, niseme ahsante sana na ninaunga mkono hoja. (Makofi)

MWENYEKITI: Mheshimiwa Zuena kabla hujakaa, tuweke rekodi zetu vizuri. Hapa kuna mahali ulisema Mradi wa CAG, nadhani ulimaanisha Mradi wa SGR.

MHE. ZUENA A. BUSHIRI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kabisa ni SGR nisamehe katika hilo. (Kicheko/Makofi)