Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

Hon. Sebastian Simon Kapufi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mpanda Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

MHE. SEBASTIAN S. KAPUFI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Awali ya yote, naomba nianze kwa kuunga mkono hoja na niipongeze Ofisi ya Waziri Mkuu kwa ujumla wake, nimeipitia bajeti yote na nimeona imesheheni maeneo tofauti tofauti ambayo yanaeleza utekelezaji wa ilani ya chama chetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nianze na suala linalogusa idadi ya watu. Kwa idadi ya Watanzania ambao ni takribani milioni 60, 60% ni vijana ambao wapo chini ya umri wa miaka 25 na karibia 32% ni vijana wa kati ya miaka 10 na 24. Kuwa na idadi kubwa ya watu inaweza ikawa ni faida au ikawa ni balaa, itategemea. Unapokuwa na timu kubwa ya watu ambao ni tegemezi na wachache ndio wanaoshiriki kujenga uchumi wa nchi, taabu ndiyo inaanzia hapo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kinyume chake, ukiwa na idadi kubwa na hasa vijana ambao ni nguvu kazi, wakitumika vizuri ni msaada kwa Taifa, lakini wakikutana na changamoto nao wakawa ni tegemezi, wakahitaji mahitaji makubwa ikiwa ni pamoja na ajira, hilo linakuwa ni bomu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nikiyasema hayo natamani kuendelea kusema kama nchi, na hapa bahati nzuri nina mkakati wa utekelezaji wa Sera ya Taifa Maendeleo ya Vijana ya mwaka 2007, lakini pia ninayo Sera ya Taifa ya Maendeleo ya Vijana ya mwaka 2007. Hizi zote zimesheheni namna ya kuwafanya vijana wasiwe tegemezi, namna ya kuwasaidia vijana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi naomba katika hilo, Ofisi ya Waziri Mkuu ina nafasi kubwa ya kuwasaidia vijana, ikiwa ni pamoja na madirisha mbalimbali, iwe ni mikopo, achilia mikopo ile ya 10% kwa maana ya four, four, two lakini pia na zile fursa nyingine. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wenzangu wazungumzaji wa mwanzo waliendelea kuishauri Serikali, yawezekana fursa hizi wengi wasizifahamu, kwa hiyo, wakati umefika sasa watu hawa waendelee kupewa nafasi ya kuyafahamu madirisha hayo ya kuzifukuzia hizo fursa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niwapongeze wadau mbalimbali wanaosaidiana na Serikali katika kuwanusuru vijana. Nimebahatika kushiriki semina mbalimbali zilizokuwa zikiendeshwa na NGO’s na watu wengine wa namna hiyo. Rai yangu kama ambavyo huko nyuma Serikali imewahi kushauri, hatukatai ushiriki wao, lakini ni pamoja na kuendelea kuwasisitiza waheshimu taratibu, kanuni na sheria, lakini ni wadau muhimu sana katika suala zima la maendeleo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimezungumzia Sera ya Taifa ya Vijana na fursa nzima ya mikopo. Nimelisema hilo kwa sababu gani? Ukizungumzia vijana ambao nimekwambia 60% wapo chini ya miaka 25, imenifanya niende kwenye sekta muhimu ya madini. Bahati nzuri nami ninajihusisha na shughuli ya madini na ninapata faida huko, ninalo la kusema katika hilo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa siku za hivi karibuni, hatukatai tumeendelea kupata wadau mbalimbali ambao wamejielekeza katika suala la uchimbaji wa madini, lakini tatizo ninaloliona kama Serikali, haitaingilia kati kuona namna nzuri kwa sababu taratibu zipo na bahati nzuri hapa nazungumza kwa Ofisi ya Waziri Mkuu, taratibu zipo, lakini sasa hivi kinachojitokeza, vijana hawa ambao nimesema, wasiposhikiliwa vizuri ni bomu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, unapokuta wengi wamejiajiri katika eneo la uchimbaji kama wachimbaji wadogo, lakini maeneo ambapo wamekuwa wakifanya shughuli zao za kila siku, sasa hivi maeneo hayo kwa namna moja au nyingine ni kama yamevamiwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hatukatai mtu mmoja mmoja anaweza akauza, lakini namna ya uuzaji ndiyo hapo ambapo nashauri Serikali itusaidie kwa sababu ni maeneo ambayo unaweza ukakuta yamekuwa yakishughulikia vijana wengi, lakini anatokea labda mwekezaji mmoja, na ukumbuke ni maeneo tumesema ya wachimbaji wadogo wadogo. Kwa namna nyingine yoyote ile anaingia mlango wa nyuma, anafanya ubia na baadhi ya wachimbaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa utakuta maeneo ambayo yalikuwa ya wasaidie wachimbaji wadogo wadogo ambao ni vijana hawa ambao nisema kwamba wasipopewa shughuli ya kufanya itakuwa ni tatizo, sasa hata kama ni maeneo ambayo yamekuwa yakiajiri vijana wengi yameanza kupotea. Hapo ndipo ninapoona ni tatizo kubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikitoka hapo, naipongeza Serikali, mara ya mwisho mimi kwa kupitia Kamati yangu ya TAMISEMI tulipita tukaona suala la shule za wasichana, na kwenye hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, amesema shule za wasichana 26 za Sayansi zimejengwa. Rai yangu, shule hizo ni nzuri, lakini kwa maana tunazungumzia sayansi kama maabara hazitofanya kazi kama hawatoshiriki kwa vitendo, tafsiri nzima ya kuwa na shule za sayansi inapoteza maana. Kwa hiyo, naomba hilo lizingatiwe pia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye huduma ya makundi maalumu nashukuru. Dira ya maendeleo niendelee kuishukuru. Nizungumzie habari ya urejeshaji wa miundombinu iliyoharibika kwa maana ya miradi ya dharura. Bahati nzuri hili limegusiwa na hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, nchi hii yote kwa ujumla wake eneo hili mimi ninaweza nikakwambia kwa mfano kule kwangu yapo maeneo yana miradi mikubwa, mradi wa umwagiliaji wa takribani shilingi bilioni 31.

Mheshimiwa Mwenyekiti, maeneo hayo kama miundombinu imeharibika, yasipoweza kufikiwa, hata tafsiri ya ule mradi mkubwa inapoteza maana. Kwa hiyo, nilikuwa naomba sana, miradi ni mikubwa, miradi ni mingi, imetapakaa kila sehemu na ndiyo maana tulikuwa tunasema hata kama ni wenzetu wa TARURA waendelee kuangaliwa kwa maana ya fedha ili kunusuru maeneo haya ambayo yanaenda moja kwa moja kushiriki suala la maendeleo yetu na uchumi wetu kwa ujumla wake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikiyasema hayo, najua suala zima la madaktari bingwa na huduma hizo za kibingwa, mimi naipongeza Serikali, lakini kwenye hili naomba twende mbali zaidi. Wakati huduma hiyo ikiendelea kuimarishwa kwa sura hiyo, basi tuione ije katika sura ya utalii wa kimatibabu (utalii wa tiba), kwa maana ya hospitali mbalimbali ikiwa ni pamoja na hospitali yetu ya Taifa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tu-take advantage ya hilo kwamba wakati Serikali imefanya vizuri kuhakikisha huduma hizi zimeboreshwa kwa kiwango chake, kama ambavyo sisi Watanzania tumekuwa tukisafiri hapa kwenda China, India, au South Africa tutumie nafasi hiyo hiyo ya kuhakikisha kwamba hilo linakuwa ni fursa au ni dirisha la kufanya utalii huo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama hiyo haitoshi, kwa nchi yetu hii njema wakati tunaendelea kuhubiri kuboresha utalii, yupo mtalii anayeweza akashindwa kufika nchini akiwa hana uhakika wa matibabu, sasa wakati sehemu hiyo ya tiba imeendelea kuimarika kwa kiasi hicho, mimi niseme inakuwa ni nafasi pia ya kuchochea hizo fursa nyingine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nami katika eneo hilo nisisite kuishukuru Serikali kwa…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. SEBASTIAN S. KAPUFI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa muda, na ninaunga mkono hoja. (Makofi)