Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

Hon. Josephine Johnson Genzabuke

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

MHE. JOSEPHINE J. GENZABUKE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi. Kwanza kabisa, namshukuru Mwenyezi Mungu, Mwenye wingi wa Rehema kwa kunijaalia afya na kunipa kibali cha kusimama ndani ya Bunge lako Tukufu. Ninaanza kabisa kwa kuunga mkono hoja. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niungane na wenzangu kwa kumpongeza Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa hotuba yake nzuri. Nampongeza Mheshimiwa Lukuvi na Naibu wake Mheshimiwa Ummy Nderiananga kwa kazi nzuri wanayoifanya. Pia nampongeza Mheshimiwa Naibu Waziri Mkuu, Mawaziri pamoja na Naibu Mawaziri, kwa kazi nzuri wanayoifanya ya kuitekeleza Ilani ya CCM. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nichukue nafasi hii kwa moyo wa dhati kabisa kumpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kazi kubwa na nzuri anayoifanya ya kuwatumikia Watanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia, pongezi nyingine ziende kwa Makamu wake wa Rais, Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango kwa kazi kubwa anayoifanya kwa kushirikiana na Mheshimiwa Rais, kwa kuwatumikia Watanzania. Nawapongeza sana na Mwenyezi Mungu aendelee kuwajaalia afya ili waendelee kuwatumikia Watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imefanya kazi kubwa katika nchi yetu. Imefanya kazi kwenye ujenzi wa barabara nchi nzima. Naomba niseme mafanikio yaliyopatikana ndani ya Mkoa wa Kigoma. Serikali imetujengea barabara ya kutoka Kabingo – Kibondo – Kasulu – Buhigwe, kilometa 260, na barabara hii inaelekea kukamilika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia, kuna barabara ya kutoka Kazilambwa – Chagu – Uvinza. Barabara hiyo nayo iko katika hatua za mwisho, inakaribia kukamilika. Kwa kweli ni jambo la kumshukuru Mwenyezi Mungu. Sisi watu wa Kigoma tulikuwa na shida ya Barabara, lakini muda siyo mrefu kilio hicho cha barabara kitasahaulika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ndani ya Mkoa wa Kigoma, tumeweza kupata umeme wa gridi ya Taifa. Tayari tumeshapata umeme kutoka Nyakanazi, na Kituo cha Kupoozea Umeme cha Kidahwe kilizinduliwa mwaka 2024 na Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango, Makamu wa Rais. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naendelea kuishukuru Serikali kuhusu suala la maji. Maeneo mengi kilio hicho cha maji kinaendelea kupungua. Suala la maji halijakamilika kabisa katika maeneo mengi, lakini kwa kiasi kikubwa Serikali imejitahidi, maeneo mengi wananchi wanapata maji. Ninaamini itaendelea kufanya kazi ili ieweze kukamilisha miradi yote ya maji, kusudi wananchi waondokane na tatizo la maji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naishukuru Serikali, kwani Mkoa wa Kigoma tumepata Chuo Kikuu cha Afya ya Sayansi kwa ajili ya madaktari na wauguzi. Chuo hicho kinaendelea kujengwa. Pia, Uwanja wa Ndege wa Kigoma unaendelea kujengwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mkoa wa Kigoma ni lango kuu la biashara. Tunaamini Uwanja wa Ndege wa Kigoma utakapokamilika, ndege zitaweza kutua usiku na mchana kwenda maeneo mbalimbali. Kwa hiyo, wafanyabiashara kutoka maeneo mbalimbali wataingia Kigoma na wataweza kufanya biashara, kwa sababu utakuwepo usafiri wa kutosha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ya Awamu ya Sita imesaini mkataba wa kujenga SGR kutoka Uvinza kwenda Msongati – Burundi. Reli hiyo ikikamilika, tunaamini kilio cha ubebaji wa mizigo kutoka Dar es Salaam kwenda Kigoma na kuvusha nchi ya Kongo kitakuwa kimekwisha. Ni mambo mengi yamefanywa ndani ya Mkoa wa Kigoma. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumejengewa hospitali za wilaya. Hospitali ya Kakonko, Hospitali ya Kasulu DC, na Buhigwe zimekamilika. Vituo vingi vya afya vimejengwa na vingine vimekarabatiwa sambamba na zahanati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kweli tuna kila sababu ya kumshukuru Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa aliyoifanya ndani ya Mkoa wa Kigoma. Mwenyezi Mungu amjaalie, nasi tunaahidi itakapofika Oktoba, tutamlipa yaliyo mema kwa kumpigia kura nyingi. Kura za Kigoma hazina wasiwasi, tutampigia kura nyingi kwa sababu ameufungua Mkoa wetu wa Kigoma. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niendelee kuzungumzia kuhusu kilimo. Nampongeza Mheshimiwa Waziri Mkuu, amefanya kazi kubwa ya kuhamasisha kilimo cha mchikichi Mkoani Kigoma. Naomba sasa, Serikali iweze kujenga viwanda vya kuchakata zao la mchikichi ili tuweze kupata mafuta yaliyo bora.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu kilimo, hapa pia naomba nimpongeze sana Mheshimiwa Bashe. Mheshimiwa Bashe tunamshukuru, kwani tangu ameingia Wizara ya Kilimo suala la mbolea ni historia. Tunamshukuru sana na Mwenyezi Mungu amjaalie. Kwa kweli tangu mwaka 2024 kilio cha mbolea kwa wananchi hakipo. Tunaishukuru Serikali kwa kuwapatia ruzuku kwa ajili ya mbolea. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi watu wa Kigoma tunalima zao la muhogo, mahindi, na maharagwe. Naiomba sana Serikali iweze kutusaidia, wananchi wameitikia wito wa kulima kilimo cha muhogo, lakini hawana soko kwa sababu soko la muhogo limeanguka. Kwa sasa kilo moja ni shilingi 300 kutoka shilingi 1,000. Tunaomba Mheshimiwa Bashe atusaidie sana kututafutia namna ya kupata ufumbuzi wa soko kwa ajili ya zao la muhogo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nizungumzie kuhusu migogoro ya ardhi. Maeneo mengi kuna migogoro ya ardhi baina ya watu wa hifadhi na wananchi. Naomba Serikali inapokuwa inakwenda kupima mipaka iwashirikishe wananchi. Ikiwashirikisha wananchi kupitia viongozi wao wa vijiji, migogoro hii itapungua.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hivi kuna sintofahamu kati ya watu wa hifadhi na wakulima kwa sababu mipaka haionyeshi ni wapi inaishia? Kwa hiyo, naiomba Serikali iendelee na upimaji wa ardhi na kuweka beacon ili wananchi wajue wanaishia wapi na hifadhi nao wajue wanaishia wapi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, niendelee tu kuwaomba watu wa hifadhi kwamba wasitumie nguvu, wawaelimishe wananchi. Wananchi ni waelewa, ukiwaelemisha taratibu, wanaelewa kuliko kugombana, na wakati mwingine haileti afya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kule kwetu Kasulu eneo la Makere Kusini kuna mgogoro mkubwa baina ya wananchi na watu wa hifadhi. Naiomba Serikali iendelee na upimaji wa ardhi. Vipo vijiji vya Kabulanzwili ambako kuna tatizo kubwa la mwekezaji pamoja na wananchi. Naomba Serikali iendelee na upimaji wa ardhi ili wananchi waweze kuwa huru wanapokuwa wanaenda kulima mashamba yao. Siyo wanaanza kulima, halafu wanafukuzwa kwamba eneo hili siyo la kwao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile, kilio hicho kipo katika Kata ya Kigembe na Kata ya Lusesa katika Vijiji vya Kacheli na Lugufu pamoja na Kigembe. Kwa hiyo, naiomba Serikali ipime ardhi kwa kuwashirikisha wananchi ili kuondoa sintofahamu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho kabisa, naomba kuzungumzia kuhusu UKIMWI. UKIMWI upo, wananchi waendelee kupima na wakigundulika kwamba wana UKIMWI waweze kutumia dawa za kufubaza UKIMWI ili waendelee na maisha yao ya kawaida ya uzalishaji mali na kuendelea kutunza familia zao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema maneno hayo, nakushukuru, naunga mkono hoja. (Makofi)