Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

Hon. Saashisha Elinikyo Mafuwe

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Hai

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

MHE. SAASHISHA E. MAFUWE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipatia nafasi nami niweze kuchangia hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu. Namshukuru sana Mungu kwa kunipatia afya na uzima.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile nampongeza sana Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa kazi kubwa anayoifanya kwenye nchi yetu. Kwa kweli, Mungu ametujaalia jamani, hii nchi ina viongozi mahiri. Tuna Waziri Mkuu ambaye akisimama, anachokiongea kinafanana naye. Anatusaidia, ameisimamia nchi, anamsaidia Mheshimiwa Rais.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza sana Mheshimiwa Waziri Mkuu pamoja na safu ya mawaziri wote, wakitanguliwa na Waziri Mzee wetu Mheshimiwa Lukuvi, ambaye ni mentor wangu, na Naibu Mawaziri. Kipekee nampongeza sana Naibu Waziri Mkuu, Mheshimiwa Dkt. Doto Biteko. Kwa kweli wanamsaidia sana Mheshimiwa Rais. Nawapongeza sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo nimetumwa na nitasema maneno yao walionituma. Katika Jimbo la Hai nimefanya Mkutano Mkuu wa CCM ili kusoma taarifa ya utekelezaji wa Ilani. Haya nitakayoyasema, wao ndio wamenituma. Nimefanya mkutano wa mabalozi wote wa Chama Cha Mapinduzi, wamenituma, nitasema hapa waliyoniambia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi karibuni nimekwenda kwenye kata zote 16, bado moja ambayo nitakwenda kuhitimisha Jumamosi, Kata ya Uroki. Nimefanya mikutano kusoma taarifa ya utekelezaji wa Ilani ya CCM kwenye kata hizi zote. Wanachoniambia watu wa Hai, wanasema, peleka salamu nyingi za shukrani kwa Mheshimiwa Rais. Heshima aliyotupa Mheshimiwa Rais, kazi nyingi alizofanya Jimbo la Hai, kwa kweli tunamshukuru sana sana sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wameniambia nimwambie Mheshimiwa Rais kuwa wanajua wana deni, Mheshimiwa Rais anatudai. Sisi Oktoba ninawahakikishia Waheshimiwa Wabunge wenzangu kuwa Wilaya ya Hai ndiyo itakayoongoza, mapema kabisa, kwa sababu mambo mengi Mheshimiwa Rais ametufanyia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wote humu ndani ni mashahidi, nimekuwa nikiimba na Soko la Kwasadala. Leo ninavyozungumza, tayari tuna barua, TAMISEMI imeshaidhinisha, na wako kwenye mchakato wa kutangaza kwenda kujenga Soko la Kwasadala. Soko ambalo mvua ikinyesha ilikuwa ni kero, leo tumepata shilingi bilioni 11.6. Si hivyo tu, na soko ambalo ndilo linakwenda kulisha Soko la Kwasadala, ndugu yangu Mheshimiwa Bashe kaupiga mwingi sana. Tayari limeshatangazwa Soko la Mula, na kero hiyo inaondoka. Hivi kwa nini tusiseme mitano tena kwa Mama Samia? Hatuna sababu, kwa sababu kazi imefanyika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kule kwangu shule mpya 10 na vituo vya afya nane vimejengwa. Kazi iliyofanyika ni kubwa sana. Kwa kweli sisi tunawahakikishia viongozi wetu mlioko hapa, Mawaziri, Naibu Mawaziri kwamba kazi mnayoifanya ni kubwa sana na sisi tunaendelea kuwaunga mkono.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nina jambo moja la kuchangia sasa baada ya kusema niliyotumwa. Nilikuwa nawaza hapa, wakati nasoma ukurasa wa 14 wa hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, kipengele kinachohusu uzalishaji wa ajira, nikasema, kwa kuwa na sisi tuna ndege zetu, tuna ndege za mizigo, tuna ndege za abiria, hivi kwa nini siku moja tusiitishe vijana wetu kutoka kule Hai, kutoka kule Kisima, na kwingineko, maeneo yote ya nchi yetu, tuwapakie kwenye ndege, nao tukawatafutie ajira kwenye nchi kama kule China na maeneo mengine?

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii itasaidia kuimarisha diplomasia yetu kwa sababu pia diplomasia imetajwa kwenye hotuba hii. Kama hilo linawezekana, itakuwa nzuri sana, lakini kama haiwezekani, tujiulize kinachoendelea pale Kariakoo ni kitu gani?

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli tunaheshimu diplomasia, na ni kweli kwamba vipo viwanda vinajengwa na hawa wenzetu, lakini jamani ndiyo kwenda kuuza hadi madafu! Ndiyo kwenda kuuza hadi herein! Kwa hiyo, wafanyabiashara wetu pale Kariakoo na maeneo mengine, hawa wafanyabiashara walioko maeneo ya Kariakoo kutoka nchi za ugenini wanaofanya biashara ndogo ndogo, naomba sana Serikali iwatazame.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikimbie haraka kwenye eneo hili hili kwa ajili ya kuimarisha ajira. Sisi tuna maeneo ambayo tukiyagusa kule Hai mtatusaidia sana kuongeza ajira, na Mheshimiwa Bashe anisikilize.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Kijiji cha Ngusero tumetenga eka 100. Pamoja na uhaba tulionao ndani ya Jimbo la Hai, tumetenga eka 100 kwa ajili ya kuanzisha bwawa ambalo Kijiji cha Ngusero pamoja na Kata za Weruweru na Rundugai zitahudimiwa na bwawa hili. Namwomba sana atenge fedha ili bwawa hili likajengwe. Amefanya kazi kubwa mno, tunajua ametuletea pale zaidi ya shilingi bilioni 19 kwa ajili ya Skimu ya Mtambo, lakini shilingi bilioni nne hapo hapo, na maeneo mengine anafanya. Najua kwamba feasibility study inaendelea, lakini hiki ni chanzo kipya cha kwenda kutupatia fedha nyingi kwenye kilimo biashara.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hapo, tuna eneo la Mkalama. Nao wametenga acre 100 plus. Tazama wale watu walivyo na uchungu na uzalishaji. Ufinyu wa ardhi tulionao, Mkalama wanazo acre 100. Tuna chanzo kipya cha Mto Mbuguni pale. Wakichukua maji ya Mto Mbuguni wakaleta hapa, wale watu watalima kilimo ambacho kitaongeza pato lao, lakini pato la Taifa ni sambamba na ile miradi yote ya umwagiliaji mliyotuahidi ifanyiwe kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine ni kuhusu Kiwanda cha Kilimanjaro Machine Tools. Nimeshasema hapa na Serikali ilikubali, hebu tukiangalie kiwanda hiki kiweze kuzalisha. Tunaenda kwenye makaa ya mawe ya Liganga na Mchuchuma, najua wanaendelea na utaratibu wa fidia. Tuanze kukipanua kiwanda hiki ili kiweze kuzalisha chuma pale.

Mheshimiwa Mwenyekiti, liko jambo la pembejeo kwenye mikutano yangu yote niliyokwenda. Naomba pia Waziri wa Kilimo anisikilize hapa. Pembejeo wakati mwingine inachelewa, na wakati mwingine inatoka nje ya maeneo yetu. Mwananchi anayeishi kule Soni analazimika kutembea, kupanda gari, tena kipindi cha mvua, kuja kuchukua pembejeo Boma la Ng’ombe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sana, tafuteni mawakala kwenye maeneo yetu ili kuruhusu wananchi wapate huduma hii kwa wakati. Pembejeo hii ya mbolea na vingine, vije kwa wakati kulingana na msimu. Tumekuwa tukisema hili mara kwa mara. Maeneo mengine wanavuna, sisi kule kwetu Hai sasa hivi ndiyo tunakwenda kuweka mbolea. Kwa hiyo, ni lazima mfanye study, mjue mahitaji ya pembejeo, na zije kwa wakati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nina jambo ambalo ni ombi kwa Mheshimiwa Waziri Mkuu. Nafahamu kwamba uwanja wa KIA kulikuwa na mgogoro kati ya wananchi wa KIA, Rundugai, na maeneo mengine. Sasa hivi mgogoro umekwisha na watu wamelipwa fidia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, yapo maeneo ambayo ndiyo yaliyokuwa yanategemewa kwa ajili ya uchumi wa Jimbo la Hai. Wananchi wa Rundugai, wananchi wa KIA na maeneo mengine yanayozunguka hapo; leo wananchi wale wameondolewa, hawaruhusiwi kulima kwenye yale maeneo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaelewa kwamba ni kweli ni maeneo ya uwanja wa ndege, lakini tunaomba turuhusiwe tulime kwa msimu, hata kwa kupewa mkataba kama ambavyo tunatumia mashamba yale ya Kilimanjaro Machine Tools, ya NDC; wananchi huwa wanapewa mkataba wanalima na awamu ikiisha wanapewa tena, tukiwa tunajua kwamba ni mashamba ya NDC. Ifanyike hivyo kwenye mashamba haya ya Kilimanjaro, Kiwanja cha Ndege cha KIA, ili wananchi waweze kupata. Kwa sababu eneo la Rundugai sasa hivi msimu huu, wananchi hawajalima. Kwa hiyo, Mheshimiwa Bashe ajiandae kutuletea chakula cha msaada.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pale KIA hawajalima. Mbaya zaidi, hata mifugo inapoingia kule inazuiliwa. Tunafahamu kwamba tunahitaji uwanja wa ndege na tunaheshimu sana, lakini turuhusiwe mifugo iweze kupata chakula. Maeneo yale yako pembezoni sana, hekta zaidi ya 11,000, na wala huwezi kuona hata uwanja wa ndege uko wapi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, yale maeneo ya pembezoni turuhusiwe watu walime kwa utaratibu maalumu kama ambavyo tulishirikiana wakati wa mchakato wa fidia, nami kama Mbunge nitasimama kuongeza jambo hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine ni kuhusu pensheni ya watumishi. Watumishi wanaomaliza vyuo vikuu kwa kweli walilipwa awamu ya nyuma kabla ya formula ya kikokotoo kipya. Wapo Maprofesa wamestaafu leo wanalipwa shilingi 80,000/= na shilingi 100,000/=; wale watumishi ambao walilitumikia Taifa hili na ambao pensheni yao bado iko chini, nawaomba sana, wangeneze data base ya wazee hawa. Wengi wako huko frustrated kwa sababu ya mazingira na pensheni na formular ambazo ziliwaumiza. Angalieni namna ya kuhuisha hili jambo ili liweze kufanikiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana watumishi wakiongozwa na Mkuu wangu wa Wilaya, Mkuu wa Wilaya mahiri kabisa, Mheshimiwa Hassan Bomboko na watumishi wote Wilaya ya Hai, namna ambavyo wakipokea fedha zinazopelekwa na Bunge wanafanya kazi zao kwa uaminifu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Naendelea kuomba, tazameni maslahi ya Watendaji wa Vijiji, na Wenyeviti wa Vijiji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja. Ahsante sana. (Makofi)