Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

Hon. Yahya Ally Mhata

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Nanyumbu

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

MHE. YAHYA A. MHATA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nami naomba nichukue nafasi hii kukushukuru sana kwa kunipatia nafasi ili kutoa mchango wangu kwenye hii Bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, namshukuru sana Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Rehema, ambaye ameniwezesha siku ya leo nami kusimama katika hili Bunge lako Tukufu kutoa mchango wangu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia, naomba nimshukuru sana mama yetu, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kazi nzuri anayoifanya katika nchi yetu. Mama ameonesha ushupavu, jinsi gani alivyoweza kuichukua hii nchi katika kipindi cha majonzi na kutuweka Watanzania pamoja ili kutuvusha katika hali ngumu tuliyokuwanayo. Kwa kweli, tunamshukuru sana Mama yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi ni mashahidi, miradi mingi ya kimkakati ambayo mama aliirithi kutoka kwa mtangulizi wake mingine ilikuwa ipo chini ya 50%. Leo hii Watanzania tunatembea vifua mbele, miradi yote ya kimkakati ipo katika hatua nzuri. Mradi wa Bwawa la Mwalimu Nyerere leo unafanya kazi, Treni yetu ya SGR ilikuwa haijaanza kazi, imeanza kazi na lile Daraja la Busisi linakamilika. Kwa hiyo, miradi mingi ambayo mama aliikuta, amefanya kazi kubwa sana kuitekeleza. Kwa kweli, tunamshukuru sana Mama yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia, naomba nichukue nafasi hii kumshukuru sana Waziri Mkuu, yeye ndio Msimamizi wa Shughuli zote za Serikali. Miradi yote hii ambayo mama ametoa fedha, kama tusingekuwa na Waziri Mkuu shupavu na mahiri, haya yasingefanyika. Kwa hiyo, namshukuru sana Waziri Mkuu kwa ujasiri na uhodari wake wa kuweza kusimamia shughuli mbalimbali za Serikali katika nchi yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi ni mashahidi, tumemwona Waziri Mkuu mara yupo Kigoma, Bukoba, Moshi na Mtwara. Yote ni katika kusimamia shughuli mbalimbali za maendeleo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile, bila kumsahau msaidizi wake, ndugu yangu Mheshimiwa Biteko, kwa kweli, tuseme kweli mnyonge mnyongeni haki yake mpeni. Ndugu yetu huyu ameonesha uzoefu mkubwa katika shughuli za utawala, na ni msimamizi mzuri. Mimi hupenda sana kusikiliza hotuba zake, zinanifundisha mambo mengi sana. Kwa kweli ni mtu makini na anachokieleza anakitambua. Tunamshukuru sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile, naomba niwashukuru viongozi wote wa Ofisi ya Waziri Mkuu, kwa maana ya Watumishi wa Serikali ambao wameshiriki katika uandaaji wa bajeti hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nichukue nafasi hii kuwashukuru sana Wapigakura wa Jimbo la Nanyumbu. Jimbo langu kwa kweli wameonesha upendo mkubwa sana kwangu. Walikuwa na wasiwasi nami, lakini wasiwasi umewaondoka. Hili nataka nitoe angalizo kwa majimbo mengine, sisi wenye style hii, mkitupatia nafasi tunaweza. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba ndugu zangu wale ambao tulishiriki katika uchaguzi, ambao hawakubahatika, nafasi zinakuja, wachukue fomu, nina imani wananchi watawafikiria. Ahsanteni sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo naomba sasa nichangie yafuatayo: Kama nilivyosema, namshukuru sana Rais wetu kwa kazi kubwa aliyoifanya. Ndani ya Jimbo langu la Nanyumbu, mtu aliyeondoka miaka minne nyuma akija leo atashangaa. Hataamini kama yupo ndani ya Jimbo lile ambalo lilikuwa duni sana kimaendeleo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii ukija kwenye maji, ilikuwa ni changamoto kubwa sana ndani ya Jimbo letu. Kwa kweli, namshukuru sana Waziri mwenye dhamana na sekta hii. Ndugu yangu Mheshimiwa Aweso ni mchapakazi mzuri sana, ana msaada mkubwa sana kwa Mheshimiwa Rais.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Aweso nilipokuwa na changamoto ya maji, anakumbuka kwenye Kata ya Maratani kuna engineer mmoja alikuwa anazingua pale, tulikwenda kwenye ile kata na pale pale akamshughulikia. Leo kata ile ina mradi mkubwa wa maji na unaendelea vizuri. Namshukuru sana Mheshimiwa Eng. Aweso. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile mama ameleta fedha ndani ya Jimbo letu, shilingi bilioni 38 ya kuvuta maji kutoka Mto Ruvuma, karibu kilometa 100 kutoka Mji wa Mangaka. Mradi huu sasa hivi una 83%. Wananchi waliopo ndani ya Jimbo langu katika Mji wa Mangaka wanategemea kupata maji muda wowote kuanzia sasa hivi kwa kweli, tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ombi langu katika bajeti hii, naomba Mheshimiwa Aweso, hebu aongeze nguvu tuhakikishe maji ambayo tuliwaahidi wananchi wetu kwamba ifikapo mwezi wa Sita wataanza kupata, wayapate, kwa sababu, wananchi wana hamu ya maji na wanataka waone. Wamehangaika sana na issue ya maji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia, naomba nimshukuru tena Mheshimiwa Rais kwa kutuletea fedha za miradi mikubwa ya maji. Tuna mradi mkubwa wa kuchota maji kutoka Bwawa la Sengenya kupeleka katika vijiji vyote vya Kata ya Sengenya, kaleta karibu shilingi 3,600,000,000/=. Mradi unaendelea. Namwomba sana Mheshimiwa Waziri wa Maji kwenye bajeti yetu hii ahakikishe ule mradi unakamilika. Mkandarasi yupo, pale kuna changamoto ya upatikanaji wa fedha. Fedha zipelekwe ili mradi ukamilike. (Makofi)

MHE. HUSSEIN N. AMAR: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MWENYEKITI: Taarifa.

TAARIFA

MHE. HUSSEIN N. AMAR: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimpatie Taarifa mzungumzaji kuhusu Waziri wa Maji. Hata mimi kwangu alikuja akasimamia, akamtia pingu mkandarasi, na maji yakatoka. Usimamizi wake ni mzuri. Nilikuwa nataka kuongezea tu Mheshimiwa. (Makofi)

MWENYEKITI: Mheshimiwa Ally Mhata, unaipokea Taarifa ya Mheshimiwa Amar?
MHE. YAHYA A. MHATA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono, kwa sababu lengo ni kuleta maendeleo kwa wananchi wetu. Kwa hiyo, kwa wale watumishi ambao hawawajibiki, nami naunga mkono hoja hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna miradi mingine ya maji ambayo ipo ndani ya jimbo letu. Kila kata ya jimbo langu tuna miradi ya maji na kwa kweli, inaendelea vizuri sana. Rai yangu ni kwenye bajeti ya mwaka huu, Wizara itie jitihada ihakikishe fedha zinakwenda ili miradi hii ya maji ikamilike.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiacha mradi wa maji, tunakwenda kwenye kilimo. Hapa napenda nichukue nafasi hii nimshurkuru sana Waziri Bashe, Naibu wake na wafanyakazi wote wa Wizara ya Kilimo. Mheshimiwa Bashe ameonesha uzalendo mkubwa kwenye sekta ya kilimo. Unavyomtazama Mheshimiwa Bashe, sivyo anavyofanya kazi, the way ambavyo Mheshimiwa Bashe anaonekana, ni tofauti na anavyofanya kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kule kwetu sekta ya kilimo, hasa Kilimo cha Korosho, ilikuwa katika wakati mgumu sana. Watu tulikuwa tunaita shamba la bibi, watu wanajichukulia fedha, hawafanyi kazi, lakini leo hii wakulima wa Jimbo langu la Nanyumbu ukiwatajia Mheshimiwa Bashe, wanakuombea, wanasema, tunamwomba Mwenyezi Mungu aendelee kumweka huyu bwana katika sekta hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo wakulima wa jimbo langu mwaka huu wamevuna karibu tani 22,000. Ninavyozungumza, hakuna hata mkulima mmoja ambaye hajalipwa fedha zake. Jambo hili lilikuwa historia, kule zamani ingekuwa ni changamoto. Watu walikuwa wanapeleka mazao yao kwenye vyama, lakini hawalipwi. Kwa mwaka huu tunamshukuru sana Mheshimiwa Bashe. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa rai yangu, naomba sana Wizara ya Kilimo, hasa kwa Mheshimiwa Bashe, pale Nanyumbu sisi ni wakulima wazuri sana wa ufuta katika Mkoa wa Mtwara, ndio tunaongoza kwenye uzalishaji wa ufuta. Tunaomba pale pawe ndiyo center ya manunuzi ya zao hilo. Hatuna ofisi maalumu ya kushughulika na masuala ya manunuzi, kwa hiyo, wenzetu wa AMCOS na MAMCU wahakikishe wanatujengea jengo ili kurahisisha manunuzi, hasa ya stakabadhi ghalani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia, namshukuru Mheshimiwa Bashe kwenye masuala ya kuhakikisha stakabadhi ghalani inafanya kazi 100%. Leo korosho tuwe na stakabadhi ghalani, ufuta stakabadhi ghalani na mbaazi. Mbaazi kwetu siyo mboga, ni zao la biashara. Hili Mheshimiwa Bashe amelikazania sana, leo wananchi wa Mtwara na wa jimbo langu wanapata fedha nyingi sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kuna zao la choroko, ninasikia wanaingiza stakabadhi ghalani. Mimi kwa mikono miwili na baraka jambo hili kwa kweli, litakuwa mkombozi kwa wananchi wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba pia, nichukue nafasi hii kuwashukuru sana viongozi wa AMCOS, katika jimbo langu mwaka huu wamefanya kazi kubwa. Wamepokea mfumo mpya wa malipo, lakini umekuwa tayari kusimamia na kuleta tija kwa wakulima wetu. Nakipongeza Chama cha AMCOS cha Kata ya Nanyumbu (Nanyumbu AMCOS) kwa kufanya vizuri na kuweza kununua gari jipya kwa ajili ya wakulima. Ninawashukuru sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, najua muda siyo rafiki, lakini naomba nichukue nafasi hii kuwashukuru sana Waziri wa Afya, na Waziri wa Elimu, kwa miradi mbalimbali ambayo wametuletea katika Jimbo letu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho ni kuhusu nishati. Leo wilaya yangu, vijiji vyote 93 vina umeme. Katika vitongoji 526, vitongoji 411 vina umeme. Namwomba Waziri ahakikishe vitongoji vilivyobaki vinapata umeme katika mwaka huu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, naunga mkono hoja. Ahsanteni sana. (Makofi)

MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa Yahya Ally Mhata, lakini kwa mujibu wa kanuni, ukipewa taarifa unatakiwa uikatae ama uipokee na siyo kuunga mkono.

MHE. YAHYA A. MHATA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa furaha niliyonayo, naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja. Ahsante sana. (Makofi)

MWENYEKITI: Mheshimiwa Yahya, nilikuwa nakuelekeza kwenye Taarifa ya Mheshimiwa Amar.

MHE. YAHYA A. MHATA: Mheshimiwa Mwenyekiti, Taarifa ya ndugu yangu, nimeipokea.