Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

Hon. Innocent Sebba Bilakwate

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kyerwa

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

MHE. INNOCENT S. BILAKWATE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi nami niweze kuchangia kwenye hotuba ya Waziri Mkuu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote, namshukuru Mwenyezi Mungu ambaye ametujalia kuwepo katika Bunge. Hili ni jambo la kumshukuru Mungu, tumekuwepo Bungeni hapa miaka mitano. Kuna wengine tulianzanao, leo hii hatukonao. Kwa hiyo, tunamshukuru Mungu sana ambaye ametuwezesha, hasa kwa kunipa nguvu kuendelea kuwatumikia wananchi wangu wa Jimbo la Kyerwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, napongeza kwa kazi kubwa, tumeona kwenye hotuba ya Waziri Mkuu, ameeleza mafanikio makubwa kwenye sekta mbalimbali. Kwa kweli kwa namna ya pekee tunampongeza sana na kumshukuru sana Mheshimiwa Rais, kwani ndiye namba moja anayetupambania kutafuta fedha. Maeneo mengi tumeshuhudia miradi mingi ambayo iliachwa na mtangulizi wake, lakini Mama huyu mpambanaji wetu amehakikisha miradi hii anaikamilisha na kuanzisha mingine. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukienda upande wa SGR, miradi hii ilikuwa bado haijakamilika kutoka Dar es Salaam mpaka Dodoma, lakini imekamilika na miradi hii kwa kweli imerahisisha maisha. Mtu anatoka Dar es Salaam, anakuja anaingia Bungeni, anaendelea na ratiba za Bunge, jioni akiamua anarudi Dar es Salaam. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia hata wafanyabiashara wanatoka hapa Dodoma asubuhi wanaenda Dar es Salaam wanafanya shopping, usiku wanarudi na kesho wanaendelea na biashara zao. Kwa hiyo, haya ni mafanikio makubwa sana kwa Taifa letu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri ambao nataka kutoa kwenye upande wa SGR, kuna haya mabehewa ya VIP, unakuta kwenye lile behewa kuna watu 20 na yale mabehewa yanabeba wakati mwingine mpaka hata watu 10. Nafikiri ni kwa sababu ya gharama kubwa za usafiri, shilingi laki moja na nusu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naishauri Serikali, kama behewa linalobeba watu 40, linabeba watu 10 au 15 mpaka 20 kwa sababu ya gharama za usafiri, kwa nini Serikali isiamue kupunguza kama ni shilingi laki moja na nusu, ikapunguza ikafanya shilingi 70,000/=? Hii inaweza ikaongeza pato kwa Serikali kuliko kuacha bei kubwa, halafu abiria wanakuwa wachache. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine tumeshuhudia mradi wa Bwawa la Mwalimu Nyerere. Bwawa hili tulikuwa tunalitegemea sana, lilikuwa bado chini wakati mtangulizi wake analiacha, lakini Mama huyu amepambana na wasaidizi wake kuhakikisha linakamilika na sasa tuna uhakika wa umeme. Nchi inapokuwa na uhakika wa umeme, ninaamini viwanda vyetu vitakuwa salama, tutaongeza uzalishaji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sekta ya umeme tunaihitaji sana. Nitoe mfano kwa upande wa Mkoa wa Kagera, umeme umekuwa ukikatika mara kwa mara. Sasa tunao umeme wa uhakika, naomba sana Serikali iunganishe Mkoa wa Kagera na gridi ya Taifa ili nasi viwanda vyetu viwe salama, kwa sababu umeme wa Mkoa wa Kagera kwa siku moja unaweza ukakatika zaidi hata ya mara 20. Naomba sana Serikali iliangalie hili ili tuunganishwe na gridi ya Taifa pia tuweze kuongeza ajira kwa vijana wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, haya ni mambo ambayo ni ya Kitaifa, ni mengi sana, hatuwezi kuyamaliza, lakini wasije wakasema yamefanyika ya Kitaifa tu, kwenye majimbo yetu hayajafanyika. Tumeshuhudia miradi mikubwa sana ambayo imefanyika kwenye maeneo yetu. Nitoe mfano, hakuna jambo ambalo lilikuwa linasumbua na Waheshimiwa Wabunge tumelisemea hapa Bungeni kama michango kwa wananchi wetu. Walikuwa wanapata wakati mgumu na maeneo mengine hata ndoa za wananchi wetu hazikuwa salama kwa sababu, kinapofika kipindi cha kuchangia vyumba vya madarasa, wananchi wanaume unakuta hawakai nyumbani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kipindi cha Dkt. Mama Samia, mimi nieleze kwa upande wa Kyerwa, tumepata vyumba vya madarasa 185 upande wa sekondari na matundu ya vyoo 80. Ukija upande wa primary, tumepata vyumba vya madarasa 175 na matundu ya vyoo 829. Haya ni mafanikio makubwa, Mheshimiwa Rais ameondoa adha ambayo ilikuwa inawapata wananchi. Kwa kweli, tunamshukuru sana, ndoa za Watanzania zipo salama kwa sababu, michango haipo tena. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeweza kujenga Shule za Sekondari mpya 10 kwa upande wa Kyerwa. Kyerwa hatukuwa na Kidato cha Tano na Sita, lakini kipindi cha Dkt. Mama Samia tuna shule 12 za Kidato cha Tano na Sita. Kyerwa hatukuwa na VETA, leo hii tunajenga Chuo cha VETA, vijana wetu wanaenda kupata ujuzi ili waweze kujiajiri kwenye sekta mbalimbali. Kwa hiyo, haya ni mafanikio makubwa ya Mheshimiwa Rais, Mama yetu Dkt. Samia Suluhu, tunaendelea kumshukuru sana na kumwombea kwa Mungu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia, Mheshimiwa Rais amegusa sekta nyingi, mimi nilipoingia hapa Bungeni tangu mwaka 2015 nimekuwa nikiongea habari ya soko la uhakika la zao la kahawa. Nimeongea, lakini hatukupata majibu. Awamu hii chini ya Mama yetu Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu, ameleta majibu ya kahawa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi walikuwa wanapangiwa bei, anayeamua kununua kwa shilingi 400/= au shilingi 1,000; lakini kipindi mwaka 2022 ilibidi ifike wakati tuongee kwa ukali sana na kukataa kuunga mkono bajeti. Mheshimiwa Dkt. Mama Samia, huyu msikivu, akamwelekeza Waziri Mkuu na Waziri wa Kilimo, Kahawa ya Mkoa wa Kagera iuzwe kwenye mnada. Kahawa imetoka shilingi 1,100/=, leo hii tunaongelea shilingi 6,500/=. Haya ni mafanikio makubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, najua kuna wengine waliokuwa wananufaika, hawapendi, na kule Kyerwa wapo. Leo hii wanapambana, wanasema, huyo ambaye ametunyang’anya kahawa tuhakikishe harudi, lakini mimi nina imani Mungu aliyeniwezesha nikapambania kahawa leo hii ikapanda, Mungu huyo huyo bado yupo kazini, na atampitisha Bilakwate. Sina mashaka na Mungu wangu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Rais amesikia kilio cha Wabunge; tumezungumza hapa juu ya miradi ya maji, wananchi hawana maji safi na salama. Mheshimiwa Rais amemwaga fedha nyingi kwenye miradi ya maji, hata Kyerwa tunayo miradi mingi inaendelea, zaidi ya shilingi bilioni 16.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninachoiomba sana Serikali, miradi hii imeanzishwa, lakini wakandarasi wanadai fedha nyingi. Walipeni wakandarasi ili nia ya Mheshimiwa Rais ya kuwapatia maji safi na salama Watanzania iweze kutimia. Naomba sana hili mlizingatie. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninao mradi wangu wa Lunyinya – Lwabwele mpaka Chanya, unahitaji zaidi ya shilingi bilioni tatu mkandarasi akamilishe. Ninao Mradi wa Kikukuru wa shilingi bilioni tano, mkandarasi ameshaujenga zaidi ya 75%, mlipeni akamilishe mradi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukija upande wa barabara, mimi wakati naingia Kyerwa, barabara nyingi zilikuwa hazipitiki. Watu walikuwa wanapita kwenye mitumbwi, lakini chini ya Mheshimiwa Rais tumejenga madaraja makubwa, tumefanya kazi kubwa, Wanakerywa wanaolima wanatoka mashambani, wanapeleka mazao yao kwenye masoko, mambo yapo vizuri. Mama Samia oyee! (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine kubwa ambalo amelifanya Mheshimiwa Dkt. Mama Samia, tulikuwa na masoko ya Kimataifa, masoko haya yalishasahaulika zaidi ya miaka 15. Nikamwendea Waziri wa Kilimo nikamweleza, nikamwambia haya masoko yalikuwa ni viwanda, naomba wewe ukayabebe kwa sababu yanawagusa wakulima. Akampelekea taarifa Mama Samia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mama Samia ametoa kila soko shilingi bilioni moja, leo hii tupo tunaezeka masoko Wanakyerwa na Wanakagera tunaenda kupata soko la uhakika. Hayo ni mafanikio makubwa yanayofanywa na Mama Samia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wanakyerwa wakati mama anaingia, vijiji 29 havikuwa na umeme, lakini tumempelekea maombi hapa Bungeni kupitia wasaidizi wake, Mama Samia ametoa fedha vijiji vyote 29 vina umeme. Hayo ni mafanikio makubwa ya Serikali ya Chama cha Mapinduzi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sana, Kyerwa bado tunavyo vitongoji zaidi ya 300, sasa tunaomba nguvu hiyo hiyo iliyotumika kupeleka fedha kwenye vijiji, ipelekwe kwenye vitongoji ili Watanzania na wanakyerwa waweze kupata umeme wa uhakika na vijana waweze kujiajiri kwenye maeneo mbalimbali kwa kutumia umeme. Kwa hiyo, naomba sana hilo lizingatiwe. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja. (Makofi)