Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

Hon. Michael Mwita Kembaki

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Tarime Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

MHE. MICHAEL M. KEMBAKI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ili nami niweze kuchangia katika siku ya leo. Kwanza kabisa, naomba nichukue nafasi hii kuwashukuru sana wananchi wa Tarime Mjini kwa kuniamini na pia uchapaji kazi wao. Wanafanya kazi vizuri katika kuijenga Tarime yetu na Taifa letu kwa ujumla. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia naomba nichukue nafasi hii kumshukuru sana Rais wetu, Mama Samia Suluhu Hassan kwa sababu amefanya mazuri katika jimbo letu la Tarime Mjini. Tulikuwa na tatizo kubwa sana la soko, ameleta fedha na tumepata soko la kisasa kabisa ambalo sasa watu wa Tarime watapa sehemu ya kufanyia biashara na uchumi wa Mji wetu kukua siku hadi siku. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo nitajikita sana katika tatizo kubwa ambalo lipo katika nchi yetu la ukosefu wa ajira kwa vijana wetu. Tarehe 07/01/2022 Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania akiwa kule katika Mkoa wa Magharibi alisema maneno haya, “Serikali yenu tunajua tatizo la ajira na tunalifanyia kazi ili kutengeneza fursa mbalimbali ili vijana wapate ajira.”

Mheshimiwa Mwenyekiti, tatizo la ajira ni kubwa sana katika nchi yetu na inasababisha umasikini kukithiri katika jamii yetu. Tatizo la ajira linafanya kupungua kwa kipato cha familia, lakini pia kuongezeka kwa umaskini katika familia. Ukosefu wa ajira unasababisha Serikali ikose kodi kwa sababu watu wengi hawana kazi ya kufanya na hivyo kusababisha upungufu huu wa kodi katika Taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia uchumi wa nchi unadorora kutokana na ukosefu wa ajira kwa watu wengi ambao hawana ajira. Matatizo mengi ya kifamilia ambayo yanatokea mara nyingi yanasababishwa na ukosefu wa ajira katika jamii yetu. Watu wengi wanakuwa tegemezi, na wanaofanya kazi ni wachache, hivyo kusababisha utegemezi katika jamii yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukosefu wa ajira husababisha pia ucheleweshaji wa malengo ya mtu binafsi, lakini pia kwa Taifa letu kwa ujumla. Hizi ni baadhi ya hasara za ukosefu wa ajira katika Taifa letu la Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama unavyojua, moja ya mambo ambayo yanasababisha ukosefu wa ajira ni kwamba watu wanakuwa wengi kuliko nafasi za kazi zilizopo. Katika nchi nyingi za Afrika, 70% ya watu ni vijana ambao ndio wanaofanya kazi zaidi kuliko wazee. Ukiangalia katika Taifa letu kulingana na sensa iliyofanyika mwaka 2022 vijana ni wengi kuliko wazee, hivyo watu wanaohitaji kazi ni wengi kuliko kazi zenyewe zilizopo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda niseme kidogo kuhusu chanzo cha ukosefu wa ajira. Binafsi nimefanya utafiti nikaona miongoni mwa vitu vinavyosababisha ukosefu wa ajira katika Taifa letu ni mfumo wa elimu unaotolewa katika nchi yetu. Mfumo wa elimu unaotolewa katika nchi yetu haukidhi mahitaji, nayo inasababisha wale ambao wanaopata elimu kukosa mwelekeo baada ya kuwa wamehitimu katika masomo yao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mfumo wa elimu unaotolewa katika nchi yetu haumfanyi mwanafunzi kujitegemea, kwani mfumo wa elimu unaotolewa katika nchi yetu unamfanya mwanafunzi kuwa mtumwa wa ajira badala ya kujiajiri. Mfumo wa elimu unaotolewa katika nchi yetu humfanya mwanafunzi asiwe mbunifu katika maisha ya siku hadi siku. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia katika mfumo wa elimu unaotolewa katika nchi yetu umeegemea sana katika mambo ambayo hayaendani na uhalisia wa maisha halisi ya Mtanzania, ili tuweze kutatua tatizo la ajira katika nchi yetu, lazima tuangalie wazee wetu; baba na babu zetu walikuwa wanafanya nini kabla mambo kubadilika? Enzi hizo wakati wa baba zetu kulikuwa hamna tatizo la ukosefu wa ajira, lakini ukosefu wa ajira umekuja baada ya elimu kuanza kutolewa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa tujifunze ni yapi ambayo yalikuwa yanafanyika enzi hizo na kutatua changamoto ya ukosefu wa ajira katika miaka hiyo. Kwanza, lazima tuangalie uhalisia, baba zetu walikuwa wanafanya nini? Baba zetu walikuwa wanafanya kazi ya ufugaji, kilimo, uvuvi, uhunzi na kazi hizi zote ndizo ambazo zimeajiri watu wengi sana katika Taifa letu la Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tukiangalia katika mfumo huu, baba zetu wakati wote walikuwa wanahamasisha vijana kwenda shambani, walikuwa wanasifia hata wakati kijana anataka kuoa walikuwa wanaangalia ni familia ipi ambayo hakuna njaa? Ni familia ipi ambayo inajua kulima? Hivyo walihakikisha kwamba wanaleta nguvu kazi katika familia ili uzalishaji uendelee. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii ninapozungumza, ukienda katika shule zetu, shule za msingi, elimu ya awali, elimu ya sekondari na vyuo vikuu tumefanya hivi vitu ambavyo ni vya asili ya Mtanzania; ufugaji, uvuvi, kilimo na uhunzi vimekua ni vitu ambavyo siyo vya wasomi. Hivyo, kusababisha watu kuchukia kilimo, kufanya watu wachukie uvuvi na kuonekana wale wanaofanya kazi hiyo ni wale ambao wamepitwa na wakati. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivyo basi, tumeenda sasa kila mtu anataka afanye kazi ofisini. Kila mtu anataka aendeshe gari, kila mtu anataka awe secretary, awe askari na hizi nafasi ni chache. Ili tuweze kutokomeza tatizo hili, lazima kwanza tufanye mambo yafuatayo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, mafunzo haya ya asili ya Mtanzania yafundishwe kutoka elimu ya awali, chekechea, watoto wajue kwamba kilimo ni sehemu ya kazi, na ni kazi ya heshima. Shule ya msingi yafundishwe, sekondari yafundishwe, na Vyuo Vikuu wafundishwe ili yakae kichwani wapende, hata wakitoka hawatapata shida, waendelee kulima ili tuweze kupata uzalishaji katika Taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia ni kwa nini viwanda haviwezi kufanya vizuri katika Taifa letu? Ni kwa nini viwanda vya pamba vinavyozalisha nguo haviwezi kufanya kazi siku zote? Ni kwa nini hata alizeti haiwezi tukazalisha mafuta ya kutosheleza? Ni kwa sababu watu wamekwepa kilimo na kila mtu anataka afanye kazi za ofisi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tukihamasisha watu waende kwenye kilimo, watu wakaenda kwenye uvuvi, tutapata samaki wa kutosha, ambayo itakuwa ni lishe kwenye Taifa letu, lakini pia tutauza nje na kupata mapato. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tukihamasisha watu waende kwenye kilimo, tutapata mazao mengi ambayo viwanda vyetu vitapata malighafi ya kutosha ili Taifa letu liwe ni nchi ya viwanda, tuweze kusonga mbele. Kwa kufanya hivi, tutakuwa tumetengeneza ajira kwa vijana wetu, tutakuwa tumeondokana kabisa na tatizo la ajira katika Taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tukifanya maboresho katika mfumo wa elimu, hakika tutakuwa hatuimbi tatizo la jira katika Taifa letu. Sasa ukienda katika vitu vinavyofundishwa shuleni, zipo kozi zinazofundishwa katika vyuo vyetu ambazo hata mtu hawezi kupata kazi baada ya kuwa amehitimu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mfano, watu wengi wanahitimu ambao wamesoma mambo ya procurement, marketing na kadhalika na kadhalika, vitu ambavyo hata wakitoka pale mtu huyu hajawahi kushika jembe, mtu huyu hajawahi kushika nyavu, sasa akitoka pale anaenda ku-market kitu gani?

Mheshimiwa Mwenyekiti, siku moja Mheshimiwa Mbunge mwenzetu hapa alisema, watu wengi tulianza kumshangaa, lakini ukweli ni kwamba ukiangalia kwa undani vyuo vyetu vimekuwa chanzo cha kusababisha ukosefu wa ajira katika Taifa letu la Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza hata vitu vinavyofundishwa katika vyuo vyetu vingi havina tija na havilengi soko halisi la ajira katika Taifa letu. Ukiangalia mfano, mtu aliyesoma marketing na kila mtu sasa hivi uchumi umekuwa mgumu akiwa anafanya kazi yake, anaitangaza mwenyewe kwenye vyombo vya habari. Sasa mtu aliyefanya marketing, anaenda kutangaza nini na vyombo vya habari vipo kila sehemu na mtu anaweza kutangaza bidhaa zake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kwanza tuangalie pia vyuo vyetu na shule zetu vitu vinavyofundishwa. Ukiangalia watu wanaohitimu katika vyuo vyetu walimu, ma-engineer na professions nyingine utaona kwamba hawana sifa zile za kufanya kazi, maana yake hawajawiva kikamilifu ambao wanaweza kwenda kuajirika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ndiyo maana Serikali imekuja na mfumo kwamba watu wamesoma; mfano, Serikali imefundisha walimu mpaka wamehitimu, lakini mwisho wake ili iweze kumwajiri mtu ambaye ametengenezwa na vyuo vyetu, tunaenda tena kuwataka wafanye interview, na wanafanya interview zaidi ya mbili mpaka tatu ili waweze kuajiriwa. Maana yake ni kwamba hata Serikali hatuviamini hivi vyuo vya kutosha mpaka tunaanza kusaili wahitimu wetu ili tuweze kuwapa ajira.

Mheshimiwa Mwenyekiti, natoa ushauri kwa Serikali, iangalie upya vyuo hivi ambavyo vinafundisha vijana wetu ambao hatimaye wanakuwa jobless katika mitaa yetu na katika nchi yetu ya Tanzania. (Makofi)

MWENYEKITI: Mheshimiwa Michael Kembaki, ahsante sana.

MHE. MICHAEL M. KEMBAKI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.