Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. DKT. THEA M. NTARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru kwa kunipa nafasi. Nianze, kwa kupongeza sana Hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu na nitaenda kwenye eneo hasa la vyuo vikuu, vyuo vya kati pamoja na viwanja vya michezo kwa sababu niko kwenye Kamati ya Elimu na Utamaduni.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumetembelea katika majengo ya vyuo vikuu kama University of Dar es Salaam, Ardhi na DIT. Niseme ukweli usiofichika kwamba, kazi nzuri imefanyika katika vyuo hivyo hasa kwenye haya majengo mapya ya DIT. Tukienda pale, kwanza ni kama sehemu ya utalii. Yale majengo yamejengwa kwa ustadi na kinachofurahisha sana, Ofisi ya Waziri Mkuu kila tulipokwenda walileta mwakilishi wa kuja kuona jinsi Serikali inavyofanya kazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kusema hivyo nina maana kwamba, Ofisi ya Waziri Mkuu kumbe inafuatilia na kusimamia ujenzi katika vyuo vikuu. Lingine ambalo lilionekana ni zuri vijana wetu ambao wamesoma katika vyuo hivyo wengi wameajiriwa pale na ndio wanaosimamia ujenzi wa hayo majengo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme tulipokwenda pale DIT kuna kitu kipya kimeanzishwa pale. Wale wanakwenda kurusha satellite. Sasa, satellite ni kitu kipya na kwa nchi yetu hii ya Tanzania kuweza kurusha kitu hicho, kuna wale wa nchi nyingine zilizoendelea wataona kama kuna wivu fulani hivi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaiomba Ofisi ya Waziri Mkuu, right from the beginning waanze kufuatilia ule mradi ili utakapokamilika na kuweza kurushwa 2026 usiwe na dosari. Hili jambo ni kubwa na ni jambo ambalo hatukutegemea, lakini kile chuo kinafanya ile kazi kikishirikiana na wadau mbalimbali ikiwemo Wizara ya Mambo ya Ndani, Wizara ya Elimu yenyewe, Wajapani wako pale na UN Organization moja iko pale. Kwa hiyo, nilitaka kusema kwamba, ni vizuri Serikali, Ofisi ya Waziri Mkuu ijue kwamba kuna project kubwa pale, hivyo waweke jicho katika mradi ule.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, bado tulitembelea viwanja. Nasema katika ujenzi wa kiwanja bora ni kile Kiwanja cha Arusha. Wizara ya Michezo wamesimamia vizuri, lakini ninaamini hata kule kulikuwa na timu ya Ofisi ya Waziri Mkuu. Kwa hiyo, niseme hii miradi mikubwa, Ofisi ya Waziri Mkuu inapoweka jicho pale kwa kweli ufanisi unaonekana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nije kwenye habari ya mikopo, nipongeze sana Ofisi ya Waziri Mkuu. Hata tuliposema kwamba mikopo sasa hivi haitoshi mmeongeza. Ni juzi tu nilipiga simu tena nilipiga saa ambazo huwezi kupiga simu. Nilimpigia simu Waziri Mkuu kwamba kuna tatizo watoto wanahitaji fedha na alifanyia kazi usiku ule ule na asubuhi wakawekewa fedha watoto ili watulie wapate fedha yao ya accommodation pamoja na tuition fee. Hongera sana, huo ndio ufuatiliaji tunaoutaka. Tatizo limesemwa, wakawajibika immediately. Hapo nawapa pongezi nyingi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hayo nisisahau hili jambo. Kuna jambo lile nimelizungumza leo ni mara ya tatu, kuhusu mafao ya wakuu wa vyuo vikuu. Mheshimiwa Lukuvi unanisikia hapo, hili jambo tumeliongea. Hao wakuu wa vyuo wamekaa wanasubiri wanasema liko kwenye meza. Niwaombe wakalichukue hapo kwenye meza walishike mkononi wamalizie hilo suala la mafao ya vyuo vikuu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, juzi juzi kuna mafao ya watu wale wa vyeti feki, walilifanyia kazi haraka sana. Hawa wahadhiri wa vyuo vikuu ambao ni Professors na wasimamizi wa vyuo bado mpaka leo hivi ninavyoongea haijulikani nini kinaendelea.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hayo niunganishe na mafao ya wale waliofanya kazi na Mheshimiwa Lukuvi, wale wakuu wa wilaya ambao bado mpaka leo wanadai handshake. Wale ndio waliojenga zile shule za kata, walisimamia vizuri mno. Mheshimiwa Lukuvi analifahamu hilo, hebu sasa ufike wakati tumalizane nao kama walivyomalizana na wale watumishi wa vyeti fake waliwalipa. Mheshimiwa Rais alikuwa na huruma akasema jamani wapeni na hawa hebu wakumbushe, lakini nafikiri yeye ameshamaliza hilo. Nimwombe sana Mheshimiwa Lukuvi yuko hapo wakawajibike kwenye hilo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine nataka kulizungumzia tena leo kwa mara ya nne ni kuhusu Teaching Hospitals. Hawa wadau wanapokuja kutaka kutusaidia jambo lolote katika hospitali zetu, huwa wanauliza, hii hospitali ina mahusiano na university ipi? Wakijua hilo, basi kuna uwekezaji wataufanya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Profesa Pallangyo na wenzake waliandika proposal nzuri ya Teaching Hospital Mloganzila. Walivyoandika, wakaomba na eneo, wakapata Mloganzila. Walivyolipata lile eneo, hospitali ikaanza kuyatamani yale majengo, wakaanza kuleta, mimi nafikiri hizo ni figisu, kwa sababu wale wameandika proposal ya hiyo Mloganzila, wameomba na kiwanja wamepata, majengo yamekaa yametulia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, watu wakaenda kusema, tena wakamshauri Waziri pale, kengele ya ngapi?
(Hapa kengele ya kwanza ililia)
WABUNGE FULANI: Mheshimiwa wewe endelea tu…
MHE. DKT. THEA M. NTARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, wakasema pale hapafai, wakaanza kuleta figisu. Wakapeleka watumishi pale Mloganzila ambao hawafanyi kazi vizuri, Mkurugenzi wa pale akawa anakosa ile NHIF. Kwa kufanya hivyo, uwajibikaji katika ile hospitali ukaonekana wa ovyo. Ninyi Wabunge ni mashahidi, mambo yalikuwa hayaendi vizuri, kwa hiyo ilikuwa kama sabotage.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baadaye iliundwa Kamati na Tume, Mheshimiwa Waziri Ummy wakati huo anafahamu. Wakaenda kuandika, wakakuta kumbe hakuna tatizo, ni watu tu wenye ubinafsi na waliokosa uzalendo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sasa ile ripoti ambayo iko kwenye meza ya Katibu Mkuu Kiongozi, mkaiangalie muone ile Mloganzila irudi iwe ni Teaching Hospital. Ikiwa ni Teaching Hospital, mimi nawaambieni, huko ndiyo kunapatikana wabunifu na wale specialists.
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii Marekani ina Teaching Hospital 50, Nigeria wana Teaching Hospital, Zambia wana Teaching Hospital, Nairobi wana Teaching Hospital, na sisi hapa lazima tuwe na Teaching Hospital Mloganzila na Benjamini. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo ushirikiano mzuri upo kati ya UDOM na Benjamini. Niwaambie, sasa hivi wameletewa mradi wa figo pale Benjamini na waliwaletea baada ya kujua Benjamini ina ushirikiano mzuri na UDOM. Kwa hiyo, nataka kusema kwamba ni lazima sasa tujipange tuwe na Teaching Hospitals zetu. Benjamini ambayo inaonekana sasa hivi inafanya vizuri, ina ushirikiano mzuri, na wanafunzi wanatoka UDOM wanakwenda pale Benjamini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, siyo hilo tu, wadau wote wa maendeleo wakiona hospitali ina ushirikiano na University ndiyo wanawekeza mradi. Hawa Wajapani walikataa mwanzoni, wakasema mlikuwa hamna uhusiano mzuri. Leo kuna uhusiano mzuri, wameenda kuwekeza pale kitu kinachoitwa mradi mkubwa kabisa kwa ajili ya figo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naliomba hili tusilichukulie mzaha sasa hivi, tuliweke kabisa seriously. Kitu kingine, hivi nchi inakuwaje na National Hospital moja? Nchi inaweza kuwa na National Hospital mbili au tatu. Mkiboresha Benjamini, na kuruhusu miradi iende pale, tutakuwa angalau tuna National Hospitals mbili. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, viongozi wote wa Kitaifa leo hapa wakiugua, mimi siyo wa Kitaifa; leo viongozi wote wa Kitaifa wakiugua, ninyi Wabunge mnakimbilia wapi? Ni Benjamini, lakini juzi wamekwenda Ubalozi wa Marekani, wametembea Benjamini, wakaona he, kumbe inafanya vizuri hivi! Kwa hiyo, unaona hata wageni, mabalozi wataiamini Benjamini, kwa sababu hii ndiyo ya Makao Makuu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nawaomba sana sana, tusisitize au tujitahidi kuifanya ile iboreke zaidi ili iwe na hadhi ya kuwa National Hospital na wanafunzi wetu waweze kufanya kazi pale, tupate wabobezi. Tutakwenda India mpaka lini? Tutakwenda South Africa mpaka lini? Tunataka tukiugua tutibiwe kwenye nchi yetu. Kwa kufanya hivyo, na ili tuweze kufika huko, lazima tuwekeze kwenye hospitali zetu hizi mbili tena, tuwekeze kwa kuruhusu wanafunzi wale wa Muhimbili University waende Mloganzila. Pia iangaliwe kwamba kuna uhusiano mzuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, nakushukuru sana, ahsante sana. (Makofi)