Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

Hon. Issa Ally Mchungahela

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Lulindi

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

MHE. ISSA A. MCHUNGAHELA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa nafasi. Ninaomba nimshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema kwa kunipa uhai. Pia, niwashukuru familia yangu kwa kuendelea kunivumilia nikiwa katika majukumu. Ninawashukuru pia wananchi wangu kwa kuendelea kunipa mkono na kunipa moyo katika kutimiza majukumu yangu ya kibunge. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kuipongeza Serikali ya Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, Serikali ya Awamu ya Sita kwa jitihada zake kubwa za kufanya maendeleo kila namna. Pongezi zangu zitajikita moja kwa moja kwenye eneo moja tu la kilimo na ni kwa sababu ninazo sababu za kufanya hivyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpongeze pia Mheshimiwa Makamu wa Rais wa nchi, Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango kwa kuifanya nchi ikawa tulivu na tunafanya majukumu yetu pasipokuwa na changamoto, kwa kumsaidia Mheshimiwa Rais katika kumshauri mambo kadha wa kadha jinsi ya kuiendesha nchi na kuifanya nchi ikawa tulivu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpongeze pia Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa kazi yake kubwa ya kulituliza hili Bunge. Kama mnavyoona Bunge linafanya kazi njema kabisa na Bunge hili ni Bunge la mfano katika Mabunge ya Nchi hii, kutokana na utendaji wake wa kazi na mafanikio ambayo Bunge hili limefikia na nchi kwa ujumla. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyosema nitajikita katika suala la kilimo. Bunge hili lilimshauri sana Mheshimiwa Rais na lilishauri kupitia Wizara ya Kilimo na hapa Mheshimiwa Waziri wa Kilimo naye atapata pongezi kwa kuchukua ushauri wetu mwingi sana kutoka kwenye hili Bunge na kuutendea kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, miongoni mwa ushauri mkubwa kabisa ambao ameuchukua kutoka kwenye Bunge hili na ambao una tija kubwa sana katika suala la kilimo ni kupandisha Bajeti ya Kilimo kutoka takribani shilingi bilioni 257 na kufikia shilingi bilioni 957 inakwenda kwenye trilioni moja na zaidi sasa hivi. Haya ni mafanikio makubwa sana na mafanikio haya utakuwa umeyaona katika maeneo kadhaa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na ushauri ambao ameuchukua kupitia Bunge hili ni ule ushauri wa kuanzisha mikakati kadhaa ya kuhakikisha zao la korosho linakwenda vizuri au linachukuliwa kwa umakini. Kwa mfano tangu mwaka 2021 tulishauri Serikali ya Awamu ya Sita kwenye suala la kilimo cha korosho kuweka pembejeo na ushauri huu ulipokelewa. Mpaka sasa hivi pembejeo zenye thamani ya Dola za Kimarekani takribani milioni 600 na zaidi zimeingia katika zao la korosho pekee. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Bunge hili lilimshauri Mheshimiwa Waziri kuhusiana na jambo la korosho hususan ushauri ulitoka kutoka kwa wadau wa Mikoa ya Mtwara, Lindi, Ruvuma na Pwani ambapo tulimshauri kutumia njia bora ya mnada kutoka katika mnada ule wa zamani wa box na kutumia mnada wa kisasa ambao ni TMX. Huu ni mnada ambao unatumika katika mtandao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri huu umeboresha sana mapato ya mwananchi kwa maana ya mapato ya mkulima. Kwanza, bei kutoka takribani shilingi 1,560 mwaka 2021, mwaka jana tulibahatika kufika bei ya korosho kwa kilo takribani shilingi 4,195. Haya ni maendeleo makubwa sana na ni matokeo makubwa sana ya kupokea ushauri wa Bunge hili. Hapo tunaweza kusema kabisa kwamba pongezi na hongera ziende moja kwa moja kwa Mheshimiwa Rais kwa kuyapokea mapendekezo yetu kwa mikono miwili pasipokuwa na mawaa yoyote. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri mwingine ambao tumeshawahi kuutoa na ukapokelewa ni kurekebisha njia mbalimbali ya uendeshaji wa shughuli zote. Kwa mfano, tulishauri suala la kuweka kiasi cha pesa kwenye Mfuko wa Bodi ya Korosho na hili lilitekelezwa. Bodi ya Korosho pia ilipewa kiasi cha pesa za kutosha za kuendesha shughuli zake kama vile za kiuchunguzi na shughuli zingine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na sifa hizi zote ambazo zimekwenda kwenye Serikali ya Awamu ya Sita, kupitia Waziri wa Kilimo na wasaidizi wake. Bado kuna mapungufu ambayo tunastahili kutaka kuyasemea ambayo nayo kwayo kama yatasikilizwa jinsi gani tunavyoshauri, bila shaka sasa hivi siku za usoni hali itakuwa nzuri zaidi ya hapa tulipo sasa hivi. Kwa mfano, kwenye zao hili la korosho bado tunaendelea kutumia kilimo cha mvua ambacho chenyewe hakina uhakika sana. Kuna wakati mvua zinanyesha kwa wingi na kuharibu zao la korosho, lakini kuna wakati inanyesha kidogo na kufanya korosho zipatikane kwa uchache sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hayo yote kama tulivyosema kwamba ni mashauri ambayo yanaweza kutusaidia huko mbeleni. Pia, katika kueleza mafanikio kuna jambo moja nilishindwa kulidokeza ambalo ni muhimu sana katika mafanikio makubwa ya kilimo ambayo yamejitokeza. Kwa mfano, mpaka mwaka jana tulipata fedha za kigeni kwa maana ya dola takribani milioni 583.7 ambazo ni sawasawa na shilingi trilioni 1.8 kwenye zao la korosho pekee.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi kwa maana ya wakulima wao walipata takribani dola 471,380,000 ambazo ni sawasawa takribani shilingi trilioni 1.4. Unaweza ukaona kwamba, ni pesa nyingi sana ambazo zimekuja kwenda kuleta mapinduzi makubwa ya kiuchumi katika nchi hii, hali kadhalika kwa mwananchi mmoja mmoja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kwa ujumla pia hata ukiangalia katika suala la mnyororo wa thamani. Kwa mfano, kumekuwa na huduma mbalimbali ambazo zilikuwa zikitolewa ambazo zimefanikisha na zenyewe kuchangia pato la wale walioshughulika na shughuli hii. Kwa mfano, kumekuwa na suala la viunganishi pamoja na huduma nyingine za kwenye mnyororo wa thamani takribani shilingi bilioni 200 zimepitia katika eneo hili. Ni kiasi kikubwa kama nilivyojaribu kusema. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na ukubwa huu wote bado tungetamani kwamba Serikali iende zaidi, tuondokane na hii hali ya kutumia mvua kama ni nyenzo pekee ya kufanya zao hili la korosho liboreke. Badala yake tuweze kuwa na kilimo cha umwagiliaji maana yake kwamba, tuchague baadhi ya watu ambao wana mashamba makubwa ya korosho tuwakopeshe visima na tutoboe visima virefu kusudi kuwakopesha hawa wakulima wenye mashamba makubwa waweke miundombinu ambayo itawawezesha kumwagilia korosho badala ya kuendelea kutumia kilimo cha mvua. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru sana kwa nafasi hii, naomba kuunga mkono hoja. (Makofi)