Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Ilemela
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. DKT. ANGELINE S. L. MABULA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa fursa asubuhi ya leo nami kuchangia bajeti hii ya Ofisi ya Waziri Mkuu. Kwanza, nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutujaalia afya njema na hatimaye tunashiriki katika bajeti hii ya Waziri Mkuu ambayo imeibeba Serikali nzima katika suala zima la kimaendeleo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninampongeza sana Waziri Mkuu pamoja na timu yake ya Mawaziri; Waziri Lukuvi, Waziri Ridhiwani pamoja na wasaidizi wao kwa kazi kubwa na nzuri ambayo wameifanya katika kipindi hiki na bajeti ni nzuri na imegusa maeneo yote hasa kwa kuonesha mafanikio ya Awamu ya Sita chini ya Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninampongeza sana Mheshimiwa Rais kwa sababu aliichukua nchi katika kipindi kigumu sana na kwa sababu ya jinsia yake kwamba ni mwanamke hawakuamini kama angeweza kufanya kazi hizi. Amefanya kazi hizi kwa utulivu mkubwa na hasa kwa kuendeleza ile miradi ya kimkakati ambayo ilikuwa imeanzishwa na awamu zilizopita na yote sasa inakamilika. Kwa kweli tumshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa kumpa hekima Rais wetu na kuweza kuyafanya maendeleo haya kwa uhakika na usahihi zaidi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, falsafa yake ya 4R’s aliyokuja nayo ni falsafa ambayo imeleta umoja, mshikamano, upendo na amani zaidi katika Taifa hili kwa sababu ukiangalia namna ambavyo tulikuwa tukiishi labda katika vyama vya upinzani na nini kidogo kulikuwa na changamoto kubwa. Baada ya kuwaleta wote pamoja watu wote waka-focus kwenye maendeleo na ndiyo maana kazi amezifanya kwa utulivu sana. Ninamshukuru sana katika hilo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla sijachangia bajeti ya Waziri Mkuu kwa uhakika kwanza nianze kwa kuishukuru sana Serikali kwa namna ambavyo Jimbo la Ilemela limenufaika na miradi mingi ya maendeleo katika kipindi kifupi sana na hasa katika kipindi hiki cha miaka minne ambacho tunakizungumzia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Rais alijikita zaidi katika suala la huduma za kijamii. Ukiangalia Ilemela ilivyokuwa awali na sasa ni vitu viwili tofauti. Unaweza usiamini, kama ulifika pale 2015 na leo ukienda huwezi kuamini. Jambo la kwanza ni kwenye suala zima la miundombinu ya elimu. Tumepata shule mpya zaidi ya 10 ambazo zote zinakwenda vizuri na kwa bahati nzuri shule ya Amali ambayo ndiyo kwanza imeanza, Ilemela tumeipata na inajengwa katika Kata ya Bugogwa. Tuna imani sasa watoto wetu wataweza kupata elimu ambayo pia itawajengea mazingira ya kuja kupata ajira kwa baadaye. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia kwenye afya tulikuwa na hospitali ya wilaya. Sasa hivi tuna vituo vya afya zaidi ya vitano na tulikuwa navyo viwili na tuna zahanati zaidi ya 13 na bado wananchi wanajenga kwa sababu slogan yetu ni, Ilemela ni yetu Tushirikiane Kuijenga. Kwa hiyo, kwa namna yoyote ile wananchi wanaibua miradi, Mbunge anawekeza pale na Serikali inakamilisha mambo yanakwenda mbele. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, unakuta miradi yote inakwenda kwa muda mfupi na inakwisha. Ukija kwenye miradi ya maji amewekeza katika mradi wa maji maeneo mengi sana. Ukija kwenye miradi ya maji amewekeza katika mradi wa maji maeneo mengi sana na fedha nyingi zimewekezwa, lakini changamoto iliyopo pengine ile miundombinu ya usambazaji bado sio mizuri sana. Ukiambiwa kwamba kuna watu hawana maji au wanapata maji mara mbili kwa wiki na ziwa liko pale huwezi kuamini. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaishukuru Serikali kwa sababu sasa hivi kuna miradi mingi ambayo inaendelea. Tuna ile miradi ya matokeo ya haraka. Tumepewa shilingi bilioni 4.7 ambayo inakwenda kusambaza maji karibu kilometa 68 eneo la Kahama, Buswelu, Nyamdoke na Ilalila, wanakwenda kuboresha chanzo cha maji cha Kabangaja ambacho kitakuwa kinazalisha lita za maji milioni 3.6 kwa siku na ambacho kitakwenda ku-save eneo la Igombe, Kayenze na Sangabuye na kimefikia 70%. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama hiyo haitoshi tuna upanuzi wa chanzo cha maji pale Capri Point ambapo napo tuna imani lita za ujazo milioni 46 zitaweza kuzalishwa pale na zitaletwa upande wa Ilemela. Kwa hiyo, inawezekana changamoto hiyo ikaisha. Ninaishukuru sana Serikali kwa sababu ilikuwa ni changamoto kubwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunalo eneo letu la Kisiwa cha Bezi hawajawahi kuona maji ya bomba; siku zote wanakunywa maji ya ziwani; wanahangaika na maji hayo. Sasa hivi tayari ameshapatikana mkandarasi; wako kwenye manunuzi nao wanakwenda kupata maji ya bomba kama wengine wanavyopata. Ninamshukuru sana Mheshimiwa Rais katika suala hilo ambalo ameweza kuwezesha katika jimbo langu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna stendi mpya kabisa, zaidi ya halmashauri sita zimekuja kujifunza. Sasa ombi langu kwa Serikali katika hilo, kwa sababu Nyamagana kuna stendi nzuri na Ilemela kuna stendi nzuri. Sasa ni namna tu ya ku-coordinate na tukaweza kuzitumia zile ili zisionekane kama ni white elephant kwa sababu ziko vizuri, lakini mabasi namna ya kwenda. Kwa hiyo, hilo ni suala la usimamizi tu ambalo linaweza likaenda vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunazo barabara zetu za TARURA na tumepokea zaidi ya shilingi bilioni 9.0 kwa kipindi hiki tu cha Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, lakini kilometa ambazo zinahudumiwa ni 875. Mzunguko wa barabara ni kilometa 1,920. Tuna barabara za lami kilometa 43 tu sawa na 5.5%. Kwa hiyo, unakuta uharibifu wa barabara zilizo nyingi kila mvua inaponyesha barabara zinapata changamoto kubwa kwa sababu ya mvua. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaiomba Serikali iwaangalie vizuri TARURA na namna bora ya kuweza kuboresha zile barabara zikawa za lami, basi angalau tukaondokana na hali ya kila mwaka kuweza kufanya mabadiliko hayo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi pia tunanufaika na mradi wa TACTIC na tayari kuna mradi wa Soko la Kirumba na kilomita 2.9 za lami zinakwenda kujengwa pale, lakini tunalo Soko la Kabwalo nalo pia linakwenda kujengwa, kwa hiyo, ninachotaka kusema tu ni kwamba miradi inapokuwa ipo tayari tuombe sasa wakandarasi waweze ku-take off haraka badala ya kufika site halafu anapotea. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa kwenye barabara tunao wakandarasi zaidi ya watano wameshafika site halafu hawapo. Kwa hiyo, namna hii wakati mwingine inaleta picha ambayo sio nzuri sana. Hali halisi ni kwamba miradi ile ipo na tayari wakandarasi wamepewa na tunakwenda kufanya kazi hiyo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikiangalia katika miundombinu kitaifa ambayo inakwenda. Kwa mfano Uwanja wa Ndege wa Mwanza unapanuliwa na katika upanuzi ule tutakwenda kunufaika kwa sababu mazao ya samaki tayari tunayo ndege ambayo inabeba mazao kupeleka nje, Watanzania watanufaika wakiwemo Wanailemela.
Mheshimiwa Mwenyekiti, changamoto kubwa iliyopo tu pale ni kwamba, niombe tu Serikali ikamilishe masuala mazima ya fidia ili watu waweze kuishi kwa amani pale. Kwa sababu fidia zimetolewa Kilimanjaro, zimetolewa Dar es Salaam sasa na Ilemela nao ninaomba wakamilishe kwa sababu ule mradi ni mkubwa ambao unahitaji kukamilika. Habari ya kusema watawapa viwanja na nini, ni kuchanganya watu tu mawazo. Kama ni fidia wapewe tujue ni fidia ili na wao waweze kuishi na ule mradi uweze kuendelea. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna suala la umeme, nipongeze sana Serikali. Umeme sasa hivi Bwawa la Mwalimu Nyerere limekamilika. Megawati 2,115 ziko tayari, ambazo zinakuja kuleta jumla ya megawati zaidi 4,000 kwa nchi nzima. Maana yake ni kwamba, tuna zaidi ya umeme kuliko ule tunaohitaji kutumia, kwa sababu katika matumizi ya umeme tunaotumia hauzidi megawati 2,190. Changamoto inakuja kukatika kwa umeme. Niombe tu kwa sababu mimi ni mdau kwenye Kamati ya Nishati na Madini. Niombe sana, umeme unaozalishwa ni mwingi, tuombe regular maintenance kwenye vituo vyetu vya kupoozea umeme na uboreshaji njia za usambazaji. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, umeme unakuja kwa kilovolti 400 kwenye kituo cha kupoozea, unatoka pale kwa kilovolti 220 au 132. Kwa hiyo, unakuta miundombinu katikati pia haiko sawa. Nguzo ziko nyingi zimelala zimeanguka, lakini hazijawekwa. Zingine zinazobadilishwa ziko zimelala. Niombe sana usimamizi uendelee kuwa wa karibu zaidi, kwa sababu namwamini Naibu Waziri Mkuu ni msimamizi mzuri na kazi inaenda vizuri. Basi hawa walioko chini waweze kufanya hasa kwenye regular maintenances ili wananchi waelewe kwamba, umeme tunao wa kutosha na umeme utaimarika kwa sababu changamoto iliyopo sasa ni usambazaji tu ambao unahitaji kufanyiwa kazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niongelee SGR. Nipongeze sana ni mradi mzuri, lakini niwaombe Serikali kuna over employment pale ambayo haina sababu. Wako watumishi wengi ambao ukiwaangalia wanachukua fursa kubwa katika kuteka yale maeneo ambayo sasa wangeweza kuweka abiria wengi na wakazalisha zaidi. Kunakuwa na watumishi wengi ambao hata yale mafunzo hawana. Ikitokea hitilafu kidogo tu anawaambia tokeni tokeni. Ilitutokea sisi bahati mbaya Kilosa, mtumishi anakuja anasema, “tokeni, tokeni moto unawaka!” Maana yake hata yale mafunzo hana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa namna hiyo ndio unakuta umeme hauja- stabilize katika kuendesha unaweza ukakuta watu wenye ugonjwa wa moyo na wengine wanakanyagana. Niombe sana ajira zile, ziangaliwe watu wawekwe wenye utaalam. Pia na lugha yao kwa abiria iweze kuwa nzuri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nipongeze Serikali kwa ajira nyingi ambayo ipo, lakini tuelekeze zaidi katika Sekta Binafsi ambazo zimekuwa hasa zinaajiri watu wengi sana. Kuhusu Bolti wamelizungumzia suala la kodi bado ni changamoto sitaki kulirudia kwa sababu amelizungumza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, usafiri wa anga; tuna ndege nyingi za kutosha, lakini route za ndani tuziangalie vizuri na hasa hapa Dodoma. Dodoma – Mwanza, Dodoma – Arusha, Dodoma – Mbeya ni muhimu kuwa na ndege hapa. Wasafiri wengi wanakuja hapa Makao Makuu, lakini anatokea Mwanza lazima afike Dar es Salaam ndio aje hapa. Anatoka zake Mbeya achukue ndege aje huku kama hana gari. Kwa nini tusiwe na usafiri wa hapa kwa sababu ndege tunazo za kutosha? Tuone namna bora ya kuboresha usafiri wa ndani. Tumeongeza usafiri wa nje ni kweli abiria wanaongezeka basi niombe tuone namna ya kuangalia ratiba zetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru sana ahsante kwa fursa uliyonipa. (Makofi)
MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa Dkt. Angeline Sylvester Mabula. Nilimtaja Mheshimiwa…
MHE. DKT. ANGELINE S. L. MABULA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaunga mkono hoja. (Makofi)